Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ndanda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi nichangie mchana huu kwa hoja tuliyonayo hapa mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nikiwa ninajijenga sasa ili niweze kuchangia hoja yangu, nilikuwa nataka kwanza nitoe taarifa ndani ya Bunge lako tukufu kwamba kuna magazeti ambayo hatuna uhakika sana, lakini kwa sura ya gazeti hili, inaonekana kama wanatumika kulichafua Bunge lako tukufu, kwa sababu kichwa cha habari cha Gazeti la Tanzanite leo, wanasema njama kukwamisha bajeti yafichuka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huku ndani kuna sura za Wabunge mbalimbali, wakiwepo wa Chama cha Mapinduzi pamoja na Wabunge wa Opposition, nikiwepo mimi pamoja na Mheshimiwa Msigwa, lakini gazeti hili ukienda ukurasa wa kwanza kuna tangazo, ukurasa wa pili, kuna tangazo la ndege hapa, safari za Bujumbura, Entebbe na ndege yenyewe ni Air Tanzania Corporation. Tunaamini kwamba chombo chochote kilicho makini kwenye kufanya kazi zake, na kama kweli kina nia njema ya kusaidia watu wake ikiwa ni pamoja na kuacha matumizi mabaya ya fedha, hatuwezi kuamini sana kama gazeti hili siyo mali ya Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwandishi ameendelea, ukienda ukurasa wa tatu anasema, mtandao hatari wa rushwa ndani ya TAKUKURU wabainika. Amewataja hapa na watumishi wengi tu, wanaofanya kazi TAKUKURU akiwatuhumu kuchukua rushwa mbalimbali, ni gazeti ambalo Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikipeleka matangazo yake kwa maana kwamba wanaliamini na kila kinachofanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa kuweka kumbukumbu sawa, niomba labda ndugu zetu wasaidizi watusaidie wampatie Waziri wakati anajumuisha atueleze, criteria zilizotumika kuwapa nafasi ya kupata matangazo Gazeti la Tanzanite ambalo hata copy zinazochapwa hazifiki 2000 na kwamba hii tunaamini ni matumizi mabaya ya fedha za Serikali, na gazeti hili linatumika na Chama cha Mapinduzi kama sehemu ya propaganda la kudhoofisha watu wanaotaka kusema na kushauri Bunge lako. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo machache, mimi nina mambo ambayo ninataka niyazungumzie. La kwanza kabisa linalohusiana na suala la ETS (Electronics Tax Stamps) na namna mabavyo tender hii imepatikana, lakini pia nataka niseme juu ya Pays As You Earn, kodi wanayotozwa watumishi wanyonge wa nchi yetu kutoka kwenye mishahara yao, kutakuwa pia suala la vitambulisho vya wajasiriamali ambavyo tunaaminishana Mheshimiwa Rais amevitoa. Sasa nataka Waziri atuambie, Rais ametoa vitambulisho au anauza vitambulisho! Nitakapojenga hoja tutafika hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa kutakuwa na suala linalohusiana na upungufu wa fedha za kigeni pamoja na mauzo yetu nje ya nchi kutokana na kutokuwa na mwendelezo mzuri wa zao la...
T A A R I F A
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Cecil Mwambe kuna taarifa, Mheshimiwa Bashe.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika, natakakumpa tu taarifa Mheshimiwa Cecil, kwamba Chama cha Mapinduzi ni chama ambacho kinaamini katika uhuru wa fikra na maoni hakiwezi kutumia gazeti la kihuni, lisilokuwa na ethics za editorial, linaloitwa Tanzanite.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tu nimpe hiyo taarifa, pamoja na kuwa naungana naye, lakini Chama cha Mapinduzi hakiwezi kutumia Tanzanite kwa sababu ni gazeti la wahuni.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Cecil Mwambe, unaipokea taarifa hiyo?
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, napokea, na nimshukuru kaka yangu Bashe kwamba ni namna gani tutaona sasa Serikali inayojiita makini inafanya kazi na wahuni ambao wenye Chama cha Mapinduzi hawataki kuipokea, kwa hiyo, mwisho wa siku nitazungumza kwenye haya mambo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nilisema hapa nataka niongee suala la ETS, sisi ndani ya kamati na mimi nimekuwa mhudhuriaji mkubwa kabisa wa kamati ya bajeti. Naomba nitoe kielelezo cha pili kinachoonyesha ubadhirifu mkubwa ikiwa ni pamoja na taarifa za PPRA, Gazeti la The Guardian la Jumanne tarehe 3 Oktoba 2017 wakionya namna ambavyo SIPA ilivyopata tender ya kutengeneza stamp kwa ajili ya kuweka kwenye mambo mbalimbali kama alama ya TRA.