Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na mimi nianze kwa kweli moja kwa moja kwa kuwapa hongera sana Waziri Mpango na timu yako wewe na Naibu na timu yako yote ya Wizara Katibu Mkuu na wenzako wote, mmefaya kazi nzuri sana. Bajeti hii imekuwa ni bajeti ya kibiashara, imekuwa ni bajeti ambayo inajielekeza kwenye uwekezaji mkubwa, ni bajeti ya Watanzania. Hongera sana Dkt. Mpango mmeonesha uwezo mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kabla sijasahau, nianze na hili ambalo limeainishwa kwenye kitabu cha Kamati ya Bajeti ukurasa wa 60, haya madeni ya walimu. Nafikiri kama nchi sasa lazima tukubaliane kuna madeni ya walimu shilingi bilioni 61, kuna kujenga Ofisi za Kibalozi na kuendelea kukamilisha maboma ya shule.

Kwa maoni yangu na ushauri wangu ni kwamba lazima tuchague kimojawapo, kipi kinaanza na ushauri wangu sincerely kabisa Waziri wa Fedha anza kupunguza madeni ya walimu. Walimu hawa ndiyo kila kitu. Ofisi za Kibalozi zinaweza zikatusubiri kidogo lakini madai ya walimu kama ambavyo yameainishwa kwenye kitabu hiki cha Kamati ya Bajeti nafikiri Mheshimiwa Waziri Mpango ni muhimu sana. Tuwalipe walimu hawa madeni yao yaliyohakikiwa. Hata kule kwangu Kasulu Mji na Kasulu Vijijini kuna shida ya walimu ambao wanadai madeni yao ya muda mrefu na hawajalipwa, nilikuwa nafikiri nianze na hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo Mheshimiwa Waziri wa Fedha nikiendelea kuwapa pongezi kubwa ni huu mkakati wenu kama tulivyochangia kwenye hotuba mwanzo kujielekeza kwenye maeneo ya kutafuta fedha yaani vyanzo vya mapato. Mimi nimefarijika sana kwamba sasa mnajielekeza kwenye uvuvi wa Bahari Kuu ambao kuna ushahidi wa kila aina kwamba baadhi ya nchi zinaendesha mambo yake kwa kutumia fedha ambazo wanapata kwenye uvuvi wa Bahari Kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia niwapongeze sana kupitia kwako na timu yako kwamba sasa TRA wamezuiliwa kufunga biashara. Mimi nashauri na nadhani Mheshimiwa Waziri muende mbali zaidi, ile migogoro inayoendelea ndani ya TRA kati ya wafanyabiashara na TRA na baadhi ya mashauri (kesi) ziko kwenye Tax Tribunal unaweza kupitia mamlaka uliyonayo wakarejea kwenye meza ya mazungumzo. Yako maeneo nina ushahidi kabisa wanabishana kati ya wafanyabiashara na TRA. Mfanyabiashara amekubali kulipa shilingi bilioni mbili, TRA wanang’ang’ania alipe shilingi bilioni sita na wanapelekana kwenye Tax Tribunal.

Ushauri wangu sincerely nilikuwa nafikiri Mheshimiwa Waziri unaweza ukaenda mbali zaidi sasa kwamba mashauri yale ambayo bado hayajaamuliwa, yarejeshwe kwenye meza wazungumze kati ya TRA na wafanyabiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu niko kwenye vipaumbele, kwenye kitabu chako Mheshimiwa Waziri umeainisha vizuri juu ya vipaumbele utaviwekea mkazo. Mimi ni mkulima na ninapenda kilimo. Ningependa nizungumzie eneo la kilimo mambo mawili; kwanza suala la mbegu. Mheshimiwa Waziri wa Fedha, nchi hii tunajitosheleza kwa mbegu za nafaka kwa maana ya mahindi, maharage, mtama na mpunga kwa asilimia 32 tu.

