Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kondoa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetufikisha katika hatua hii asubuhi hii ya leo ikiwa ni kuhitimisha hotuba ya bajeti ya nne ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba pia niwashukuru sana wazazi wangu wawili kwa kuendelea kuniweka kwenye maombi mtoto wao ili niweze kuwatumikia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuendelea kuniamini kwa mwaka wa nne huu nikiwa ndani ya Wizara ya Fedha na Mipango, hakika imani hii ni kubwa kwangu na naomba kumhakikishia kwamba sitamuangusha yeye wala Wanakondoa walioniamini kunileta katika Bunge hili tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba pia nikushukuru sana wewe kama kiongozi wa Bunge hili Tukufu kwa jinsi unavyoliendesha Bunge hili kwa viwango na kwa jinsi ambavyo upo imara kusimamia maendeleo ya Taifa letu. Nikushukuru sana ukiwa kama kaka yangu kutoka Mkoa wa Dodoma kwa miongozo na malezi yako kwangu hakika unaendelea kunijenga. Nakushukuru sana na nakuombea kwa Mwenyezi Mungu baraka tele na afya njema. Ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba pia shukrani hizi nizielekeze kwa kiongozi wetu wa Serikali ndani ya Bunge lako Tukufu Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa kwa miongozo na maelekezo yake anayoendelea kutupatia kama Wizara na kama Serikali. Nina hakika Watanzania wanaiona kazi nzuri unayoifanya Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mwenyezi Mungu aendelee kukujalia busara na afya njema ili uendelee kuwatumikia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba pia nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, kwangu mimi kufanya kazi na huyu Mheshimiwa Waziri ni fursa kubwa sana, najifunza mengi, mazuri kutoka kwake. Hakika naendelea kuwa mwanafunzi mzuri kwake na namwahidi kuendelea kuwa msaidizi wakw wa karibu ili aweze kutekeleza majukumu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia niwashukuru sana familia yangu, mume wangu Dkt. Muhajiri Kachwamba na rafiki yangu wa karibu kwa miaka 20 sasa. Hakika nafasi aliyonipa ni kubwa sana kwenye maisha yake na mchango wake kwenye mafanikio yangu ni mkubwa sana. Namshukuru sana kwa kuendelea kuniamini, kuendelea kunisaidia niweze kutenda majukumu yangu. Kwa watoto wangu pia nawashukuru sana, najua wamekuja likizo, lakini mama anarudi saa tano, saa sita usiku wanaendelea kunivumilia, nasema waendelee kunivumilia kwa sababu niliiomba nafasi ya kuwatumikia Watanzania na nimeipata nafasi hii waendelee kunivumilia, nitarejea kukaa nao pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, shukrani zangu za mwisho lakini si kwa umuhimu, ni kwa wapiga kura wangu wa Jimbo la Kondoa, hakika waliniamini mwaka 2015, wakiwa wananijua kidogo sana, lakini sasa wamenijua kwa utendaji wa kazi katika Jimbo la Kondoa, lakini kwa kuwatumikia Watanzania. Naomba niwaambie Watanzania, Wanakondoa kwamba, sitawaangusha, nitaendelea kulisimamia Jimbo la Kondoa, liko imara na nawahakikishia Chama cha Mapinduzi mwaka 2019 Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa tutashinda kwa asilimia 100 na mwaka 2020, mimi Mbunge wao nitarejea ndani ya Bunge hili kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sasa nianze kuchangia hotuba hii iliyowekwa mezani na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango na naomba nianze kwa kulisemea jambo la biashara, hali ya biashara ndani ya Taifa letu, ambalo yalisemwa maneno makali sana dhidi ya Waziri wa Fedha na Mipango, dhidi yangu mimi msaidizi wake kwamba sisi tunashangilia ufungwaji wa biashara ndani ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, tukaambiwa, Kariakoo imekufa kwa sababu ya Waziri wa Fedha na Mipango na Naibu wake kwa sababu tumeshindwa kusimamia. Pia ikasemwa kwamba, kwa nini tumechelewa kufanya maamuzi ya kuzuia ufungaji wa biashara, hadi mwaka wa nne ndiyo Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango anakuja kuzuia ufungaji wa biashara.
