Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtera
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nichukue fursa hii kumshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai na afya ili niweze kuchangia katika mchango unaoendelea sasa wa Wizara ya Fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Mpango pamoja na dada yangu, Mheshimiwa Dkt. Ashatu ambaye ni Mbunge wa Mkoa huu wa Dodoma, wanafanya kazi nzuri sana, kazi yao ni njema na tumeona Mheshimiwa Rais akionesha njia kwa kukutana na wafanyabiashara pale Dar es Salaam watano toka kila wilaya na wafanyabiashara wakamwambia mambo mengi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina hakika wakuu wa mikoa na Waziri mwenye dhamana ya Wizara hiyo watakuwa wamepata mwongozo kutoka kwa Mheshimiwa Rais wa namna ya kukutana zaidi na wafanyabiashara wengine wengi zaidi, isiishie pale tu alipoishia Rais, Rais yeye ameonesha njia wao sasa wachukue nafasi hiyo kuendeleza ambayo Mheshimiwa Rais ameyafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitabu cha Mheshimiwa Dkt. Mpango kinaonesha uchumi unakuwa takribani kwa asilimia saba. Na kila siku nimekwa nikisisitiza sana kwamba hesabu hizi wakati mwingine tuwe tunazihusisha na maisha ya kawaida ya raia wa nchi yetu, tukifanya hivyo tutauona uchumi namna unavyokuwa. Tuwe tuna sample ya pengine wilaya iliyokuwa maskini mwaka jana au mwaka juzi hali yao kwa sasa ikoje, tukifanya hivyo tunaweza tukapata picha ya moja kwa moja namna ambavyo uchumi wa nchi yetu unakuwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona safari hii TRA wakiondoa kodi kwa biashara mpya. Kitendo hiki kitachagiza sana wafanyabiashara hawa kuweza kujua katika miezi sita amezalisha kiasi gani na anaweza kutozwa kodi kiasi gani. Mwanzoni yalikuwa ni maajabu kabisa, unamkamua ng’ombe halafu ndiyo unakwenda kumlisha, yaani biashara inaanza leo na kodi unaanza sasa. Kwa kweli pale haikuwa sawasawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, na ndiyo maana nikawa natafakari, wakati mwingine maafisa wetu wa kutoza kodi hawa ingekuwa kama zamani ambapo viongozi tulikuwa tunasisitizwa unapotaka kuhamaisha kilimo na wewe uwe na heka yako moja ya kilimo, kwa hiyo, unaweza ukawaonesha wananchi kwa vitendo kwamba wewe unalimaje na unfuataje taratibu za kilimo. Na maafisa wetu watoza kodi hawa na wao wangekuwa walau na biashara, walau duka, anauza ili na yeye tuje tumuone katika miezi sita atakuwa amepata faida kiasi gani.
Mheshimiwa Naibu Spika, unajua ukitaka kupima adha anazopata mlemavu wa macho hebu funga kitambaa cheusi halafu nenda sokoni, ukikoswa na bodaboda ya kwanza tu utakitoa kile kitambaa. Kwa hiyo, kwa kweli wakati mwingine tunafanya vitu kwa sababu sisi hatuishi maisha hayo. Kwa hiyo, rai yangu kwa watu wa TRA ni yaleyale maelekezo ya Mkuu wa Nchi kwamba wawe rafiki na wafanyabiashara badala ya kuleta lugha ambazo zitakuwa zinaudhi baadhi ya wafanyabiashara na kuwakatisha tamaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo nachangia vitabu vyote viwili; kitabu cha Mheshimiwa Dkt. Mpango na kitabu cha Kambi Rasmi ya Upinzani. Na kwa kweli sikusudii kukichana hata kidogo, labda pengine ntakichana kwa hoja tu. Kuna watu wanajaribu kuzalisha hoja kwamba Serikali, Mawaziri, sijui wanahofia maelezo ya Kambi Rasmi ya Upinzani, si kweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikinukuu katika hotuba yao ukurasa wa kwanza anasema, namnukuu Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani:-
“Mheshimiwa Spika, kama mkakati ndiyo huo wa kudhoofisha Upinzani Bungeni kwa kuwafukuza Wabunge wa Upinzani. Napenda kulithibitishia Bunge lako kwamba mkakati huo umeshindwa kabla hata haujaanza kutekelezwa. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iko imara zaidi leo kuliko jana ndiyo maana kila wakati tunapowasilisha maoni yetu hapa Serikali yote inahaha kutujibu”. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haya maneno si ya kweli nataka nieleze hapa kwamba kama ikitokea Mwalimu Nyerere akarudi hapa akiwa na rafiki yake Bob Makani, hawa watu wawili wote watakuwa na mshangao mkubwa sana. Mwalimu Nyerere kuna mambo yatamshangaza na Bob Makani kuna mambo yatamshangaza. Bob Makani alikuwa Mwasisi wa CHADEMA, Mwalimu Nyerere Mwasisi wa CCM, hawa wawili wanatashangaa!
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Mwalimu akifika Lumumba atashangaa kukuta ofisi ya ghorofa ambayo hakuiacha, Bob Makani atashangaa kukuta ule mgahawa bado upo pale. Yaani nataka niwaambie hawa watu watashangaa sana. Bob Makani kila atakapojaribu kwenda Kinondoni atakuta hata rangi zilizopakwa za CHADEMA bado ni zilezile, hazijawekwa mpya, atashangaa sana Bob Makani, kwamba hawa watu ndio walikuwa wa maendeleo hawa?
