Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kasulu Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa jioni ya leo ambayo nimepata na mimi kuungana na wenzangu kwenye kuchangia bajeti hii ambayo ni bajeti inayoonekana inakwenda kumkomboa Mtanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na mambo matatu; jambo la kwanza, nimpongeze kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya bila kuchoka kuweka mikakati vizuri kwa ajili ya maendeleo ya nchi hii kwa ujumla. Dhamana aliyopewa ni kubwa na sisi tunamuombea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kumkaribisha Ikulu pacha wangu, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Papa Félix Tshisekedi. Sisi watu wa Kigoma uchumi wetu kama Mkoa una mashirikiano makubwa sana na nchi ya Kongo. Kwa hiyo Rais alivyomuita Rais mwenzake wa Kongo kumkaribisha Ikulu tunaamini kwamba wamezungumza mambo makubwa na mazuri ambayo yatapunguza baadhi ya vikwazo mpakani pale na hatimaye tutaendelea kupokea Wakongomani wengi Kigoma kwa ajili ya kufanya nao biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye bajeti; nipende kushauri yafuatayo, jambo la kwanza, upande wa mawakala hawa wa kutoa mizigo bandarini. Kaka yangu Dkt. Mpango, mimi hili sijalielewa vizuri, ninapenda Serikali ije na maelezo mazuri na ya kina tuweze kuelewa kwa sababu tunaamini clearing and forwarding ni profession ya watu ambao wamesoma vyuoni wamemaliza na wana-practice vizuri ili kuweka waraka wa kufanya shughuli hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa anapokuja mtu wa kawaida tu ambaye hana knowledge hiyo wala haelewi hicho kitu, tunapaswa kujua lakini tuelewe hatma ya makampuni haya ya watu ambao wanafanya clearing and forwarding, tuweze kujua kwa sababu kuna ajira nyingi ambazo ziko huko. Mimi nadhani kama kungekuwa kuna matatizo kwa hao ma-agent ilikuwa ni busara zaidi kuwafanyia vetting na kuwaondoa wale ambao hawastahili kuliko kusema kwamba kila mtu aweze kufanya clearing and forwarding ya mzigo wake. Sina maana ya kupinga hili, lakini nataka Serikali ije kunishawishi, iweze kutueleza tuweze kufahamu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mifugo; mimi nipende kushauri jambo moja, nchi hii imekuwa na migogoro ya wakulima na wafugaji kila siku. Bunge lililopita niliuliza mkakati wa Serikali kupunguza mifugo labda ili kuweza kupunguza migogoro hii kati ya wakulima na wafugaji, lakini nikaona kwamba kupunguza mifugo kwa kweli ni jambo ambalo ni gumu kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninashauri jambo moja kwamba Serikali nadhani inapaswa kutenga vijiji vya ufugaji ambavyo vitakuwa havina wakulima. Yapo maeneo ambayo Mheshimiwa Rais anasema kwamba yamepoteza sifa za uhifadhi, nadhani tutenge vijiji vya ufugaji ambapo wafugaji wote tutawaambia waende kule na watakuwa hawakutani na wakulima. Hii itaweza kupunguza migogoro kati ya wakulima na wafugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye sekta ya Utalii; watu wengi ambao wamewekeza kwenye sekta hii wanalalamika kwamba vibali vya uwindaji ambavyo wanapewa ni vifupi. Kwa hiyo, wanashindwa kufanya uwekezaji wa muda mrefu kwa sababu wanapewa vibali vya mwaka mmoja. Kwa hiyo, nashauri Serikali ilitazame hili, itoe vibali vya muda mrefu ili wawekezaji hawa waweze kutoa hela zao mfukoni kufanya uwekezaji kwenye maeneo husika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano sisi pale Kagerankanda tuna mwekezaji wa kitalu cha uwindaji, alitaka atujengee mabwawa ya samaki kwa ajili ya ile jamii inayozunguka, lakini mradi ule unaenda miaka miwili na ana kibali cha mwaka mmoja kutoka Serikalini. Kwa hiyo amesitisha kwa sababu inawezekana akianza kujenga ule mradi kibali chake kiki-expire basi asiweze kuongezewa na hatimaye akapewa mtu mwingine kwa hiyo inakuwa ni tatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda kushauri ni kwenye upande wa hawa…
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Taarifa, taarifa.
