Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Korogwe Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hotuba hii ya Waziri Mkuu aliyoiwasilisha jana.
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuunga mkono hotuba hii ya bajeti ya Waziri Mkuu lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu mwenyewe, Mawaziri na Manaibu Waziri, Makatibu Wakuu pamoja na watendaji wote wa Serikali kwa namna ambavyo kwa kipindi cha miaka minne wamefanya kazi kubwa ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mambo makubwa yamefanyika hakuna mtu ambaye anaweza akapinga juu ya mambo makubwa ambayo yamefanyika mwenye macho haambiwi tazama mambo yanaonekana na wananchi wetu huko vijijini kwenye miji yetu wanaielezea vizuri Awamu hii ya Awamu Tano kwamba mambo makubwa yamefanyika katika kipindi kifupi namshukuru sana Mheshimiwa Rais pamoja na watendaji wote wa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikupongeze na wewe mwenyewe katika kipindi chote hiki cha miaka minne kuelekea huu wa tano, umekuwa kiongozi bora wa kutusimamia na kutuongoza katika Bunge lako hili Tukufu umekuwa ni mtu mbunifu tumekuwa tumekutana kwenye vikao vyetu vya Tume ya Utumishi wa Bunge ulianzisha hili na kutueleza hili suala la Bunge Mtandao mimi wakati huo unalielezea nilikuwa sikuelewi lakini kadri tulivyoendelea na nilivyokuja kuona sasa haya mambo ndiyo nikajua haa! Huyu kaka yangu kumbe mambo aliyokuwa anayazungumza ni mambo makubwa yenye manufaa kwa nchi yetu kwanza kwa kupunguza matumizi ya fedha katika vitendea kazi hususan makaratasi na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunakushukuru tunakupongeza sana sana sana kwa namna ambavyo umekuwa ukitusimamia na kuhakikisha tunapitisha bajeti ndani ya Bunge hili ambazo zimekwenda kufanyakazi za utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Spika, niungane na Watanzania wenzangu juu ya gonjwa hili la corona. Ugonjwa huu ni mbaya kwa bahati mbaya kulikuwa na ugonjwa huo mwingine ambao mwenzangu ametoka kuuzungumzia wa UKIMWI ulikuwa unaonekana wanasema ugonjwa huu umekaa sehemu mbaya huu hauna sehemu mbaya ni mbaya moja kwa moja unaua tuendelee kuwaelimisha wananchi wetu ili waendelee kuzingatia maelekezo wanayotoa viongozi wetu hususan Rais wetu, Waziri Mkuu, Waziri wa Afya yale maelekezo wanayoyatoa basi wananchi wetu waendelee kuyazingatia ili kusudi yaweze kutusaidia tuweze kuwa salama.
Mheshimiwa Spika, vinginevyo tukiwaacha wananchi wetu hawa bila kutoa maelekezo bila kuwasaidia kutoa elimu tutapoteza Taifa letu. Wako watu wanafanya mzaha na jambo hili, hili jambo halina mzaha wala dhihaka hata kidogo tunahitajika tuendelee kufanya kazi kubwa hasa kwenye maeneo kwa mfano kwenye stendi. Kwenye stendi za mabasi bado tatizo hili la kuwa karibu karibu msongamano wa watu bado hatujafanikiwa sana. Kwenye maeneo ya masoko bado hatujafanikiwa sana pamoja na kwamba watu wakifika kuna maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya kunawa maji wengine wanapitiliza hawanawi. Kwa hiyo, ni vizuri tukaendelea kuwaelimisha wananchi wetu waweze kutambua juu ya gonjwa hili kwamba ni gonjwa hatari kila mmoja ajitambue akae mbali na wenzake ili kusudi aweze kujisalimisha kwa maana kukiepuka kifo.
Mheshimiwa Spika, niishukuru Serikali kama nilivyosema imefanyakazi kubwa lakini bado baadhi ya maeneo bado tunahitaji kuendelea kuyasimamia ili kusudi wananchi wetu waweze kunufaika kwa mfano suala la maji Waziri Mkuu nikupongeze ulikuja Korogwe ulifanya mkutano Korogwe kubwa ambalo ulilisikia kwa wananchi wa Korogwe lilikuwa ni suala la maji.
Mheshimiwa Spika, niishukuru Wizara ya Maji kwamba wametupa vimiradi midogo midogo lakini bado havijakamilika kwahiyo niombe kwa kuwa nipo katika ile miji 28 ya fedha za mradi wa India basi niombe basi ile miradi midogo midogo waikamilishe ili iweze kuwasaidia wananchi wakati wanaendelea kusubiri huu mradi mkubwa. Kwa hiyo, ni ombi hili kwa wenzetu wa Wizara ya Maji waone ni namna gani sasa watatusaidia angalau kukamilisha ile miradi midogo ambayo tuliyo nayo ili kusudi wananchi waendelee kupata maji wakati tunasubiri ule mradi mkubwa wa fedha zile za India.
Mheshimiwa Spika, kuna suala la afya, Wizara ya Afya ina vyuo vya Maendeleo ya Jamii pale Korogwe nina Chuo cha Uuguzi. Chuo kile kwa bahati nzuri kilijengwa jengo la utawala ambalo linavyumba kwa ajili ya madarasa lakini toka limejengwa lile jengo kwa awamu ya kwanza ni miaka 15 halijawahi kutengewa fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo lile. Sasa kwa sababu tunazungumzia haya masuala ya afya, masuala haya ya ugonjwa wa Corona na vijana wetu wanasoma katika kile chuo, ningeiomba Serikali waifikirie sana kile chuo cha uuguzi pale Korogwe angalau kuweza kukitengea fedha kiweze kukamilika na kiweze kuanza kufanya kazi yake vizuri kama ambavyo ilikuwa imekusudiwa. Wananchi wanashindwa kuelewa kwa sababu jengo lile ni miaka 15 sasa halijawahi kutengewa bajeti kwa hiyo niombe sana Wizara ya Afya ione umuhimu wa kukipatia fedha chuo kile cha afya.
Mheshimiwa Spika, suala la mkonge Mheshimiwa Waziri Mkuu nichukue nafasi ya kukushukuru sana na kukupongeza sana sana kwa kazi kubwa ambayo umetusaidia. Mkoa wa Tanga sisi uchumi ni mkonge, Tanga ukiizungumza ilikuwa ni mkonge lakini sasa umeamua kwa makusudi kabisa kwa maana ya Serikali kuturudishia heshima ya Mkoa wa Tanga kwa kurudisha suala la mkonge umesimamia yale mambo ambayo yalikuwa yakilalamikiwa na wakulima wadogo wadogo na sasa umeelekeza kwamba wale wakulima wadogo wadogo waendelee kupewa maeneo ili waweze kulima mkonge ambao kwa kweli wakishakuwa wamelima huu mkonge kwa vyovyote vile utawasaidia sana kuwainua kiuchumi mkoa wa Tanga ulianza kudorora kutokana na mapato ambayo tulikuwa tunayapata sana kutokana na mkonge kwa hiyo tunakupongeza sana kwa kazi kubwa ambayo umeifanya Mwenyezi Mungu akubariki kwa sababu wananchi wa Tanga wataendelea kukumbuka sana na wanaendelea kukuombea kwa Mwenyezi Mungu ikiwezekana urudi bila kupingwa huko kwenye Jimbo lako ili kusudi uendelee na mapambano haya katika kutusaidia katika haya masuala yanayohusiana na mkonge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niliona kwa siku ya leo angalau niweze kuchangia haya machache nashukuru sana naunga mkono hoja.