Sasa nilikuwa nakuomba sana kama ulivyoeleza kwenye mkakati wako wa kibajeti tunaelekea kwenye uchumi wa viwanda ambao msingi wake ni kilimo, basi tuboreshe eneo hili la mbegu. Mheshimiwa Waziri, Serikali ni moja, tuna JKT sasa, Magereza, Wakala wa Mbegu na Vyuo vya Utafiti tuelekeze fedha nyingi kwenye utafiti ili tuweze kupata mazao ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, juzi tu Mheshimiwa Rais ametuonesha kitu kipya kabisa, alipokwenda Zimbabwe tumepata soko la mahindi karibu tani 800,000 huu ni ushahidi kabisa kwamba Mheshimiwa Waziri tuelekeze nguvu huko ili hatimaye mazao ya nafaka nayo yawe ni mazao ya kiuchumi, mazao kwa ajili ya kuuza kwenye masoko yetu ya nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine Mheshimiwa Waziri wa Fedha ambalo ningependa nilizungumzie, ulizungumza siku ile ya hotuba yako unahitimisha ulishukuru juu ya kikosi kazi cha kodi sasa sielewi labda unaweza ukalieleza vizuri zaidi kwanini kikosi kazi cha kodi hicho hicho kisiwe basi ni kikosikazi cha kusaidia uwekezaji na menejimenti ya uchumi. Siku ile nilikutajia baadhi ya watu ambao mimi nawafahamu nilifanya nao kazi wenye maarifa makubwa kabisa, nikamtaja Profesa Ndullu, ni mtu mwenye uwezo mkubwa, nikamtaja Ndugu Mafuru aliekuwa TR lakini bado kuna watu kama Dkt. Kimei aliyekuwa Mkurugenzi wa CRDB hawa ni watu wenye maarifa makubwa sana, watumie watu hawa tutoke hapa tulipo. Kupunguza umaskini kutoka asilimia 28 kuja asilimia 26 nadhani Waheshimiwa Wabunge mtakubaliana na mimi kwamba hiyo kasi ni ndogo sana. Ni vyema tujikite watu wenye maarifa watusaidie katika maeneo ambayo nina hakika tunaweza tukajikwamua.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Waziri kwa muktadha hu huo haya mazao muhimu nimemsikia sana ndugu yangu Ndassa amezungumza vizuri sana zao la pamba, hayo mazao ya kimkakati, zao la pamba, korosho, kahawa na chai, Mheshimiwa Waziri hayo mazao yanaanguka/yanaporomoka. Ushauri wangu kikosi kazi hicho hicho wataalam wanaokusaidia Mheshimiwa Waziri basi wakae chini waangalie ni kwa nini pamba inaanguka sasa hivi, ni kwa nini korosho tunaingia kwenye migogoro mikubwa sana. Ni kwa nini kahawa inaanguka vilevile katika masoko yetu. Nafikiri mambo hayo yatatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuema hayo, nina mawili madogo ya mwisho; la mwisho ni ujenzi wa reli ya SGR. Mimi Mbunge wa Kigoma nisipozungumza SGR hakuna atakayenielewa. Mheshimiwa Waziri, naendelea kukusisitiza katika mikakati endelevu na bahati nzuri juzi Rais wa Congo/Rais wa DRC Mheshimiwa Tshisekedi amezungumza juu ya biashara. Huwezi ukafanya biashara na Congo kama huwezi kujenga SGR kwenda Kigoma. Lile tawi la Tabora – Kigoma kwa maoni yangu tulipe kipaumbele kwa sababu fedha nyingi na mzigo mkubwa uko Congo ya Mashariki ambapo msigo ukifika Kigoma utaingia kwenye tishari na utavuka kwenda DRC Congo. Pia usisahau ile Nickel ilioko Msongati ya Burundi ni tawi lile la kutoka Uvinza kupita Kasulu kwenda mpaka Msongati ya Burundi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nafikiri tujielekeze kiuchumi, kibiashara na hayo ni maeneo ambayo yana mzingo mkubwa na mzigo mkubwa huo ndiyo utakaosaidia uchumi wetu na kujenga matawi mengine ya reli na mambo mengine ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa nizungumzie suala la... na hili nalisema sana, mikoa ambayo iko nyuma nchi hii ina mikoa minne iko nyuma kuliko mikoa mingine yote na sababu za kuwa nyuma si kwamba wale watu ni watu wajinga, la hasha! Ni watu wenye maarifa lakini wamekwazwa na madhila ya historia. Mikoa hiyo ni Kigoma, Katavi, Singida na Rukwa. Nilitarajia Mheshimiwa Waziri kuliko kugawa rasilimali tu pro rata tunaita, kwa watu wote sawa, nafikiri wakati umefika nammshauri Mheshimiwa Rais Magufuli ana uelewa mkubwa katika masuala haya kwamba ile mikoa ambayo iko nyuma kwa sababu za kihistoria nashauri kabisa Mikoa ile ipewe upendeleo maalum na upendeleo huo maana yake slow match na quick match. Ile mikoa iliyoko nyuma na yenyewe iweze kuwa katika usawa na mikoa mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa ni Gridi ya Taifa; mikoa miwili bado Mheshimiwa Waziri wa Fedha haijaungwa kwenye Gridi ya Taifa. Ni muhimu sana mikoa hii ya Kigoma na Katavi nayo ifanane na mikoa mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja hii na nasisitiza hotuba hii/bajeti hii ni ya msingi sana. Imejikita kwenye maeneo ya msingi kabisa. Hongereni na chapeni kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Ahsante sana. (Makofi)