Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Eng. Christopher Kajoro Chizza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buyungu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nakushukuru na nafasi hii naomba kwanza na mimi niwapongeze mawaziri hawa mahiri kabisa ndugu yangu Mpango na dada yangu Kijaji, kwa kweli ninyi ni mahiri kwa sababu hata mnavyojenga hoja zenu na mnavyojibu maswali yetu hapa inaonesha kabisa kwamba ninyi ni mahiri na kwa maana hiyo ndio maana mmetuletea bajeti proposal ambayo pia ni mahiri inatekelezeka, kwa kweli nawapongeza sana. (Makofi)

Pia naomba kabla sijaingia kuchangia niwashukuru kwa sababu Serikali inapotenga bajeti hata kama mambo mengine yanajitokeza hata kama hatuwezi tukatekeleza bajeti yote kila mwaka, kwa kweli sidhani kama kuna bajeti ambayo inatekelezwa 100% lakini ukiweza kuitekeleza kiwango percentage fulani hilo ndilo tunalolitaka. Kwa maana hiyo nataka niwashukuru leo hii nikiwa hapa hapa nataka niwashukuru Serikali yangu sikivu dada yangu Ndalichako amepeleka fedha shilingi milioni 66 kule Kigoma kwenye shule ambayo aliahidi alipotembelea kule shilingi milioni 66; nakushukuru sana Mheshimiwa Ndalichako nashukuru sana Serikali kwa sababu ndio maana ya kutenga bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nikiwa hapa hapa nimepata taarifa kwamba Profesa Mbarawa ametuma ma- engeneer kule kwangu baada ya kukagua miradi ya maji ambayo imejengwa wakati ule wa vijiji kumi tukapoteza shilingi bilioni 1.8, miradi haikujengwa vizuri lakini akaja akaahidi kwamba sasa nitatuma wataalam na wataikarabati ili iweze kufanya kazi iliyokusudiwa na hapa nikiwa hapa hapa nimepata taarifa kwamba ametuma kwa kweli nakushukuru sana, naishukuru Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizo naomba pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri na mwenzake na Wizara nzima kwa kuleta pendekezo la kuondoa tozo hizi mbalimbali 54 na nitajikita kwa chache kama muda utatosha nitakwenda kwa mambo mengine. Naomba nizungumzie pendekezo la marekebisho kwenye Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, nadhani iko kwenye ukurasa wa
57. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, asubuhi nadhani alikuwa Mheshimiwa Shabiby alizungumzia masuala ya mashine za EFD, na hapa nimeona Serikali inapendekeza kuondoa ushuru au kupunguza ushuru wa mashine za EFD kutoka 10% mpaka 0%. Kwa kweli ni jambo jema kwa sababu mashine hizi zinatusaidia kukusanya mapato. Nataka nikwambie Mheshimiwa Waziri, mimi niliwahi kuhudhuria mkutano wa TCCIA na alikuja mtu wa TRA akatufundisha jinsi mashine zile zinavyoagizwa. Akatuonesha pia kwamba mashine zile kama zilivyo gadgets nyingine hizi za simu, hata zile nazo watu wanaweza ku-temper nazo na kwa maana hiyo mashine zile wakati mwingine zinaweza zikawa hazitoi taarifa sahihi, zikawa ama zinaiumiza Serikali au zinamuumiza mlaji. Kwa hiyo, mimi ushauri wangu hapa ni kwamba mashine hizi zikaguliwe mara kwa mara, kwa sababu mtu huyu aliyetuambia alikuwa mtu wa TRA mwenyewe. Naamini watu wa TRA ndiyo wanaozisimamia mashine hizi, bila shaka alikuwa anasema kitu anachokijua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la pili kwa Mheshimiwa Waziri, kwa mfanyabiashara anayetaka kutunza taarifa zake ili baadaye aweze kujikagua au akaguliwe anahitaji kutunza kumbukumbu. Mashine nyingi za EFD hasa hizi za kwenye mashine za petrol ukiweka nyumbani baada ya miezi mitatu, minne haisomeki tena yamefutika yote, kama hujaweza kuzipiga photocopy basi hizi taarifa na kumbukumbu utakuwa hunazo tena.

Kwa hiyo, naomba kwa kweli hizi ziangaliwe upya, kama ikiwezekana zikaguliwe, kama ni mashine ziwe improved kwa sababu tunapopata zile risiti tunazihitaji kuzitunza ili mwisho wa mwaka tuweze kufanya tathmini kwamba na sisi katika biashara zetu tumefanya nini, lakini unapokwenda kukagua tena risiti zako unakuta haisomeki huna tena mahali pa kufanyia reference. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kidogo sasa nizungumzie habari ya sukari; umependekeza kupunguza ushuru wa sukari hasa ile ya matumizi ya kawaida (brown sugar) kutoka asilimia 100 kwenda asilimia 35. Hili ni jambo ambalo nadhani mara nyingi karibu kila mwaka tunapopata upungufu wa sukari linajitokeza na kwa kushirikiana na wenzetu Afrika Mashariki linatekelezwa. Jambo ambalo sikuona Mheshimiwa Waziri labda sikusoma vizuri, lakini sikuona ukizungumzia habari ya sukari ya viwandani (industrial sugar).

