Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muleba kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Spika, nami naomba niungane na waliotangulia kukupongeza wewe na timu yako, Makamu wako na Katibu wa Bunge kwa jinsi mnavyotuendesha. Mimi mwenyewe hapa nasimama kwa nguvu za Mwenyezi Mungu nikiamini kabisa kwamba Bunge litakapokutana Novemba, 2020, nitakuwa nimeng’atuka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru sana kwa muda ambao tumekaa pamoja na hasa nikijielekeza kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye tunajadili hotuba yake. Mheshimiwa Waziri Mkuu amekuwa karibu sana na sisi watu wa mbali, wa Kagera, ametembelea Jimbo langu. Juzijuzi kama mlezi wa Chama cha Mapinduzi, Mkoa wa Kagera alikuja kututembelea na kuangalia hali yetu. Naomba tumpigie makofi Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ni nzuri, mipango ni mizuri lakini nyakati zenyewe ndiyo siyo rafiki. Kwa hiyo, nami sina budi kuungana na Wabunge wengi, wanasema the time demand action, Corona ni tukio ambalo limetokea na huwa linatokea miaka mia moja mia moja ukiangalia historia ya pandemic. Mara ya mwisho limetokea 1918/1920, Spanish Influenza ambayo iliua watu takribani milioni 15, 20 au hata zaidi maana takwimu zinatofautiana na sasa hapa tuna hii pandemic.
Mheshimiwa Spika, naomba nijikite kwenye suala hili kwa sababu ni muhimu sana na lina demand kwamba tuliangalie kama Bunge. Uwezo wetu Afrika ku-respond kwa mambo ambayo nayaona kwenye mtandao yaliyotokea China, London St. Thomas ambapo Mwalimu wetu Nyerere alitibiwa na umauti umemkuta pale, wagonjwa wamelala chini na hata St. Mary’s. Juzi nimemuona Meya wa New York akilia hana ventilators sisi ventilators hatutaweza kuzipata.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nirudie alichokisema kwa ufupi sana Mheshimiwa Ngeleja kwamba sisi ni lazima tuwe na mpango mbadala ambao unajikita katika jamii yetu. Lazima tuhimize kunawa lakini tunapozungumza hapa kuna hospitali zingine hazina maji. Kunawa ni lazima lakini wananchi wetu wengine hawana maji. Kwa hiyo, huwezi kusema kwamba mkakati ni kunawa wakati unajua nusu ya watu hawana maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisemi kwamba tusinawe nasema kwamba ikiwa zahma ikitufikia kama tunavyoiona kule itakuwa kizungumkuti. Hapa ndipo naungana kabisa na kumpongeza Rais wetu tunaanza na sala kwa sababu lazima tukiri kwamba mpaka sasa hivi Mungu ametuhurumia, tumshukuru Mungu jamani. Ametuhurumia kwa sababu yale yanayotokea yangefika hapa hatuna uwezo wa ku-respond. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sasa nachotaka kupendekeza, hapa ndipo nasema jamii inahitaji survival strategies ambapo kujiuliza tiba zetu mbadala (za asilia) ziko wapi? Hakuna jamii yoyote itakayokaa na kusubiri kifo lazima itajihami. Kwa hiyo, Mwenyezi Mungu asipopitisha dude hili mbali tukafikia pale walipofika ni lazima tuangalie makabila yetu mbalimbali maana yana mbinu mbalimbali za kukabiliana na homa za mapafu.
Mheshimiwa Spika, wanasema Covid19 ni mpya lakini siyo mara ya kwanza kwa virus kama hivi kutokea. Kufukiza ni muhimu lakini unahitaji mkaa na kuni. Kwa hiyo, ni lazima sisi kama Serikali tuhakikishe watu wanapata mkaa yaani wawe nao karibu, watu wawe na sigiri, wawe na kuni karibu maana katika tiba zetu nyingi asilia inabidi uwe karibu na joto.