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: …upande wa elimu.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Vuma, kuna Taarifa. Mheshimiwa Mchungaji Peter Msigwa.
T A A R I F A
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka nimpe taarifa mchangiaji kwamba katika jambo analolisema kwamba wawindaji wanapewa vitalu muda mfupi, ninataka nimuongezee taarifa kwamba kwa kweli limekuwa ni tatizo na hivi sasa Wizara ilitoa mpango wa mnada, mnada umeshindikana, kwa hiyo hivi vitalu kuna uwezekano wa kuvipoteza na tukapunguza mapato kwenye mpango wako Mpango kwa sababu mpango huu wa kunadisha vitalu karibu 90 vimekosa wateja, ni mipango mibovu ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka nimpe taarifa tu katika hili analolisema.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Vuma, unapokea taarifa hiyo?
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa naipokea na Serikali ije kutoa majibu hapa wakati wa majumuisho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye upande wa elimu hakuna…
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upande wa elimu napenda kushauri jambo moja…
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Vuma kuna taarifa kutoka Mheshimiwa Constantine Kanyasu.
T A A R I F A
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninaomba nimheshimu sana Mheshimiwa mchangiaji, lakini ninataka tu niweke kumbukumbu sawa. Mnada ambao unaendelea sasa wa vitalu haujafungwa na mnada huo umepandisha thamani ya kitalu kutoka dola 60,000 kwenda dola 150,000 na ninataka kumhakikisha Mheshimiwa Mbunge kwamba katika marekebisho yetu ya Kanuni suala la mwaka mmoja halipo, tulikuwa na miaka mitano tunakwenda miaka kumi. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Augustine Holle Vuma unapokea Taarifa hiyo?
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa na ninawatakia utekelezaji mzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Nabu Spika, niseme kwenye suala la elimu; hili nashauri kitu kimoja; hapa mtaani kuna vijana wengi ambao tumewakopesha fedha nyingi sana ambao wamemaliza vyuo, sisi tunawadai pesa, lakini wao wanaidai Serikali ajira na wakati huo huo Serikali haina watumishi wa kutosha kwenye idara za walimu, katika hospitali na sekta zingine. Sasa nikasema, kwa nini hawa vijana ambao wanamaliza shahada zao ambao wana mikopo, kwa nini tusiwape mikataba mifupi ambayo tutakuwa tunawapa hela za kujikimu na hatimaye waende kufundisha au kufanya kazi katika hospitali huko na kwenye sekta mbalimbali huku wakiwa wanalipa madeni ambayo wanadaiwa na Bodi ya Mikopo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu wale vijana tunawadai pesa, wao wanatudai ajira na hatuna watumishi. Sasa tuangalie sehemu ambayo tutakutana hapo katikati; vijana hawa wakimaliza wakienda kufanya kazi kwanza watakuwa wanalipa madeni yao, lakini pia watakuwa wanapata uzoefu. Kwa sababu vijana wengi wako mtaani, lakini uzoefu wa kufanya kazi hawana mpaka wanashindwa kupata kazi kwenye sekta binafsi kwa sababu hawana uzoefu, kwa hiyo tutawapa uzoefu lakini pia watakuwa wanalipa madeni yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali barabara ya kutoka Buhingwe – Kasulu – Nyakanazi, naomba sana utekelezaji wake. Lakini pia naomba barabara ya kutoka Kasulu kwenda mpaka Uvinza.
Mheshimiwa Naibu Spika, niweze kuja kwenye suala la SGR; nimemsikia ndugu yangu, kaka yangu hapa, Mheshimiwa Mwakajoka anasema kwamba wao hawapingi miradi ya SGR na Stiegler’s Gorge lakini hawataki fedha nyingi ziende kwenye miradi ile; kituko kabisa hiki, hiki ni kituko, yaani miradi unaitaka lakini hutaki fedha nyingi ziende kwenye miradi ile kwa sababu miradi ya matrilioni inatengewa mabilioni…
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: …kila mwaka wewe hautaki hela ziende kule ila miradi unaitaka…
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: …yaani unajitekenya halafu unacheka mwenyewe. Sasa hili ni jambo ambalo ni la kusta… (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Vuma, kuna taarifa. Waheshimiwa Wabunge, hii ni taarifa ya mwisho kwa Mheshimiwa Vuma kwa sababu hii ni taarifa ya tatu tayari. Mheshimiwa Mwakajoka.
