Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
ACT
Constituent
Kigoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ZITTO Z. KABWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kutoa mchango wangu katika Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2019/2020.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2018 Serikali ilikuja na pendekezo kwenye Bunge lako Tukufu la kuweza kutoa unafuu kwa wanawake milioni 13 wa nchi hii katika matumizi yao ya taulo za kike kila mwezi. Mwaka huu Serikali imeona kwamba pendekezo lile halijaleta yale matokeo ambayo ilikuwa inayataka. Ukurasa wa 38 Waziri wa Fedha anasema, kwa kuwa pendekezo lile halijawezesha kupatikana kwa bidhaa hiyo, muhimu kwa bei nafuu kwa walengwa na badala yake pendekezo lile limefaidisha wafanyabiashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, inawezekana kabisa kwamba Serikali ikawa concerned kwamba bei ya taulo za kike haikushuka kutokana na mapendekezo ambayo Serikali iliyaleta, lakini Serikali inapaswa kujitafakari; je, mwaka mmoja ambao utekelezaji umefanyika unatosha kuweza kupima matokeo ya sera ile ambayo iliyefanya mwaka 2018? Katika hilo naomba niikumbushe Serikali kwamba mwaka 2018 Serikali ilikuja na pendekezo la kuongeza kodi kwenye mafuta ghafi yanayotoka nje ili kulinda wazalishaji wa mbegu za mafuta hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika na Bunge lako Tukufu kwa pamoja, nataka tutazame nini matokeo ya pendekezo lile ambalo Serikali ililileta? Mwaka 2017 kabla ya kodi zile kupandishwa katika uzalishaji wa mazao ya mafuta tulikuwa tunazalisha tani 6,600,000 mwaka 2017 kabla ya kupandisha kodi ili kudhibiti uagizaji wa mafuta kutoka nje. Mwaka 2018 tumezalisha tani 1,600,000 ni ukurasa 135 wa taarifa ya hali ya uchumi; pungufu la negative seventy six per cent (-76%) kwamba pendekezo ambalo Serikali ililileta mwaka 2018, matokeo yake ukurasa wa 135 wa Taarifa ya Hali ya Uchumi. Matokeo ya kuweka kodi hayakuzalisha tegemeo la uzalishaji wa mbegu kuongezeka, lakini Serikali mwaka huu haijaja na pendekezo la kufuta lile pendekezo la mwaka 2018. Matokeo yake imeendeleza pendekezo lile.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kuna transition period. Huwezi ukaweka pendekezo la kikodi sasa ukategemea matokeo ya haraka hapo hapo. Kodi imeanza tarehe 1 mwezi Julai, kuna watu walikuwa wana stock ambazo walizinunua hazikuwa na hiyo exemption. Lazima wataendelea kuziuza kwa fedha zile. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Mheshimiwa Waziri wa Fedha anafahamu, tumepata mtikisiko hapa katikati wa fedha yetu kuporomoka thamani dhidi ya dola za Kimarekani. Taulo za kike zote tunazoagiza nchi hii zinatoka nje. Factor ya exchange rate tumeitazama?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi natoa rai kwa Serikali kwamba siyo sahihi kuja kufuta ile exemption tuliyoiweka mwaka 2018. Serikali inapaswa kutazama vizuri, kutoa muda wa kutosha, kama namna ambavyo imetoa muda kwenye mafuta licha ya kwamba uzalishaji umeshuka, tutazame pia tutoe muda kwenye eneo hili la taulo za kike. Uamuzi wa mwaka 2018 uliipa sifa nchi yetu, tulikuwa ni a pioneer country katika kulinda wanawake wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, India wametufuata, wametuiga sisi, Australia wametufuata, wametuiga sisi na nchi nyingine mbalimbali. Mwaka huu South Africa wametuiga sisi. Sisi tunarudi nyuma kwa sababu tu ndani ya mwaka mmoja, bei haikushuka, hapana, siyo sahihi. Naisihi Serikali itazame upya pendekezo hili na itazame upya pendekezo hili kwa kuwa tayari ndani ya bajeti ya mwaka huu Serikali imependekeza kuondoa ushuru kwenye malighafi zinazozalisha taulo za watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, malighafi za taulo za watoto ndiyo malighafi za taulo za kike. Meza ambayo inapaswa kufanya kwenye taulo za watoto, ndiyo meza hiyo hiyo inatakiwa kufanywa kwenye taulo za kike. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naisihi Serikali, moja, pendekezo…
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango.
