Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rufiji
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa mambo machache kusema kwamba, Tanzania is a sovereign state. Tanzania ni nchi huru na Taifa lolote kuwa huru kuna mambo mawili lazima yatimie, jambo la kwanza ni Taifa hilo kuwa huru kutunga sheria zake za ndani na kufanya maamuzi ya ndani bila kuingiliwa na Taifa lolote. Jambo la pili, Taifa lolote kuwa huru ni kuamua kufanya siasa za nje bila kuingiliwa na Taifa lolote. Ndiyo maana tunasema Tanzania is a sovereign state.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeamua nianze kusema haya kwa sababu miezi michache iliyopita tuliona clip iliyokuwa inasambaa kutoka kule Ujerumani ikiwaonesha Wabunge wa kutoka Ujerumani wakituambia Watanzania tusimamishe utekelezaji wa mradi wa Stiegler’s Gorge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huu ni upungufu wa fikra tuseme na pengine wenzetu wanapaswa kutambua kwamba, Taifa lolote linapokuwa huru, linakuwa huru kutunga mambo yake na kufanya mambo yake bila kuingiliwa na Taifa lolote. Kwa namna hiyo katika clip ile inawaonesha Wabunge wa Ujerumani wakisema kwamba, wao ni koloni la Tanzania wakiamini kwamba bado ni koloni lao. Niiombe Serikali kufanya maamuzi yafuatayo:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa Serikali ifanye tathmini ya athari za ukoloni hapa nchini, ukoloni ulituathiri nchi yetu kwa kiwango gani? Wakati huo tunatambua kwamba Ulaya imejengwa na Afrika kupitia raw materials zilizotoka hapa Tanzania na nchi nyingine za Afrika. Tuombe Serikali ifanye tathmini ya athari za ukoloni, lakini baada ya kufanya tathmini ya athari za ukoloni Serikali ifungue kesi katika Mahakama ya Kimataifa kudai fidia zinazotokana na ukoloni.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania haitakuwa nchi ya kwanza kufanya hivyo, Kenya imefanya hivyo na Mahakama za Kimataifa zimeamuru wenzetu waweze kulipwa fidia kutokana na athari za ukoloni, niliona nianze hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya vita ya Dunia Tanzania tuliachwa chini ya League of Nations, tuliachwa chini ya Waingereza, lakini tunatambua kwamba, Waingereza hawakufanya lolote kwa Taifa letu, walitufanya Tanzania tuendelee kudumaa kiuchumi. Serikali pia, ikiwezekana ifanye tathmini ya athari zozote zilizofanywa na Taifa la Uingereza ili tuweze kufungua mashtaka kwenye Mahakama ya Kimataifa ya kudai fidia zilizotokana na athari hizi za ukoloni ambazo zimefanywa na wenzetu hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi lazima niipongeze sana Serikali lakini pili nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kudhamiria kutekeleza Mradi wa Stiegler’s Gorge. Mradi huu ni nembo (symbol) ya Taifa letu. Mwalimu Nyerere mwaka 1956 wakati wa kupigania uhuru, wakati ule alivyokuwa akija Rufiji alidhamiria kuhakikisha kwamba mradi huu unatekelezwa. Wamepita viongozi wengi wa nchi hii, Marais wengi wamepita, maamuzi yaliyofanywa na Rais Dkt. John Joseph Pombe Magufuli ni maamuzi magumu na ya kizalendo ya kwenda kutekeleza mradi huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu unakwenda kuongeza pato la Watanzania. Tukiweza kuzalisha umeme megawatts 2,100 inamaanisha kwamba viwanda vyetu vyote vitaweza kupata umeme wa kutosha. Tutambue kwamba umeme kutokana na mradi huu utakwenda kuuzwa kwa bei ya chini kabisa. Ni kiongozi gani ambaye anaweza kukubali kufanya maamuzi haya magumu, ni Rais peke yake aliyedhamiria kuwakomboa Watanzania. Kwa hyo, sisi tunaipongeza sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nami lazima niseme sisi watu wa Rufiji tumetunza vyanzo vile kwa muda mrefu sana. Kupitia kwa Mbunge wao Mchengerwa, mara kadhaa nimeleta hoja hapa kabla hata Serikali kuamua kufanya maamuzi haya. Lazima tukiri kwamba huu ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba wakati Serikali inakwenda kutekeleza mradi huu, tuwakumbuke watu wa Rufiji kwa sababu zipo kelele za wananchi wetu wa Rufiji kwamba kwenye ajira hawajachukuliwa wengi. