Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Maria Ndilla Kangoye

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuchangia kwa maandishi. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kunipatia pumzi kwa siku nyingine tena. Nampongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango na Naibu Waziri wake, Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kumshauri Mheshimiwa Rais kwa roho ya kizalendo kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa sijatenda haki kama sikumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanyia nchi yetu na wananchi kwa ujumla. Ameleta mabadiliko makubwa ya kimaendeleo kiasi kwamba nikianza kuorodhesha hapa kurasa hizi hazitatosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge limepokea mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2019/2020. Hakika taarifa imekaa vyema kabisa na hili nazidi kuipongeza Wizara.

Mheshimiwa Naibu Spika, mara zote wananchi wamekuwa wakiguswa siku zote kupitia tozo katika mafuta na hata vinywaji lakini leo hii tunaona unafuu mkubwa uliowekwa katika hotuba hii. Tunashuhudia mapendekezo ya kufutwa kwa kodi na tozo nyingi na kuleta unafuu wa kuendeleza biashara nchini. Kwa kweli bajeti hii italeta unafuu mkubwa sana kwa wananchi, naweza sema ni bajeti ya wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kuhusu Suala la Taulo za Kike; kama Wizara ilivyoeleza katika hotuba yake, inakusudia kufuta VAT iliyokuwa imesamehewa kwa kuwa haikuwa na tija katika kushusha bei za taulo za kike kama Serikali ilivyotegemea. Ni kweli ndivyo ilivyokuwa na siwezi kuilaumu Serikali kwa kuja na wazo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami nipendekeze kwamba kwa kuwa Serikali ilikuwa tayari kufuta kodi hiyo ili wanafunzi na wanawake wa hali ya chini kiuchumi waweze kunufaika kwa kupata nyenzo salama kipindi cha hedhi, basi itafakari upya katika suala hili na kama ikiwezekana taulo hizi zianze kutolewa bure katika shule kwa kupitia mpango wa ku-ring- fence ile VAT ya 18% itakayotozwa kutoka kwenye taulo za kike.

Mheshimiwa Naibu Spika, nazidi kuisisitiza Serikali kwamba ni kweli utoaji wa taulo hizi (kwa kuanzia katika shule) utanyanyua sana jinsia ya kike kielimu na kiafya. Ni imani yangu hili halitashindikana kutokana na Serikali, kupitia ruzuku za shule, yaani 10,000/= kwa kichwa imekuwa ikielekeza kiasi kwa ajili ya mahitaji muhimu ya mtoto wa kike. Hii inaleta picha nzuri ya namna gani Serikali tayari ina mpango huo wa kumsaidia mtoto wa kike katika mpango wa elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa ni kwamba fedha hii imekuwa haitoshi kununua taulo hizo kwa ajili ya wanafunzi wa kike. Malalamiko mengi yamekuwa yakielekezwa Serikalini kwa kutotoa fedha hiyo kikamilifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali kuiangalia upya ruzuku hii ili ifikie kiwango kitakachotekeleza mchanganuo, ya 10,000/= kwa kila kichwa cha mwanafunzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika upande wa taulo za kike, naendelea kuipongeza Serikali kwa msamaha wa corporate tax ambayo inasamehewa kwa viwanda vipya. Hii inaonesha ni namna gani Serikali ina mpango wa kukuza uwekezaji katika sekta hii. Kwa kuzingatia hilo, naleta ombi maalum kwa Wizara kusamehe VAT – Ushuru wa Forodha bandarini katika malighafi za taulo za kike zinazotumika zaidi ya mara moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni muda sasa Serikali imekuwa ikisamehe ushuru wa forodha bandarini kwa bidhaa za aina ya taulo za kike pamoja na malighafi za taulo hizo zinazotumika mara moja na kutupwa ilhali malighafi za taulo zinazotumika zaidi ya mara moja zimekuwa zikitozwa kodi hiyo. Ni ombi langu Serikali iliangalie hili kwa ukaribu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali ina mpango wa kuanzisha programu ya Universal Health Insurance kwa miaka ijayo, basi naishauri kutumia fursa hiyo kuona uwezekano wa kutoa taulo za kike walau za kutumika zaidi ya mara moja (reusable sanitary pads) ili kupunguza maradhi na magonjwa yatokanayo na hedhi zisizo salama kwa kukosa nyenzo salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii ya kuchangia. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.