Mheshimiwa Spika, naomba kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, kuanzia hotuba ya bajeti ya mwaka wa kwanza, Mheshimiwa wa Fedha aliyewasilisha ndani ya Bunge lako tukufu, mwaka 2016/2017, aliwaelekeza watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, ni marufuku kufunga biashara ya mfanyabiashara yeyote yule bila kufuata utaratibu na sheria zinazowaelekeza hivyo.
Mheshimiwa Spika, mambo hayo yalisemwa ndani ya Bunge lako Tukufu, kwa hiyo kuja leo kumlaumu Mheshimiwa Waziri wa Fedha, siyo sahihi hata kidogo na amechukua jitihada za kutosha Mheshimiwa Waziri wa Fedha kuhakikisha biashara hazifungwi kwa sababu tu ni watumishi wa Mamlaka ya Mapato wanataka kufunga, hapana, zipo sheria zinazowaelekeza kufanya hivyo.
Mheshimiwa Spika, lakini niseme jambo la pili, katika soko huria, moja ya sifa za uchumi wa soko huria ni uhuru wa kuanzisha biashara na uhuru wa kufunga biashara, yaani tunasema kuna free entry and exit from the market. Kwa hiyo, tukiangalia sana wengi waliofunga biashara siyo kwa sababu wamelazimishwa kufunga biashara na watumishi wetu wala na viongozi wa Serikali yetu wala na Waziri wa Fedha na Mipango.
Mheshimiwa Spika, kwenye uchumi wa soko huria ambao Taifa letu lipo, ifahamike kwamba biashara pia zinaweza kufungwa kwa sababu mbalimbali. Sababu ya kwanza, yaweza kuwa ni kubadilisha aina ya biashara, mfanyabiashara ambayo amekuwa akiifanya, lakini pia yaweza kuwa kwa sababu ya ushindani mkali katika biashara husika, hiyo inaweza kupelekea pia mfanyabiashara akabadilisha biashara yake. Vile vile yawezekana, ni kushindwa kuisimamia biashara yake husika, lakini yawezekana pia biashara ambayo wamekuwa wakiifanya, walikuwa kwenye shareholding na wameshindwa kuelewana, wanaamua kui-dissolve biashara yao ili waweze kufanya biashara nyingine.
Mheshimiwa Spika, katika sababu hizi, haijaachwa nje pia hata sababu ya kwamba mfanyabiashara huyu ana mzigo mkubwa wa madeni, aidha kwenye benki za biashara au kwenye taasisi zozote za kibenki, lakini pia hata yawezekana ana madeni ya kikodi na kama tunavyofahamu, kodi hukusanywa kwa kufuata sheria.
Mheshimiwa Spika, hizi zaweza kuwa ni sababu zilizopelekea baadhi ya biashara kufungwa. Nipende kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, zipo tafiti ambazo zimefanyika duniani na zote zikabainisha kwamba, zaidi ya asilimia 50 ya biashara za ukubwa wa kati na ukubwa mdogo, hufa kabla ya kusherekea birthday yao ya mwaka wa tano. Kwa hiyo, yawezekana hii pia ikawa ni hali ile ya kawaida ya biashara hizi za saizi ya kati na saizi ya ukubwa mdogo ambazo zinaweza kuwa zinakufa ni kwa sababu ya sababu hizi nilizozitaja na hii si kwa Tanzania tu, hii ni kwa dunia nzima kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge, kwamba, nilituhumiwa pia kwamba nimekuwa nikijisifu kwa kuzifunga biashara hizi ndani ya Taifa letu. Naomba nikiri ndani ya Bunge lako Tukufu, kitu ambacho nimekuwa nikikisimamia kama Naibu Waziri wa Fedha na Mipango ni kuhakikisha sheria zinafuatwa ndani ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, nikitoa mfano, wakati nachangia hotuba ya Viwanda na Biashara, liliongelewa sana tatizo la kufungwa kwa biashara na zikatolewa takwimu ambazo siyo sahihi ndani ya Bunge lako Tukufu. Ilinilazimu kueleza ukweli, kuwaeleza Watanzania, nini uhalisia ndani ya Taifa lao ili waweze kufahamu.
