Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nsimbo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuzungumzia Bajeti yetu ya Taifa kwa siku hii ya leo. Kwanza kabisa ninaomba nimshukuru Mungu aliyetuumba ametupa uzima na uhai leo tunazungumzia bajeti yetu ya Nne kwa ajili ya Awamu ya Tano. Namshukuru sana Mungu.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niipongeze sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi kubwa sana ambayo imeifanya mpaka leo kupitia miradi mbalimbali ambayo Watanzania wanaona miradi inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ile ya manufaa ya wananchi wa Tanzania kwa sababu inaonekana na pesa ambazo zinapelekwa kwenye miradi ile na ile miradi inaonekana siyo kusema labda haionekani, inaonekana sasa ndiyo maana watu wanahangaika sana kwa ajili ya hiyo miradi, kwa sababu italeta mafanikio makubwa sana katika nchi yetu na Watanzania watanufaika sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna Mtanzania yeyote ambaye anafunga mkanda Watanzania wote wameridhika wanafanya kazi zao kwa sababu wamejua wanatakiwa wafanye kazi ili Tanzania iweze kwenda juu na tumeona kabisa jinsi gani Serikali imefanya kazi kubwa na leo hii uchumi wetu umepanda asilimia 7.1. Hongereni sana Serikali msirudishwe nyuma songeni mbele.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango pamoja na Naibu wako, mnafanya kazi nzuri sana na kazi mnayoifanya tunaiona na jitihada mnazozifanya tunaziona na mmekuwa wasikivu tunavyowaelekeza ndiyo mnavyofanya, hongereni sana endeleeni kuwa wasikivu nchi yetu itasonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Awamu zote Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi ilisema itaunganisha Mikoa kwa ajili ya uchumi, Mkoa kwa Mkoa lazima barabara za lami ziweze kufunguka kwa ajili ya uchumi wa Watanzania, ni jambo zuri na imefanyika tumeona kila sehemu barabara za lami zimejengwa na watu wanafanya shughuli zao za maendeleo, ombi langu katika Mkoa wa Katavi, ndani ya Mkoa wetu wa Katavi, Mkoa wa Rukwa na Katavi haujaungana kwa lami, kuna kipande kama kilomita 90 hivi bado hakijawekewa lami, nayo ilitakiwa iwekewe lami lakini sasa kuna tatizo kwa sababu ni Mbuga ya Wanyama ya Katavi, sasa katika ile Mbuga yetu, ina barabara mbili kuna barabara iko juu na barabara nyingine iko chini, kuna barabara ambayo inatoka Kizi kwenda Stalike na nyingine ya chini Kibaoni kwenda Stalike.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo hapa wanyama wanazaliana sana, lakini tukiangalia upande wa chini huku Kibaoni Stalike ndiko mazalia ya wanyama wanakozaliana na kuna mabwawa mengi na kuna uchumi mkubwa sana kwa ajili ya hiyo barabara, barabara ya kutoka Kizi kwenda Stalike Wanyama ni wachache sana, tunaiomba Serikali kupitia uchumi wa wananchi wa Mkoa wa Katavi Mkoa wa Katavi, tunaomba katika barabara hiyo moja au ya Kizi - Stalike iwekwe lami ili Mkoa ule uweze kufunguka kwa ajili ya mchumi na kwa sababu sasa hivi Mheshimiwa Waziri nimeona katika vitabu vyako unaelekeza kujenga bandari katika eneo letu la Kalema ili uchumi Mkoa wa Katavi uweze kukua zaidi, naomba ili basi Mkoa wa Katavi uweze kufunguka tuwekewe barabara ya lami kutoka Kizi mpaka Stalike.
