Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Allan Joseph Kiula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Spika nashukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hotuba hii ya Waziri Mkuu. Nashukuru sana kwa sababu nakuwa mchangiaji wa kwanza na hili Bunge ni muhimu kwa sababu sasa tunamaliza miaka mitano.

Mheshimiwa Spika, cha pili, nampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano; na Waziri Mkuu alipokuwa anatupitisha kwenye hotuba yake, alikuwa anatembea kwenye kazi ambazo zimefanyika. Ni kazi ambazo unaweza ukaziona kwa macho, ukazigusa na ukapapasa. Kwa hiyo, hayo siyo maneno matupu ila kazi zilizofanyika. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, napongeza Viongozi Wakuu wa Serikali akiwepo Makamu wa Rais. Vile vile siyo kwa umuhimu, lakini nikupongeze wewe Mheshimiwa Spika kwa kutuongoza kwa miaka mitano. Mambo mengi mazuri yamefanyika na mambo makubwa yamefanyika. Hili linalozungumzwa “Bunge Mtandao” watu waliona haliwezekani, lakini leo hii hata sisi tulikuwa tunafikiri Bunge baada ya Corona tutaendanalo vipi? Sasa jinsi ulivyolipima na kuliratibu Spika, basi umekuwa Spika mahiri sana. Nakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizi, naanza kwa kuunga mkono hoja iliyowekwa mbele yetu. Yako mambo ambayo ningependa kuyazungumza kidogo, kutokana na mazingira tuliyonayo sasa hivi na angalizo langu liko kwenye suala la mapato; tuna sehemu ya matumizi na mapato. Leo hii wakati hotuba hii imesomwa, tuna changamoto ya ugonjwa huu, janga la Corona ambalo janga hili limefanya sekta nyingi zisimame au zisifanye kazi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, pamoja na kwamba tunapitisha bajeti hii, nashauri sana Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara zinazofuata, pesa tutakazopelekewa wazitumie kwenye maeneo muhimu kwa sababu hatuna uhakika kama flow ya hizo pesa itaendelea hivi, kwa sababu mchango wa sekta mbalimbali za kiuchumi ikiwepo utalii, madini na sehemu nyingine tunaona kwamba zinaathirika na hili janga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya angalizo hilo nampongeza Mheshimiwa Rais kwa hatua alizochukua za suala nzima la kuangalia namna ya kudhibiti janga hili la Corona. Jambo la muhimu hapa ni usimamizi; tunasimamia vipi hizo hatua ambazo tumejiwekea sisi wenyewe? Hilo ni jambo muhimu sana, maana hii social distancing inatupa shida kidogo, lakini ni utamaduni ambao tunatakiwa tuuchukue.

Mheshimiwa Spika, tukifuatilia hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu, yako mambo mengi yamezungumzwa, kazi nyingi zimefanyika, zile nguzo kuu za uchumi ambayo ndiyo mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano zimeelezwa kikamilifu na hatua ambazo tumefikia. Sasa pamoja na mafanikio tuliyoyapata, tukienda kwenye suala la miundombinu; ujenzi wa reli ya mwendo kasi na maeneo mengine, kwa sababu Ofisi ya Waziri Mkuu inaratibu, basi zile rasilimali inatakiwa zisimamiwe kikamilifu ili miradi hiyo isiweze kuathirika na hali inavyoendelea sasa hivi. Nazungumza hali ya kiuchumi inavyoendelea.

Mheshimiwa Spika, Sekta mbalimbali zimegusiwa katika hotuba hii. Nikigusa Sekta ya Kilimo, Sekta ya Kilimo ni sekta muhimu sana. Kwa hiyo, tunamba Ofisi ya Waziri Mkuu ikaratibu Sekta ya Kilimo lakini imtambue mkulima mdogo, pia twende mpaka chini tumwangalie mkulima mdogo tuone tunamsaidia vipi? Kwa sababu tunapozungumza viwanda, malighafi zinatoka huko chini kwa wakulima wadogo wadogo ambao ni wengi. Kwa hiyo, ni jambo muhimu sana. Tunashauri jicho la karibu liweze kutupiwa huko.

