Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Sikudhani Yasini Chikambo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nami napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijalia kusimama katika Bunge hili na kuungana na Wabunge wenzangu katika kujadili bajeti ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijafanya hivyo, naomba kwanza niwapongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na viongozi wote katika Wizara kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno hayo ya utangulizi, naomba niseme kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajadili bajeti ya mwaka 2019/2020, tunajadili Makadirio ya Mapato na Matumizi katika kipindi hicho cha 2019/2020, lakini tukiwa tunafanya hivyo, tumepitisha bajeti mbalimbali huko nyuma. Nimesimama hapa kwa ajili ya kutaka kumkumbusha Mheshimiwa Waziri, tukiwa tunataka kupiga hatua katika mwaka wa fedha huu 2019/2020, ni vizuri tukaangalia bajeti hizo za nyuma, ni mambo gani tuliyajadili hapa lakini hayakupata ufanisi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo mbalimbali ambayo tumeyajadili ikiwemo miradi ya maendeleo, lakini kwenye miradi ya maendeleo yako maeneo hatukufanya vizuri. Sasa ni jukumu letu kama Serikali, kujipima na kuona sasa tunapotaka kupita hatua, ni lazima tuangalie yale mambo ambayo tumeyapitisha huko nyuma na hayakufanya vizuri. Kwa mfano, tulijadili masuala mbalimbali yanayohusu ujenzi wa madarasa, ujenzi wa zahanati na majengo mbalimbali ambapo wananchi wetu wamekuwa wakijitolea. Wamefanya hizo kazi lakini iko miradi mpaka hivi nilivyosimama hapa, bado hatujafanya vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nawaomba Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, ni vizuri tukajipima kwa kuangalia kile tulichokifanya. Kwa nini nasema hivyo? Nasema hivyo kwa sababu katika hiyo miradi yako maeneo mengine ambayo wananchi wetu wamekuwa wakidai fidia mbalimbali. Niseme tu, katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, yako maeneo ambayo wananchi wetu wamekuwa wakipisha miradi hiyo ifanyike na miradi hiyo imekuwa ikigusa makazi yao. Kwa mfano, tulikuwa tunatekeleza mradi wa barabara kwa kiwango cha lami, barabara ambayo ilikuwa inaanzia Namtumbo – Kilimasela – Tunduru - Nakapanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza miradi hii wako wananchi ambao walitakiwa wapate fidia zao lakini mpaka hivi ninavyosema hawakupata fidia na ninaomba nieleze, wananchi wale wako katika makundi yasiyopungua manne, naomba Mheshimiwa Waziri anisikilize. Liko kundi la kwanza ambapo wananchi walilipwa fedha katika kutekeleza mradi ule wa barabara kwa kiwango cha lami, lakini walihisi kwamba wamepunjwa, Serikali ilitoa tamko kwamba hawasitahili kulipwa walichopata ni kile kile ambacho ni halali yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lipo kundi la pili, wananchi walivunja nyumba kabla ya kupewa notice, Serikali ilisema kwa kuwa walivunja kwa hiari yao haiwezi kuwalipa. Liko kundi la tatu ambapo wananchi walipewa notice, kabla ya kufanyiwa tathmini walivunja nyumba zao. Serikali ilitoa tamko kwamba wangeweza kupata kifuta jasho au kifuta machozi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lipo kundi lingine la nne ambalo mimi binafsi nimesimama hapa na linanisikitisha zaidi na ninaomba Serikali ilifanyie kazi. Kundi hili, wananchi walifanyiwa tathmini, walipofanyiwa tathmini, walionekana kwamba wanastahili kulipwa na waliingia kwenye mpango wa kulipwa, lakini wakati wa malipo walirukwa. Sasa nimesimama katika kuwasemea hawa wananchi. Nafahamu tuko hapa, pamoja na kazi zote za Mbunge, lakini ni pamoja na kuwasemea wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kupitia Serikali, kama wapo ambao wanastahili kulipwa basi walipwe. Kwa sababu kila siku wanapokuja kufuatilia, wakati mwingine wanaambiwa anayestahili kulipwa mmoja. Wakati mwingine wanaambiwa wanastahili kulipwa wawili, wakati mwingine wanaambiwa wote hamstahili kulipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali, kwa sababu wale walikubali kufanya hivyo, nami nafahamu wakati tunatekeleza miradi ya maendeleo, iko miradi ambayo inategemea fedha za ndani, lakini iko miradi ambayo inategemea fedha za wafadhili. Katika fedha za wafadhili kunakuwa na masharti ambayo wanayaweka katika mikataba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia barabara hii wakati inajengwa, maelekezo ilikuwa kwamba suala la fidia ni suala la Serikali yenyewe, kwa maana ya mapato yetu ya ndani. Sasa kinachosikitisha zaidi, barabara hiyo tayari imeshafunguliwa. Mheshimiwa Rais bahati nzuri alitembelea kule kwetu karibuni, katika Mkoa wetu wa Ruvuma, alipokuja kule wananchi walijiandaa pale kutaka kushika mabango, lakini viongozi wakawaambia msishike mabango, wakakubali wakaacha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba, kwa kuwa