Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Ignas Aloyce Malocha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia katika Wizara hii kama ifuatavyo:-
Mhshimiwa Mwenyekiti, Elimu ya Awali ni muhimu sana katika kumwandaa mtoto kuanza Darasa la Kwanza kwa mwaka unaofuata, hivyo ni vyema Walimu wa kufundisha watoto hawa wakawa rasmi na kupewa cheti cha kufuzu masomo hayo kwa kufaulu badala ya kuchukua Walimu waliochoka, wasio na taaluma hiyo kama ilivyo sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Elimu ya Ufundi ni nyenzo muhimu sana kwa vijana wetu ambao hawakubahatika kuendelea na masomo ya elimu ya juu, hivyo ni jambo la muhimu vijana hao wakapata mafunzo ya ufundi ili elimu hiyo iwasaidie katika kumudu maisha yao, pia kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa lao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tutambue kwamba sera ya Serikali ni kwamba kila Wilaya kuwa na Chuo cha Ufundi (VETA) angalau kimoja. Je, sasa nataka Mheshimiwa Waziri anieleze ni lini sasa Wilaya ya Sumbawanga vijijini itajengewa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi (VETA)? Ni lini Mkoa wa Rukwa utajengewa Chuo cha Ufundi VETA? Naomba majibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali ianzishe haraka Kidato cha Tano na Sita ili kwenda sambamba na uanzishaji wa sekondari kila Kata ili wanafunzi wanaomaliza Kidato cha Nne wapate nafasi ya kuendelea na Kidato cha Tano na cha Sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itasaidia sana na hasa kwa familia masikini ambao wazazi wao hawana uwezo wa kuwapeleka mbali. Nitolee mfano wa Wilaya ya Sumbawanga vijijini, inazo Shule za Kata zinazofika Kidato cha Nne 19, ikiwa tunayo shule moja tu ambayo imepandishwa kufikia Kidato cha Sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa Mheshimiwa Waziri atukubalie kupandisha shule zifuatazo kufikia Kidato cha Sita; Vuna Secondary School, Mazoka Secondary School, Mzindakaya Secondary School, Milenia Secondary School. Naomba majibu ya Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kuchangia kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitengo cha Ukaguzi kimezorota sana ukilinganisha na ilivyokuwa hapo awali, hivyo kitengo hiki kiimarishwe kwa kupewa vitendea kazi kama vile, magari pikipiki, vifaa vya Ofisi na Ofisi zao zijitegemee bila kuingiliwa, kuwe na mafunzo ya mara kwa mara, fungu la kutosha kwa maana ya OC ili kuwezesha kitengo hiki kufanya kazi vizuri na kwa uhuru bila mashindikizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inapaswa kujipanga juu ya ujenzi wa hosteli ili kunusuru vijana wetu na hasa watoto wa kike ili kuwapa fursa nzuri ya kusoma na kuwaepusha na vishawishi wanavyovipata wanapokuwa huru katika mazingira ya uraiani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wamejitahidi sana katika ujenzi wa maabara, hivyo tunaomba Serikali itoe vifaa vya maabara ili kuboresha na kuiimarisha, vijana wetu waweze kupata elimu bora katika masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali itoe posho kwa Walimu wanaokwenda kukaa katika umbali na ukosefu wa huduma muhimu kama vile umeme, mabenki, mawasiliano na usafiri. Naunga mkono hoja.