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaja hapa nimeongea na Bodi ya Sukari, wakaniambia mahitaji ya sukari yote yaani ile ya mezani na ya viwandani tani 670,000. Mahitaji ya viwandani kwa maana ya sukari ile ya kutengeneza bia, pipi, biscuit na vitu vingine peremende ambavyo ni viwanda hivyo ni tani 155,000. Sukari yote hii tani 155,000 hakuna inayozalishwa ndani, hakuna labda kama wameanza sasa, lakini mimi ninavyojua viwanda vyetu vyote TPC, Kagera, Mtibwa, Kilombero sidhani kama kuna kiwanda kinachozalisha industrial sugar, yote hii inatoka nje. Kama inatoka nje kwa uzoefu najua na yenyewe huwa inasamehewa kodi na ikisamehewa kodi sukari hii ikiingia basi inabidi kwa kweli iangaliwe vizuri maana uzoefu umetuonesha wakati ule wa sakata la sukari kwamba sukari hii hii ambayo inaingizwa ikiwa imesamehewa ushuru mara nyingine tena unaikuta kwenye supermarkets ikitumika kama sukari ya kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili siyo jambo zuri, kwa kweli hata kwa wafanyabiashara siyo jambo zuri lakini hata kwa walaji maana yake ile sukari sidhani kama inatakiwa itumike kwa ajili ya chai au kwa ajili ya uji. Ile ni purely kwa ajili ya viwandani, I stand to be corrected, lakini mimi ndivyo ninavyoelewa, sasa sikuiona ikizungumziwa katika hotuba yako.

Mheshimiwa Naibu Spika, matumizi ya kawaida ni tani 515,000 na uzalishaji wa ndani mwaka huu kwa brown sugar nimeambiwa ni tani 359,219 angalau kwa mwaka huu. Ukitazama hesabu zote hizi ukijumlisha ile sukari ya viwandani na sukari ya mezani ambayo ni upungufu wa tani 155,781 unakuta bado tuna upungufu wa zaidi ya tani laki tatu na kitu. Maana yake ni kwamba lazima tutaendelea kuagiza sukari na hii ya industrial sugar hii ndiyo hasa nataka niizungumzie.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri, mimi ushauri wangu ni kwamba tuongeze uwekezaji katika mashamba ya miwa, lakini mashamba ya miwa hayawezi kuendelezwa bila umwagiliaji. Mashamba ya miwa lazima yaende sambamba na umwagiliaji, yako mazao karibu matatu ambayo sasa kitaalamu huwezi uka- break even bila kumwagilia. Moja ni miwa, lingine ni mpunga na lingine ni mazao ya bustani (hot cultural crops). Mazao haya sitaingia kwa undani kwa nini, lakini huwezi uka-break even bila kumwagilia, mengine utakuta kwamba hata circle yake uzalishaji yanakwenda zaidi ya miezi sita hakuna mvua inayokwenda zaidi ya miezi sita katika nchi hii lazima ufanye supplementary irrigation.

Kwa hiyo, katika kuwekeza katika uzalishaji wa miwa ni lazima tuongeze uzalishaji, tuwekeze katika kilimo cha umwagiliaji vinginevyo hatutaweza ku-break even. Kwa maana hiyo ni kwamba wale wanaolima miwa wakiwa ni wazalishaji wakubwa wao wanaweza kuweka miundombinu yao, lakini wale wana-nuclears farms, outgrowers lazima wasaidiwe. Ukienda Kilombero kuna outgrowers, wale hawawezi kujiwekea miundombinu wenyewe ya umwagiliaji ili wazalishe miwa mingi ya kukiuzia kiwanda kwa hiyo hapa ni lazima Serikali itusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu namba mbili, naomba sasa kwa kuwa viwanda vyetu vya ndani havizalishi sukari ya viwandani na ninajua sababu kubwa, sababu kubwa ni kwamba wanaogopa kuweka mitambo ile ya kusafisha sukari maana ile industrial sugar ile siyo sukari nyingine ni kwamba ni hiyo hiyo inakuwa refined vizuri, sasa hawaiweki hii mitambo hii. Kwa hiyo, ninaomba wakati tunawahamasisha wawekezaji hawa tuwawekee na component hii kwamba jamani eeh mnapotuzalishia sukari mjitahidi kuweka na mitambo ya kusafisha sukari hii tuzalishe sukari ya viwandani. Maana sukari ya viwandani hii ni malighafi kwa ajili ya viwanda vyetu, viwanda hivi vya pipi vinginevyo viwanda hivi tutaendelea kuagiza malighafi kutoka nje kwa ajili ya kulisha viwanda hivi. Ushauri wangu namba tatu kwa Mheshimiwa Waziri ni kwamba nimeshausema lakini nataka nirudie, industrial sugar isiuzwe kama sukari ya kula mezani, isikutwe katika supermarkets. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nirudi tena kwenye kilimo, wengi wamezungumzia kilimo, wamezungumzia umwagiliaji na kwamba ili tutoke kwenye agrarian reforms sasa tuingie kwenye mambo ya viwanda, kilimo bado ndicho kitaendelea kuwa mhimili wa kutoa malighafi. Ninachotaka kuzungumza…. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Muda wako umeisha Mheshimiwa, kengele ya pili imeshagonga. Ahsante sana. (Makofi)

MHE. DKT. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na nakushukuru sana. (Makofi)