Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Raphael Michael Japhary

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Naibu Spika, vitambulisho vya ujasiriamali; changamoto zake ni kama zifuatazo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, kupora mapato ya halmashauri kwa watu ambao wanatumia miundombinu ya masoko ya halmashauri. Mfano Manispaa ya Moshi kuna masoko matatu makubwa yaliyokuwa yanaipa halmashauri shilingi za Kitanzania takribani milioni mia tatu lakini wafanyabiashara/ wajasiriamali ambao wengine wana uwezo mkubwa wa mauzo ghafi ya zaidi ya shilingi milioni ishirini (20,000,000).

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Serikali Kuu imepoteza mapato kwa vile baadhi ya wafanyabiashara/ wajasiriamali waliokuwa wanalipa kodi ambao wana maduka madogo kama dawa, migahawa na mengine kama hayo wamejifunika kwenye vitambulisho. Ushauri wangu kwa Serikali ni kwamba ni muhimu sana kuangalia upya mpango huu wa vitambulisho vya wajasiriamali ili iweze kufanikisha nia njema ya Serikali ya kuwatambua wajasiriamali wadogo wadogo bila kuathiri mapato ya Serikali Kuu na mapato ya Serikali Kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tax base (wigo wa walipa kodi); hotuba ya mapendekezo ya bajeti inaonesha kwamba Serikali inategemea kukusanya trilioni 23.05 kwa mapato ya ndani ambapo trilioni 19.01 ni mapato yanayotokana na kodi, trilioni 3.18 mapato ya vyanzo visivyo vya kodi na bilioni 765.5 mapato ya halmashauri. Mashaka yangu kwa mapendekezo ya kiwango hicho cha makusanyo ya ndani hususani yanayotokana na kodi ni namna ambavyo Serikali itafikia malengo hayo wakati mwaka 2018/19 makusanyo kwa wastani wa kila mwezi ni trilioni 1.2 ambapo wafanyabiashara wamekamuliwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia TRA lazima ipanue tax base ya nchi ili utafutaji wetu wa kodi usiwaumize wafanyabiashara wachache kiasi kwamba inawafanya washindwe biashara. Kwa mfano, Watanzania walipa kodi hawazidi 2,700,000 ambapo waliosajiliwa kwenye VAT hawazidi milioni moja (1,000,000). Kwa taifa ambalo lina watu zaidi ya milioni 55, mzigo huu ni mzito sana kwa hao Watanzania 2,700,000 ambao wamekuwa wakibeba jukumu hilo kila siku la kuzalisha fedha kwa ajili ya kundi lote la Watanzania. Nashauri Serikali iyatazame kwa karibu makundi yafuatayo ili yachangie kwa usahihi katika makusanyo ya kodi:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, kundi la wakulima wakubwa na wa kati ambapo mpaka sasa hawajaratibiwa vizuri ili kushiriki katika wajibu wao wa kulipa kodi. Mpaka leo katika nchi yetu kundi la wakulima linawekwa katika daraja moja bila kutenganisha wakulima wakubwa na wakulima wa kati. Eneo hili linaficha watu wengi, zaidi ya asilimia tano ya wakulima ambao ni wakubwa na wa kati lakini hawalipi kodi lakini wanamiliki utajiri mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kundi la wafugaji wakubwa na wa kati. Kundi hili lazima liratibiwe vizuri ili lilipe kodi. Mwananchi anapomiliki ng’ombe zaidi ya mia moja anapaswa kuingizwa kwenye mfumo rasmi wa kulipa kodi. Kundi hili linaharibu sana miundombinu ya nchi lakini halishiriki kikamilifu katika kulipa kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, kundi la watu wanaomiliki majengo makubwa na ya kati; mwananchi anamiliki ambayo ameweka wapangaji lakini hajaratibiwa vizuri katika kulipa kodi. Kundi hili ambalo ni kubwa la watu wenye kipato cha kati limeachwa nyuma sana kwenye kulipa kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuongeza idadi ya wafanyakazi katika Mamlaka ya TRA. Serikali katika mapendekezo yake ya bajeti inaonesha kwamba itaongeza juhudi za kukusanya kodi. Naishauri Serikali iongeze idadi ya wafanyakazi wa TRA ili waweze kufikia walipa kodi wengi zaidi kadri inavyowezekana ili kupanua tax base yetu. Serikali inatakiwa itambue kwamba kuongeza wafanyakazi katika Mamlaka ya TRA ni uwekezaji kwa vile ni kwa dhamira ya kukusanya mapato zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa ukaguzi wa mahesabu unaofanywa na TRA kwa wafanyabiashara. Serikali lazima ipitie upya sheria inayoipa mamlaka TRA kufanya ukaguzi wa mahesabu ya mlipa kodi kila baada ya miezi mitatu mpaka mitano. Sheria hii imekuwa mwiba sana kwa wafanyabiashara kwa vile kuna ugumu wa kutunza kumbukumbu za biashara kwa miaka mitano. Pia kodi zinazopatikana baada ya ukaguzi wa TRA zinakuwa kubwa kiasi kwamba haziakisi uwezo wa wafanyabiashara, hivyo kupelekea kufungwa na kufilisika kwa wafanyabiashara. Nashauri Serikali ibadilishe muda wa ukaguzi uwe kwa kipindi kisichozidi miaka miwili kwa TRA kufanya ukaguzi wa mahesabu kwa wafanyabiashara ili kuwafanya wafanyabiashara wanapokutwa na malimbikizo, riba na faini waweze kulipa kwa kiasi kidogo kuliko malimbikizo ya miaka mitano.

Mheshimiwa Naibu Spika, muda wa kulipa malimbikizo na faini uwe mrefu wa kutosha. Nashauri Serikali ipitie upya utaratibu wake kuhusu muda ambao mlipa kodi anatakiwa kulipa malimbikizo, riba na faini baada ya ukaguzi wa TRA. Muda wa miezi mitatu kwa awamu tatu unaokubalika kikanuni za TRA unakuwa siyo rafiki kwa walipa kodi kwa vile kama kiasi cha malipo kitakachopatikana baada ya ukaguzi kinakuwa kikubwa inakuwa ni vigumu kwa mlipa kodi kutekeleza. Nashauri muda wa kulipa hayo malimbikizo, riba na faini uwe muda usiopungua miezi 12 na usiopungua miezi 24. Muda huo utafanya mlipa kodi kulipa kwa awamu 12 au 24 kwa kila mwezi kulipa installment moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, vyanzo vya mapato ya halmashauri; Serikali lazima itazame upya uamuzi wake wa kuchukua vyanzo vya halmashauri kwa sababu zifuatazo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, miradi midogo ya elimu, afya na huduma nyingine za jamii imekuwa ikitekelezwa na halmashauri hivyo kuipa nafasi Serikali Kuu kutekeleza miradi mikubwa. Ni vizuri halmashauri ziimarishwe zaidi ili ziweze kuisaidia Serikali Kuu majukumu ya maeneo ya chini ambayo ndiyo yana wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, TRA haina wafanyakazi wa kutosha kufikia vyanzo vyote vya kodi, hivyo, kwa kutumia halmashauri wanakuwa wamepata msaada mkubwa sana. Kwa maoni yangu, mpaka sasa bado TRA haijaweza kukusanya kikamilifu vyanzo vikubwa ilivyonavyo. Nashauri Serikali iimarishe uwezo wa halmashauri ili ziwe na uwezo wa kukusanya kwa ukamilifu mapato yake.