Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Katavi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu, nahitaji kuchangia katika maeneo machache kutokana na udhaifu na nini kifanyike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kuhusu matatizo ya elimu duni nchini na kufeli kwa wananfunzi hasa katika Mikoa inayofanya vibaya kama Mikoa ya Tanga, Tabora na Mikoa ya Kusini. Hii inasababishwa na Walimu kukosa makazi mazuri kwa ujumla na hivyo Walimu kukosa moyo wa kufundisha katika shule walizopangiwa hasa vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ukosefu wa miundombinu hiyo na umbali mrefu kufika mjini. Mfano, Mkoa wa Katavi inamchukua Mwalimu muda mrefu kufika mjini kufuatilia madai yake kutoka kijijini mpaka mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu madai ya Walimu, hili limekuwa ni tatizo kwa nchi nzima. Walimu wanachukua muda mrefu kulipwa madai yao, madeni ya nyuma na kadhalika. Hii imesababisha Walimu kupoteza muda mwingi wakiwa mijini kufuatilia madai yao na hivyo kushindwa kufundisha na muda wa kufundisha wanafunzi unapotea bila sababu za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kifanyike? Naomba sasa Wizara iweke mipango kwa namna ya kusaidia Walimu hawa wasipoteze muda mrefu mijini kufuatilia madai yao na hivyo wajikite zaidi kufundisha wanafunzi hawa ambao wanasoma katika mazingira magumu. Uchache wa Walimu na Walimu kuishi katika mazingira magumu, hivyo Serikali sasa ihakikishe utekelezaji wa ujenzi wa nyumba za Walimu kwa wakati ili kuondoa usumbufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tatizo la baadhi ya shule hasa vijijini kuendelea kuwanyanyapaa wanafunzi ambao wanakuwa wamepata mimba kwa bahati mbaya (mimba za utotoni) kutokana na mazingira ambayo wanafunzi hao wanatoka. Nini kifanyike? Serikali itoe agizo sasa ili wanafunzi hawa waliojifungua mashuleni, warudishwe waendelee na masomo na wasinyanyapaliwe. Pia Serikali iweke mpango mkakati wa kuhakikisha wanafunzi hao wanaonyonyesha wawe na darasa lao maalum ili wawe huru na wale wasionyonyesha wasije kuharibika kisaikolojia kutokana na kuchangamana nao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa mabweni ya wanafunzi umekuwa ukisuasua na kusababisha wanafunzi kukosa huduma nzuri za malazi na hivyo wanafunzi kutokana na umbali kushindwa kuingia darasani (utoro) na kusababisha wanafunzi kufeli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa Serikali iwape nguvu wananchi katika baadhi ya maeneo ambao tayari wananchi wamechangishana pesa kwa ajili ya ujenzi wa mabweni na hivyo wameshindwa kumaliza. Sasa Serikali ione umuhimu sasa wa kuwasaidia wananchi maana wamebeba majukumu ya Serikali, isiwapuuze wananchi, imalizie majengo hayo (Mabweni) ili kunusuru wanafunzi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya shule za binafsi zimekuwa zikitoza ada kubwa na kuwaumiza wananchi. Hivyo Serikali iangalie upya ada hizi katika shule binafsi.