Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kondoa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa kunipa fursa hii ya kuchangia hoja hii ya hotuba ya makadirio ya bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka 2019/2020 kama ilivyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango.
Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupatia fursa tena ya kukutana katika Bunge lako tukufu kwa ajili ya jambo hili kubwa kwa ajili ya Taifa letu na Watanzania kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu Mheshimiwa Makamu wa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa niaba ya Watanzania, kwani waliwaamini na sisi tunaona na Watanzania wanaona utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi unavyotekelezwa kwa kasi kubwa kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru na wewe binafsi pamoja na Mheshimiwa Naibu Spika, Wenyeviti wote wa Bunge kwa miongozo yenu mnayotupa tunapokuwa kwenye Bunge hili Tukufu ili tuweze kuwatumikia Watanzania kwa ujumla wake tunawashukuruni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nimshukuru sana, Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango Kaka yangu Dkt. Philip Mpango kwa kazi kubwa anayoifanya kwa ajili ya Watanzania kwenye Wizara hii ngumu kama ambavyo imeelezwa na Waheshimiwa Wabunge huu ndiyo moyo wa Serikali yetu, ndiyo roho ya Taifa letu hakika nakupongeza sana Dkt. Philip Mpango kwa kazi kubwa unayoendelea kuifanya na mimi nakutia moyo uendelee kulitumikia Taifa letu wala usirudi nyuma kwamba lazima apatikane Mtanzania wa kulibeba hili kwa kipindi hiki na Mtanzania aliyechaguliwa, Mtanzania aliyeaminiwa, Mtanzania aliyeteuliwa na Mwenyezi Mungu ni wewe kwa ajili ya Taifa letu, usikate tamaa endelea kusimama imara naamini mishale yote inapiga lakini naamini bado uko imara, endelea kusimama imara Mheshimiwa Waziri wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema maneno hayo, naomba pia niwapongeze sana, watendaji wetu ndani ya Wizara ya Fedha na Mipango na wao pia naomba niwatie moyo, waendelee kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu wa hali ya juu, wameipata nafasi ya kuwatumikia Watanzania, wawatumikie Watanzania kwa moyo wote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya maneno hayo ya utangulizi naomba sasa niseme maneno machache kwenye hoja ambazo zimechangiwa na Waheshimiwa Wabunge na nianze na hoja ya kwanza ambayo ilisema makusanyo ya kodi yameshuka sana kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano.
Mheshimiwa Spika, naomba niseme jambo hili siyo la kweli hata kidogo, siyo la kweli kwa sababu Watanzania wanaona, Watanzania wanaona yanayotendeka ndani ya Taifa lao, ni kupitia makusanyo ya kodi haya ambayo leo tunaambiwa yameshuka.
Mheshimiwa Spika, kama makusanyo ya Kodi yameshuka, tungeweza wapi kuanza utekelezaji wa mradi wa reli ya kisasa, isingewezakana hata kidogo, isingewezekana leo hii Stiegler’s Gorge kule Rufiji, mradi ule umeanza kutekelezwa kama makusanyo yangekuwa ni ya chini kama inavyodaiwa kwenye Bunge hili tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwaombe Waheshimiwa wabunge, tuwape moyo watumishi wetu wanaoshughulika na kazi hii ngumu ya ukusanyaji wa mapato ya Taifa letu, wanaifanya kazi katika mazingira magumu, wanaifanya kazi hii kwa kujitolea maisha yao, ni kazi ngumu, ni kazi yenye viahatarishi vingi lakini wanaifanya kwa nguvu zao zote.
Mheshimiwa Spika, nimeanza kusema kwamba siyo kweli makusanyo yamepungua kwa sababu ukiangalia kwa miaka mitano mfululizo, tukianza mwaka 2014/2015 makadirio ya ukusanyaji wa Kodi yalikuwa ni shilingi trilioni 11.9, kipi kilikusanywa mwaka 2014/2015.
Mheshimiwa Spika, kilichokusanywa ilikuwa ni trilioni 10.66 hicho ndicho kilichokusanywa 2014/2015 kabla Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli ya Awamu ya Tano haijaingia madarakani, leo tunapoongea mwaka 2017/2019 kipi kimekusanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi ya Awamu ya Tano.
