Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika bajeti hii. Kwanza nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Naibu Waziri wa Fedha na timu yake yote. Sambamba hilo, nitoe pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi nzuri anayoifanya hasa ikionyesha wazi kwamba ana nia njema ya kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa manufaa ya Watanzania wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Pamoja nakuunga mkono hoja, nataka nimtoe wasiwasi Waziri wa Fedha na timu yake kwamba ndugu zangu tumewazoea, watasema pale, baada ya dakika mbili watgeuka watakuja huku huku, watapita kwa Mawaziri, watawanong’oneza, Jimboni kwangu hakuna maji, Jimboni kwangu nataka shule, Jimboni nataka barabara, wanakuja huku huku. Mimi nakaa hapa hapa wanawaona. Mara wameenda kwa Waziri wa Fedha, mara Waziri wa Ardhi, mara Waziri wa Maji, mara wa TAMISEMI, mimi niko hapa hapa nawatazama; lakini wakipewa fursa ya kuchangia, wao ni hapana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hapana hizi ifike sehemu na sisi tujirekebishe, tusiwe tunapenda mno anaposema hapana tunamlazimisha kumpa kitu. Hii ni bajeti ya nne katika Awamu hii ya Tano. Mara ya kwanza tumesema hapana, tumefanya kazi nchi nzima bila ubaguzi Majimbo yote, kazi imeonekana. Hakuna Jimbo lolote ambalo litasema halina shule ya msingi, halina shule ya sekondari, halina kituo cha afya, hana mwalimu, hana nesi, hana mtendaji, hana mkurugenzi. Hawa wote bajeti yao inapita hapa na tunachangia. Juu ya hilo …..
TAARIFA
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Angelina Malembeka, kuna taarifa Mheshimiwa Yosepher Komba.
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba nimpe taarifa mama yangu mzungumzaji kwamba maendeleo ambayo yanatokana na bajeti ya humu ndani siyo kwamba ni hisani ya Wabunge na hawapewi Wabunge, bali wanapewa wananchi kutokana na kodi zao. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Angelina Malembeka endelea na mchango wako.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee ila nikukumbushe, kuna wakati tunaingia Bungeni, niliomba Wabunge tukapimwe akili. Matokeo yake tukaletewa semina hapa ya matumizi sijui ya bangi, matumizi ya pombe, matumizi ya sigara, tukaonyeshwa udhaifu wake. Umbali kutoka hapa mpaka kwenda pale kwenye kituo cha wagonjwa wa akili kupima, siyo mbali. Hivi tunapata shida gani kwenda kupimwa akili sisi Wabunge? Kwa sababu inafika sehemu mtu anaongea lingine, anakupa mambo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nashangaa, hebu nendeni Majimboni kwenu kwanza halafu tuone kama utekelezaji wa ilani haufanyika katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kuchangia kama ifuatavyo:-
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utaratibu.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Angelina Malembaka kuna kanuni inavunjwa. Mheshimiwa Selasini.
KUHUSU UTARATIBU
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama kwa mujibu wa Kkanuni ya 64 (1) (g). Mheshimiwa anasema Wabunge waende kupimwa akili. Sasa hii siyo akili nzuri. Kama yeye anajisikia akili yake ina matatizo, akapime. Sisi wengine hususan mimi, akili yangu ni nzuri kabisa ni timamu sihitaji kwenda kupima akili Milembe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ama afute kauli yake au usaidie afute kauli yake kwa sababu Bunge zima litaonekana kwamba sisi ni vichaa. Au athibitishe kwamba kuna Wabunge humu ambao wana akili ambazo siyo nzuri. (Kicheko)
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Selasini amesimama kuoneshwa kwamba kanuni ya 64 (1) (g) imefunjwa na Mheshimiwa Malembeka kwa kusema kwamba Waheshimiwa Wabunge akili.