T A A R I F A
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka kumpa taarifa mzungumzaji, siyo kwamba tumesema kwamba hatupingi halafu fedha nyingi zimekwenda kule. Tulichokizungumza hapa ni kwamba maeneo ambayo wananchi wengi wanatakiwa kupata huduma fedha hazijapelekwa.
Kwa hiyo, tulikuwa tunaishauri Serikali muda wote na tumeishauri Serikali muda wote kwamba fedha zipelekwe katika maeneo hayo; ndege, umeme, kila kitu tunakihitaji, lakini fedha ni nyingi mno ndiyo maana tumesema tunahitaji mgawanyo ambao uko sawa kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kingine ni kwamba haja...
NAIBU SPIKA: Taarifa ni moja Mheshimiwa Mwakajoka. Mheshimiwa Augustine Holle Vuma unapokea taarifa hiyo?
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, hii taarifa siipokei kwa sababu huyu mtu anajichanganya na niseme, unajua sisi Mkoa wa Kigoma unapozungumza reli ni identity yetu, ni utambulisho wetu, ndiyo maana Mkoa wa Kigoma umekuwa unaitwa kwamba ni mwisho wa reli. Kwa hiyo, sisi Kigoma tunahitaji reli kwa gharama yoyote ile na ninaishauri Serikali iendelee kupeleka pesa kwenye SGR ili tupate reli, SGR ifike Kigoma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unajua kuna watu hapa ambao kwao wanakotoka maeneo yao hakuna shida za usafiri, wao zimeshaisha. Sasa Kigoma unapokwenda kupinga reli tunakuita ni msaliti wa Mkoa wa Kigoma, kwa hiyo sisi tunaiunga mkono kabisa Serikali, tunahitaji SGR Mkoa wa Kigoma kwa sababu tunaamini itakuwa ni mkombozi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme tunaamini kwamba SGR hii ina faida za muda mfupi katika ujenzi wake lakini na faida za muda mrefu. Faida za muda mfupi, jambo la kwanza SGR hii Lot One na Lot Two inayoendelea kujengwa imeajiri sasa hivi mpaka leo tunavyozungumza Watanzania 17,000 wamepata ajira kwenye SGR. Lakini kama haitoshi kumejengwa kiwanda cha mataruma kwa hiyo unavyozungumza ujenzi wa SGR hauzungumzii vile vyuma kutandikwa peke yake, kuna element ya viwanda kwenye ujenzi wa SGR. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama haitoshi kuna kuchochea uchumi ndani ya SGR; niseme tu kuna watu wengi sana wanafanya shughuli za kimaendeleo wakati mradi ule unajengwa. Ukiangalia kwa mfano vifaa ambavyo mradi ule unatumia ukianzia na cement, inakadiriwa kwamba Lot One na Lot Two itatumia mifuko milioni 9.2 ya cement ambayo yote inanunuliwa hapa Tanzania; lakini itatumia nondo kilo zaidi ya milioni 100, yote inanunuliwa Kamal hapa hapa Tanzania. Sasa ukiangalia haya yanaendeelea kuchochea uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukiangalia bodaboda, mama lishe ukienda kwenye mradi huu wamejaa wanafanya shughuli zao za kiuchumi, huku ni kuchochea uchumi. Kwa hiyo, unavyoangalia reli, ujenzi wa SGR usi-focus kwenye kutandika vyuma tu, kuna vitu vingi viko ndani yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nadhani kuna suala la uelewa; watu wengi huu mradi hawauelewi vizuri, wanausoma na kusikia tu michango ya Bungeni, wanasoma kwenye whatsApp na wapi, wanapaswa waende kutembelea mradi huu waweze kuona au ije presentation Bungeni hapa watu waweze kupewa shule juu ya Mradi wa SGR ili waweze kuelewa kilichopo ndani yake, ule ni zaidi ya mradi wa reli kuna vitu vingi vilivyopo ndani yake; hizo ndiyo faida za muda mfupi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini zipo za muda mrefu; tunaamini kwamba Mradi wa SGR, reli ikikamilika itakwenda kuongeza thamani ya mazao katika nchi yetu. Kwa sababu tunaamini, kwa mfano Mchina amekuja akatangaza soko la muhogo, Kigoma tunalima muhogo lakini gharama za kusafirisha muhogo kutoka Kigoma kuupeleka mpaka bandarini