Mheshimiwa Spika, makadirio yalikuwa shilingi trilioni 17.3 haya ni ya kodi, na nini kilikusanywa, kilichokusanywa ilikuwani trilioni 15.25 ukilinganisha haya mambo mawili unaweza ukaelewa, ni kweli mapato yamepungua, makusanyo yamepungua, taarifa hizi bahati nzuri, takwimu za kikodi huwa hazijawahi kudanyanya na hili naomba Waheshimiwa Wabunge tuwatendee haki Watanzania.
Mheshimiwa Spika, Kwa sababu wao ni mashahidi wanaona, wao ni mashahidi wanadhihirisha kile ambacho kinatendwa na Serikali yao waliyoiamini.
Mheshimiwa spika, limeunganishwa jambo hili na jambo la pili kwamba tunaangalia sasa kati ya uwiano, kati ya mapato ya Kodi na Pato la Taifa. Wanasema kwamba limepungua ni kweli uwiano wa Kodi dhidi ya Pato la Taifa kutoka asilimia 13.2 mwaka 2016/2017 hadi imefika Pato la Taifa asilimia 12.8 kwa mwaka 2017/2018.
Mheshimiwa Spika, nini kimetokea? Kilichotokea hii ndiyo naomba Watanzania waelewe, calculations hizi zimefanyika kwa kufuata rebasing ambayo ni marekebisho yaliyofanywa kwenye takwimu za Pato la Taifa, kwamba yamefanywa mabadiliko, na kama tusingetumia rebasing mabadiliko ya takwimu za Pato la Taifa, mchango, uwiano wa kodi dhidi ya Pato la Taifa ilikuwa ni asilimia 3.6. Kwa hiyo kama tungetumia mwaka wa kizio wa 2017, uwiano huu usingekuwa umepungua.
Kwa hiyo, hili linadhihirisha kwamba mapato haya hayajapungua, mapato yako vizuri tukiangalia makadirio yameongezeka na makusanyo halisi yameongezeka, kwa hiyo, tuwatendee haki Watanzania, tuwaeleze ukweli kile ambacho Serikali yao waliyoiamini kipi Serikali inafanya.
Mheshimiwa Spika, naomba niseme kuhusu jambo la pili nayo ni kuhusu Ofisi ya Msajili wa Hazina kwamba ofisi hii bado haijaonyesha uimara wake kwenye kusimamia kampuni na mashirika ya umma. Naomba kulihakikishia Bunge lako tukufu kwamba Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa sasa, ni imara sana, na sisi sote ni mashahidi tunaona utendaji mzuri wa watumishi wetu kwenye ofisi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nasema hili kwa sababu tunaiona Ofisi ya Msajili wa Hazina ikiendelea kufanya tathmini na ufuatiliaji ili kuimarisha usimamizi na ufanisi wa mashirika ya umma pamoja na kampuni ambazo Serikali yetu imekeza huko, tunafatilia kwenye hisa chache, lakini pia kule ambako Serikali yetu ina hisa nyingi.
Mheshimiw Spika, matokeo ya hili tumeona kabisa kwamba hata mapato yaliyokusanywa kutoka kwenye gawio, kutoka kwenye kampuni hizi na mashirika ambapo Serikali yetu ina hisa yameongezeka kwa kiwango kikubwa sana.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kwa mwaka huu wa 2018/2019 ambapo hadi tarehe 30 Aprili, 2019 Ofisi ya Msajili wa Hazina ilikuwa imekusanya shilingi bilioni 602.64 ikilinganishwa na ilichokuwa kimetarajiwa kukusanywa ambayo ilikuwa ni shilingi bilioni 597.77 hii tunaiona ni zaidi ya asilimia 101 na hii ni tarehe 30 Aprili; je, tukienda mpaka tarehe 30 Juni, 2019 tunaiona Ofisi ya Msajili wa Hazina ikiwa inafanya kazi yake vizuri katika kipindi hiki.
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Msajili wa Hazina inaendelea pia kushughulikia ukaguzi maalum katika taasisi ambazo Serikali yetu ina hisa chache ambapo tayari mpaka tarehe 30 tulishakagua taasisi 33 na tayari tumeona mapungufu yaliyokuwa yamebainika na mapungufu hayo yanaendelea kufanyiwa kazi ili sasa tuweze kuona taasisi hizi na mashirika haya yakifanya kazi kwa tija kwa ajili ya Watanzania.
