Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Yussuf Salim Hussein

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Chambani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba nianze kwa maneno ya mshairi yafuatayo na naomba Waheshimiwa Mawaziri wanisikie namna gani mshairi huyu aliiiasa nafsi. Alisema; huku giza lajikita nafsi yangu inuka, inuka uje nakuita nafsi yangu itika, sikuiti kwa kukuteta nafsi yangu isijeshituka. Akasema, nakuita uje na zibo nafsi yangu isijezibuka, kama hakiyo ni robo, nafsi yangu kilo epuka, siwe na matobotobo nafsi yangu utaaibika, nakuita uje na fungo nafsi yangu isijefunguka, umeumbwa kwa udongo nafsi yangu utaondoka, basi uache maringo nafsi yangu jua tauka. Unijie na stara nafsi yangu umesitirika, uje ukitia idhara nafsi yangu utaumbuka, maisha ni msafara nafsi yangu unakumbuka, usinijie na hasira nafsi yangu utaathirika, usinije na papara nafsi yangu utanichoka, bali uje na subira nafsi yangu utatukuka, kama waja na kiburi nafsi yangu bora geuka, kwangu uje na hadhari nafsi yangu utasalimika, yadhahiri ama siri nafsi yangu yameandikwa. Haya basi, anasema haya kuwa msikivu nafsi yangu semezeka, dunia mti mkavu mara waweza kung’oka, huwabwaga wenye nguvu nafsi yangu utanusurika…

SPIKA: Mheshimiwa Yussuf bajeti sasa.

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nimeanza maneno haya kusudi madaktari wetu hawa wa uchumi wanisikie. Kwa muda wa miaka mitatu mfululizo tulikuwa tunaionesha Serikali namna gani uchumi wetu unaanguka, namna gani tunapata hasara, namna gani maisha ya Watanzania yanakuwa magumu lakini kiburi, dharau na jeuri kikawa ndiyo kimewatawala madaktari wetu hawa wa uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulisema mfumo wao wa kodi zilizopitiliza kiasi zinaua biashara, tukasema binafsi nimesimama kwa microphone hii na kiti hiki nilichokaa mwaka jana nikawaambia zaidi ya hoteli 56 pale Kariakoo zimefungwa na majumba yamebadilishwa matumizi. Kwa hiyo, hakuna wageni wanaoingia, mabasi yaliyokuwa yanaleta wageni wale hayana kazi, wafanyakazi waliokuwa pale hawana ajira, porters waliokuwa wakifunga mizigo hawana, restaurant zile hazifanyi kazi, wakawa hapa wanakuja na maneno ya kwamba wao wamejidhatiti na wapo vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya miaka mitatu Mwenyezi Mungu ameleta rehema zake, Rais ameona kwamba nchi inadidimia, amekutana na wafanyabiashara tuliokuwa tukiyaeleza sisi kwa muda wa miaka mitatu, lipi ambalo wafanyabiashara hawakumweleza Mheshimiwa Rais?
(Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, wajitathmini madaktari hawa wana haki ya kuwepo pale kama ni waungwana, kama ni waungwana wajiuzulu kwa sababu kila kitu tuliwaeleza na tukawashauri na wakaleta dharau kwamba wao wamejipanga katika uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jana mchangiaji mmoja amesema kwamba miradi hii tunayofanya mikubwa ni mizuri na inatakiwa ifanywe; well, ndivyo, lakini katika uchumi wetu huu? Niliwapa mfano kwa sababu wameleta mtaalam wao mmoja hapa akatupa semina anatupa mifano kutoka Wizara yao hiyo ya Biashara anatupa mifano tunamuuliza maswali anakwepa. Tukawaeleza namna gani Sweden/nchi za Scandinavia zinakuza uchumi wao tukawaeleza Waheshimiwa Mwenyezi Mungu mkubwa, juzi kuna shirika moja hili la mawasiliano limempa Rais shilingi bilioni tatu, Airtel wamempa Rais shilingi bilioni tatu.

