Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Nkasi Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Ninamshukuru Mungu nami kupata nafasi kuchangia bajeti muhimu kwa Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yoyote makini ina kipaumbele, Serikali yoyote makini kipaumbele chake ni kipaumbele cha wananchi wake. Tunapozungumza hapa bajeti iliyopita na bajeti hii tunawatazama Watanzania ambao wametupa dhamana leo tunazungumzia hali ya uchumi kwenye vitabu kila siku inaonekana uchumi unakua lakini ukienda kwenye uhalisia hali ya Watanzania inazidi kuwa mbaya hasa katika hii Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Serikali ni vizuri takwimu hizi zinazoongezeka kwenye vitabu zipelekwe kwenye uhalisia wa maisha ya Watanzania na baada ya kupeleka huko na haya mambo yote itaonekana kama yana ufanisi endapo utawala bora utazingatia Sheria ndani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo watakaosema kwamba Serikali imefanya nini Watanzania kupitia Wawakilishi. Kwa mujibu wa Katiba tuna haki ya kufanya mikutano kuwaeleza Watanzania nini kinaendelea kwenye nchi hii. Mikutano imezuiliwa, kwa hiyo ninyi mtatengeneza wenyewe na mtakuja kujisifia wenyewe, lengo letu ni moja kuijenga nchi yetu, pelekeni takwimu hizi ziende kwenye uhalisia kwa Watanzania, maisha ya Watanzania bado ni magumu.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachosababisha uchumi wa nchi hii uonekane bado ni butu, ni kero zinazoendelea kuhusu tozo na ushuru ambao unakuwepo kuanzia kwenye bandari na maeneo mbalimbali. Nitolee mfano mmoja tu, leo ukiagiza gari kwa milioni kumi na moja, mpaka ukaichukue pale bandarini bei yake inafanana na ile uliyoagizia.
MBUNGE FULANI: Kweli. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nini tunafanya? Ukiangalia kero ambazo wafanyabiashara walienda kuzungumza Ikulu kwa Mheshimiwa Rais inaonesha ni jinsi gani Wabunge tumeshindwa kutimiza wajibu wetu. Zile ni kero ambazo wanazipata Wafanyabiashara na kama unataka kukuza uchumi wa nchi yetu lazima tuangalie watu ambao wanaweza kukuza uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza wanazungumzia kilimo ambacho ndiyo kinaajiri vijana wengi na watu wengi kwenye Taifa letu, tumejipangaje kwenye kilimo chetu. Serikali ya Awamu ya Tano ilikuja na slogan ya Serikali ya Viwanda, tumejipangaje kwenda kwenye viwanda, ni lazima tuboreshe kilimo nchini. Leo tunapozungumzia kilimo hali ni ngumu sana kulingana na pembejeo ambazo wakulima hawawezi gharama bado ni kubwa sana, kama slogan ni Serikali ya Viwanda lazima tuwekeze kwenye viwanda, viwanda hivyo vikijengwa nchini vitapunguza gharama za pembejeo ambazo zitawaidia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama pembejeo bado ni ghali kwa wakulima hawa lakini rudi kwenye hali halisi ya soko ambayo ni wajibu wa Serikali kuhakikisha inatafuta masoko kwa hawa wakulima, bado Serikali haijajikita kutafuta masoko. Ushauri wangu, tunatumiaje Muungano wetu wana Umoja wa Afrika Mashariki kuweza kuuza mazao yetu ambayo wanaweza kuyalima Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine niliona kwenye hotuba kuna tozo zimeondolewa lakini ukitazama sekta ya uvuvi haijaguswa kabisa. Hawa wavuvi wanapata leseni kutoka Serikalini na wanalipa kodi inakuwaje wao wasiguswe na wana kero nyingi sana kwenye nchi hii? Tusijivunie kukusanya kodi bali tujivunie kutengeneza mazingira rafiki kwa wavuvi na wakulima wetu, hapo ndiyo tutazungumzia ukuaji wa uchumi ndani ya Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa napozungumza leo ziwa tunalotumia sisi la Ziwa Tanganyika suala la usafirishaji ni mgumu. Nategemea Serikali itakuja ituambie hapa suala la MV Liemba mmefikia wapi mpaka sasa ambapo ni usafiri ambao utatusaidia kwenda kuuza mazao yetu Burundi, Congo na maeneo mengine, hiyo mtakuwa mmetusaidia kama Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa nini tumejipanga sisi kukusanya kodi kwa hawa wavuvi badala ya kujipanga kuwatafutia masoko kwanza. Hawa Watanzania leo kama mkulima na mvuvi analia, huo uchumi unakua kutoka wapi? Ni vizuri Serikali ikaangalia Watanzania hawa, kama tunataka kukusanya kodi na wao waone faida ya kodi wanazozitoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)