Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa nami kuchangia hoja iliyo mbele yetu katika hili Bunge lako Tukufu. Kwanza naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, mwingi wa ukarimu kwa kunipa uhai wa kuweza kuchangia hoja hii.

Mheshimiwa Spika, naomba niungane na Wabunge wenzangu wote kwa ajili ya kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mawaziri wote pamoja na watendaji wote kwa kuandaa hotuba hii. Kazi ambayo imefanywa na uongozi chini ya uongozi wa Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Magufuli inaonekana. Tunachotakiwa sisi ni kuendelea kumtia moyo, kumpongeza, pamoja na wale wote ambao wameunda timu kuhakikisha kwamba, Tanzania yetu inafikia ile azma ambayo wamejiwekea.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nizungumzie kuhusiana na suala kwanza la ugonjwa huu wa corona. Wenzangu wengi wamelizungumzia, niungane na wenzangu kutoa pole kwa Watanzania wenzangu ambao Ndugu zao wamepatwa na ugonjwa huu, lakini pia ambao wameondokewa. Niipongeze sana Serikali kwa juhudi kubwa sana ambayo inaifanya kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, wananchi wanapata elimu ya kutosha kuhusiana na ugonjwa huu.

Mheshimiwa Spika, lakini bado suala la misongamano lipo na hii inaweza ikaleta athari kwa baadhi ya maeneo. Sambamba na hilo elimu katika maeneo ya pembezoni inahitajika sana, Ndugu zetu wa vijijini bado hawana elimu ya kutosha kwa hiyo, nilikuwa naomba nitoe rai kwa Serikali pamoja na Wizara tuone ni jinsi gani elimu katika maeneo ya pembezoni inafika, ili kusudi Wananchi hawa waweze kujikinga na huu ugonjwa hatari ambao umeleta maafa makubwa sana katika dunia yetu.

Mheshimiwa Spika, ugonjwa huu wa corona umesababisha baadhi ya wafanyabiashara hali ya biashara zao kudorora. Nichukulie kwa mfano, najua kwamba nia nzuri sana ya Serikali kufunga vyuo, kufunga shule, hii ilikuwa ni katika kuhakikisha kwamba, huu ugonjwa hauenei, lakini sambamba na hilo sasa kuna baadhi ya wafanyabiashara ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa kuzihudumia taasisi hizi. Wafanyabiashara hawa sasa biashara zao kwa kweli, zimedorora na kuna baadhi yao wamechukua mikopo. Je, Serikali inaona hawa watu itawasadia kiasi gani kwa sababu, katika kipindi hiki cha mpito ambacho sasa hili janga linaendelea kuwepo na hawa baadhi ya wafanyabiashara wengine waliochukua mikopo benki. Sasa nilikuwa naiomba Serikali ijaribu kuona itawasaidiaje hawa watu, ili kusudi sasa baada ya hiki kipindi cha mpito waweze kuendelea na shughuli zao.