Mheshimiwa Spika, nataka kuomba Wizara ya Afya na Mheshimiwa Dkt. Ndugulile nimeshamwandikia barua rasmi nikimweleza kwamba ni lazima tuangalie pia option B. Sisemi kwamba tusitekeleze option A, tuvae mask, tutafute ventilators lakini kama watu wengi watakuwa wameambukizwa ni lazima tuangalie namna ya kuwaokoa na mimi naamini kwamba wataokoka. Nimeangalia figures leo, Ghana sasa hivi wameshapona watu 33 wakati Holland hakuna hata mtu mmoja amepona kwa sababu wao wamerudi kwenye muarobaini, wanafukiza wagonjwa na wanapona. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mambo haya naomba kusema kwamba Wazungu hapo wametupoteza. Tuna kasumba nyingi na huwezi kuwalaumu Madaktari wetu, wengi wamekuwa trained kwenye western tradition; oxford tradition, wanabeza mambo yetu kana kwamba sisi kabla ya Wazungu kuja tulikuwa hatuishi au tulikuwa hatuugui. Kwa hiyo, tiba mbadala ni kitu muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimeona niliseme hili kwa sababu ni survival strategy, ni lazima Serikali sasa isaidie. Kule kwangu kuna barrier fulani wanazuia watu wa mkaa, sijui wanataka watu wapikie nini! Unamwuliza mtu wa mkaa; mtu haruhusiwi kuwa na mkaa wake wa kupikia kwa mfano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka kusema kwamba nionavyo mimi katika kukabiliana na hili Covid- 19 ni kwamba tuangalie Plan A na Plan B. Plan A ni hii ambayo tunayo standard procedure, hospitali; Plan B ni kwamba kama tukizidiwa, lazima tupeane maarifa; Wagogo wanafanyaje? Wapogoro wanafanyaje? Wanyakyusa wananyaje? Wahaya tunafanyaje? Kwa sababu hii knowledge ipo, ni indigenous knowledge, lakini inakuwa ignored watu tumekuwa brainwashed. Sasa sisi na wengine wengi humu ni vijana siwalaumu, ninyi hamkukulia vijijini. Sisi tumelelewa na wazee, tumeshuhudia haya mambo. Sasa watoto wa mjini hawayajui haya mambo kwamba Plan B iwepo kusudi Afrika iweze ku- survive. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaposema hivyo, niseme pia, magonjwa mengine tusiyasahau, kwa sababu na yenyewe yatakuja kukuza hili tatizo. Kule kwangu Muleba, kule kwenye Hospitali ya Wilaya hatuna damu salama. Kwa hiyo, kuna wanawake watatu walipoteza maisha wakiwa wanajifungua kwa kukosa damu salama. Kwa hiyo, naomba hili nalo liangaliwe. Kwa sababu tusipoweka mambo ya kulinda sehemu nyingine ambazo zitatuletea matatizo, hata na hii Corona Virus, kama Mungu akitusaidia; na vile vile tusali; na tunaposali hata nyumbani unaweza ukasali, sio lazima uwe na mkusanyiko mkubwa kusali, lakini Mungu yupo kila mahali, au sio! Hata na hapa Bungeni tunaweza tukasali, mahali popote ni mahali pa ibada.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nadhani hilo nimelisema, lakini nawasiliana na Mheshimiwa Dkt. Ndugulile, nimeshamwona, nami najaribu kutoa mawazo kwa sababu the time reminds it. Ni dhana kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sababu muda ni mfupi, hilo nadhani tutaendelea na naomba nimpongeze Mheshimiwa Ummy Mwalimu, kwa kweli naona kama ni Jemedari. Namsikia kila siku anatangaza, yaani she is doing a great job. Sasa tumsaidie na sisi katika kutafuta hii Plan B.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana Profesa.
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Spika, ni dakika saba, nimeweka stop watch hapa. Ni dakika saba. Nimeweka stop watch, ninayo hapa dakika ya nane sasa. (Makofi)
SPIKA: Basi malizia, inaelekea stop watch ya Katibu wangu ina matatizo.
