Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hoja iliyowasilishwa na Waziri Mkuu hapa Bungeni. Na mimi nitaanza mchango wangu kwa kujielekeza katika ugonjwa huu wa Corona.

Mheshimiwa Spika, watu wamekuwa na mitizamo kwamba ugonjwa huu siyo wa kutisha sana ukilinganisha na ugonjwa mwingine kama UKIMWI, kansa na magonjwa mengine. Hata hivyo, ni ukweli kwamba ugonjwa huu wa Corona unatisha sana kuliko magonjwa mengine kwa sababu ya njia ya uambukizaji wa ugonjwa wenyewe na unatishia uhai wa binadamu na umesababisha vifo vingi katika mataifa mbalimbali ulimwenguni tena kwa muda mfupi sana.

Mheshimiwa Spika, bado hatujaona jitihada za dhati za Serikali za kuhakikisha ugonjwa huu unadhibitiwa. Tumeambiwa na wataalamu na tumeona kwamba tunawe mikono, kwa kweli tunajitahidi kunawa mikono hata Watanzania wananawa sana mikono popote walipo. Tumeona shule na vyuo vimefungwa na mambo mbalimbali ikiwemo makongamano, semina, michezo mbalimbali vyote zimeahirishwa ili wasipate maambukizi haya ya Corona.

Mheshimiwa Spika, hiyo ni hatua moja lakini bado hatujaona hatua nyingine katika maeneo yenye misongamano mikubwa mfano stand za mabasi, mabasi yanayotoka mikoani yanaingia kwenye miji mikubwa, kwenye mabasi kuna misongamano na tumeambiwa ugonjwa huu unaambukizwa kwa njia ya hewa. Sokoni tunakoenda bado kuna misongamano mikubwa sana. Kwenye magereza yetu kuna misongamano, magereza yetu yamejaa kupitiliza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukumbuke pia tuna cell zetu polisi ambazo wahaalifu kila siku wanaingizwa. Cell za polisi kwa utamaduni uliopo zinajaza wahalifu kupitiliza na hawapimwi. Mfano muhalifu akipatikana leo wala yeye hatawekwa kwenye chumba kingine cha karantini kwa siku 14 halafu achanganywe na wahalifu wengine kwa sababu hatuna hata hivyo vyumba vya kuwahifadhi katika vituo vyetu vya polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika,ndiyo maana nikasema hatua za awali zilizochukuliwa kukabiliana na ugonjwa huu bado hazitoshi, tunahitaji jitihada kubwa sana za kukabiliana na ugonjwa huu kwa sababu ya namna ambavyo unaambukizwa na jinsi ambavyo tumeona katika nchi za Ulaya, Marekani na China watu walivyokufa. Siyo huko tu, tujiangalie hata katika block ya Afrika Mashariki jinsi ambavyo ugonjwa huu umeweza kuuwa watu wengi.

Mheshimiwa Spika, kwa nini bado nasema Serikali inahitaji kujipanga sana kwenye ugonjwa huu wa Corona? Tuna maabara moja tu ambayo ndiyo inapima na kutoa majawabu ya watu walioathirika na virusi hivi vya Corona. Maabara hii ipo Dar es Salaam tu, hata hapa Makao Makuu ya nchi haipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tunajiuliza, kama mfano ikitokea kuna mgonjwa katika Wilaya ya Tanganyika labda kule Katavi au Kigoma mpaka sampuli iletwe Dar es Salaam itolewe majawabu, kama mtu huyu hajawekwa karantini huko aliko, kwa kweli tutakuwa tunajiweka kwenye wakati mgumu kama nchi. Serikali iliyopo madarakani nyie mmejipambanua kama ni Serikali wanyonge lakini tutawaonaje mkiwatetea wanyonge hawa wa Tanzania katika janga hili kubwa la Corona ambalo linauwa watu kwa upana mkubwa sana.