Waheshimiwa Wabunge, ningetamani kama ambavyo huwa nasisitiza siku zote; moja, kuzingatia kanuni zetu; lakini la pili, ni uvumilivu. Haya mambo ya kupimwa akili, kuna wakati kuna Mbunge alishapata kusema Watanzania wote inabidi wakapimwe akili. Wakati huo haikuonekana kama ni jambo la ajabu Watanzania kuambiwa wakapime akili.
Wakati huo huo sisi Wabunge hapa ni Wawakilishi wa hao wananchi ambao tunawatuma ili wakapime akili. Sasa nakuwa sielewi ni wakati gani kipimo tayari kinakuwa kimeshajulikana kabla hatujaenda.
Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo, tuwe tunafuatilia sisi wenyewe michango yetu na maneno tunayoyatumia. Maneno yale ambayo siyo lugha ya Kibunge, hayo yatakuwa yanaondolewa kila wakati. Yale ambayo matumizi yake huwa tunayatumia sisi wenyewe, basi tuwe wavumilivu hata vile ambavyo huwa yanatoka sehemu nyingine.
Mheshimiwa Malembeka, endelea na mchango wako. (Makofi)
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi, tunaendelea kusisitizana kupima afya zetu ikiwemo Malaria, UKIMWI, TB, vyote tukapime. Nasi Wabunge ni binadamu kama wengine, lazima tukacheki afya zetu kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumwambia Mheshimiwa Waziri wa Fedha kama nilivyosema mwanzo, wao mara zote wanachangia, wanakataa, wakishamaliza, wanakuja huku kuomba. Sasa hilo nanyi mliweke sawa, kwamba isifike sehemu sisi ambao tunakuja tunatetea hoja zetu, tunatete kauli zetu na yule ambaye kila siku anapinga, tena anapiga kwa uwazi, halafu tunaonekana wote tupo sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo Majimbo ambayo watu kila siku wanasimama hapa wanapiga kelele, lakini Majimbo yao hayajafanyiwa kazi.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Kuna wengine kila kitu wanakataa, lakini wanafanyiwa kazi. Mimi lengo langu kubwa ni kwamba kwa kuwa Ilani ya Chama cha Mapinduzi inatekelezwa nchi nzima, sasa…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Malembeka, kuna taarifa.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Sasa wasiwe kila kitu wanakataa. Vile ambavyo wamefanyiwa, wawe wanakubali kuwa…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Malembeka, kuna taarifa. Mheshimiwa Khatib.
TAARIFA
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nampa taarifa mwongeaji kwamba Wabunge wanapowafuata Mawaziri kuomba ni haki yao kwa sababu ni Serikali yao na kodi zinajumlisha Majimbo yao. Hivi ni nani bora...
NAIBU SPIKA: Taarifa ni moja Mheshimiwa Khatib. MHE. CECIL D. MWAMBE: (Aliongea nje ya microphone) NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Cecil, taarifa ni moja Mheshimiwa Khatib. Mheshimiwa Malembeka, endelea na mchango wako.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kesho ni siku ya kupiga kura na Watanzania wapo wanatuona. Hizo taarifa, taarifa zao wanazotaka kunivuruga ili nisimalize ninayosema, nitayasema mpaka dakika ya mwisho.
MHE. CECIL D. MWAMBE: (Aliongea nje ya microphone)
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilindie muda wangu.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Malembeka naomba unyamaze kidogo.
Mheshimiwa Cecil Mwambe, Michango ya harusi sasa hivi inahusikaje? Hebu kuwa mtu mzima kidogo, tafadhali. Hebu kuwa mtu mzima kidogo for once tafadhali. (Kicheko/ Makofi)
Mheshimiwa Angelina Malembeka endelea kuchangia na harusi ni wewe unapanga namna ulivyoona; na watu tuliokuchangia tumenyamaza, wanaopiga kelele hata hawakukuchangia.
Mheshimiwa Mbunge, endelea la mchango wako.
MBUNGE FULANI: Rudisha hela wewe mamaa!
