Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi hii ya kuwa mchangiaji katika bajeti hii ya Waziri Mkuu. Binafsi nianze na pongezi kwa Serikali yetu ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa ambayo inafanyika na inaendelea kufanyika na pia wasaidizi wake wa karibu, Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, kiranja mkuu wa shughuli za Serikali, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa anafanya kazi kubwa sana ambayo kila mwenye macho anaona na asiye na macho anaweza akapapasa hatua kubwa za maendeleo ambazo zimefikiwa katika awamu hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kipekee pia nakupongeza wewe mwenyewe kwa namna ambavyo unaendesha Bunge letu Tukufu. Mara nyingi sana binadamu mpaka asiwepo ndiyo sifa zake zinaelezwa kedekede, lakini ni vizuri zaidi tukazieleza sifa hizi wakati wewe mwenyewe ukiwa unashuhudia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika awamu hii ambayo tumekuwa na Bunge mtandao, kwa kweli nilikuwa nataniana na ndugu yangu Musukuma hapa, alikuwa anasema, hivi huyu mtani wako naye ana utabiri kidogo? Maana alituletea falsafa hii ya Bunge mtandao, halafu mwaka huu tukakutana na changamoto ya Corona. Sasa unaweza ukapata wateja safari hii kuhusu utabiri wa uchaguzi unaokuja, kwa sababu umeonekana katika eneo hilo ni mahiri. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, nianze kuchangia bajeti iliyoko mbele yetu katika eneo la fungu 37 - Ofisi ya Waziri Mkuu haswa suala la linalohusu Mfuko wa Maafa.
SPIKA: Eh, Nilikuwa namsikiliza vizuri sana Mheshimiwa Shangazi alipokuwa hasa anatamka neno Corona, kwa sababu wao kule wanasema Coona. Mheshimiwa endelea. (Kicheko)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa. Kule tunazo Coona za kuchakata mkonge.
Mheshimiwa Spika, Fungu Na. 37 - Ofisi ya Waziri Mkuu linahusu maafa, lakini kwa muda mrefu sasa hatuoni ukiwekewa fedha kiasi kwamba limekuwa ni tatizo kubwa sana. Mwaka huu tumepata neema ya mvua nyingi katika nchi yetu na hasa mikoa ya kaskazini na mashariki. Kwa kweli watumishi wa Serikali wamekuwa wakipata shida sana katika eneo hili la maafa kwa sababu hakuna hata zile pesa za mwanzo za kufanya intervention. Hata Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria Mheshimiwa Mchengerwa, tumeona wiki mbili hizi akiwa amepanda kwenye boti anazunguka katika maeneo mbalimbali huko Rufiji, lakini unamwona yeye kama Mbunge, hata huwezi kumwona DC wala watu wengine. Kwa hiyo, unaona kabisa ni tatizo la kutokuwa na fedha katika Mfuko huu wa Maafa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri eneo hili tulitafutie mwarobaini wa kudumu. Tutafute vyanzo vya uhakika vya kuweza kuweka pesa katika Mfuko huu wa Maafa. Tena ikiwezekana zipatikane hata kwa asilimia, kwa sababu majanga ni mengi yanayotokea nchi hii. Tumeona tu kwa mfano kwa mwaka huu wa fedha ambao tunaenda kuukamilisha, tulianza na tatizo la nzige; kulikuwa na tishio la nzige, lakini Mwenyezi Mungu ameepushia mbali, hawakuingia katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa tumekutana na changamoto ya mvua, hali ya barabara zetu siyo nzuri huko vijijini, kiasi kwamba kwa ile asilimia 30 TARURA wanaipata naamini katika eneo hili mwaka huu haiwezi ikatosha, hivyo inaweza ikaadhiri hata namna ya usafirishaji wa vifaa mbalimbali wakati wa uchaguzi. Kwa hiyo, tunaomba eneo hili tulitizame kwa kina sana.
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ningetaka nilizungumze ni eneo la kuhusu anuani za utambulisho wa makazi (post code). Hili ni eneo ambalo limeanza Dar es Salaam kama pilot study, lakini eneo hili nalo limefika mwisho na waliokuwa wanasimamia mradi huo ambao ulikuwa ni pilot ni TCRA kupitia Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi.