Mheshimiwa Spika, ukiniruhusu naombakunukuu nilichokisema. Siku ya tarehe 15 mwezi wa tano mwaka 2019 nilisema maneno yafuatayo:-
“Kwamba ni kweli zipo biashara zinazofungwa na zipo biashara zinazofunguliwa. Nikasema, kwa Tanzania kwa mwaka huu mmoja biashara zilizofungwa ni 16,252 na biashara zilizofunguliwa ni 147, 817.”
Mheshimiwa Spika, nililazimika kutoa takwimu hii kwa sababu ilihojiwa ndani ya bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara. Hata hivyo, siyo sahihi, tukiangalia takwimu hizi siyo sahihi kusema ndani ya Taifa letu biashara nyingi zinafungwa kuliko zinazofunguliwa. Kisayansi kinachotakiwa kufanyika, baada ya kujiridhisha na biashara zinazofungwa na kufunguliwa, ni kwenda kufanya utafiti sasa wa kisayansi, tuweze kujiridhisha biashara zinazofunguliwa ni za ukubwa gani, ni katika sekta zipi na sababu zipi zinazopelekea kufungwa kwa biashara hizi. Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Kitengo chake cha Utafiti na Sera kinaendelea kufanya utafiti huu ili tuweze kujiridhisha, nini kinasababisha biashara hizi kufungwa na ni zipi zinazofunguliwa na sababu zinazosababisha zifunguliwe ili tuweze kama Serikali kuzilea biashara hizi.
Mheshimiwa Spika, pia nilisema kwenye Bunge lako Tukufu siku hiyohiyo kwamba, ni muhimu tukajiuliza maswali, kama kweli yanayosemwa, tunayotaka kuamisha Watanzania, kwamba biashara nyingi zinafungwa kuliko zinazofunguliwa, nilihoji maneno yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, nilisema na leo naomba nirudie kuyahoji maswali haya; swali la kwanza nikasema; kama ni kweli biashara nyingi zinafungwa, je Serikali ingeweza wapi kuongeza ukusanyaji wa mapato tangu Serikali ya Awamu ya Tano imeingia madarakani, kwa mwezi kwa zaidi ya asilimia 75, kama biashara kweli zinafungwa? Tumetoka shilingi bilioni 870 kwa mwezi na sasa tunakusanya trilioni 1.3, kama biashara zinazofungwa ni nyingi zaidi kuliko zinazofunguliwa wapi tungeyapata mapato haya.
Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili la kujiuliza, kama kweli biashara nyingi ambazo ni chanzo kikubwa cha mapato ya Serikali yetu, Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi ya Awamu ya Tano, isingiweza kulipa mishahara ya watumishi wetu ndani ya tarehe 20 kila mwezi zaidi ya bilioni 580 kila mwezi, kama kweli chanzo hiki cha mapatao kimefungwa, wapi tunazipata fedha hizi.
Mheshimiwa Spika, vile vile nikasema, ni vizuri tukajiuliza, zaidi ya asilimia 85 ya bajeti iliyokwenda kwenye miradi ya maendeleo kwa mwaka huu wa fedha, ni fedha zetu wenyewe za ndani. Kama biashara zinafungwa, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli inatoa wapi fedha hizi kwenda kugharamia zaidi ya asilimia 85 ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa!
Mheshimiwa Spika, ni vizuri pia tukafahamu kwamba Wiraza ya Fedha na Mipango, hatuwezi kukaa kimya tunapoona watumishi wetu wanaendelea kuvunja sheria na hatuwezi kukataa, wapo baadhi ya watumishi wetu, ambao siyo waaminifu wakishirikiana pamoja na wafanyabiashara ambao siyo waaminifu kulinyima Taifa letu mapato. Hili hatuwezi kulivumilia, tunapogundua mfanyabiashara anakwepa kodi kwa makusudi, hatuwezi kulivumilia, kwa sababu tumeaminiwa ili kuhakikisha Taifa hili linapata mapato yake, lazima tusimame imara.
