Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Babati Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kunipa fursa nami nichangie katika Bajeti hii Kuu ya Serikali. Nimshukuru pia Mwenyezi Mungu, huyu Mungu ambaye anatupa pumzi ya uhai bila kuilipa VAT au chochote, ni kwa neema yake tu, namshukuru sana, anatufanya tutimize wajibu wetu tukiwa na afya njema.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze viongozi wetu kuanzia Mheshimiwa Rais, Waziri Mkuu, Waziri wa Fedha, Mawaziri na watendaji wa Serikali kwa kuendelea kutumikia Taifa letu kwa upendo na moyo wa uzalendo. Hongereni sana, na sisi tunawaombea pia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi hii bajeti, mimi binafsi nilivyoipokea nikawa najiuliza ni nani huyu anakwenda kuthubutu kuipinga bajeti hii? Nitatoa sababu za kutosha tu; kwa sababu naamini Wabunge tunawakilisha wananchi ambao wametutuma, tunaishauri Serikali lakini bajeti hii imekwenda kuonesha vitu vikubwa ambavyo havijawahi kufanyika. Nafikiri siku ya kura kama vile haifiki, tuone ni nani anasema hapana kwenye bajeti hii, na sababu ntazitoa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wachache wanasema hii bajeti ni ya vitu siyo ya watu, lakini vitu hivi wanavyovisema naomba nivitaje, ambavyo wao wanaona ni vibaya sana kwa Watanzania, vimeorodheshwa ukurasa wa 19 kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri; ni ujenzi wa barabara ya njia nane kutoka Kimara, Dar es Salaam hadi Kibaha, kilometa 19. Wananchi wa Dar es Salaam walikuwa wanahangaika na foleni huko, wanapoteza muda, lakini hiki kwa wengine ni kitu kibaya, haigusi watu, sasa sijui ni watu wapi wanataka waguswe.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi vitu wanavyovisema vingine mfano ni ujenzi wa Daraja la Mto Kilombero. Natoa tu mfano, michele, mipunga ilikuwa inakwama inazamia kwenye ule mto lakini leo daraja limejengwa watu wanasema ni bajeti ya vitu. Bajeti hii ya vitu inayotajwa ni bajeti ambayo inakwenda kutatua tatizo la upungufu wa umeme katika nchi yetu lakini watu wanaona kwamba tunapeleka pesa nyingi huko, ni tatizo, ili viwanda vianze na huku chini wananchi wanufaike na energy ambayo imekuwa ikiwa na upungufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia hao watu wanathubutu kubeza hata jitihada za ununuzi wa ndege na vitu vingine. Ukiona watu wamekosa vitu vya kuongea utashangaa wanabaki sasa kuzungumzia mambo madogo madogo, mara wigi, wigi, wigi. Hata hivyo wananchi wetu waliotutuma, naamini wengi tunaowawakilisha huko vijijini hawavai haya mawigi ambayo tunayatetea, wengi wanahitaji maji, umeme na barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya pili, wanasema milioni 50 hazijatolewa. Nitoe mfano tu, mimi ni wa Babati hapo, ujenzi wa barabara hii kutoka Dodoma mpaka Babati, kilometa zaidi ya 260 ni milioni 50 ngapi kwa vijiji vingapi zimepelekwa kupitia barabara hii tu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa mradi wa maji tu, mfano kijiji change, juzi nimetoka kuzindua huo mradi tukiwa na mwenge pale…
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Taarifa.
MHE. PAULINE P. GEKUL: …ujenzi wa mradi wa maji wa Imbilili wa milioni 600…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gekul, kuna taarifa; Mheshimiwa Salome Makamba.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Napenda nimpe taarifa mzungumzaji kwamba wakati wa kampeni, wakati Chama cha Mapinduzi kinaomba ridhaa ya kuongoza, pamoja na milioni 50 walizoziahidi, waliahidi wataleta barabara, maji na kujenga reli. Kwa hiyo wasipotoshe kwa ku-substitute vitu wanavyojengea wananchi na milioni 50, wapeleke milioni 50 za wananchi. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, nilikumbusha jana, nimekumbusha na leo; matumizi ya Kanuni ya 68(8), tuisome tunazo nakala, ni taarifa ya namna gani unayoweza kuitoa.
Nasisitiza tena; tuisome Kanuni ya 68(8) matakwa yake. Mheshimiwa Gekul, endelea na mchango wako.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu niendelee.
Mheshimiwa Naibu Spika, natolea mfano Kijiji kimoja tu cha Imbilili cha jimboni kwangu, milioni zaidi ya 600 wamepeleka pale mradi wa maji ambao walikuwa hawategemei katika maisha yao. Hata hivyo, kuna watu wanajificha milioni 50, labda sasa kuna tatizo la kihesabu, Walimu wa hesabu watusaidie, kati ya milioni 600 ambazo wamepelekewa wanakijiji wanakunywa maji na milioni 50 kipi kikubwa? Huo ni mfano tu, ndiyo maana nasema watu hapa tunachanganyana kwa sababu wamekosa vitu vya kuongea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine mtu anasimama kabisa Mbunge anasema bajeti imekuwa haijaongezeka, ya Kenya imeongezeka; so what? Wakati huo huo mtu anasimama tusipotekeleza bajeti ile ya trilioni 32 anakwambia hii bajeti hewa. Hawa watu watatupotezea sana muda, Watanzania wanasubiri tupeleke maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niseme ni kwa nini yeyote humu ndani hatakiwi kusema hapana kwenye bajeti hii. Baada ya kutoa utangulizi huo niende kwenye details za wananchi wetu vitu gani wameguswa, mfano wale wa majimbo ya mijini lakini kwa wananchi wa nchi hii wafanyakazi ni takribani kama milioni moja tu. Wananchi wa Tanzania wengi wao ni wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo wadogo, kila mmoja anawakilisha hawa watu kwenye Bunge hili. Unakataaje bajeti hii, la kwanza, Serikali kuondoa Ushuru wa Forodha wa EFD machines kutoka asilimia kumi mpaka sifuri, wafanyabiashara wadogo wadogo walikuwa hizi mashine wananunua kwa gharama kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo Serikali imepunguza hili ili wafanyabiashara wapate hizi mashine kwa bei rahisi, kodi ikusanyike, mtu anasema hapana kwenye hii bajeti, nitamshangaa, labda kama hawakilishi wananchi. Kwa sababu hizi mashine zilikuwa zinasumbua, leo Serikali imepunguza hizi gharama ili wapate kwa bei rahisi kodi ikusanyike unakataaje hii bajeti?