Mheshimiwa Spika, sasa tungeweza kuoanisha Mfumo wa Utambuzi wa Makazi pamoja na Vitambulisho vya Taifa, ingekuwa na maana sana; kwa maana kwamba mtu anakuwa anatambulika kwa anuani ya makazi lakini pia na kitambulisho cha Taifa, kiasi kwamba hata kuzuia uhalifu inakuwa rahisi kwamba unafahamu kwa kupitia kitambulisho hiki, huyu mtu anaishi maeneo gani na mambo mengine hata katika mifumo ya kibiashara na mambo mengineyo.
Mheshimiwa Spika, pia katika eneo hili tumeona kabisa kwamba kwa mfano kwa Mkoa wa Dar es Salaam, wenzetu wale wenye utaratibu wa taxi zile za UBA unasaidia sana kiasi kwamba mtu popote alipo kwa sababu kwa Dar es Salaam wameshaingiza kwenye mtandao na ipo mpaka kwenye google unapata, inasaidia hata kurahisisha biashara.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunatamani sana kwamba hili eneo la utambuzi wa makazi liwe eneo la nchi nzima ikiwezekana, eneo hili liendelee lakini pia liunganishwe na mfumo wa vitambulisho ili hata mtu anapohama eneo moja kwenda lingine, inaweza kuwa ni rahisi kufuatilia vitambulisho vya Taifa na pia kupitia anuani za makazi.
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo ningetaka kuzungumza ni hili la NIDA, katika eneo la watumishi. NIDA wana watumishi wachache sana nitatoa mfano kwa Wilaya ya Lushoto ambayo ina takribani watu 600,000 inao watumishi watatu tu wa NIDA katika wilaya nzima. Sasa utaona kwamba wale wazee walioko vijijini watu wenye shida mbalimbali zikiwemo za ulemavu hawawezi kufika Lushoto au wengine inabidi watumie gharama kubwa kwenda kufatilia vitambulisho hivi sasa tungependa kuona kwamba angalau hili liangaliwe ikiwezekana waongeze idadi ya watumishi lakini pia wapatikane hata watumishi wa kuwasaidia wasaidizi maana tumezungumza hili eneo la wasaidizi na wenyewe wanajitetea kwamba hawana mafungu. Kwa hiyo, ni vizuri wakawekewa mafungu ya kutosha ili na eneo hili nalo waweze kutusaidia vizuri.
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo ningependa kushauri ni katika uanzishwaji wa mfuko wa ugharamiaji elimu kwa maana ya student loan fund tunatumia pesa nyingi sana kila mwaka ambazo ni lazima zitengwe kutoka hazina lakini kama tutaanzisha mfuko mahususi wa kugharamia elimu maana yake Serikali pamoja na wadau mbalimbali katika taasisi za kifedha kama mabenki lakini pia ni mifuko ya hifadhi wanaweza wakatengeneza mpango wa ku-capitalize pesa katika mfuko hata kwa muda fulani na baadaye sasa mfuko huu ukawa unakopesha wanafunzi kwa ngazi hata ya diploma na degree lakini pia hata wa digrii ya pili na hata wa udaktari. Ili sasa tuondokane na hii hali ya kuweka pesa kila mwaka shilingi bilioni 500 nakadhalika nadhani tukiweza kutengeneza eneo hilo tukalitengenezea mpango mahususi hata kwa kutumia mikopo nafuu kutoka vyanzo vingine vya kimataifa mikopo ya muda mrefu inaweza likawa ni eneo ambalo tunaweza tukaondoka na hii adha ambayo kila mwaka lazima tutenge bilioni 500 kwa ajili ya kusaidia wanafunzi katika eneo hili.
Mheshimiwa Spika, lakini katika nukta hiyo ningependa sana kupongeza Benki ya Dunia kwa kutuachia ule mkopo wa milioni 500 US Dollar ambao kwa kweli ni kazi kubwa sana imefanywa na Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana Mambo ya Nje tunakupongeza sana pia watanzania kwa pamoja tunashukuru sana kwa mkopo huu kwa sababu hapo mwanzo ulikuwa na figisu nyingi za baadhi ya watu kukosa uzalendo lakini kwa nukta hii tunashukuru sana kwa msaada huu tunaamini kwamba msaada huu utaenda kuongeza tija katika utoaji wa elimu yetu hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana ahsante sana kwa nafasi hii. (Makofi)