Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii.

Mheshimiwa Spika,awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema. Pia nitoe pole kwa Wanachama wenzangu wote wa Chama cha Wananchi CUF kwa kuondokewa na Katibu Mkuu wetu Mheshimiwa Maalim Khalifa. Nikupe pole wewe pia najua ni mtu uliyefanya naye kazi muda mrefu hapa ndani ya Bunge.

Mheshimiwa Spika, nianzie na suala la Corona. Nilitaka tu niongezee kitu kimoja na naunga mkono hoja yako kwamba tuishauri Serikali. Ushauri wangu mimi ni kwamba Serikali iongeze ulinzi kwenye zile hoteli zilizotengwa kwa ajili ya watu wanaowekwa karantini. Kama kuna wageni wanaingia kutoka nje wanapelekwa kwenye hoteli tupeleke na Jeshi la Polisi na vyombvo vingine vya ulinzi tusiachie wale walinzi wa hoteli.

Mheshimiwa Spika, ziko taarifa kwamba wamekuwa hawakai siku zote wanaondoka. Kama hizi taarifa ni za kweli basi kuna haja ya kuchukua hatua zaidi na hatua zenyewe ni kuzilinda zile hoteli. Ukiangalia wenzetu wa Uganda, Rwanda majeshi yao ndiyo yanalinda zile hoteli kwa sababu hili jambo ni la kiusalama na sisi tunapaswa kuzilinda hizi hoteli ambazo hawa watu wanaotoka nje wanawekwa pale karantini, tusiwaachie tu wale walinzi binafsi za hoteli zile. Kwa hiyo, mimi ushauri wangu ni huo.

Mheshimiwa Spika, lakini pia liko jambo lilizungumzwa hapa; suala la Corona hata sisi kwenye dini ya Kiislamu, mimi ni Muislam limezungumzwa namna gani ya kuchukua hatua yanapokuja magonjwa ya kuambukiza. Iko hadithi sahihi kabisa ya Mtume Muhammad (S.A.W) kwamba unapowafikieni ugonjwa wa tauni basi msiruhusu wageni waingie. Tumezuiwa pia kwa mujibu wa hadithi hii kwamba tusiruhusu wageni waingie kwenye vijiji vyetu au kwenye maeneo yetu unapokuja ugonjwa wa tauni.

Mheshimiwa Spika,nadhani ugonjwa huu una viashiria vya kufanana na ugonjwa wa tauni. Ikibidi kabisa, inapobidi kabisa, ushauri ni kwamba bora tubaki wenyewe ili tuchukue hatua madhubuti za kudhibiti kuenea ndani ya nchi yetu. Kwa hiyo, huo ulikuwa ushauri wa namna gani tunaweza tukaenda katika kukabiliana na ugonjwa huu wa corona.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni maafa ya mafuriko. Mkoa wetu wa Lindi umekumbwa na kadhia hii ya mafuriko na mimi kwenye eneo langu la Jimbo la Mchinga limekumbwa sana, Jimbo la Mheshimiwa Waziri Mkuu limekumbwa na kadhia hii na Majimbo mengine ya wenzangu. Kwa bahati mbaya maji yote yanayotoka Jimboni kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu yanaishia kwenye Jimbo langu kwa sababu mwenzangu yuko Mgharibi, mimi niko Mashariki, yale maji yale yote ya mito ile mingi iliyokuwa kule Jimboni Ruangwa basi yanaingiza maji yake pale kwangu, kwa hiyo, hali ya barabara ni mbaya sana.

Mheshimiwa Spika,kwa bahati mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Utawala na TAMISEMI, nafahamu kilichopo kwenye TARURA, pesa ya TARURA ni ndogo kabisa. Kwa adha iliyotokea mwaka huu kuna haja Bunge lifanye maamuzi ya kuiongezea TARURA fedha. Kile kiasi kilichowekwa pale ambacho nakijua ni kidogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika,kwa mfano, barabara zilizopo katika Jimbo la Mchinga pekee ambazo zimeharibika completely hazipitiki kabisa, kwa mujibu wa taarifa za TARURA zinahitaji shilingi bilioni 5,892,000,000 ili ziweze kufunguliwa. Kwenye kikao cha RCC tulichokifanya wiki tatu zilizopita pale Lindi, Mkoa wa Lindi pekee tunahitaji fedha ya dharura ipelekwe TARURA zaidi ya shilingi bilioni 62, ndiyo barabara ziweze kufunguliwa.

Mheshimiwa Spika, hivi tunapoongea, barabara za Jimboni kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu nyingi zimefungwa.

Barabara ya kutoka Jimboni kwangu pale Milola - Ruangwa imejifunga kwa sabbau ya mafuriko; barabara ya kutoka Kilwa - Kilanjelanje - Ruangwa kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu imejifunga na barabara nyingine nyingi. Kwa hiyo, Mkoa peke yake tunahitaji zaidi ya shilingi bilioni 60 tuweze kufungua barabara hizi.