uende China ni very expensive. SGR itakapokuwa imekamilika tunaamini muhogo utatoka Kigoma mpaka Dar es Salaam kwa muda mfupi na gharma zitakuwa chini. Na study inaonesha SGR itapunguza gharama za usafiri kwa asilimia 40; nani anapinga SGR na kwa nini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama hiyo haitoshi, tunaamini kwamba itaweza kulinda barabara zetu ambazo tumezijenga kwa gharama kubwa. Mizigo mingi mikubwa itakuwa inapitia kwenye reli hii ambapo itaweza kulinda barabara zetu kwa sababu barabara zitabaki zinatumiwa na magari machache, mizigo yote itakuwa inasafirishwa kwenye treni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nipende kuwaomba kwamba wajitahidi kusoma huu mradi wa SGR. Na niseme; hizi bajeti mbadala hizi ambazo zinakuja na vijembe, zinapinga miradi mikubwa kama SGR ni za kuchana hizi, hakuna kitu. Lazima tuwe serious katika mambo kama haya ili watu waweze kuelewa kwamba… [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]
(Hapa Mhe. Augustine V. Holle alichana kitabu cha hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, Kuhusu Utaratibu.
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: …hili jambo ni jambo ambalo sisi watu wa Kigoma tunahitaji lifanyike. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, Kuhusu Utaratibu.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, Kuhusu Utaratibu.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwakajoka umesimama na Mheshimiwa Esther Matiko amesimama na mnazungumzia utaratibu. Mheshimiwa Mwakajoka.
KUHUSU UTARATIBU
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli kuna mambo ambayo yanafanyika ndani ya Bunge...
Mheshimiwa Naibu Spika, Kuhusu Utaratibu, natumia Kanuni ya 64; mambo ambayo hayakubaliki.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchangiaji aliyekuwa anachangia sasa hivi amesimama hapa amechana hotuba ya Upinzani ndani ya Bunge hili. Ninafikiri jambo hili ni dharau kubwa lakini pia ni kutokujielewa kwa Mheshimiwa Mbunge kwamba yuko humu kwa sababu gani na hajui kwa nini hiki kitabu amepewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba meza yako iweze kutoa sababu na ni namna gani huyu Mheshimiwa Mbunge asiyejielewa achukuliwe hatua ili kidogo akili yake ikae sawasawa maana yake tumemuona kama kichaa fulani hivi ndani ya Bunge. Ahsante sana. (Kicheko)
(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tusikilizane.
Amesimama Mheshimiwa Mwakajoka akaitaja Kanuni ya 64 kwamba ndiyo ambayo imemfanya asimame japokuwa ufafanuzi wake haukuwa hasa kwenye kifungu kipi cha Kanuni ambacho anaona kimevunjwa. Lakini Kanuni hii ya 64 Waheshimiwa Wabunge, yako mambo mbalimbali ambayo yanakatazwa na inazungumzia kwa ujumla wake mambo yasiyoruhusiwa Bungeni. Sasa ukisoma Kanuni hiyo ya 64(1)…
Waheshimiwa Wabunge, tusikilizane, huwa napenda kusikilizwa na kwa mujibu wa Kanuni zetu nikiwa nimesimama mnapaswa kunyamaza ili mjue nasema nini.
Kanuni ya 64(1) ukiisoma (g) inazungumza kuhusu kutokutumia lugha ya kuudhi au inayodhalilisha watu wengine. Kwa hiyo kwa mchango wa Mheshimiwa Vuma, hoja iliyopo itakuwa si kuchana kitabu maana amezungumza wakati akichana kitabu.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Vuma kwa muktadha wa Kanuni hii ya 64(2) ukizisoma zote kwa pamoja, Mheshimiwa Vuma maneno ya kuhusu kukichana kitabu hicho nitakupa fursa ili uweze kuyafuta na jambo hili Waheshimiwa Wabunge lisirudiwe wakati mwingine.
Mheshimiwa Vuma.
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, napokea busara za Kiti, nafuta maneno yale. Lakini ilikuwa ni kuonesha namna gani ambavyo hotuba hii haina maslahi kwa umma. Ahsante sana.