Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Martha Moses Mlata

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nakushukuru kwa nafasi hii. Kwa sababu bajeti hii inagusa na Mfuko wako wa Jimbo wa Bunge nilikuwa naanza nataka nianze kwa kutoa shukurani kwanza kwako, nikianza na Mwenyezi Mungu kwa hali hii niliyosimama hapa.

Mheshimiwa Spika, nina mwaka sasa zaidi na miezi kama mitatu/minne sijasimama hapa Bungeni kuchangia, lakini leo Mungu ni mwema sana kwangu, nimeweza kupata nafasi hii ya kuweza na mimi kusimama na kuongea mbele ya Bunge lako Tukufu kuweza kutoa mchango wangu. Mungu wetu ni mwema na atukuzwe sana, tuzidi kumwamini na kumtegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kumshukuru Mheshimiwa Rais, nikushukuru wewe kwa sababu Mfuko huu wa Bunge umetajwa na umetaja huduma za afya kwa Waheshimiwa Wabunge kwa ajili ya matibabu. Siwezi kusimama nianze kuzungumza tu bila kuupongeza mfuko huu ukiongozwa na wewe pamoja na Katibu wa Bunge na Viongozi wengine ukisaidiwa na Mheshimiwa Jenista Mhagama anayeshughulikia masuala ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, mmenitunza, mmenitibu na leo nimesimama hapa. Mungu akubariki sana na wote waliohusika. Naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye alifuatilia sana afya yangu. Mungu akubariki sana. Sina maneno mengine ya kusema, bali Mungu aendelee kukubariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema maneno hayo, ninashukuru madaktari wote na Mheshimiwa Waziri Ummy pamoja na Naibu wake. Nasema waendelee hivyo kwa sababu wataokoa maisha ya watu walio wengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya shukurani hizo, kwa kweli bado nitaendelea kutoa pongezi. Mheshimiwa Waziri Mkuu nakupongeza sana pamoja na Mheshimiwa Jenista Mhagama, tunaye Mheshimiwa Angellah Kairuki, tunaye Mheshimiwa Stella Ikupa mama yangu. Nikimtaja Mheshimiwa Stella Ikupa mama yangu, ninataka nimpongeze Mheshimiwa Rais, kwa sababu nami nikimtaja Mheshimiwa Stella Ikupa, mama yangu ni kama Mheshimiwa Stella Ikupa. Nafikiri mnanielewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kutambua mchango mkubwa wa watu wenye ulemavu, kuwapa nafasi kubwa kwenye Serikali yake. Ameonesha kwamba anaweza. Ni kweli wanaweza. Mheshimiwa Rais Mungu ambariki sana, kwa sababu sisi ni watoto wa akina Mheshimiwa Mama Stella Ikupa kama Stella. Mama yangu amenilea mpaka nimefikia hapa nipo ndani ya Bunge, siyo kwa sababu ya ulemavu, bali ni kwa sababu wanaweza. Nakupongeza sana Mheshimiwa Stella Ikupa.

Mheshimiwa Spika, pia kijana wetu Mheshimiwa Mavunde, ni kweli vijana wanaweza na ameonesha mfano mzuri na vijana wataendelea kuaminiwa kwenye Uongozi Serikalini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kazi kubwa ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu aliyoifanya, nataka niseme ameongoza vizuri. Mawaziri wote tumewaona jinsi ambavyo wamechapa kazi kwa sababu yeye amekuwa mchapakazi. Nilikuwa namwita Mheshimiwa Mzee Kamwele pale, nimesema leo nitaanza kukuita mzee. Nilimwona ameingia kijana, lakini sasa hivi naona amezeeka; ni kwa sababu ya kuchapa kazi; asubuhi huku, jioni huku, usiku yumo, kwa hiyo, ni lazima anaonekana mzee kwa sababu amechapa kazi. Mheshimiwa Waziri Mkuu umeongoza kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Spika, nikimwangalia Mheshimiwa Mzee Mpango pale, namwita Mzee Mpango kwa sababu aliingia kijana, sasa namwona ni mzee kwa sababu ya gwaride ambalo wamelichapa. Kwa kweli wanaweza, wamefanya kazi nzuri sana, ninaamini huko Majimboni watakapokwenda hawatakuwa na Wapinzani kabisa kwa sababu Taifa hili bado linawahitaji sana. Ni pongezi hizo za kwako Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna jambo moja ambalo pia nataka tu nipongeze wakati namwangalia Mheshimiwa Mpango pale, kweli Watanzania wamelipa kodi sana. Mara ya kwanza tulikuwa tuna wasiwasi, watu wakasema kuna watu wanaondolewa leseni zao, miradi inafungwa, nani atakayelipa kodi? Kwa kweli tuna kila sababu ya kuwapigia makofi Watanzania, wamelipa kodi ndiyo maana maendeleo yamerudi kwao. Huu ni usimamizi mzuri wa Serikali, wamekuwa waadilifu walipa kodi na sisi tumerudisha.

Mheshimiwa Spika, ukirudi nyuma pesa ambazo tulikuwa tukipitisha hapa zilikuwa haziendi au zinaenda kidogo, lakini safari hii zimekwenda, watu wamefanya kazi. Michango imelipwa, kodi zimelipwa, maendeleo yamekwenda, ukienda kwenye upande wa afya, tumefanya vizuri; ukienda kwenye upande wa barabara, tumefanya vizuri; ukienda kwenye upande wa elimu, mpaka hii elimu bure, nilikuwa namwangalia yule mtoto wa pale Simiyu, machozi yalinitoka. Nikasema hivi isingekuwa elimu bure, mtoto genius kama huyu tungemwona wapi? Sasa kwa sababu ya elimu bure, kuna watoto wengi kama yeye ambao hatukuwaona wameweza kufanya vizuri na wamebadilisha maisha yao. Kwa kweli nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na tunampongeza Mheshimiwa Rais, hongera sana.