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili anijibu ambaye anategemea kuikataa hi bajeti; kima cha chini cha kodi kimepunguzwa kwa shilingi 50,000 mpaka 100,000, mtu ambaye mauzo yake si zaidi ya milioni 14 zaidi ya 100,000 imepunguzwa, wananchi wetu wamepunguziwa mzigo wa kodi; mtu anakataaje hii bajeti, hawa wafanyabiashara wadogo wadogo tunaowakilisha? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ambalo natamani nijibiwe kwa nini huyu mtu akatae hii bajeti; hawa wafanyabiashara wadogo wadogo walikuwa wanaandaa mahesabu yao mtaji wa kuanzia milioni 20 alikuwa anatakiwa ampate mtu wa CPA amuandalie bajeti yake, lakini sasa hivi ni mpaka mtu mwenye mtaji wa milioni 100, hao wa chini wameachwa ili mitaji yao ikue; unakataaje hii bajeti? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la nne; Mheshimiwa Waziri ameongeza tena muda wa miezi sita kwa wale ambao walikuwa wanadaiwa riba za kodi mpaka mwezi wa 12 ili walipe zile kodi wanazodaiwa, amewapunguzia mzigo huo. Huyo anayekataa hii bajeti wananchi wake wamepunguziwa huo mzigo ni nani? Labda kama hawawakilishi wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tano, kuanzisha Kitengo cha Ombudsman, cha kupokea malalamiko ya wafanyabiashara ambao walikuwa wanaombwa rushwa, ambao walikuwa wanafungiwa maduka yao, kodi zinadaiwa kwa nguvu. Leo Serikali imeona iandae kitengo maalum kabisa cha kusikiliza malalamiko ya wafanyabiashara pale wanapoonewa. Mtu anasema hataki, maana yake wafanyabiashara wetu waendelee kutozwa kodi kubwa ambayo hawastahili, wafanyabiashara wetu waendelee kuchukuliwa rushwa. Mimi kama Mbunge ninayeongoza Jimbo la Babati Mjini ambalo hawa wafanyabishara wamekuwa wakiteseka nasema bajeti hii haijawahi kutokea. Sasa nasubiri huyo anayekataa kwenye jimbo lake kuna wafanyabiashara au hakuna wafanyabiashara?
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa kuliko yote, wafanyabiashara walikuwa wanalia hapakuwa na grace period ya kodi. Unakwenda tu unapewa TIN na kodi unakadiriwa hapohapo, leo Serikali imewapa miezi sita kafanye biashara yako halafu tuje tukukadirie kodi. Halafu mtu unasimama unasema hapana kwenye bajeti hii, labda kama unaongoza fisi, ngedere, siyo binadamu hawa tunaowaongoza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni bajeti ambayo mimi binafsi sijawahi kuiona. Pia kuna watu walikuwa wamechimba visima vyao, kila mwezi wanalipa Sh.100,000, Serikali imeondoa hiyo, mtu anasema hapana kwenye bajeti hii ili wananchi waendelee kutozwa wapate tatizo la maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho katika haya mazuri kwa siku ya leo; tozo zaidi ya 54 zile za TFDA, TBS, zimeondoshwa. Kulikuwa na halmashauri inakwenda kukagua biashara ya mama lishe, TFDA wanakwenda kukagua inatozwa mara mbili, wananchi walikuwa wanalalamika. Leo hii Serikali imeondoa tozo zaidi ya 54 halafu eti siku ya kupitisha bajeti mtu anasema hapana. Mimi nafikiri siku hiyo TV zionyeshe kabisa Watanzania watu gani ambao hawataki wananchi wapate maisha nafuu, wawaone kwa haya mazuri atakayesema hapana kwenye bajeti hii, huyo ni adui wa Watanzania na wajasiriamali wadogo wadogo na Watanzania zaidi ya milioni 45.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri siku hiyo TV zionyeshe kabisa Watanzania watu gani ambao hawataki wananchi wapate maisha nafuu wawaone kwa haya mazuri, atakayesema hapana kwenye bajeti hii, huyo ni adui wa Watanzania na wajasiriamali wadogo wadogo na Watanzania zaidi ya milioni 45. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu tu kwa Serikali yangu, nawaomba, suala la watumishi siyo la kwao. Mmelipa madeni, mmeendelea ku-review madeni yao na kuyalipa, kamilisheni hilo la upande wa wafanyakazi. Wasijifanye wao ndio wanabeba, mnafanya mambo mazuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)