Mheshimiwa Spika, lakini bado tunahitaji kupata majibu na Serikali ituambie. Binafsi nilitegemea tulipoanza Bunge hili Serikali ingetuletea mkakati wa kina na wa dhati wa namna gani wanaenda kupambana na ugonjwa huu wa Corona. Tunajiuliza kama nchi hivi ongezeko likiwa kubwa, mpaka jana tumeona wagonjwa wamefika 20, tulikuwa na wagonjwa 13 leo wamefika 20. Tunajiuliza kama idadi hii ya maambukizi itaendelea kuongezeka, hivi tuna vitanda vya kutosha vya kulaza wagonjwa hawa? Tuna madawa ya kutosha kusaidia kama ambavyo wanafanya kwenye nchi nyingine, tunajua dawa haijapatikana lakini angalau kutibu katika zile hatua za awali? Je, tuna mashine za kutosha za kusaidia kupumua kwa wagonjwa hao? Kwa sababu tumeambiwa ugonjwa huu unashambulia mfumo wa upumuaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tunajiuliza hivi tuna madaktari na manesi wa kutosha wa kuhudumia kama janga hili likiongezeka? Leo tuna upungufu wa asilimia 52 ya watumishi wa afya hapa nchini. Je, idadi hii ikiongezeka, hatuombi iongezeke kila mtu hapa anatishika kwa sababu ugonjwa huu ukija haijali wewe ni CCM, CHADEMA, CUF, Muislam au Mkristo, yeyote yule unaweza kumpata. Ugonjwa huu hauchagui mtu lakini tunajiuliza ni kwa namna gani Serikali mmejipanga tuone jambo hili linadhibitiwa kama ambavyo nchi zingine wameweza kudhibiti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kubwa zaidi na sijui kama Serikali mnakiri kwamba ugonjwa huu ukiendelea hapa nchini ni kwa hakika uchumi unakwenda kuanguka. Hili siyo la kubisha, uchumi wa nchi na wa mtu moja moja unaenda kuporomoka.

Mheshimiwa Spika,nitoe mfano, sekta ya utalii, mimi natoka Wilaya ya Karatu, tuna hoteli za kitalii 58, leo hoteli zinafungwa, wafanyakazi wanarudi majumbani, wengine wanarudishwa hakuna kazi tena mpaka pale ambapo hali itatengamaa. Hoteli hizo zinategemea watalii wengi kuja na watalii wetu wengi wanatoka nchi za nje na hawaji kwa sababu huko kwao tayari hali ni mbaya. Je, hapa hatujagusa uchumi wa mtu mmoja mmoja na uchumi wa taifa?

Mheshimiwa Spika,lakini leo tunapoanza tu kujadili bajeti ya nchi kwenye sekta ya utalii tu Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika mwaka 2018/2019 inaingiza shilingi bilioni 143, kwa hali hii ya Corona hizi fedha tunaenda kuzipata? Hatuwezi kuzipata. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, je, hapa hatujagusa uchumi wa mmoja mmoja na uchumi wa taifa? Leo tunapoanza hata kujadili bajeti ya nchi, kwenye Sekta ya Utalii tu, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika mwaka 2018/2019 inaingiza shilingi bilioni 143. Kwa hali hii ya Corona hizi fedha tunaenda kuzipata? hatuwezi kuzipata.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali kupitia Waziri wa Fedha, lazima atuletee mpango wa haraka hapa Bungeni wa namna gani ya kukabiliana na suala la uchumi wa nchi na uchumi wa mtu mmoja mmoja hasa kutokana na janga hili la Corona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tusijifunze tu, tuangalie katika nchi za karibu tu hapa, kwa sababu kuna watu wanaosema kwamba tusitazame nchi zilizoendelea; Italy, Marekani na kadhalika. Hapana, hebu tutazame wenzetu wa jirani; Kenya na Uganda kwa hatua ambazo tayari wameshazichukua. Mfano tu mmoja, leo benki za Kenya zimetoa unafuu wa mikopo kwa siku karibia 90 kwa watu wao. Serikali ya Kenya imewataka wenye nyumba wawape nafuu wapangaji wasilipe kodi kwa kipindi fulani. Hii ni kwenda kumsaidia mtu mmoja mmoja kutokana na hali iliyoko. Sasa sisi kama Serikali ya hapa, watuambie wamejipangaje na jambo hili? Hili jambo halihitaji mzaha wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine hapo hapo kwenye kuwasaidia wapangaji, tunashangaa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam; kwanza mnakataza msongamano, yeye anaenda Mwenge, anaenda Ubungo, anakusanya watu, anaongea, anasema sijui naye anaanza kuongea na wenye nyumba wasamehe wapangaji. Hivi kweli tuko serious? Tumesema tufute misongamano yote kila mahali, kiongozi unaenda unakusanya watu.

