Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Biharamulo Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwa namna ya pekee kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutupa afya na uhai na tunaendelea kumwomba atusaidie kwenye hili dhoruba ambalo linaikumba dunia kwa sasa. Napenda pia nichukue nafasi hii kwa kuendelea kuwashukuru wananchi wa Biharamulo kwa kuendelea kuniamini na kuniunga mkono kwamba tunaendelea kufanya shughuli za maendeleo. Tatu niipongeze Serikali; Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli; Makamu wa Rais, Mheshimiwa Mama Samia; Waziri Mkuu, Mheshimiwa Majaliwa; na Mawaziri wote kwa kazi nzuri. Kazi ni nzuri, ni wazi hakuna mtu anaweza akamaliza matatizo yote duniani kwa miaka mitano. Kwa hiyo tunachoangalia hapa ni hatua imepigwa na imepigwa kwa kiasi gani, kwa hiyo nawapongeza kabisa tumesikia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imeainisha kabisa kazi zilizofanyika.
Mheshimiwa Spika, mahususi kwa Biharamulo lakini pia inagusa Taifa zima, naipongeza Serikali kwa ule mpango wa kuja na miradi ya kimkakati kwenye halmashauri. Sisi Biharamulo ni moja ya halmashauri za Wilaya ambazo tulifaidika na jambo hilo na tumepata mradi wa ujenzi wa maegesho ya maroli kwa sababu pale Nyakanazi njiapanda ya kwenda Kigoma, Rwanda na Kahama ni mradi mkubwa sana maegesho ya maroli na stendi kubwa ya mabasi na soko, mradi mzuri sana. Hata hivyo, napenda kutoa wazo hapo kwamba awamu inayofuata hebu Serikali tujikite kwenye wazo zuri la miradi ya kimkakati, hebu tutumie mashirika kama haya ya hifadhi kama ya NSSF na mengine, kuyaunganisha na halmashauri ili sasa miradi hii iwe, sawa ipo ya upande wa huduma, lakini sasa twende kwenye upande wa uzalishaji, kwa sababu ukiangalia stendi ya mabasi na maroli ni mradi wa huduma, halmashauri itapata kipato, lakini tukienda kwenye miradi ya uzalishaji nafikiri tutafungua fursa zaidi.
Mheshimiwa Spika, Biharamulo ni kitovu cha wafugaji na mnakumbuka vita ya hifadhi na wafugaji center mojawapo ilikuwa ni Biharamulo, tuna wafugaji wengi na sasa hivi baada ya hii kampeni ya kuondoa wafugaji hifadhini, wafugaji bado hawajapata namna sahihi ya kuendesha shughuli zao za kiuchumi. Kwa hiyo hii miradi ya kimkakati, tukiyaunganisha na haya mashirika ya hifadhi ukatumia hiyo fursa ukatengeneza kitu ambacho kinabadilisha ule ufugaji wao unakwenda kibiashara zaidi, nafikiri kuna nafasi pale tutatoka kwenye huduma tunaenda kwenye uzalishaji, kwa hiyo nawapongeza Serikali lakini ni vizuri tukaenda mbele zaidi tukaongeza tija. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nigusie pia ugonjwa wa Corona maana yake ndio suala la sasa, ni vizuri kuligusia kidogo. Nianze kwa kujaribu kuweka kumbukumbu sawa, nimemsikia Mheshimiwa Sugu akiunganisha imani na sayansi, nataka kuseme tu kwamba, sayansi ni zao la elimu na elimu ni moja ya mapaji ya Roho Mtakatifu, kwa hiyo sayansi na elimu ni matokeo ya imani. Sasa kinachosemwa hapa sio kwamba watu kuwa na laissez faire, watu wajae Kanisani bila utaratibu, lakini pia sio kwamba kama wengine wamefikia hali ya kufunga Makanisa na sisi tufunge, hata kama hatujafikia, sisemi hatujafikia lakini tuipe nafasi Serikali na Serikali wafanye kazi yao ya ku- control, ku- balance vizuri panic na laissez faire, nafikiri ndio kazi kubwa ambayo Serikali tunatakiwa kufanya.
Mheshimiwa Spika, kwenye Corona hapo hapo pia ningemwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, nampongeza sana kwa kazi nzuri inayoendelea sana kabisa, lakini hebu kama alivyosema tujaribu kuwashauri kuliko kuwashambulia na kuwawekea presha, naomba tuongeze kidogo nguvu kwenye ile multisectoralapproach ya kupambana na corona kwamba sio suala la afya kama ambavyo Mheshimiwa Waziri Mkuu ndio amelichukua.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Serikali kupitia Mheshimiwa Waziri Mkuu ilizuia ilifunga shule ambayo ni hatua ya awali nzuri kabisa, lakini hivi tunavyoongea kuna mahali watoto wanakwenda kufanya masomo ya ziada tuition, sasa hilo ukimsubiri Mheshimiwa Waziri wa Afya utachelewa, kuna Wakuu wa Mikoa tuwaambie wafanye kazi yao , kuna Mawaziri wanaohusika wafanye kazi yao, wazuie hiki kitu. Hatua ya kwanza wameshafunga shule, watu waelewe kwamba tumefunga shule ili kuwaondoa watoto kwenye hatari kwa sababu wao sio rahisi kufuata maelekezo, lakini sasa kama huko nyuma watu wanawapeleka kwenye masomo ya ziada, ina maana hata hii jitihada ya kwanza ya kufunga shule unaipunguzia nguvu yake.