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba na hii iingie kwenye taarifa hapo na Mheshimiwa Waziri aje atujibu baadaye atakaporudi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi ninachokisema kama Mheshimiwa Rais Magufuli anasikiatunavyoyasema hapa na yuko tayari kuwasaidia watanzania, hatua ya kwanza ambayo tungependa aichukue ni pamoja na kuichunguza Kampuni ya SIPA inayotengeneza electronic stamps zinazotumika na makapuni mbalimbali kuwataarifu Serikali kwamba ni namna gani ambavyo makampuni hayo yamezalisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kampuni hii ni ya kifisadi, Uganda wamekataa hawataki kufanya nayo kazi, Kenya wamekataa hawataki kufanya nayo kazi, nchi zenye uchumi mkubwa kuliko Tanzania. Wanachokifanya wao kazi yao kubwa ni kuhesabu, kwa mfano, packets za sigara. Packet moja ya sigara gharama yake ni shilingi nane, lakini kwenye packet hiyo hiyo ya sigara, Serikali inapata shilingi tatu! Sasa tunataka kufahamu, kwa nini mtu anayefanya kazi ya kuhesabu anapata fedha nyingi kwenye item moja, tofauti na ambavyo Serikali imekuwa ikikusanya kwenye eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, gharama za stamps ni kubwa zaidi kuliko na gharama za kodi inayokusanywa na Serikali, lakini, Serikali hii na Mheshimiwa Mpango kama yuko hapo very genuine, leo au kesho atakaposimama kuhitimisha hoja yake siku hiyo, atueleze! Tender ya kuwapa hawa watu kampuni hiyo ya uchapishaji ilipatikanaje? Swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, tunataka atueleze, kwamba hao SIPA ambao wako hapa Tanzania, mkataba wao unasemaje. Kwa sababu taarifa zilizoko mtaani na sisi tunazisikia, kama wawakilishi wa watu ni kwamba mwisho wa siku watakapomaliza mkataba wao wa miaka mitatu, wataondoka na mashine walizozileta ambazo Watanzania wamezitumia! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii haiishii hapo tu, mlisema Rais anataka kuwasaidia wanyonge, lakini tumekuja kugundua kwamba Baraza la Mawaziri linataka kumgombanisha Rais na wanyonge kutokana na maamuzi wanayoyafanya. Kampuni hii ya SIPA inapokwenda kwenye vinywaji baridi, tuchukulie labda mfano wa soda, Coca Cola. Kwenye Coca Cola moja, stamp inawekwa kwa shilingi hizo hizo saba, shilingi nane, Coca Cola hii Serikali wanakwenda kupata labda shilingi moja tu, nilitumia hiyo mifano ya namba kwa sababu mambo ya namba kidogo magumu, kwa hiyo, nitaomba Waziri aje atuelezee. Katika kila stamp moja ni shilingi ngapi na katika kila chupa moja wanakusanya shilingi ngapi na mwisho wa siku, hizi gharama zinakwenda ku-affect wanyonge ambao Mheshimiwa Rais anataka kuwatetea! Hili linahusiana na masuala ya ETS. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo hapa lingine, na sisi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni leo tulitaka tushauri, pamoja na figisu zilizofanyika lakini tungeomba labda baadhi ya maeneo Serikali iyachukulie maanani. Kwenye ukurasa wa 39, wanaongea kuhusu habari ya Pay As You Earn. Wanyonge hawa, sasa hivi kwa takribani miaka mitatu hawajaongezewa mshahara, mategemeo ya wanyonge wengi, wakiwemo walimu, madaktari na watumishi wa umma kiujumla, kwamba walifikiri basi Serikali hii makini inayowapenda wao kama wanyonge, leo ingekuja hapa ikasimama, ikasema tunapunguza kodi ya mishahara ya wafanyakazi na kupeleka kwenye digit moja kama ambavyo imefanya kwa wafanyabiashara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini matokeo yake, nao tunawachukua kama sehemu ya mtaji wetu! Ajira hatutoi, fedha kidogo wanayoipata, inakwenda kule, halafu tunasimama hapa tunakwenda kuambiana na Waziri anasimama akijinasbu, tena Waziri wetu ni mtu wa mahesabu ni mchumi, anasema uchumi wetu unakua kwa asilimia saba, inflation imesimama sijui kwa muda gani hata haieleweki, bei ya sukari wakati mwalimu wa shule ya msingi kima chake cha chini kilikuwa shilingi 350,000, sukari ilikuwa shilingi 1,500. Leo hii Serikali ya Awamu ya Tano haijaongeza mshahara hata shilingi moja, bado bei ya sukari imepanda mpaka shilingi 3,000 lakini kodi ya mshahara imeendelea kumtoza kiasi kilekile, sawasawa na miaka itatu iliyopita, jambo ambalo aliliacha Rais, mzee wetu Jakaya Kikwete. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunajiuliza, tunaposema uchumi umepanda, ni nini sasa hapa kinafanyika na ukiangalia hapa kwenye hiki kitabu ambacho nimesema Waziri akakisome kwa sababu ya muda hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna jambo lingine, sisi tunataka tuelezane hapa ukweli, hivi ni kweli tuna nia ya dhati kabisa ya Muungano kati ya Tanzania na Zanzibar? (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wazanzibar wengi najua watasimama watakapopata nafasi, lakini sidhani kama wanaweza wakasema jambo hili. Kwenye kitabu chetu tumesema hivi, toka mwaka 1977 liko kwenye ukurasa wa 34, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haijawahi kupeleka gawio lao Wazanzibar ili wakafanye shughuli zao za maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, awamu hizi zote zimeongozwa na Chama cha Mapinduzi wala siyo CHADEMA, kule pia hivyo hivyo na wale sisi ni ndugu zetu. Sasa Waziri akisimama atueleze, kama wanataka Kisiwa cha Zanzibar kipotee kwa sababu ya masuala ya kiuchumi, asimame na aseme, kwa nini hawapeleki fedha kwa ajili ya Wazanzibar! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, suala la vitambulisho vya wajasiriamali, imekuwa kero sana kwa wananchi na Mbunge yeyote wa Zanzibar atakayesimama akisema anaunga mkono jambo hili, akawe kafara ya wananchi hawa ambao wanadhurumiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia kwa muda mrefu na mimi naomba...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)