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri kwamba wakati sasa tunakwenda kutekeleza mradi huu, kipaumbele cha kwanza kabisa cha ajira kiwe ni kwa wananchi wetu wa kutoka Rufiji kwa sababu ndiyo wameutunza mradi huu kwa miaka mingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mradi huu kutengenezwa utaendelea kubaki Rufiji na ndiyo maana tunasema kwamba Warufiji tuwaangalie kwanza kwa sababu wao ndiyo wanautunza mradi huu lakini kupitia Mbunge wao, ndiyo tulileta hoja hapa kuhakikisha kwamba mradi huu unatekelezwa. Yako maeneo yatahitaji uboreshaji wa miundombinu kupitia kwenye mradi huu, tunaipongeza sana Serikali imejenga barabara na madaraja. Tunaomba sasa barabara hizi ambazo zimejengwa na Serikali zijengwe kwa kiwango cha lami. Ili mradi huu utekelezwe kwa miaka mitatu anayoitaka Mheshimiwa Rais, kipande cha kutoka Kibiti - Mkongo ni kibovu sana, tunaiomba Serikali kuhakikisha kwamba eneo hilo linaboreshwa vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutoa mchango wa namna gani tunaweza kuongeza kodi, ipo kodi inasahaulika. Pengine Mheshimiwa Waziri wa Fedha akisimama hapa atuambie ipo kodi ambayo kimsingi inawekwa kwa ajili ya ku-discourage consumption. Kodi hii mara nyingi tunaita excise duty au sin tax. Kodi ambayo inatakiwa itozwe kwenye sigara na pombe lakini kodi hii imesahaulika kwa muda mrefu. Serikali inatumia mabilioni ya fedha kutibu watu TB lakini haijafanya nyongeza yoyote ya kodi kwenye sigara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niliwahi kuandika andiko moja 20 iliyopita kuhusiana na makusanyo ya kodi ya sin tax. Tuombe Mheshimiwa Waziri aangalie Watanzania wanaathirika sana na sigara, Serikali inapaswa ku-discourage consumption kwa kuongeza kodi hii ili Watanzania waache kutumia sigara. Pia hata kodi kwenye pombe Serikali iangalie uwezekano ili iweze kuongeza mapato lakini pia ku- discourage consumption ya vitu hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Taifa tumekuwa tukiangalia sana madini ya dhahabu lakini yapo madini mengine ambayo yanatumika kwenye viwanda, Serikali imesahau sana. Tumuombe Waziri wa Fedha atakaposimama hapa atuambie Serikali imefikia hatua gani kuhusu kuimarisha na kuboresha mchakato wa matumizi ya madini ya soda ash ambayo yanapatikana kule Arusha.
Mheshimiwa Naibu Spika, madini haya yana fedha nyingi sana kuliko hata dhahabu lakini Serikali imekaa kimya, haizungumzia jambo lolote kwenye eneo hili. Tunatambua kwamba Wajapan walitoa fedha nyingi sana na fedha hizi walipewa watu wa NDC. Waziri wa Fedha akisimama hapa atuambie fedha hizi zimekwenda wapi na kama kuna wanaohusika kuzila fedha hizi, basi Serikali ichukue hatua kali kwa wahusika wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua madini haya (industrial minerals) ndiyo yananufaisha nchi nyingi sana. Bajeti ya Marekani inategemea madini ya viwandani. Kwa hiyo, niombe Serikali kuzingatia hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa asilimia 100, ahsante sana. (Makofi)