tunakusudia kupiga hatua, ni vuzuri tukaangalia viporo tulivyoviacha nyuma. Wananchi wangu wamekuwa wakilalamika, na siyo barabara hiyo tu, yako maeneo mengine wananchi wanapisha mashamba yao, wanaacha mashamba yao wanapisha Serikali miradi iendelee, lakini mwisho wa siku wanahangaika kila siku maofisini, wanadai fidia zao na hawapati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, nami nimepata habari kwamba miongoni mwa vitu ambavyo Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango havipendi ni kutokulipwa wananchi wetu. Sasa namwomba Mheshimiwa Waziri, kama kweli tathmini imefanyika na wako ambao wanastahili kulipwa, basi ni vizuri jukumu la Serikali kuwalipa wale wananchi ili tuwatie moyo. Mwisho wa jambo hili ni mwanzo wa jambo lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuongea hayo, kwa kweli nilisema kama sitaongea hayo inawezekana ningepoteza fahamu, kwa sababu nilikuwa na hamu kweli ya kuongea jambo hili kwenye Bunge ili lifanye utekelezaji na wananchi wale naamini watakuwa wananisikia, kwa sababu ndicho walichotuagiza tuje kuwasemea. Kuwasemea siyo tu kuhimiza miradi ya maendeleo, lakini kuwasemea pia na kuangalia kero zile ambazo wanazipata wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine naomba nizungumzie suala la Halmashauri. Mimi kabla sijawa Mbunge, nimekuwa Diwani katika vipindi vinne kwenye Halmashauri. Naelewa vizuri sana masuala ya Halmashauri. Halmashauri zilizopo leo kwenye maeneo yetu ni tofauti na huko nyuma. Hali za Halmashauri zetu siyo nzuri. Tulifuta baadhi ya vyanzo vya mapato, tukawa tumeahidi kwamba Serikali itakuwa inafidia vile vyanzo. Kwa sasa ni kama haviendi kabisa. Kwa maeneo ambayo tunapeleka hivyo vyanzo, basi haviendi kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe kwamba vile vyanzo ndivyo ambavyo Halmashauri wanakaa wanapanga bajeti kupitia vile vyanzo. Wanaangalia miradi ya maendeleo. Kutopeleka fedha kwa wakati maana yake ni kuzifanya zile Halmashauri zizidi kudidimia na kutoendelea na ile miradi ambayo wameipanga kwenye Halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, sisi ni Wabunge, lakini tukiwa kwenye Halmashauri sisi pia ni Madiwani. Tunaona matatizo ambayo wanayapaya Madiwani wetu kwenye Halmashauri. Ziko Halmashauri, Diwani inafikia mpaka miezi kumi hajapata posho yake wala hajapata stahili yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili linakatisha tamaa. Sisi tunakaa huku miezi mingi, lakini shughuli nyingi za kwenye Halmashauri wanafanya Madiwani wetu. Ni vizuri sasa Serikali ione uwezekano wa kupeleka fedha kwa wakati ikiwepo kuwatia moyo hao Madiwani nao wawe wanapata posho kama tunavyppata sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme, sisi tunao utaratibu, ikifika siku ya Jumanne, mtu anaangalia kama kuna chochote kimeingia, Jumatano, Mbunge anaangalia kama kuna chochote kimeingia, lakini kama hakikuingia tunaanza hapa; hatujapata, hatujapata, posho, haijatoka, haijatoka. Sasa kama jambo lile linakuuma wewe, lazima urudi umwangalie na mwenzio nyuma kwamba naye linamuuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tumetangulia, tumesimama mbele lakini huko nyuma wako wenzetu wanaotufuata. Wanaotufuata ni pamoja na Madiwani. Kwa hiyo, nilikuwa niiombe Serikali, tuangalie Madiwani, hali zao siyo nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la Madiwani, waliingia hata kwenye bima za afya. Naomba nikwambie, ziko Halmashauri mpaka sasa zinashindwa kulipa hata bima za afya za wale Madiwani. Wanakwenda kutibiwa wanaambiwa bima yako haisomi. Sasa vitu kama hivi vinakatisha tamaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeyasema haya kwanza nikiwa naamini kwamba mimi ni sehemu ya Madiwani. Pia kuna suala la mikopo, wamekopa ile mikopo, kwenye mabenki hawalipi. Sasa mwisho wa siku kile ambacho walistahili kukipata hawatakipata na wanafanya hivyo siyo kwamba Wakurugenzi hawapendi kufanya, uwezo unashindikana, kwa sababu tulichukua vile vyanzo, lakini katika kuchukua vile vyanzo tuliahidi kwamba tutarudisha, hatupeleki kwa wakati, hali imekuwa ngumu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona niyaseme haya na ninarudia tena mimi ni sehemu Madiwani, lakini yako mambo ambayo tunajadili kwenye Halmashauri kama hivyo nilivyosema miradi ya maendeleo, kama hatupeleki fedha kwa wakati ile miradi haiwezi kufanikiwa. Haiwezi kufanikiwa kabisa na Wabunge wenzangu wameyasema haya; zahanati, vituo vya afya, madarasa, na miradi mingine, wananchi wamefyatua tofali kwa nguvu zao, lakini leo tofali zimegeuka kuwa vichuguu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, inatia huruma sana kama Serikali, kama Wawakilishi, wasingeweza kuja wote, sisi tumekuja kuwasemea. Naiomba Serikali yangu sikivu isikie maneno haya ninayoyasema hatimaye itekeleze.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja mia kwa mia. (Makofi)