Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee, nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi zake kubwa sana kuleta maendeleo ya Watanzania. Awamu hii ya Tano wananchi wameweza kuona utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo iliyosimamiwa na Serikali kupitia usimamizi bora wa fedha za ndani. Watanzania kwa ujumla wameanza kufahamu umuhimu wa ulipaji kodi na athari zitokanazo na kutolipa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaiomba Serikali iendelee kutoa elimu kwa walipa kodi kupitia vyombo mbalimbali na kuchukuliwa hatua za kinidhamu wakwepaji kodi. Pia usimamizi zaidi wa fedha uimarishwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iendelee kusimamia wafanyabiashara ambao bado wanaendelea kutumia risiti za mkono na kukwepa matumizi ya risiti za kielektroniki. Kumekuwa na baadhi ya wafanyabiashara huwalazimisha wanunuzi kulipa bei ndogo bila risiti za kielektroniki na bei kubwa kwa risiti, hivyo, malengo ya makusanyo ya fedha kutokufikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti iliyopita tumeweza kuona upungufu katika fedha iliyopangwa kutolewa na wafadhili katika miradi ya maendeleo na kusababisha baadhi ya miradi kutokukamilika. Naiomba Serikali kutekeleza mpango wake madhubuti wa ushirikiano wa wadau wa maendeleo ili kuendelea kupokea misaada na mikopo kwani bado hatujaweza kusimama wenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, vipaumbele; pamoja na vipaumbele vilivyoainishwa katika bajeti hii ambapo njia na vyanzo muhimu vya mapato ya Serikali nashauri:-
(1) Kilimo na mifugo viongezewe fedha zaidi ili kuimarisha mapato zaidi ya Serikali.
(2) Utafiti uboreshwe kwa kutengewa fedha ya kutosha.
(3) Uvuvi wa Bahari Kuu uainishwe katika vipaumbele vya bajeti kwani tunapoteza rasilimali nyingi sana wakiwemo samaki kupitia meli za nje wanazovua katika mipaka yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali kuangalia namna itakavyowezekana kuhusu baadhi ya sheria ambazo zinatofautiana na Zanzibar na kuleta vikwazo kwa wananchi na wafanyabiashara wa Zanzibar na kwingineko nchini. Utaratibu bora ufanyike ili kuwawekea mazingira mazuri ya kibiashara na kuondoa kero zisizokuwa za lazima kila mara.
Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunaamini na kutambua kwamba biashara ndiyo miongoni mwa vyanzo vikuu vya mapato ya Serikali. Juhudi za Mheshimiwa Rais kukutana na baadhi ya wafanyabiashara tunaendelea kuzipongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo machache, naunga mkono hoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kusamehe jumla ya shs. 22 billion za Kodi ya Ongezeko la Thamani kupitia umeme unaonunuliwa na Shirika la ZECO Zanzibar. Kitendo hiki kimewatia moyo sana wananchi wa Zanzibar. Naiomba Serikali iendelee kutatua baadhi ya kero zinazowaletea adha wananchi kadri pale uwezo utakaporuhusu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo, niendelee kuipongeza Serikali kwa kuondoa tozo mbalimbali zilizokuwa zinakwaza wananchi. Ni ushahidi tosha kwamba Serikali yetu ni sikivu na inajali wananchi wake. Hongera sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Mgufuli, hakika wewe ni mtetezi wa wanyonge.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali kutilia nguvu suala la utafiti ili kukuza na kupanua uchumi katika nyanja mbalimbali kwa uhakika.