Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Naanza kwa kumshukuru Mungu aliyenipa uwezo na nguvu ya kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu na kutoa mchango wangu.
Mheshimiwa Spika, kwa dhati kabisa na kwa sauti kubwa, naomba nichukue nafasi hii ya kwanza kabisa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa jinsi anavyosimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kusimamia maendeleo ya wananchi na uchumi wa nchi yetu Tanzania. Vilevile niwapongeze wasaidizi wake wakuu, Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri wote kwa jinsi walivyosimama na kuwajibika katika kusimamia maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninayo mambo mawili makubwa ya kuanza nayo. Jambo la kwanza ni hili lililotokea hivi karibuni lililoikumba nchi yetu nalo ni mafuriko. Mvua zimekuwa nyingi na zimeleta uharibifu kwenye makazi, mashamba, watu wanahangaika, mifugo inapotea na mazao yanaharibika.
Naamini Serikali inachukua hatua za kutosha katika kuwasaidia hawa waliopatwa na madhara haya. Nawapa pole kwa sababu hili jambo ni kubwa lisipochukuliwa vizuri watu wetu wengi wanaweza wakapata shida baadaye. Kwa hivyo, nina imani Serikali inafanya kazi yake kama inavyostahili kuli-address jambo hilo.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo ni kubwa na ni tishio kwa dunia nzima ni hili la Covid19, hii Corona ambayo kwa kweli imeangamiza maisha ya watu wengi hapa duniani na inatia wasiwasi na taharuki sana. Niombe tuendelee kusikiliza na kutekeleza yale ambayo tunashauriwa na Serikali katika kudhibiti maradhi haya yasienee. Naamini kwamba Serikali yetu pamoja na wale ambao walipewa dhamana ya kushughulia jambo hili akiwemo Waziri, Mheshimiwa Ummy, Naibu Waziri wake na wote wale ambao wanashughulika kwamba wanafanya kazi nzuri na watajipanga vyema katika kuhakikisha vifaa vyote vinavyohusika vinapatikana pamoja na hizo ventilators ambazo tumekuwa tukiona katika taarifa za habari huku duniani hata Marekani hazipatikani kwa hiyo watu wenye tatizo la kupumua inakuwa shida. Hii ikienda sambamba na kuwaandaa madaktari na wahudumu wote watakaowasaidia watu wanapopatwa na matatizo haya ya pumzi. Tunamwomba Mungu atusaidie balaa hili litokomee mbali kabisa.
Mheshimiwa Spika, baada ya hayo, nataka kuchukua nafasi hii ya kipekee pia kumpongeza Rais wa Zanzibar, Dkt. Ally Mohamed Shein ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa utekelezaji wake wa Ilani kusimamia mapinduzi na kuyalinda na kuulinda Muungano ambao umepelekea nchi yetu kuwa na amani na utulivu na sisi wengine tuko hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo, nije kwenye Wizara hii ya Waziri Mkuu. Natoa pongezi kwa Mawaziri Mheshimiwa Jenista, Mheshimiwa Angellah Kairuki, Mheshimiwa Antony Mavunde na Mheshimiwa Stella Ikupa. Hawa wote wamefanya kazi nzuri sana kusimamia utekelezaji wa majukumu katika Wizara hii. Hongereni sana ndugu zangu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikiendelea na mchango wangu, nije kwako wewe special. Wewe unatisha, umesimamia mabadiliko makubwa katika Bunge letu hili (Bunge mtandao). Pongezi nyingi sana kwako, leo Wabunge tunafanya kazi zetu kwa njia ya kisasa zaidi, kwa wepesi zaidi kwani taarifa zote ziko katika finger tips, huu ni ukombozi mkubwa. Vilevile hii itaokoa pesa nyingi ambazo zilikuwa zinatumika kuzalisha makaratasi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pongezi pia kwa Naibu Spika, Wenyeviti, Katibu wa Bunge na watendaji wote wa Bunge kwa jinsi tulivyoweza kushirikiana katika kufanya kazi mpaka Bunge letu hili ambalo ni la mwisho.
