Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Kiza Hussein Mayeye

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uzima na afya na kuweza kuchangia katika bajeti hii muhimu ya Serikali. Naomba nianze na kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha Dkt. Mpango pamoja na Naibu Waziri wake Dkt. Kijaji kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeisikia bajeti lakini nimepata fursa ya kuisoma. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha na jopo lake kwa kuyafanyia kazi baadhi ya mambo. Niwapongeze sana kwanza kwa kuondoa tozo ya uchenjuaji madini, kwa hili niseme Mheshimiwa Waziri umesaidia sana sekta ya madini kwani kwa uchenjuaji kufanyika hapa hapa nchini kwetu itasaidia sana kuleta ajira hapa hapa nchini, tofauti na awali ambapo madini kama ya Tanzanite yalikuwa yakipelekwa nje kama India kwa ajili ya uchenjuaji ambapo tulikuwa tukipoteza ajira lakini fursa nyingi kwa nchi yetu. Pamoja na mazuri haya ya kuondoa tozo mbalimbali ikiwemo tozo ya kila mwezi ya visima (maji) bado kuna mambo ningependa kumshauri Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la taulo za kike (pads). Kama kuna jambo Mheshimiwa Waziri naomba nichukulie na kukuomba leo basi ni suala la VAT katika taulo hizi za kike. Mimi ni mtoto wa kike naelewa changamoto zinazopatikana katika kipindi cha hedhi. Mimi nakaa na wanafunzi wa kike, naona, najua shida wanayoipata pindi tu wanapoingia katika siku zao. Mtoto huyu wa kike kila mwezi anapoteza takribani wiki nzima ya kutuingia darasani kutokana na kushindwa kwenda shule kwa kuwa tu anaohofia kuchafuka na kuonekana awapo shuleni na ni kwa sababu tu hana taulo ya uhakika ya kujihifadhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, taulo hizi za kike ziweze kuingizwa bila VAT ili kurahisisha upatikanaji wa taulo hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, huko vijijini hali ni mbaya, watoto wa kike kuna maeneo ambayo wanatumia mpaka majani kutokana na uwezo wao kuwa duni, maisha ya wananchi ni masikini, mzazi hawezi kununua pads hizi kwa bei iliyopo. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri acha kumbukumbu kwa watoto wa kike katika uongozi wako, wasaidieni taulo hizi zipatikane kwa urahisi; hivyo hakuna budi kuondoa VAT ili taulo hizi zipatikane kwa wingi vijijini na mijini na utakuwa umemsaidia sana mtoto wa kike aliyepo hata kule kwetu Kigoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la uwekezaji katika nchi zetu zilizoendelea. Suala la uwekezaji ni muhimu sana sana. Sasa Mheshimiwa Waziri niombe Serikali yetu ipeleke pesa katika uwekezaji wote uliofanyika nchini. Kwa wakati miradi ya umeme wa Mto Rufiji Mradi wa Standard Gauge na bandari zote, kwa miradi hii kukamilika tutaweza kupiga hatua kama nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la uwekezaji niombe sana Mheshimiwa Waziri, ni lazima watu wa TRA watengeneze mazingira mazuri na wafanyabiashara ni lazima tuwakaribishe na kuwapa fursa wawekezaji binafsi.

Tumeona wananchi wakilalamikia hali ya biashara kuwa ngumu na tuhuma zikienda kwa TRA; hata namna ya ukusanyaji kodi na hasa wafanyabiashara wengine wamefikia kufunga biashara. Nimuombe sana Mheshimiwa Waziri kwa hali yoyote ile Serikali yetu ihakikishe tuna encourage wawekezaji kwani kwa kufanya hivyo tutaongeza ajira za kutosha na mapato pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nizungumzie suala la malipo. Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango wafanyakazi hasa walimu wamekuwa wakicheleweshewa malipo mbalimbali. Niombe sana malipo kwa wafanyakazi yaweze kufanyika kwa wakati na madeni wanayodai Serikali basi waweze kupatiwa kwa wakati ahsante.