Mheshimiwa Spika, nitoe mfano mmoja wa jinsi tunavyoshughulikia, kwa mfano, kati ya mwezi Mei, 2017 hadi mwezi Aprili, 2019, zaidi ya watumishi 30 wa Mamlaka ya Mapato Tanzania walisimamishwa kazi kutokana na utovu wa nidhamu katika kazi zao za kila siku, hili hatuwezi kulivumilia, tutasimamia kwa watumishi wa Mamlaka ya Mapato, tutasimamia kwa wafanyabiashara ambao siyo waaminifu kuhakikisha kwamba biashara zinaendelea kufanywa, biashara halali kwa ajili ya mapato halali ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitoe mifano miwili ili tuweze kuelewa na Watanzania waielewe Serikali yao ya Chama cha Mapinduzi nini inataka. Tarehe 19 Aprili, nilipokea wageni ofisini kwangu, walikuwa ni vijana watatu wakiwa wametoka Mkoa wa Kagera na kutoka Mkoa wa Mwanza, wamekuja ofisini kwangu wakija kulalamika, wanakuja kulalamika kwamba wamepewa assessment kubwa ya kodi.
Mheshimiwa Spika, nilianza kuifuatilia ile kesi, nilipoifuatilia ile kesi yaliyojiri, ndiyo maana nasema, tunao baadhi ya watumishi wetu ambao siyo waaminifu na baadhi ya wafanyabiashara ambao siyo waaminifu. Kilichojiri, zilikuwa ni malori manne ya tani 10 yaliyobeba vitenge vilivyotoka China, maroli haya manne yalikuwa yametoka wapi, maroli manne haya yalikuwa yamepita Bandari ya Dar es Salaam yakiwa ni transit, ni mizigo inayokwenda nchi jirani. Malori yale yanaonekana yamepita mpaka katika mpaka wetu wa Mtukula, yalipopita Mtukula hayakwenda Uganda yakageuza kurudi Tanzania tena. Yalipofika mpakani tukawa tumepata taarifa hizi, yakasimamishwa, kuangalia hawana document hata moja inayoonyesha malori hayo yamekwenda Uganda na kwa nini yanarudi Tanzania.
Mheshimiwa Spika, kuja kufuatilia, tayari kuna mfumo, kati ya watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kutoka Bandari ya Dar es Salaam, Makao Makuu na mipaka yote mpaka yalipoingia Uganda. Walipokuja wale vijana, hawakuwa wenye mizigo, wale vijana waliokuja walikuwa ni madalali ambao wanakusanya kodi halali kutoka wa wafanyabiashara, lakini wao madalali wanalipa kiwango kidogo sana cha fedha waki-collude na watumishi wetu. Kwa jambo kama hili, hakika tumeaminiwa, lazima tulismamie, lazima walipe kodi na lazima mfanyabiashara wa aina hii kulingana na sheria, zile lori zote nne zilitaifishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hili lazima tulisimamie, kwa sababu tunahitaji mapato ili tuweze kuwahudumia Watanzania, kwenye afya zao, Watanzania kwenye shule zao na Watanzania kwenye, watoto wetu kulipiwa ada na Serikali yao.
Mheshimiwa Spika, kama hilo ndilo linalotafsiriwa, Ashatu anakuja kushangilia kufungwa kwa biashara, hilo naomba nimwambie Rais wangu, nitaendelea kusimamia. Hilo naomba niwaambie Watanzania, sitoruhusu waibiwe, nikiwa Naibu Waziri wa Fedha, sitofanya hivyo. Lazima nitasimama imara na kodi zote zitakusanywa kulingana na sheria tulizozipitisha ndani ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sasa niende kwenye hoja ya pili, hoja ya pili ambayo ningependa kuisema mbele ya Bunge lako tukufu, nikiwa nachangia hotuba hii ya Bajeti Kuu ya Serikali, ni kuhusu kufutwa kwa kodi ya ongezeko la thamani kwenye taulo za kike.