Mheshimiwa Spika, kwenye upande wa afya ukienda hata kule kwetu Mkalama kwa Wahadzabe tulikuwa hatuna hospitali, lakini sasa hivi aka! Mambo ni safi. Akina mama wakiingia, mtoto wake wa kike, wa kiume anatoka salama bila matatizo, kwa sababu vituo na zahanati zimefika kwenye maeneo yote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kitu kingine tu nilikuwa nataka kusema, nilikuwa nasikiliza sana, jana nimesikiliza ile speech ya Mwalimu huwa inarudiwa ya yule mposaji. Kwanza ilikuwa ni baada ya Aridhio TBC. Pamoja na kutamka TBC, niseme tu, Mwenyezi Mungu aiweke mahali pema Peponi roho ya Marehemu Marin Hassan Marin kwa sababu alikuwa ni mtangazaji mahiri sana.

Mheshimiwa Spika, kile kipindi kilionyesha Mwalimu Nyerere akisema, yule kijana mposaji; ile kuzomewa huyo, huyo, huyo, eeh, huyo! Mimi nilikuwa natafakari sana, nikasema Mheshimiwa Waziri Mkuu zile kelele za huyo, huyo, huyo, tumeshinda. Kwa sababu kuna mambo mengi ambayo tusingeweza kuyafanya kama Mheshimiwa Rais asingeziba masikio. Tumenunua ndege, bwawa la kufua umeme, reli inakuja na mambo mengine mengi kweli. Kama angeweza kusikiliza zile kelele za huyo mkamate, huyo hawezi, huyo anadondoka, tusingeweza kufika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaomba tuendelee, tusonge mbele kwa sababu bado hatujafika. Kwa hili nataka tu niseme kwamba namwombea Mheshimiwa Rais wangu, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, kazi aliyoifanya ni kubwa sana, hatuna sababu kwa sababu mimi najua kabisa ndugu zetu hawa wako kwa ajili ya kukosoa yale mambo ambayo hatuwezi kufanya, lakini yale mambo yaliyofanyika hakuna sababu hata ya kumpeleka Mheshimiwa Rais akaanza kuomba kura. Anaomba kura wapi?

Mheshimiwa Spika, wananchi wameziona kazi; anaomba kura za nini tumsumbue barabarani huko, azunguke akaombe kura! Tunamwacha, sisi tupambane kwenye Majimbo huku, nafasi ya Rais ibaki yule yule. Ninyi njooni kwenye Majimbo tupambane, lakini Rais abakie yule yule kwa sababu anatosha kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho kabisa, wewe ni mtani wangu, najua utarudi tu, mimi nitakutambikia, wewe usiwe na wasiwasi, hakuna mtu atakuja pale, wewe tulia tu. Wewe chukua fomu, rudisha, njoo endelea kuandaa Bunge linalokuja kwa sababu wengi wetu tutarudi kutokana na kazi kubwa ambayo Serikali hii imeifanya na wananchi wameiona. Kwa hiyo, hakuna mpinzani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ambalo nilitaka nizungumze ni suala la Corona. Mheshimiwa Rais alionesha mfano mzuri sana wa imani na watu wameendelea kusali. Nataka niwaambie, tuendelee kusali lakini pia huku tukichukua tahadhari, tukiwafuata viongozi wetu wataalam wanatuambia nini? Ukisali na huku ukamwomba Mwenyezi Mungu na ukachukua tahadhari, huwezi ukawa juu ya mtu ukasema wewe jirushe tu Mungu atatuma Malaika, hapana. Ni kwamba unashuka taratibu na Mungu atakusaidia, utashuka kwenye huo mti. Kwa hiyo, tuendelee kusali, tumwombe Mwenyezi Mungu huku tukichukua tahadhari zile ambazo tunaelekezwa na viongozi wetu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Profesa Mama Tibaijuka yeye amezungumza kuhusu tiba asilia nikamkumbuka, mimi ni wifi yangu. Ukienda kwa shemeji zangu kule wana dawa moja hivi; ukiumwa Malaria hawakupeleki hospitali. Nikapima, wanakwambia wewe tulia, kuna dawa moja inaitwa Omushana. Kwa hiyo, nikamkumbuka, nikasema siyo ajabu ameshaanza kunywa Omushana ile ambayo huwa inapandisha immunity zile ambazo zinasaidia kupambana na maradhi. Ila kitu kikubwa ni kuwasikiliza wataalam wetu, Mheshimiwa Rais ameshakabidhi Mheshimiwa Waziri Mkuu. Mheshimiwa Dada Ummy ambaye anafanya kazi nzuri sana pamoja na Mheshimiwa Dkt. Ndugulile tuendelee kuwasikiliza.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu sijagongewa kengele ya mwisho kabisa kuhusu ushirika; pale Manyoni tumeletewa barua watu wamezuiwa kuuza mazao yao; zile Dengu, Ufuta na nini, eti mpaka wakauze kwenye Chama cha Ushirika. Hebu ushirika wajipange kwanza...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Mungu akubariki.