Mheshimiwa Spika, naomba kwa kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu inaratibu Wizara zote, suala la fedha kwenye TARURA mwaka huu tuliangalie kwa sababu tatizo la mafuriko ni nchi nzima sasa hivi, watani zangu Wandengereko pale Rufiji wana malalamiko makubwa na hata juzi nilisema hapa hali ni mbaya sana. Kwa hiyo, naomba suala la mafuriko na bajeti ya TARURA mwaka huu ikiwezekana tuongeze ile parcentage kutoka silimia 30 kwa 70 angalau tufike 40 kwa 60 lakini ile asilimia 30 haitaweza kabisa kushughulikia matatizo haya. Tutamlaumu Waziri Mheshimiwa Jafo, kila Mbunge hapa atasimama hapa atasema lakini kiasi cha pesa ni kidogo hakiwezi kutosheleza mahitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni uwezeshaji wa Vituo vya Utafiti vya Kilimo. Kumekuwa na magonjwa mbalimbali yanajitokeza katika mazao ya wakulima. Nitazungumzia ufuta ambapo kwa sasa ni kama zao kubwa la biashara kwa Mkoa wa Lindi. Sisi tunafahamika, Tanzania sasa ni karibu nchi ya tatu kwa kuzalisha ufuta mwingi duniani na mwingi unatoka Mkoa wa Lindi. Mwaka huu ufuta unapambana na magonjwa mbalimbali. Kila Kijiji ukipiga simu ufuta mara unanyauka, unafanya nini; ukizungumza na watu wa Naliendele shida ni bajeti. Kwa hiyo, naendelea kusisitiza Wizara ya Kilimo lazima itenge fedha za kutosha kupeleka kwenye Vituo vya Utafiti vya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika,sambamba na ufuta, nilizungumza mwaka uliopita suala la minazi kwamba kwenye maeneo mengi inakauka. Kila siku natoa kilio hiki, natolea mfano Kisiju kulikuwa na minazi mingi imekufa, pale Lindi maeneo ya Ng’apa, Milola, Mchinga, Nangalu na maeneo mengine ambayo yalikuwa na minazi mingi sana sasa hivi kumetokea ugonjwa wa kunyauka minazi. Nazi ni chanzo cha mafuta na ni kiungo kizuri, hasa sisi watu wa Pwani kupika wali bila nazi haujakamilika. Kwa hiyo, naomba sana Serikali walichukulie jambo hili very seriously, nazi zinaingiza kipato kwenye nchi kwa sababu zinaleta biashara kwenye Halmashauri zetu. Halmashauri ya Manispaa ya Lindi kwa kiwango kikubwa sana inategemea kipato chake kutokana na kodi inayotokana na nazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie kidogo suala la korosho. Mwaka juzi Serikali iliamua kuingilia kati ununuzi wa zao la korosho. Napozungumza mpaka sasa kuna fedha shilingi bilioni 32 za msimu wa mwaka juzi wakulima wa korosho hawajalipwa.

Mheshimiwa Spika,nashukuru jana nimepata taarifa kutoka Lindi kwamba kuna fedha shilingi bilioni 10 zimepelekwa kwa ajili ya kupunguza deni lile. Naomba fedha za wakulima za msimu wa mwaka 2018/2019 zipelekwe kwa wakati ili wakulima wale waweze kulipwa madeni yao. Imagine, fedha za mwaka 2018 mpaka leo hawajalipwa na hawa ni wakulima masikini kabisa.

Mheshimiwa Spika, Waziri wa Biashara ananisikiliza lakini pia Wizara ya Fedha, kwa sababu watu wa Wizara ya Kilimo ukiwafuata wanasema tatizo bado hatujapewa fedha kutoka Wizara ya Fedha. Shilingi bilioni 32 wakulima wa korosho msimu wa 2018/2019, naomba walipwe fedha hizi. Nimepata taarifa ambazo zina ahueni kwamba mmepeleka shilingi bilioni 10 malizieni shilingi bilioni 22 zilizobaki ili wakulima hawa waweze kupata fedha yao stahiki.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine na nadhani litakuwa la mwisho, niishukuru Serikali lakini pia nishukuru uamuzi wa Mheshimiwa Rais wa kuhamisha eneo la Jimbo la Mchinga kututoa kwenye iliyokuwa Halmashauri ya Lindi Vijijini na kutupeleka Manispaa. Kuna watu walibeza wakati naijenga hoja hii, nilijenga hoja mara nyingi sana kwamba tuna haja ya sisi kuondokana na wenzetu wa Jimbo la Mtama tubaki kwenye eneo letu la Jimbo la Mchinga ama tupelekwe Manispaa kwa sababu ndiyo tupo karibu nao, jambo hili watu walifikiria haliwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika,nashukuru mwezi wa Oktoba, Mheshimiwa Rais alifanya maamuzi ya kulitoa Jimbo zima la Mchinga kulihamisha kutoka Lindi Vijijini na kutupeleka Manispaa ya Lindi. Tunashukuru sana, sana, sana na hiki kilikuwa ni kilio chetu na kwa nini tunalia? Mheshimiwa Rais aliongelea vizuri siku ile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wewe ni Mbunge wa siku nyingi humu unafahamu siku za nyuma namna Wabunge wa Majimbo hayo ya Mchinga na Mtama walivyokuwa wanalumbana. Kwa hiyo, mgogoro ule ulituambukiza hata sisi tuliopo sasa, wakatunyang’anya na Hospitali ya Wilaya akina Mheshimiwa Nape hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa uamuzi wa Mheshimiwa Rais kutupeleka Lindi Mjini Manispaa tunauunga mkono. Kwa niaba ya Wananchi wa Jimbo la Mchinga tunamshukuru na tunampongeza kwa uamuzi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.

SPIKA: Mheshimiwa Bobali, hiyo uliyomalizia hata sijaielewa vizuri kufurahia kwenda Manispaa lakini Jimbo si linabaki palepale?

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Jimbo liko palepale.