Mheshimiwa Spika, Serikali yetu pia imechukua hatua mbalimbali, haya yote yasingewezekana kama Serikali isingeimarisha Ofisi hii ya Msajili wa Hazina na Serikali inaendelea na mambo mbalimbali kuhakikisha Ofisi hii inaendelea kuwa imara ili tuweze kupata faida kwenye taasisi na mashirika haya ambayo tumewekeza, kwa mfano, Serikali tayari imeandaa Waraka wa Baraza la Mawaziri wenye lengo la kurekebisha Sheria ya Ofisi ya Msajili wa Hazina ili kuendelea kuiimarisha zaidi, ili iweze kufanya kazi kwa tija zaidi kwa ajili ya Watanzania wote, lakini pia tumeona Serikali yetu imeongeza Bajeti ya kutosha kwenye Bajeti ya maendeleo kwenye Ofisi hii ya Msajili wa Hazina hadi kufikia shilingi bilioni
2.3 kwa mwaka wa fedha 2019/2020 kutoka bilioni 1.6 tu zilizokuwa za mwaka 2018/2019.
Mheshimiwa Spika, hii yote inalenga kuimarisha mifumo ya usimamizi ya kielektoniki ili tuweze kuyafatilia mashirika na taasisi ambazo tumewekeza kama Serikali yetu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu utendaji wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, liko jambo ambalo limehojiwa nalo ni malipo ya mafao ya wastaafu 1071 wa TAZARA yamefikia wapi.
Mheshimiwa Spika, napenda kuliambia Bunge lako tukufu kwamba kundi la kwanza ni la wastaafu 1172 walioacha kazi baada ya muda wao wa kustaafu kutimia kama ambavyo ilivyoainishwa katika makubaliano ya pamoja kati ya TAZARA na watumishi hao.
Mheshimiwa Spika, hivyo basi, kwa kuwa wastaafu hawa hawakustahili kulipwa kiinua mgongo kwa sababu walikuwa wametimiza vigezo vya kupata malipo ya pensheni ambayo yanaendelea kulipwa kila mwezi. Pia kulikuwa na kundi la pili ambalo kundi la pili la wastaafu hawa wanastahili kulipwa ambapo Serikali imeridhia kuwalipa kama ifuatavyo na hatua za malipo zimefikia katika hatua mbalimbali, kundi la kwanza ilikuwa ni Shauri la S. Dagaa na wenzake 271 kesi namba 88 ya mwaka 2009 hawa Serikali imeridhia baada ya kesi kuisha waweze kulipwa shilingi trilioni 1.422.
Mheshimiwa Spika, kundi la pili lilikuwa ni Shauri la Kiobya na wenzake ambapo Serikali inatakiwa kulipa jumla ya shilingi bilioni 41.549; Shauri la tatu ambalo ni kundi la tatu wanaostahili kulipwa ilikuwa ni Shauri la Kassim Mshana na wenzake 79 ambapo jumla ya shilingi 814,695,000 zinatakiwa kulipwa kwa ajili ya Kassim Mshana na wenzake 79.
Mheshimiwa Spika, kundi la nne, ilikuwa ni Shuari la Kaduma na wenzake 130 ambapo wanatakiwa kulipwa jumla ya shilingi bilioni 8.042, Ofisi ya Msajili wa Hazina inaendelea kushughulikia malipo yao kwa makundi haya niliyoyataja na muda siyo mrefu basi watalipwa mafao yao kama ambavyo imeelekezwa na mahakama.
Mheshimiwa spika, jambo lingine ambalo limeelezwa kwa urefu na ambalo limekuwa likirudia mara kwa mara nayo ilikuwa ni malipo ya wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika, malipo kwa ajili ya wastaafu hawa Serikali ilishayamaliza, hii ni kwa mujibu wa hati ya makubaliano yaani deed of settlement ya tarehe 20 Septemba, 2005 na kuthibitishwa na mahakama kama hukumu tarehe 21 Septemba, 2005 Serikali tayari ilishawalipa stahiki zao wastaafu hawa waliokuwa 31,788 wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyovunjika tarehe 30 Juni, 1977.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, naomba nirejee kusema naunga mkono hoja hii ya Wizara ya Fedha na Mipango na nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)