Mheshimiwa Spika, sasa tuchukulie mashirika yote ya simu yafanye vile, tuwe na viwanda 20 vifanye vile, tuwe na makampuni ya kilimo na wachimba madini wafanye vile, ndiyo Sweden inavyoendesha uchumi wake. Ile bajeti yao yote ni zile donations zinazotokana na wafanyabiashara na zinatokana kwa sababu wameweka mazingira sawa/wezeshi na uwazi katika biashara zao. Kwa hiyo, mfanyabiashara hana hofu ya kufanya biashara yake, anafanya biashara, inapofika mwisho wa mwaka anafanya hesabu anaichangia Serikali yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa fedha ile inatosha wao kwa bajeti yao na surplus ile ndiyo wanatusaidia sisi katika nchi zetu. Kwa hiyo, ile income inayotokana na makusanyo ya Serikali ndiyo wanakuja kwenye miradi yao mikubwa kama ya kwetu hii ya Stiegler’s au SGR na ndege. Sasa sisi tunaichukua bajeti ndogo tunayokusanya ambayo haitoshelezi tunaiingiza kwenye miradi mikubwa, unawakuta Watanzania leo wana-suffer katika maisha ni kwa sababu ya mipango yenu mibaya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na tulikuwa tukiwashauri humu ikawa hapa Mheshimiwa Dkt. Ashatu anakuja hapa anatushikia kiuno anakwambia Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imejidhatiti, hatuna hofu, tutakwenda hivi na hivi. Leo baada ya miaka mitatu kwa nini mnaramba matapishi yenu? Kilekile tulichokuwa tunakieleza mnakikataa leo mnakirudia, kwa nini mnaramba matapishi yenu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wataalam hawa ndio kweli wanamshauri vibaya Rais na wanatupeleka kubaya…

SPIKA: Mheshimiwa Yussuf, mimi naona unalaumu lakini husemi concretely ni maeneo gani, ni kitu gani, yaani unapiga lawama za jumla tu.

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nimesema, nilisema mwaka jana hapa kodi ya kontena moja milioni 40 pale bandarini inatuulia biashara yetu na wafanyabiashara wanachukua kontena hilo hilo, linapita as a transit likifika Uganda wanalipa milioni kumi biashara ile ile inarudi, haya mashati na vitenge tunavyouziwa hapo nje na mashuka vinatoka Uganda, vinapita hapo, niliyasema hayo. Jeuri na kebehi ikaja hapa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nataka kuwashauri tena wachumi wetu hawa, wapi tutapata fedha ili kuokoa hapa tulipo. Kuvunja ni mara moja, lakini kujenga inakuchukua muda mrefu, wametuulia uchumi kwa muda wa miaka mitatu, si kazi rahisi kuujenga uchumi. Nilisema huwezi kuona maendeleo ya Taifa kiuchumi kwa miaka mitano au kumi, siyo rahisi, nilisema. Kwa sababu kama Taifa kujenga uchumi ni kitu kimoja kinahitaji mipango na muda mrefu, nilisema hivyo.

Mheshimiwa Spika, sasa nawaonesha; la kwanza, Mheshimiwa Mattar siku zote anapiga kelele kuhusu uvuvi wa bahari kuu. Meli moja ya uvuvi kwa utafiti uliofanywa inaweza ikaingizia Serikali yetu dola milioni 65 kwa mwaka. Hayo yanazungumzwa tu, hayajafanywa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama tutaimarisha utalii katika ukanda wa bahari huu, utalii wa fukwe, tukafanya diving, snorkeling, fishing, utalii wa historia, utalii wa kiutamaduni, pato la utalii, GDP ya Taifa inaweza kutoka asilimia 17 hadi asilimia 40 kwa muda mfupi sana. Kinachohitajika hapa katika utalii ni triangle, vitu vitatu tu; waweke pamoja jamii, iweke pamoja wawekezaji (serious investors), ikae na Serikali waweke mfumo ili sheria zisigongane, serious investors waje wawekeze tuta-boost uchumi wetu. Tunawaeleza hilo la pili tunapiga kelele mwaka wa tatu, bado hakuna mkakati wowote wa utalii uliopangwa katika ukanda wa bahari kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, biashara ni lazima uweke mazingira wezeshi, uweke mazingira ya uwazi. Mtanzania awe ana uwezo wa kujua nakwenda kuchukua simu hii China, nainunua shilingi ngapi, ntailipia kodi shilingi ngapi awe anaweza kufanya kulekule…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Yussuf, malizia.

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Spika, mimi nimewashauri na wakiwa tayari ntawashauri wataalam wao waliosoma Amerika wametudanganya na tuliwauliza maswali wakajibu, tutawapa mifano ya nchi mbalimbali. Sisi hatukusoma, na Mheshimiwa Marehemu Karume alituambia tumesoma hatukujua, tumejifunza tumetambua. Tukienda huko kwa wenzetu tunajifunza kwa nini waendelee sisi tukwame; kwa nini, tunajifunza hayo mambo. Kwa hiyo tunapowashauri Waheshimiwa tunaomba muwe wasikivu. Nakushukuru. (Makofi)