Mheshimiwa Spika, halafu tunajiuliza, yeye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salam ndio amekuwa msemaji wa nchi hii? Suala la kuangalia namna gani wenye nyumba wanatoa unafuu kwa wapangaji, mimi nadhani lichukuliwe na Serikali lifanyiwe na…

SPIKA: Mheshimiwa Cecilia, nilidhani sisi Wabunge tungekuja na mapendekezo kwa Serikali badala ya kuitegemea Serikali peke yake ndiyo ifikirie halafu ije na mpango fulani. Pamoja na Serikali kutakiwa ikifirie, ije na mpango, lakini nasi tuwe tunapendekeza.

Nilikuwa nawaza tu, hili la kusema kwamba Serikali itoe amri, mwenye kajumba kake basi apangishe bure, sijui kama una nyumba yako halafu ipangishwe bure kwa sababu Serikali imesema, sijui kama… hebu weka sawa kidogo hili, maana yake, nilikuwa namwona Mheshimiwa Lema, maana yeye ni tajiri wa nyumba nyingi, sasa anasita hapo. Itakuaje hapo?

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nadhani hujanisikia vizuri, sijasema hivyo na nimeshauri kwamba Serikali ijifunze kwa majirani zetu katika bloc ya Afrika Mashariki jinsi wanavyofanya na tuangalie na sisi hali ya kwetu ikoje. Ndiyo maana nikashauri kwamba Waziri wa Fedha naye atuletee mpango wake kwa jinsi gani tunaenda kuangalia uchumi wa nchi utakavyoporomoka na hatua gani zitachukuliwa kwa uchumi wa nchi na kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja. Ndicho nilichosema. (Makofi)

SPIKA: Ndiyo ukatoa mfano kwamba Kenya imesema nyumba sijui imefanyaje.

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, naomba niendelee. (Kicheko)

SPIKA: Si unaona lilivyo gumu. Haya endelea Mheshimiwa Cecilia. (Kicheko)

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, kingine ambacho Serikali inapaswa kukifanyia kazi na kuchukua ushauri huu, kama tatizo litaendelea, ni kwa kiasi gani kama nchi tuna hifadhi ya chakula? Huo nao utakuwa ni mtihani mkubwa sana kwa sababu tunaelewa hali ya watu wetu. Watu wetu ni wa kwenda asubuhi…

SPIKA: Mwaka huu chakula kingi sana. Hata kabla Serikali haijasema, kingi kweli kweli! Hata Dodoma hatuombi chakula mwaka huu.

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama unasema kingi, basi Serikali ituletee taarifa hapa Bungeni kwamba ni namna gani inaweza kukabiliana na hali ya upungufu wa chakula kama hali ya maambukizi ya ugonjwa wa Corona itaendelea na ugonjwa wagonjwa wataendelea wengi? Sasa hilo litakuwa la msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesema hayo kwa sababu tunaelewa watu wetu ni wa kwenda sokoni leo akanunue kitu kidogo apate riziki, siku iende kesho hivyo hivyo. Sasa kama ikifikia hatua wagonjwa wataongezeka, maana yake lazima tutaenda lockdown. Kama tutaenda kwenye lockdown, namna gani watu hawa tunahakikisha kunakuwa na chakula cha kutosha?

Mheshimiwa Spika, Serikali yoyote duniani panapotokea majanga na milipuko, jamani kitu cha kwanza ni mwananchi. Uhai na afya ya mwananchi, mengine ndiyo yanafuata. (Makofi)

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ushauri wangu kwa Serikali…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Naambiwa tayari. Malizia hiyo sentensi yako ya mwisho.

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Serikali, bado Watanzania wanahitaji majibu na mikakati ya dhati, Serikali iwaambie Watanzania kwamba namna gani inaenda kukabiliana na ugonjwa huu wa Corona?

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)