Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema na leo hii kusimama hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya jambo la busara sana kukutana na wafanyabiashara ili kuwasikiliza kero zao, alizikuta kero zao ni kodi ya TRA kuwapandishia kwa muda mrefu na wafanyabiashara hao wakashindwa kulipa kodi hizo na wakafunga biashara zao na wengine wakaondoka katika nchi, Waziri siku zote hizo alikuwa hajaliona. Sasa hivi kasema biashara isifungwe mpaka apewe kibali, haya mapato ya Serikali yameshapotea kwa wingi ndiyo leo tunaamka na siku zote Wapinzani walikuwa wakisema neno hilo lakini ilikuwa bado hamjatafakari, kupotea njia ndiyo kujua njia. Ahsante.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii kwa kweli bado haijampenda mnyonge, kwa sababu Rais wa Muungano anasema yeye ni Rais wa wanyonge lakini hii haijawapenda wanyonge. Nitazungumzia kuhusu nguo za mitumba. Nchi yetu asilimia 80 wavaa mitumba hawawezi kuvaa nguo mpya kwa unyonge wao, leo mnawapandishia kodi kutokea asilimia 25 mpaka 35 kwa nini? Waziri nakuomba chondechonde hizi asilimia 10 uziondoe ili wanyonge wapate kuvaa nguo za mitumba ili wasitirike, nakuomba.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kuhusu Dodoma. Serikali yetu imeipandisha hadhi Dodoma inakuwa Jiji la Dodoma na ndiyo Makao Makuu lakini bado ilikuwa haijajipanga vizuri.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mgeni weka vizuri hiyo Microphone yako ili kumbukumbu zisikike vizuri, hapo nimezima nakuelekeza wewe uiweke vizuri isimame karibu na kinywa chako.
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Serikali haijajipanga kwa sababu haiwezekani Makao Makuu ya nchi mpaka leo hii ikawa bado hawajaweka mtambo wa kuchapishia magazeti. Magazeti mpaka yatoke Dar es Salaam ndiyo yafike hapa ni kwa nini? Kwa hivyo jipangeni mkianza kufanya mambo ili mambo yote yaendane kwa sababu hapa ndiyo kitovu cha nchi, panapotungwa sheria, kwa hiyo leo mpaka gazeti litoke Dar es salaam lije hapa?(Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nataka kuzungumzia ni kuhusu Zanzibar. Serikali ya Muungano ni pamoja na Serikali ya Zanzibar ndiyo ikaitwa Muungano. Sehemu ya Serikali ya Muungano ni pamoja na Zanzibar ndiyo ikaitwa Muungano ni sawa lakini bado Muungano haujaitendea haki Zanzibar. Kwa sababu haiwezekani Kitabu cha Bajeti kuanzia ukurasa wa 25 mpaka 35 zote zinajenga Tanzania Bara wakati Tanzania Visiwani nayo inayo haki katika Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi Waziri wa Fedha wa Zanzibar alipohitimisha bajeti yake ya fedha alisema kuwa kuna miradi mitatu imeshindwa kutekelezeka kwa sababu Serikali ya Muungano hawajaweka saini na miradi mitatu hiyo kwanza ni barabara inayotoka Mkoani kwenda Chakechake, kilometa 40, vilevile akazungumzia kuhusu gati ya Mpigaduri.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Zanzibar uchumi wetu ni bandari, uchumi wetu ni biashara Airport leo bandari ile ni nyembamba sana ikiingia meli moja tu inaweza kupakua mizigo kwa muda wa wiki nne haiwezi kuingia meli nyingine. Meli nyingine zinakuja inabidi zipindishe zikateremshe mizigo katika nchi jirani ya Kenya bandari ya Mombasa. Kwa hivyo, tukasema tutengenezeeni bandari ya Mpigaduri ili tuweze kufanikiwa lakini wameshindwa kutia saini, ni kwa nini? Hapo kweli Muungano mnautendea haki?(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikizungumzia Airport ya Chakechake sasa ni mwaka mzima, mashine ya ukaguzi haifanyikazi. Haifanyi kazi ukipita pale mizigo inabopabopa kama mafenesi au wewe mwenyewe, mpaka madawa ya kulevya yanaweza yakapitishwa kwa sababu hapana usalama katika Airport hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, jingine nazungumzie kuhusu Bandari ya Wete. Juzi niliuliza swali nikaambiwa pesa zimetengwa, itatengenezwa na mwenzangu amezungumzia hapa lakini hakuna kinachoendelea, kwa hivyo tunaiomba Zanzibar siyo wana wa kambo, tupo nasi katika sehemu ya Muungano, yaliyo ya Muungano tuyaaingize kwenye Muungano, yasiyokuwa ya Muungano basi tutafanya wenyewe lakini isiwe kutuonea.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Bandari ya Wete…
NAIBU SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa, ahsante sana.
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)