Mheshimiwa Spika, tukienda kwenye Sekta ya Elimu, mambo makubwa yamefanyika na mafanikio makubwa yameweza kufanyika. Yapo mambo kadhaa ambayo inabidi yaangaliwe kwa karibu. Elimu bila ada imekwenda vizuri sana isipokuwa tumekuwa na changamoto ya miundombinu kwa maana ya madarasa, nyumba za walimu na walimu wenyewe. Kwa hiyo, ni eneo ambalo linatakiwa liangaliwe kwa karibu sana kwa maana ya uratibu. Wizara husika inafanya kazi vizuri, lakini eneo hilo linatakiwa liangaliwe vizuri likiwepo suala nzima la uratibu wa mikopo ya elimu ya juu. Hilo ni jambo muhimu pia.

Mheshimiwa Spika, Sekta ya Maji na yenyewe inahitaji kuangaliwa kwa karibu sana. Takwimu zimetolewa hapa zinaonyesha tunapiga hatua nzuri na tunaipongeza Serikali kwa hatua inazochukua na kwa uwekezaji mkubwa unaofanyika kwenye Sekta ya Maji, isipokuwa bado uko umuhimu wa kuhakikisha kwamba rasilimali kwenye Sekta ya Maji zinaongezeka hili tatizo hili liweze kutatuliwa. Tumeona kwamba maji vijijini sasa hivi ni asilimia 64, kwa hiyo, tunatarajia kwamba asilimia hiyo iweze kuongezeka kupitia huo Mfuko wa Maji.

Mheshimiwa Spika, miundombinu imezungumziwa. Atakuja Waziri mhusika kuzungumza habari ya miundombinu hapa, ninachokiona, mwaka huu tumepata mvua nyingi. Mvua hizo zimeharibu sana miundombinu kama barabara na madaraja. Kwa hiyo, chochote ambacho tutakuwa tumekipanga hapa kitakwenda kwenye miundombinu, lakini hakitakwenda kwenye kutengeneza miundombinu mipya, itakwenda kwenye kukarabati miundombinu hii. Kwa mfano, daraja la Kiyegeya halikuwepo kwenye mpango, lakini sas limeshatumia rasilimali kubwa. Kwa hiyo, suala hilo na lenyewe inabidi liangaliwe kwa ukaribu tuweze kuona tunasonga mbele vipi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesema suala nzima la ukusanywaji wa mapato, sasa ni muda muafaka kabisa kupanua wigo lakini na Halmashauri zetu kuziwezesha. Siku za nyuma katika bajeti zilizopita, Halmashauri ziliombwa ziandike miradi ya mikakati; jambo hilo lilikwenda baadaye likasimama kidogo, lakini tunaiomba Ofisi ya Waziri Mkuu iweze kusimamia hilo jambo hili Halmashauri ziwe na hiyo miradi ya kimkakati ili ziweze kuzalisha mapato zaidi.

Mheshimiwa Spika, tukienda Sekta ya Afya, kazi kubwa imefanyika na takwimu kwenye hotuba ya Waziri Mkuu zimeonyeshwa dhahiri. Nami namshukuru Waziri Mkuu alifika hata Jimboni kwangu kule, alikagua hiyo Sekta ya Afya na alifanya kazi kubwa sana. Sasa hizo hospitali zilizojengwa zinahitaji vifaa na zinahitajika zianze kufanya kazi. Kwa nguvu kubwa iliyowekwa na ofisi zote kuanzia Mheshimiwa Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu, sasa inatakiwa ionekane kule kwa wananchi kwamba hizo hospitali, zahanati na vituo vya afya, vinafanya kazi kwa kupelekewa vifaa.

Mheshimiwa Spika, fursa za uwekezaji zimezungumzwa kwenye hotuba ya Waziri Mkuu. Tumeweka nguvu sana na msukumo mkubwa kupata wawekezaji, mimi niseme wawekezaji wa nje. Sasa ni muhimu tukangalia namna ya kuwawezesha wawekezaji wa ndani, kuwawekea mazingira mazuri waweze kupata mikopo kwenye mabenki au kwenye taasisi nyingine za fedha lakini pia hata kuwasaidia kuona maeneo ambayo wanaweza…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Allan.

MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.