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi Mwalimu atakapokuja atakwenda Chimwaga akidhani ndiyo Ukumbu wa CCM, ataambiwa ni chuo kikuu, atashangaa Mwalimu kwamba hii kazi imefanywa. Atapotea atakuwa anakwenda Kizota anafikiri bado tunafanyia mikutano Kizota, ataambiwa hapana, shuka hapo katikati kwenye daraja, Mwalimu atashangaa sana, atakuta mabadiliko ni makubwa ambayo Bob Mnyanga Makani hatayaona CHADEMA. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Bob Makani kuna kitu atataka kujiuliza, atasema labda niende sasa kwenye demokrasia maana ndiyo jina la chama chetu, hebu niulize demokrasia inatendekaje ndani ya CHADEMA, atakuta Mwenyekiti ni yuleyule, atashangaa sana Bob Makani. Hawa watu ndiyo mnasema eti sisi tunawahofia, hawa, ambao hata Bob akija leo atawashangaa. Atauliza Mwenyekiti wa chama nani, ataambiwa yuleyule uliyemuacha, wakati huku Mwalimu ataambiwa Mkapa alimaliza, akaja kijana wako Kikwete kamaliza sasa yuko Magufuli, Mwalimu atashangaa kukuta demokrasia inatekelezwa ndani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka niseme kweli kwamba hawa jamani hata mzee wa paka huwa anapokea, hawa ndio mnasema tuwaogope? Hatuwezi kuwaogopa hawa. Mwalimu Nyerere atauliza chama changu vipi mfumo wake wa Viti Maalum unafanya kazi, ataambiwa wapo, Wabunge wa Viti Maalum wapo. Bob Makani akiuliza CHADEMA atasema wapo lakini wanapangishwa chama, milioni moja na laki tano kila mwezi wanalipia chama. Kwa hiyo atashangaa sana, hawa watu siyo wa kututisha sie. Pia kila atakapokuwa akiuliza, ataambiwa basi chama kingine ataambiwa, cha Cheyo Mwenyekiti bado Cheyo; cha Mrema, Mwenyekiti bado Mrema, NCCR Mageuzi ataambiwa bado Mbatia; hawa ndio waje watutishe sisi? Hawa? Akiuliza ataambiwa na Dovutwa bado anaendelea, akiuliza ataambiwa na Lipumba naye ni Mwenyekiti; kwa kweli Mwalimu atashangaa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nataka niwasihi Watanzania kwamba sisi hatuko hapa kwa ajili ya kushughulika na hawa, hawa wameshajifia jamani, hakuna upinzani nchi hii, wamejifia wao wenyewe kutokana na tabia zao na maisha yao, wamefika mahali wamejiua wamegonga ukuta. Kwa hiyo tusisumbuke kabisa na watu hawa na wala viongozi wa Serikali msihangaike na watu hawa, wameshajiua. Mtu kama anakufa kwa asali huna sababu ya kumtilia sumu jamani, unamuacha tu anajifia mwenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vichaa walikuwa wamekubaliana watoroke hospitali. Wakakubaliana kwamba wafike getini wamnyonge mlinzi halafu watoroke. Vichaa wale walipofika getini wamkakuta mlinzi hayupo wakasema dili limeharibika turudi; dili limeharibika turudi.
Mheshimiwa Naibu Spika, unaweza ukaona namna ambavyo tunafanya siasa za ajabu. Tumeona Serikali ya Awamu ya Tano ikifanya kazi kubwa; inajenga hospitali kila wilaya inajenga vituo vya afya kila jimbo; Wizara ya Maji imeboresha mfumo wake tunaona maji yanapatikana. Kazi yetu sisi ni kuwatieni moyo tu ili muendelee. Migogoro ya ardhi sasa hivi ukifika kila kona ya nchi yetu inaondolewa. Mimi nasema hivi hakuna sababu ya kuwavunja moyo Waheshimiwa Mawaziri pigeni kazi; Dkt. Mpango pamoja na mwenzako pigeni kazi ili uchumi wa nchi hii uweze kukua na wananchi wapate maendeleo. Hizi rabsha rabsha chache mnazozisikia hizi zisiwapotezee muda; hawa Wabunge mnaowaona humu ndani wamepangishwa chama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na kwneye hili nataka nimwambie Dkt. Mpango, kuna kodi mpya hutozi hapa, hapa lazima TRA watoze kodi mpya. Ni kwamba, Wabunge wa Viti Maalum wa CHADEMA wanalipishwa kodi ya upangaji kwenye chama 1,500,000 kila Mbunge kwa mwezi, kasoro Wabunge wateule wachache tu kama wawili, watatu ambao nao wakiniudhi nitawataja siku moja hapa, hao hawalipi na sababu mimi nazijua, nao nawaweka kiporo; lakini wengine wote ni wapangaji hawa, wamepanga kwenye chama, wanalipishwa kodi hawa na wasipolipa wanafukuzwa chama. Wabishe si wako hapa mimi naongea vitu vya ukweli, hawa ni wapangaji. Hapa hatuna Wabunge; hapa tunawapangaji wamepangishwa, sasa na sisi tutoze kodi mpya ya mapato ambayo aliyewapangisha anapata ili walipie.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)