Mheshimiwa Spika, hata nisipo-declare interest mimi ni mwanamke, mimi ni mwanamke na mimi nina mchango wangu kwenye kila kinacholetwa na Waziri wa Fedha ndani ya Bunge lako Tukufu. Yameongelewa maneno magumu sana, ambapo, nikamwambia Mheshimiwa Waziri wa Fedha jambo hili naomba nilibebe mwenyewe. Naomba niwaeleze Watanzania, mimi nikiwa kama mwanamke, naijua adha hii na halipendezi hata kidogo Waheshimiwa Wabunge, naomba tu niseme, haipendezi hata kidogo kwa maneno aliyoelezwa Waziri wa Fedha ndani ya Bunge hili Tukufu na lazima tufahamu Waheshimiwa Wabunge, Waziri wa Fedha anapoleta hoja hapa ndani ya Bunge hili, inakuwa ni hoja ya Serikali, siyo hoja ya Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunapotoa tuhuma hizi, hasa zile ambazo ni personal attack, naomba tufahamu ana moyo, hakuondolewa nyongo Mheshimiwa Waziri wa Fedha, anaumia kama mwanadamu, lazima tujitafakari, lazma tuvae viatu vyake, lazima tujiulize ningekuwa ni mimi nikaelezwa maneno haya ningejisikiaje. Inakera na inaumiza, lakini naomba niwaambie Watanzania, dhamira ya Serikali yao ni njema sana. Kama ambavyo nimekuwa nikisema siku zote kwenye Bunge hili Tukufu, kodi ina mchango mdogo sana kwenye bei ya mwisho ya bidhaa. Hili limejidhihirisha, Bunge lako Tukufu kwa dhamira njema, kama ambavyo Serikali yetu ilileta ndani ya Bunge lako Tukufu, tulipitisha kuondolewa kwa kodi hii ya ongezeko la thamani kwenye taulo za kike.
Mheshimiwa Spika, yamesemwa maneno mengi sitaki kuyasikia, kwamba bajeti hii is gender insensitive! Nikasema nirudi pale ofisini kwangu nikaangalie, hivi ni kipi kinachosababisha bajeti ya Serikali, Serikali iliyoaminiwa na wananchi kuliongoza Taifa hili, kwamba iambiwe bajeti yake ni insensitive, hivi kweli, ni taulo ya kike ya Sh.2,500 tu! Nikajiuliza maswali mengi, nikarudi kuangalia what is gender budgeting. Gender budgeting haimaanishi item moja na item hii mchango wake ni upi katika uchumi wa mwanamke, katika uchumi wa Taifa.
Mheshimiwa Spika, nikarudi kikasema nianze na afya ya mwanamke, Serikali ya Awamu ya Tano imefanya nini, Serikali ya Awamu ya Tano imefanya makubwa kwenye afya ya mwanamke. Nikisema kwa mikoa michache, nikianza na vituo vya afya, hospitali za wilaya tulizojenga katika mikoa yetu, tunakwenda kum-target mwanamke. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikiongelea Mkoa wa Simiyu peke yake tumepeleka bilioni 4.5 kwa ajili ya kujenga hospitali kwenye halmashauri zake ili wanawake waweze kupata huduma bora za afya.
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Geita tumepeleka bilioni tatu; hii ni kwa mwaka mmoja tunaangalia afya ya mwanamke.
Mheshimiwa Spika, tukiichukua Kanda ya Ziwa yote tumepeleka kwa mwaka mmoja bilioni 22.5 kwa ajili ya afya ya Watanzania ambapo mtu wa kwanza tunayemwangalia ni mwanamke wa Kitanzania.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wanajua; katika vitabu vya Wizara ya TAMISEMI vya bajeti tulionesha nini tumepeleka. Serikali ya Chama cha Mapinduzi inamjali sana mwanamke, na sisi kwa pamoja tumekiri hapa mwanamke wa Tanzania akiwa kijiji, akiwa mjini ndiye anayelilisha taifa hili. Nikajiuliza sana, kwamba huyu Mwanamke anayelilisha taifa ndiye anashindwa kuwa na shilingi 3,000 kwa ajili ya kununua taulo ya kike kwa mwezi? Hili lazima tuliangalie katika uwanda mpana ili tuweze kuelewa kwa pamoja.