Mhesimiwa Naibu Spika, vilevile tuwekewe barabara ya lami kwa sababu hata Standard Gauge inakwenda Kalema na bandari inajengwa Kalema na tunashukuru tunaipongeza Serikali gati lile limekwisha na kwenye vitabu vyako Mheshimiwa Waziri umeandika gati limekwisha, sasa hivi ni mwendelezo wa kujenda bandari, kwa sababu ya mazao yote ambayo yanaenda katika nchi yetu ya jirani ya DRC. Naomba tujenge barabara ya lami kutoka Mpanda mpaka Kalema ili Standard Gauge itakapofika inakuta barabara ya lami tayari imeshajengwa basi yale mazao ambayo yanatarajiwa kwenda kwenye bandari au vifaa mbalimbali vinavyoenda kwenye bandari yetu ya Kalema viweze kwenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile hii barabara kwa nini tunaomba ili uchumi ufunguke kwa sababu bandari ya Kalema ikijengwa mazao yote ambayo yanahitajika kwenda Congo yatapita na barabara ya lami ambayo tayari tutakuwa tumeshaunganisha kile kipande cha Kizi, ambako barabara sasa ya lami itakuwa imeungana ile ya Rukwa Kizi Kibaoni, Kizi Stalike itakuwa imeshakamilika kwa kiwango cha lami, uchumi utakuwa mkubwa sana ndani ya Mkoa wetu wa Katavi ninaomba sana Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tulikuwa tunajua barabara ya lami imeishia Vikonge, tunaomba ili tuweze kufika Kigoma kile kipande cha Vikonge kwenda Uvinza nacho tuwekewe barabara ya lami ili sasa tuunganishe Mkoa wa Katavi pamoja na Mkoa wa Kigoma ili uchumi ndani ya Mkoa wa Katavi uendelee kukua zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mazao ya kibiashara kama tumbaku, pamba, korosho, kahawa ndani ya Mkoa wetu wa Katavi tunalima sana Tumbaku, ninaomba zao hili ndani ya Mkoa wetu wa Katavi limeshuka sana katika na wengine watu wa Tabora wamesema tunaomba Serikali sasa kwa sababu zao hili lilikuwa zao la kibiashara wananchi wa Katavi walikuwa wanalitegemea sana kwa ajili ya uchumi, naomba tuweze kulipangia mkakati mzuri ambao wananchi wote wanaolima zao hili la Tumbaku waweze kufaidika na kunufaika ili uchumi wa wananchi wa Tanzania wale wanaolima tumbaku waweze kurudisha uchumi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya Mkoa wetu wa Katavi, hili kila mwaka ninalisemea, tuna Ziwa Tanganyika, kwa wananchi Katavi matatizo ya maji mkitusaidia kama wenzetu wa Ziwa Victoria ambao walipata maji katika Mkoa wa Mwanza, Shinyanga, sasa maji yale yanaenda mpaka Tabora, naomba sana Ziwa hili la Tanganyika nasi watu wa Mkoa wa Katavi litatusaidia sana matatizo ya maji yakaisha kabisa tunaomba tutolewe maji kwenye Ziwa Tanganyika kuletewa ndani ya maeneo yetu ya Mkoa wetu wa Katavi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la scheme, tunalima sana na sasa hivi mvua zetu hazitabiriki lakini tuna mabonde mengi makubwa na Awamu zote zilijaribu kutengeneza scheme mbalimbali, kuna scheme ambazo zilitengenezwa zikatoa manufaa makubwa sana, naomba Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi ijikite kwenye scheme ili kilimo cha umwagiliaji kiweze kufuatiliwa kwa undani zaidi, kitaleta manufaa makubwa na tija ndani ya nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana Serikali yangu sikivu, umwagiliaji sasa ndiyo utatutoa, utaleta tija kwa sababu katika mabonde yetu tayari kuna unyevunyevu na mvuke mvuke, ule mvuke utatusaidia na kuweka utaalam mkubwa kwenye ulimaji wa mazao mbalimbali kupitia mabonde yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mabonde yetu Mkoa wa Katavi tuna mabonde mengi tunaona jinsi gani wananchi wanajitahidi kupitia hayo maji ya kuchotelea kwenye vikopo wakamwagilia lakini wanatoa mazao. Serikali ikiingiza nguvu yake katika scheme mbalimbali katika nchi yetu nafikiri tutapata manufaa makubwa sana na ukombozi wa Kilimo katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bado tuna tatizo TRA, leo hii kuna ndugu yangu mmoja ameenda TRA amehangahishwa kupata TIN amefungua kampuni mpya ili apate TIN, leo siku ya saba kupata TIN, huko TRA kuna tatizo gani, TIN inatolewa siku moja na ana kila kitu kafungua Kampuni ana vigezo vyote lakini leo anakwenda siku ya saba anaambiwa bado sijui hujaleta sijui hiki, hujaleta hiki, sasa kwa nini siku ya kwanza wasimwambie, wasimwandikie vitu vyote TRA? Imeshakuwa usumbufu TRA mpaka yule Dada akaanza kuwafokea watu wa TRA anasema ninyi Vijana ndiyo mnaowafanya hawa watu wakubwa wanatumbuliwa kila siku kwa ajili yenu ninyi. Ninaomba bado huyu Kamishna mpya bado ana kazi kwa sababu bado Vijana wako hawajaelewa somo. (Makofi)