Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Katavi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia bajeti hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaenda mbali zaidi, nilitaka nifahamu kupitia bajeti hii uamuzi wa Serikali kutangaza safari za ndege za ATCL na kuanzisha safari za kwenda South Africa wakati tulitegemea ili kukuza masuala ya utalii kwenye sekta hii mngeweza kuweka vipaumbele katika nchi ambazo zinaingiza watalii wengi. Tukiangalia South Africa ni nchi ya 8 kati ya nchi 15 duniani, sasa kupeleka ndege kwenye nchi ya 8 na kuacha nchi kama Kenya, Marekani, Burundi jambo hili nilitaka nifahamu kwa kina Serikali ilikuwa inapanga kukuza sekta gani kama siyo kukuza sekta ya utalii kupitia huu uboreshaji wa masuala ya ndege kwenye Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la vitambulisho ambalo Wabunge wameliongelea kwa upana wake linawaumiza sana Watanzania. Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha ili tufahamu, kwa sababu huku mikoani kumekuwa na kero kubwa, akinamama wanateseka sana kwa sababu Serikali bado haijatoa mwongozo wa moja kwa moja kuonyesha nani mhusika anatakiwa hicho kitambulisho cha Sh.20,000. Akinamama wanamwagiwa samaki, hata hawa Mgambo badala ya kuwaelimisha akina mama wengine wamekuwa wanapigwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wangu wa Katavi ukienda Kasokola, Kakese, Mpanda Vijijini, Ikola, Inyonga na maeneo mengine watu wanalazimishwa vitambulisho, imekuwa ni kero akinamama wanashindwa kwenda kwenye masoko yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Sasa hivi ukienda kwenye masoko ya Mpanda Hoteli, soko kuu, Mishano akina mama wanashindwa kupeleka biashara zao. Mkuu wa Mkoa sasa amekuwa ndiyo kero, ndiyo kama mfalme pale, kulazimisha akina mama kuchukua vitambulisho. Watu wanatishiwa na Wanajeshi na Polisi, Serikali mna mpango gani kusaidia hili kundi ambalo mnasema ni la wanyonge? Mheshimiwa Waziri, mwalimu wangu, atakapokuja kuhitimisha atueleze maana amekuwa na matamko ambayo hayaeleweki, hususani sasa ni nani mlengwa wa hivi vitambulisho vya ujasiriamali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la bodaboda na bajaj, nataka kufahamu kwenye ulipaji wa TRA kwa sababu kwa Mpanda wanalipa TRA lakini wamelazimishwa kuwa vitambulisho. Nataka nifahamu ni bodaboda na bajaji nchi nzima wanatakiwa kulipa TRA au ni wa Mpanda Mjini tu? Nataka kufahamu kwenye masuala ya makusanyo ya kodi jambo hili liko nchi nzima au ni Mkoa wa Katavi peke yake kwa kuwalenga hawa madereva wa bajaji pamoja na bodaboda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la tumbaku ambalo kimsingi Mkoa wa Katavi ni wakulima wa tumbaku na ukiangalia kwenye Jimbo la Katavi, Mpanda Mjini na Tanganyika ni maeneo ambayo yanajikita zaidi katika zao la tumbaku. Wakulima hawa 2016/2017 na 2017/2018 kumekuwa na malalamiko mengi kwenye hivi vyama vya ushirika hususani katika Chama cha Msingi cha Ukonongo kilichopo katika Jimbo la Katavi na Chama cha Msingi cha Mpanda Kati. Wakulima hawa wamekuwa na malalamiko mengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nataka kufahamu kwa sababu watu hawa ni kundi kubwa na wanapoteza pesa nyingi sana kwenye masuala ya urasimu katika mauzo ya tumbaku. Kuna shilingi milioni 315 zimeibiwa na hiki Chama cha Mpanda Kati lakini mpaka sasa haijulikani ziko wapi. Hiki kikundi cha hawa wanachama wa Chama cha Msingi Mpanda Kati wamekuwa wakihangaika kwa muda mrefu. Ofisi ya Waziri Mkuu ina taarifa ya wizi huu wa zaidi ya shilingi milioni 315 lakini kuna wizi wa fedha zaidi ya shilingi milioni 400 kwenye Chama cha Msingi Ukonongo katika Jimbo la Katavi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunashindwa kuendelea mbele kwa sababu kila tukitoa mbinu ya kutatua changamoto hizi kwa wakulima na wananchi ambao Serikali hii inajinadi kwamba inasaidia wanyonge hatuoni mrejesho wa moja kwa moja kuwasaidia hawa wakulima ambao ndiyo kundi kubwa. Naomba mambo haya yazingatiwe pia tuone namna gani tunawasadia hawa wakulima, wafanyabiashara wadogo ambao ndiyo walipa kodi na mpunguze tozo ambazo zinawanyima usingizi Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)