Mheshimiwa Spika, naomba niseme, baada ya kuwa tumeondoa kodi hii ya ongezeko la thamani kwenye taulo hizi za kike nini kimetokea; Serikali yetu haikukaa kimya tukasema tulifuatilie jambo hili, kwamba je, kuna athari yoyote iliyokwenda kwa wanawake? Ikafanywa study katika Wizara ya Viwanda na Biashara, Mamlaka ya Mapato Tanzania na Fair Competition Commission. Nini kilijiri mpaka leo tuje tuseme kwamba bajeti hii haikumuangalia mwanamke kwa jicho la pekee? Kilichojiri ni kwamba tuligundua kwamba kuondolewa kwa kodi hii; kwanza wanawake wengi hawajui kama kodi hi imeondolewa. Hili lilikuwa jambo la kwanza.
Mheshimiwa Spika, kwenye Bunge lako ikasemwa wapo kwamba watu walioalikwa mpaka mikutano ya kimataifa kwenda kupongezwa kwa ajili ya kuondolewa kwa kodi hii; unapongezwa kwa ajili ya jambo gani?
Mheshimiwa Spika, nilishaona watu wanapewa tuzo kwa ajili ya wanawake lakini unaulizwa umefanya nini kupewa tuzo hiyo? Unaitwa kwenda mataifa mbalimbali kwenda kupongezwa wakati ndani ya taifa lako hujasimama kuwaambia wanawake kwamba kodi hii imeondolewa kwa ajili yenu. Kwahiyo hili lazima tiliangalie kwa jicho pana ili tuweze kuelewa.
Mheshimiwa Spika, baada ya kujua wanawake wengi hawajui pia tukakuta jambo la pili. Kwamba athari iliyopatikana bei haijapungua kule ambako tulidhamiria bei ipungue. Bado taulo iliyouzwa shilingi 2,500 leo hii bado inauzwa shilingi 2,500, taulo iliyouzwa 5,000 bado leo hii inauzwa shilingi 5,000.
Mheshimiwa Spika, badaa ya kuondolewa kwa kodi hii nini kilitokea kwenye viwanda vyetu vya ndani? Kilichotokea kwa viwanda vyetu vya ndani ni viwanda vyetu vya ndani kupunguza uzalishaji wa bidhaa hii. tunapopunguza uzalishaji nini tunajifunza? Tukipunguza uzalishaji tunakwenda kuondoa ajira za vijana walioajiriwa kwenye viwanda hivi vya ndani. Hizi ni athari hasi baada ya kuondoa kodi hii ya ongezeko la thamani kwenye taulo za kike.
Mheshimiwa Spika, Serikali yetu haikuishia hapo; tukakaa chini tukatafakari nini cha kufanya? Tukasema jambo la la kwanza ni kuendelea kuodoa asilimia 10 ya import duty (ushuru wa forodha) kwenye mali ghafi zote zinazozaloisha taulo za kike. Hii iliondolewa tangu mwaka 2012, lakini ilisemwa kwenye Bunge hili kwamba haijaondolewa. Naomba niwaambie Watanzania tunawajali sana wanawake. Tuliondoa uhuru huu wa forodha wa asilimia 10 tangu mwaka 2012.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili tukasema; ukiangalia bidhaa hii ya taulo za kike ni bidhaa ya muhimu ambayo whether bei imepanda au haijapanda lazima itatumika tu. Unapokuwa na bidhaa ya namna hii wachumi tunaiita ni necessity goods, haiwezi kutibiwa kwa ajili ya measures za kikodi peke yake. Unapokuwa na bidhaa ya aina hii lazima uwe na measures za kikodi lpamoja na measures za kibajeti na measures nyingine za kiutawala ili uweze kuwasaidia hawa wanaotakiwa kutumia bidhaa hii.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi inamjali mwanamke wa Tanzania, baada ya kuondoa asilimia 10 ya ushuru wa forodha tukasema tunaondoa asilimia tano ya kodi ya mapato ya viwanda vipya vitakavyoanzishwa kwa ajili ya kutengeneza taulo hizi za kike.