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Spika, katika dakika zangu hizo mbili kwa ruhusa yako, niendelee. Kitu kingine ambacho nataka kuongea na ni cha kimkakati, tunampongeza Mheshimiwa Rais wetu, anafanya kazi nzuri sana, lakini naomba kwa kupitia Bunge lako hili Tukufu nipeleke maombi maalum kwa Mheshimiwa Rais Magufuli. Program ya NIDA kwa sasa hivi ni kama imefeli.
Mheshimiwa Spika, NIDA kama ilivyo sasa hivi, imekuwa kero kubwa kwa wananchi kwa sababu simu zao zimefungwa. Sasa sijui ninyi wenzangu huko kwenu mkoje, lakini kule kwangu Muleba, watu simu zao zimefungwa na mtu ambaye umemfungia simu, hata kama umefanya mambo mazuri mangapi atakuona kwamba umemharibia. Kwa hiyo, naomba kitu hiki kilipofika; na zoezi lenyewe la NIDa ni zuri lakini mkakati ndiyo kwa kweli haujitoshelezi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu ni kwamba Afisa Uhamiaji wanaodhibiti uhakiki wa hizi namba, warudishe na wakasimu madaraka yao kwa Watendaji wa Vijiji. Kwa sababu mtu atakayejua kama mimi ni Mnyarwanda au ni Mtanzania ni kijiji changu au siyo! Haiwezi kuwa ni mtoto mdogo, migration officer namkuta kwenye Wilaya eti ndio anasema mimi sio Mtanzania. Kwa hiyo, unakuta hizi ni kero kwa wananchi na kwa upande wa Muleba na mikoa ya pembezoni. Huko pembezoni kwa kweli imekuwa kero kubwa. Sisi kwa upenzi wa Rais wetu lazima tutoe feedback ya hali halisi ilivyo. Kwa hiyo, hilo naona niliseme kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho kwa kupitia ofisi yako, nashukuru kwamba umemwandikia Mheshimiwa Jenista Mhagama, nakukabidhi hoja yangu binafsi ambayo nimehangaika nayo tangu Bunge la Kumi. Naomba kabisa Bunge lako tukufu, kwa kuwa naamini kabisa wewe unaendelea kabisa, tutakuwa nawe katika Bunge linalofuata, Mheshimiwa Jenista Mhagama naomba record ya Hansard irekodi kwamba nimekukabidhi hoja yangu binafsi, kwa sababu najua kwamba Mheshimiwa Spika, alikukabidhi hoja ile.
Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Waunge, hoja hiyo ilikuwa inasema hivi, baada ya kukumbwa na tatizo la ESCRO nikajikuta katika situation ambapo nahukumiwa na Bunge, niko ndani ya Bunge, ni Mbunge na siruhusuwi kusimama kujitetea. Nikaona tuna upungufu mkubwa sana katika mfumo wetu. Kwa hiyo, nimehangaika na hoja binafsi na Muswada binafsi.
Mheshimiwa Spika, Bunge la Mheshimiwa Makinda wakasema hatuna wakati; Bunge lako hili wakati haukupatikana, lakini angalau umepiga hatua umeikabidhi Serikalini. Kwa hiyo, naomba niikabidhi rasmi for the sake of the record nina historia kwamba ionekane kwamba Muswada binafsi, lazima Wabunge wawe na uwezo wa kuandika Miswada binafsi. Kazi ya Mbunge ni kutunga sheria, siyo lazima kujadili tu sheria zinazoletwa na Serikali, mwisho wa siku lazima Serikali itakuunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni jambo kubwa na la msingi ili kuboresha demokrasia yetu. Nadhani muda wangu umekwisha. Nakushukuru kwa kunivumilia. Nawashukuru sana wananchi wa Muleba Kusini kwa kunipa nafasi kuwa na ninyi katika Bunge hili. Miaka 10 nimejifunza mengi, naenda kuandika vitabu.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, unafanya kazi nzuri. (Makofi)