Mheshimiwa Spika, katika ukurasa wa 26 wa hotuba hii umezungumzia kuhusu shughuli zilizochangia ukuaji wa pato la Taifa ambao umefikia 6.9%. Niipongeze sana Serikali yangu kwa jinsi inavyofanya kazi nzuri ya ukusanyaji wa mapato, lakini sambamba na hilo kuna kundi ambalo natamani kundi hili kwa mfano Serikali imekuwa ikitoa mikopo kwa makundi ya vijana, makundi ya wanawake, watu wenye ulemavu, lakini pia na wajasiriamali mbalimbali. Nilitamni nione kwamba, hawa nao tunaona wanachangiaje katika pato letu la Taifa, ili mwisho wa siku na wenyewe nao ufanyike utaratibu, kama ni tathmini, au utafiti waweze kuweza kuchangia katika hili pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika, naomba pia nizungumzie kwenye issue ya utalii. Naipongeza sana Serikali kwamba, katika hotuba hii kumekuwa na matangazo mengi sana ya vivutio vya utalii katika maeneo mbalimbali, lakini Serikali imebainisha kuwa kuna mkakati wa kuwekeza zaidi katika utalii na hasa katika utalii wa fukwe, utalii wa meli, utalii wa mkutano, utamaduni, mali kale, ikolojia na jiolojia. Nilikuwa naomba niishauri Serikali kwamba, mkakati huu uendane pia na kupatikana na wataalam ambao wataweza kusimamia aina hii ya utalii. Ninaamini kabisa kama tukiwa tuna wataalam wa kutosha basi utalii huu utaleta tija kubwa sana katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie pia suala la UKIMWI. Nimesikia wenzangu wengi wamelizungumza na tunafahamu kwamba Serikali imejitahidi sana naipongeza sana kwa kufanya kampeni kubwa sana. Zimefanyika kampeni kubwa sana katika kuhakikisha kwamba UKIMWI unapungua au unakwisha kabisa. Hata hivyo, kuna hii AIDS Trust Fund, nashauri Mfuko huu tuone tunafanya utaratibu gani wa kuweza kupata rasilimali za kutosha. Kutokana na taarifa zilizopo ni kwamba hawa wafadhili ambao wamekuwa wakitoa ufadhili kwa ajili ya dawa na kadhalika wameanza kupungua.

Mheshimiwa Spika, naona kama litapatikana tozo la kuweza kusaidia Mfuko huu ukatunishwa, ina maana kwamba sisi wenyewe kama nchi tutaweza kujitegemea na hivyo suala zima la prevention na mambo mengine ambayo yanahusiana na hayo Mfuko huu utaweza kusaidia. Hivyo, kupitia makampuni mbalimbali kama ya simu au pengine taasisi mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanya miradi mbalimbali tunaweza tukawawekewa utaratibu maalum wa kuwa na tozo maalum kwa ajili ya Mfuko huu, naamini kabisa nayo hiyo inaweza ikasaidia.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka kushauri ni kuhusiana na suala zima la mkakati wa behavioral change kwa ajili ya vijana wetu kuanzia miaka 15 – 24 kwa sababu inaonekana kwamba hili ni kundi kubwa ambalo limekuwa likiathirika.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka nizungumzie ni kuhusiana na ukuzaji wa lugha ya Kiswahili. Kwanza nipongeze sana Mkutano wa Wakuu wa nchi wa SADC kwa kuamua kwamba Kiswahili kiwe ni mojawapo ya lugha rasmi katika mikutano hiyo. Sambamba na hilo, imeonesha kwamba bado wataalam wa Kiswahili tunao wachache sana. Kutokana na taarifa iliyopo katika ukurasa 104 wa hotuba hii, imebainika kwamba wataalam waliopo wa Kiswahili ambao wamesajiliwa ni 1,159. Hii ni idadi ndogo sana, kwa hiyo naiomba Serikali basi vijana wengi zaidi wahamasishwe ili kusudi wawe wataalam wa Kiswahili na hatimaye waweze kutangaza Kiswahili chetu katika nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, najua muda sio rafiki sana naomba nizungumzie kuhusiana na suala la mikopo kwa elimu ya juu. Ukurasa wa 66 unazungumzia kuhusu mikopo, niipongeze Serikali kwa ule wigo kuwa mkubwa wa upatikanaji wa mikopo. Kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya hawa wanufaika wa mikopo kwamba hii mikopo wakati wa urejeshaji kumekuwa na sintofahamu. Kwa mfano utakuta kwamba pengine mtumishi au kijana katika salary slip yake inaonesha kwamba ile outstanding loan ni milioni 20 lakini akienda kule Bodi ya Mikopo anakuta outstanding loan ni milioni 24. Kwa hiyo natamani labda ungefanyika utaratibu wa kuhakikisha haya madeni ili kusudi hawa vijana wetu wasije wakaona kwamba kuchukua mkopo imekuwa ni burden kubwa sana kwao. Kwa hiyo akianza kufanya kazi ile pesa nyingi inachukuliwa, kwa hiyo naomba Serikali ijaribu kuona jinsi gani itaweza kuangalia.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)