Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpwapwa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Kwanza nampongeza Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze la kwanza kwa kuishukuru Serikali, tangu nimeingia Bungeni mwaka 1990 naiomba Serikali ijenge barabara ya kutoka Mpwapwa kwenda Kongwa mpaka Mbande kwa kiwango cha lami, sasa baada ya miaka 25 naishukuru sana Serikali mwaka huu imekubali kujenga barabara ya lami kutoka Mpwapwa kwenda Kongwa mpaka Mbande. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nakushukuru sana na nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Magufuli kwa kusikiliza kilio cha wananchi wa Mpwapwa cha muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, jukumu/kazi yetu sisi Wabunge tupo hapa kupitisha Bajeti ya Serikali na mimi nina hakika bajeti hii itapitishwa bila kupinga, nina hakika kabisa tutapitisha bajeti, lakini Mheshimiwa Waziri, tunapitisha bajeti lakini jambo la kushangaza kwa sababu mikoa inapangiwa bajeti yake na Halmashauri inapangiwa bajeti yake, lakini jambo la kushangaza hizi fedha zote ambazo zinatengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo hazifiki zote, kwa nini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano, katika Mkoa wa Dodoma mwaka 2017/2018 tulitengewa shilingi bilioni 35 lakini mkoa ulipewa shilingi bilioni 15, asilimia 43 tu na mwaka 2018/ 2019 tumetengewa karibu shilingi bilioni 46, tumepewa shilingi bilioni 30. Sasa na ndiyo maana miradi mingi inakwama, mikoa mingi.
Mheshimiwa Spika, bahati nzuri mimi nipo kwenye Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa na ndiyo tunachambua bajeti ya mikoa yote, bajeti ya Serikali. Hakuna mkoa ambao fedha zinazopitishwa na Bunge mkoa unapata zaidi ya asilimia 60. Sasa tutatekelezaje hii miradi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama fedha zote hazifiki basi angalau Mheshimiwa Waziri uwe unatueleza kwamba fedha hazikwenda zote kwa sababu moja, mbili, tatu; kama kuna majanga yametokea, milipuko ya magonjwa imetokea au kama kuna jambo lolote. Lakini kama hutuelezi na wananchi kule wanahoji, mmeahidi kuchimba visima vya maji, havichimbwi.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi kuna miradi inayoendelea Wilaya za Mpwapwa na Kongwa, Jimbo la Kibwakwe, lakini miradi inachukua muda mrefu kukamilika kwa sababu fedha hazipelekwi na wakandarasi hawalipwi. Kwa hiyo, hili limekuwa ni tatizo kubwa sana. Kwa hiyo, nakuomba sana Mheshimiwa Waziri, fedha ambazo zinapitishwa hapa kwa ajili ya miradi ya maendeleo mikoani na Halmashauri zipelekwe zote.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna miradi kwa mfano ya vituo vya afya na zahanati, mwaka jana mlijitahidi katika Jimbo la Mpwapwa nilipata fedha kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya cha Mima, nashukuru. Lakini mwaka huu Jimbo la Mpwapwa sikutengewa fedha kujenga hata kituo kimoja cha afya na mimi nimeomba kituo cha afya ambacho kimeanza kujengwa sasa miaka kumi, Kituo cha Afya Mbori.
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Mbori ni muhimu, kituo hiki kikikamilika watakaohudumiwa pale ni wananchi wa Chamkoroma, Tubugwe, Mseta, Matomondo, Mlembule, Mpeta, Godegode na Kimagai. Hiki kituo kitahudumia watu wengi. Sasa kama sikupata fedha ya kujenga kile Kituo cha Afya cha Mbori na Kituo cha Afya cha Belege, nitafanyaje? Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba sana kituo hiki tupewe fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo jingine ni barabara; nimezungumzia barabara ya lami kutoka Mpwapwa kwenda Kongwa – Mbande lakini kuna barabara kwa mfano barabara ya kwenda Mima kutoka Mpwapwa – Gulwe- Belege – Chitemo – Mima unakwenda Igoji I, Igoji II, Isalaza pale mpaka Seruka. Mheshimiwa Spika wewe umekaa Mima, unaifahamu sana hii barabara; hii barabara ni muhimu. barabara hii kuna kata nane zinahudumia barabara hii, barabara hii haipitiki, inapitika kwa shida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilikuwa nakuomba sana Mheshimiwa Waziri zitengwe fedha za kutosha kwa ajili ya ukarabati hii barabara ya kutoka Mpwapwa kwenda Mima mpaka Seruka. Hii light grading haitatusaidia, tunataka heavy grading barabara ilimwe, ishindiliwe, ijengwe na mifereji ili iweze kuhudumia wananchi wa maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kilimo cha umwagiliaji; katika Jimbo la Mpwapwa na Jimbo la Kongwa kuna miradi mingi ya umwagiliaji, lakini miradi hii sasa kuta zote zimebomoka, kwa hiyo miradi hii haifanyi kazi. Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana Wizara ya Kilimo ifanye ukarabati wa miundombinu hii skimu za umwagiliaji ili wananchi kwa mfano wa Kata za Matomondo, Chamkoroma, Tubugwe kule pamoja na Lumuma na Malolo, hizi skimu za umwagiliaji zitasaidia sana. Kilimo cha umwagiliaji ndiyo mkombozi wetu katika Wilaya ya Mpwapwa na Kongwa ili kuondokana na tatizo la njaa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono asilimia mia moja, ahsante. (Makofi)