(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila kufuata utaratibu)
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza, siwezi kuchanganyikiwa na kelele ya mtu yeyote kwa sababu havinihusu. Mimi ninaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono moja kwa moja mapendekezo ya Hotuba ya Waziri wa Fedha kwa sababu za kwanza zifuatazo:-
(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila kufuata utaratibu)
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza katika hotuba yao ya mapendelezo wameelezea kwamba wana nia nzuri ya kupanua wigo wa kodi na usajili wa walipa kodi. Pili, wameelezea nia yao ya dhati kuwekeza kwenye maeneo ambayo Serikali inaweza kupata mapato zaidi ikiwemo katika Sekta ya Uvuvi, ndani ya bahari kuu na ujenzi wa bahari za uvuvi lakini pia katika ununuzi wa meli za uvuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika mapendekezo hayo nimeona wamelezea ni jinsi gani ambavyo wanaweza wakaongeza ufanisi katika usimamizi na ukusanyaji wa kodi za ndani. Pamoja na hayo, wameonyesha kwamba wana nia ya dhati kabisa ya kuimarisha uwezo wa ufautiliaji na udhibiti wa uhamishaji wa faida na unaofanywa na makapuni ya nje. Pamoja na hilo, wameelezea nia yao ya dhati kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na katika taasisi za Serikali ambazo zinatakiwa zitoe makato yao katika Mfuko Mkuu kwa muda muafaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia wameahidi na wameelezea kwamba wako tayari sasa hivi kuimarisha usimamizi wa misamaha ya kodi ambayo mapato yake yataenda katika miradi ambayo imekusudiwa. Mheshimiwa Waziri, mimi nataka niseme kidogo kwamba katika suala la kilimo yamezungumziwa mazao mengi ya mkakati. Naomba niwakumbushe, katika mazao ya mkakati, lipo zao la minazi ambalo wengi hawajalizungumzia. Zao lile ni zao ambalo lipo katika mikoa ya Pwani na limekuwa na faida nyingi sana ikiwemo masuala ya mapambo, mafuta yenyewe, urembo, dawa na kila kitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wengi ambao wanavuna minazi sasa ni ile ambayo ilipandwa na mababu zao. Haijaoneshwa msimamo wakati sasa hivi kuonyesha na kuhamisha zao la minazi lipandwe nalo liingie katika biashara kama ilivyo mawese na mazao mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna suala la Wakandarasi. Wengi wana madeni na tulikuwa tunasisitiza Wakandarasi wa ndani wapewe fursa ya kuwekeza ndani, lakini madeni yale yamekuwa yanawakatisha tamaa. Utakuta wanadai miaka miwili mpaka mitatu. Naomba katika bajeti hii wawaangalie Wakandarasi waweze kulipwa fedha zao ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo suala zima la taulo za kike. Mimi naunga mkono kwamba kwa kuwa huku zinaingizwa kodi, halafu upande wa pili wawekezaji wa ndani wanapunguziwa kodi ili waweze kutengeneza taulo za kike, ni vizuri kwa sababu pamoja na kupunguza hizo gharama kwa wanafunzi na akina mama, lakini suala kubwa hapo kuangalia lisiwe kwenye suala la taulo tu tuangalie uwezekano wa kupata maji katika maeneo yao. Kwa sababu hata kama watapewa mataulo, hata kama kodi itapunguzwa, lakini ikiwa maji hamna katika maeneo yale, bado tutakuwa tuna hangaika. Kwa hiyo, suala la maji naomba liwekewe umuhimu sana katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la reli ya kisasa, wapo wanaolalamika kwamba ujenzi wa reli ya kisasa kwamba tunasaidia nchi nyingine badala ya kunufaika sisi Watanzania. Ninaamini kabisa, ujenzi wa reli ya kisasa utatoa ajira kwa Watanzania, lakini pia itatusaidia katika usafiri na katika kuinua uchumi wa nchi yetu. Hili jambo zuri na kubwa lazima lipongezwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nizungumzie suala la Madiwani. Tunao Madiwani ambao tunafanya nao kazi muda mrefu. Posho zao bado zimeendelea kuwa chini. Naomba katika bajeti hii tungalie Madiwani ili nao waweze kufanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na yote…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa, ahsante sana.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja tunakutana kesho. (Makofi)