Mheshimiwa Spika, ushauri kwa Serikali nzima of course kupitia Wizara ya Afya, sasa hivi nimeona kwenye Mtandao hapa wasilisho zuri kabisa la Wizara ya Afya linaonyesha ramani ya case zetu ziko wapi, wapi una wale contacts unaotafuta kwa wingi vizuri kabisa Dar es Salaam, Arusha, Kagera na Zanzibar, maana yake ni kwamba tunatarajia kwa ramani hii Dar es Salaam na Arusha nguvu ya kupamba tuisikie ni tofauti kuliko kwingine kwa sababu hatuwezi kufanana. Kwa hiyo tujaribu namna ya huu mtawanyiko wa ramani ambao tunaupata kutoka kwa watalaam tusaidie kufanya mambo yetu kwa kusukuma kwa ngazi ya utekelezaji.
Mheshimiwa Spika, baada ya hapo naomba nizungumzie kidogo namna ya kutumia rasilimali kidogo tulizonazo kwa tija kubwa zaidi. Najua Serikali tunafanya hivyo kwenye maeneo mengi, lakini kuna eneo moja ambalo ningeomba nilisemee. Nilipata fursa ya kwenda Chuo Kikuu cha Teknolojia Nelson Mandela Arusha, Chuo Kikuu kile tofauti na Vyuo Vikuu vingine, Vyuo Vikuu vingine vyote kazi yake ni ile academic excellence yaani ubora kwenye taaluma lakini Chuo Kikuu kile zaidi academic excellence wanakwenda kwenye ubunifu, wanafanya ubunifu kila Master’sdegree inayotoka pale au Ph.D lazima itoke na ubunifu wa jambo fulani ambalo linakwenda kutatua tatizo kwenye jamii, lakini wanakwama kwenye pesa za uwatamizi wa ubunifu huo.
Mheshimiwa Spika, vile vile wanakwama kwenye namna gani tunaweza tukachukua ubunifu uliofanyika pale kuuleta kwenye mazingira ya viwanda na mazingira ya sera ili ubunifu huo utumike kwa Taifa zima; kwa mfano, wana ubunifu wameufanya wa teknolojia inaitwa non filter, Mtanzania kijana ametengeneza chombo cha maji kinachuja uchafu wote, sasa ameshindwa kuchuja chumvi, lakini uchafu mwingine wote wote anauchuja na maji yanaweza kuwa safi na salama na wamepata tuzo ya WHO na kwingineko wanatambulika kidunia. Sasa tutafute namna ya kimfumo ambapo sisi watunga sera tunaweza kuwa tunakwenda kule kuwa na appetite ya kujua kule kuna nini na kuchukua kuingiza kwenye sera. Kwa mfano hili la maji lina faida kwa Wizara ya Afya na kwa Wizara ya Maji.
Mheshimiwa Spika, kuna utafiti hapa unaonyesha vifo vya watoto kwenye nchi za Afrika Mashariki vimepungua, lakini vingepungua zaidi endapo tungekuwa tumeshughulika kwa kiwango kikubwa zaidi tulichonacho sasa kwenye habari ya maji ya kunywa ya watoto na vitu kama hivi. Pia ninao utafiti mwingine wa watu wa maji wanasema mpaka sasa hii informal access ya maji ni kubwa zaidi kuliko formal. Kwa hiyo huyu mtu mwenye teknolojia hiyo Nelson Mandela ukimtengenezea mazingira watunga sera tukaenda, tukawa appetite ya kwenda kuchukua ubunifu na kuingiza kwenye sera, watu wengi zaidi hata kama sio wote watapata fursa ya kupata maji salama ya kunywa na kutumia na hivyo itakuwa kazi ya wanasayansi ni kufanya ubunifu, sisi ni kuchukua na kutengeneza mazingira.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, tukiwa na chombo independent kidogo kinaongozwa labda na Rais mmoja mstaafu ambaye bado ana nguvu ya kukimbiambia, kina Makatibu Wakuu wawili wa nguvu, kina Wabunge wawili, watatu, halafu Spika labda ni mlezi, kinatengeneza appetite ya kwenda kwa wabunifu kuchukua mambo ya kupandisha kwenye policy, basi itatusaidia sana na nchi hii itabadilika na kutumia rasilimali kidogo tulizonazo kwa ajili ya kupata matoke makubwa.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja naomba kuwasilisha. (Makofi)