Mheshimiwa Spika, hii tumeiondoa kwa muda wa mika miwili. Hata hivyo, Bunge lako Tukufu na Waheshimiwa Wabunge wakasema hii haitoshi na Serikali yenu ya Chama cha Mapinduzi inawasikiliza, imekubali kwamba tunaondoa tena asilimia tano kwa ajili ya kodi ya mapato kwa viwanda vya ndani vinavyozalisha bidhaa hii kwa miaka miwili mfululizo. Kwahiyo mwanzo tulisema viwanda vingine hatuna uhakika kama vitakuja lakini sasa tunaondoa kwa viwanda vya ndani ambavyo tayari vinazalisha, tunawapunguzia asilimia tano ili waweze kuionyesha kama ina athari hiyo.
Mheshimiwa Spika, nimsema measures za kikodi pake yake haziwezi kujibu jambo hili. Serikali yenu ya Chama cha Mapinduzi iliyoaminiwa na Watanzania tumekuja na suluhisho pia la aina nyingine, nayo ni kuanzishwa viwanda vinavyotumia PPP ambavyo vimefika kwenye hatua kubwa ambayo tunaamini ndani ya mwaka huu wa fedha viwanda hivyo vitakuwa vimekamilika.Ni kiwanda kinachojengwa katika Mkoa wa Simiyu ambacho kinajengwa na NHIF na kinajengwa na Workers compensation pale Bariadi-Simiyu ili kiweze kuzalisha taulo hizi za kike. Kitakapozalisha taulo hizi za kike kwa sababu Serikali ina mkono wake, Serikali sasa itakuwa na uwezo wa ku-control bei za bidhaa inayozalishwa na kiwanda hiki.
Mheshimiwa Spika, tukiweza ku-control bei nini maana yake; hata wazalishaji wengine sasa wakiona viwanda vyetu hivi vimezalisha bidhaa za kutosha nao watashusha bei. Hiyo ni Serikali ya Chama cha Mapinduzi ikiwa inawaangalia Watanzania wote kwa ujumla wake pamoja na kuangalia makundi mbalimbali ili yaweze kufanya majukumu yao ya kimaendeleo.
Mheshimiwa Spika, tukiacha kiwanda hiki cha Simiyu kuna kiwanda kingine kinajengwa Pwani. Kiwanda hiki kinajengwa Pwani na MSD ambao nao wako katika hatua ya mwisho na mkataba unasainiwa ndani ya siku hizi mbili. Ndani ya mwaka huu mmoja kiwanda hiki pia kitakuwa kimeanza kuzalisha bidhaa hii na hatimaye tutaiuza kwa bei ya chini na tutamfikia mwanamke kule alipo.
Mheshimiwa Spika, haya ndiyo ambayo tumesema tuyaseme kama Serikali kwa ajili ya bidhaa hii kwa kuwa sisi ni wasikivu tumesikia na tunakuja na suluhisho za aina tatu ili kiukweli tuweze kuwasaidia Watanzania.
Mheshimiwa Spika, naomba niseme jambo moja la mwisho nalo ni kuhusu miradi ya PPP, kwanini Serikali haitaki kutekeleza;
Mheshimiwa Spika, Serikali inalishukuru Bunge lako tukufu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Malizia Mheshimiwa Waziri, dakika moja.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, Serikali inalishukuru Bunge lako Tukufu kwa kuwa iliruhusu kufanya mabadiliko kwenye Sheria ya PPP na tukisoma kwenye mipango yetu ya maendeleo, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na pia Mpango wa Maendeleo wa Mwaka Mmoja, Serikali iko tayari kushirikiana na wadau binafsi katika kuwekeza kwenye maeneo muhimu kwa ajili ya uchumi wa taifa letu.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya naomba niseme naunga mkono hoja na nashukuru kwa kunipa fursa hii.