TAARIFA
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa msemaji kwamba tozo anayosema imepunguzwa kwenye malighafi za diapers, tozo hiyo pia kwa miaka minne mfululizo imeondolewa kwenye malighafi za kutengeneza taulo za kike. Kwa hiyo, hili jambo lipo, siyo kwamba ni jambo geni ambalo linatakiwa kupendekezwa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Zitto Kabwe unaipokea taarifa hiyo?
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwa hiyo, VAT exemption kwenye taulo za kike mwaka huu, labda kuwe na sababu nyingine, lakini kwa sababu ya bei kutokushuka, naomba Serikali itazame upya kwa sababu ni jambo ambalo linaweza kutatuliwa administratively. Tuna tatizo kwamba retailers, wauzaji wa mwisho margin yao kwenye taulo za kike ni kubwa sana na jambo hili linaweza likatekelezwa administratively kwa kuhakikisha kwamba wanakaa na kuweza kupata suluhisho la kudumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni suala zima la uwekezaji katika nchi yetu. Serikali inazungumza kwamba pato letu la Taifa linakua kwa 7%. Sitaki kuingia kwenye ubishani kati ya Serikali ya takwimu zao na takwimu za taasisi nyingine. Hata hivyo tumeona kuwa ndani ya mwaka mmoja, kwa mujibu wa taarifa ya hali ya uchumi, uwekezaji nchini umeporomoka kwa asilimia 44.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2017 thamani ya uwekezaji ndani ya nchi yetu ilikuwa ni dola za Kimarekani bilioni 5.2. Sasa hivi imeshuka mpaka dola za Kimarekani bilioni 2.8. Mauzo yetu nje yameporomoka sana na urari umekuwa hasi na tumewahi kuwa na urari wa bidhaa kati ya biashara ya ndani na nje ukiwa chanya miaka ya nyuma iliyopita. Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango anafahamu na ni wote wawili; Waziri na Naibu Waziri anafahamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pato la Taifa, unachukua consumption, unachukua investment, unachukua government expenditure, unachukua export minus imports. Investment negative forty four (-44) growth ya matumizi ya Serikali kwa maana ya bajeti ya Serikali inaongezeka kwa 2% tu sasa hivi. Export minus imports negative, kwa sababu tuna-import zaidi kuliko ku-export, pato la Taifa litakuwaje katika mazingira kama hayo? Ni lazima Serikali ifanye kazi ya bidii kuhakikisha ya kwamba tunaongeza zaidi exports nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia, licha ya miradi ambayo inazungumzwa, hali ya uchumi wa wananchi, uzalishaji wa wananchi unashuka sana. Angalieni mazao yetu ya kilimo, ukiangalia Taarifa ya Hali ya Uchumi unaona na baadhi ya maeneo tunaona uzalishaji unashuka kwa sababu tu ya sera za Serikali ambazo siyo sahihi. Naomba Serikali iweze kutazama kwa umakini. Haiwezekani ukawa na growth kubwa kama foreign direct investment na export zetu zinazidi kushuka mwaka hadi mwaka kwa sababu unakosa inflows kwenye nchi ambalo ni jambo la muhimu sana kwa ajili ya kuweza kuhakikisha kwamba uchumi unaweza kukua.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kuna continental free trade area, Waafrika tunatakiwa tuwe katika uchumi wa pamoja.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Ni ya pili? Samahani, nashukuru sana, ahsante.