Mheshimiwa Spika, vilevile siwezi kusahau watu wetu ambao wametufanya tukakaa hapa Bungeni vizuri, hawa ni wahudumu wa sekta ya afya. Nayo hii ni timu kubwa ikiongozwa na mwenyewe Dkt. Temba na madaktari wenzake Dkt. Nuhu na Dkt. Ruge; Wauguzi, Sister Disifa, Sister Farida; Mfamasia Salma; Madereva wa Ambulance; Wahudumu wa Hospitali na Technician wa Lab. Hawa wote wametufanya sisi tumekuwa imara kuliko tulivyokuja. Mimi hapa mnavyoniona niko imara kuliko Halima Mdee na ninyi mnaniona leo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, nimefurahishwa sana na utekelezaji…
SPIKA: Mheshimiwa Asha na bahati nzuri hajabisha kabisa, kwa hiyo, endelea kuchangia. (Kicheko)
MHE. ASHA ABDALLUH JUMA: Mheshimiwa Spika, naomba sasa niongelee miundombinu, hii Standard Gauge inanipa raha sana na kwa kweli ni ukombozi mkubwa kwa sekta ya usafiri. Hii ni reli ambayo inatoka Dar es Salaam kupitia Morogoro hadi Mwanza na Kigoma. Reli hii itakuwa msaada mkubwa kwa usafirishaji wa bidhaa, abiria, mazao na kuunganisha miji na vilevile kusaidia katika uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Spika, mbali na hayo lakini reli hii inaweza kuja kuzalisha ajira nyingi sana zipatazo 13,177. Ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wetu. Naamini itakamilika kwa muda na ni jambo ambalo nchi yetu hii tutajivunia.
Mheshimiwa Spika, wakati Waziri Mkuu anazungumzia suala la bajeti yake lakini kuna wananchi na wao wanafikiria bajeti zao. Kuna kadhia moja kubwa imewakumba baadhi ya wananchi wale ambao walikuwa wateja na wafanyakazi wa FBME Bank. Watu hawa suala lao lilikuwa likiletwa hapa Bungeni mara kadhaa lakini limekuwa likipata majibu mepesi, mepesi. Watu hawa fedha yao iko kule hawapati msaada wowote, wengine wanakufa, familia zao bado zinateseka na jambo hili haliishi.
Mheshimiwa Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri Mkuu wafanye utaratibu wa kuandaa Kamati, kama ile iliyokwenda kuzungumzia kuhusu madini yetu ikapata suluhu. Namna gani Kamati hiyo itakuwa wanajua wao. Kama wataweka Maprofesa wao waliobobea katika sheria pamoja na wadau lakini watu hawa ni kweli wana dhiki kubwa kwa sababu pesa zao nyingi zilikuwepo kule. Najua Serikali yetu ni sikivu na iko hapa kuwatetea wanyonge ambao pesa yao ya maisha iko kule na sasa hivi kazi imekuwa ngumu, kila kitu kimekuwa kigumu. Waziri Mkuu naomba alione jambo hili liweze kufikia mwisho wake kipindi hiki.
Mheshimiwa Spika, naomba niendelee kuchangia katika miradi ya Mahakama. Utekelezaji wa miradi hii umekuwa mzuri sana (first class), majengo ya Mahakama yamekuwa mazuri mno, kila mtu anayekwenda kule hawezi kusema katoka kule kaonewa. Majengo ya Mahakama Kuu Kigoma, Chato yamejengwa vizuri sana na Mahakama za Wilaya zote zimekarabatiwa na nyingine zimejengwa upya ziko kwenye hali nzuri sana pamoja na kupata furniture nzuri sana.
Mheshimiwa Spika, ila kuna baadhi ya majengo haya ya Mahakama hayana uzio (fence) kitu ambacho ni hatari. Hii ni kwa sababu imeshawahi kutokea incident Mahakama ya Wilaya ya Uyole ilipigwa mabomu. Kwa hiyo, nashauri Serikali ijitahidi iweze kujenga uzio kwenye Mahakama hizi.
Mheshimiwa Spika, hali kadhalika pia katika watendaji ambao wamesimamia kazi hizi ni huyu Injinia Katunzi. Injinia huyu kwa miradi ya Mahakama amefanya kazi nzuri sana.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa Asha, naona muda hauko upande wako.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, naam.
SPIKA: Muda wako umeisha.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, hapana, ndiyo kwanza kengele ya kwanza.
SPIKA: Leo sijui Katibu ana matatizo gani Mheshimiwa Asha.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, basi naunga mkono hoja lakini uchaguzi na Tume ya Uchaguzi ni huru. (Makofi/Kicheko)