Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Vedasto Edgar Ngombale Mwiru

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Kilwa Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili walau niweze kuwa mchangiaji wa mwisho katika siku hii njema ya leo.

Mheshimiwa Spika, nami naungana na wenzangu kwanza kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri ambayo kusema ukweli imejitosheleza. Hili ndilo Bunge letu la mwisho, tunamaliza miaka yetu mitano na tuna nafasi ya kurudi tena kwa wananchi wetu waangalie kwa yale tuliyowaahidi katika kurejea tena katika angle nyingine.

Mheshimiwa Spika, labda niseme jambo moja tu la shukrani ambazo napaswa kumpa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Mwaka 2015 alipokuja pale Musoma wakati wa kampeni, naomba umfikishie hizi salamu, tulimuomba mambo manne ambayo yote ameyamaliza vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la kwanza, tulikuwa na tatizo kubwa la maji pamoja na kwamba tunaishi karibu sana na maji. Kusema kweli amelisimamia vizuri, tulipata fedha zisizopungua shilingi bilioni 45, leo tatizo la maji kwa Musoma Mjini ni historia. Kazi iliyobaki ni kumalizia tu katika maeneo machache kwa maana ya usambazaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili ambalo tulimuomba wakati ule, tulikuwa na matatizo ya barabara, barabara zetu nyingi hazikuwa katika kiwango cha lami. Leo nafurahi na umpelekee salamu kwamba ameweza kutupatia fedha zisizopungua shilingi bilioni 13. Kwa hiyo, barabara zetu pale mjini nyingi sasa zipo kwa kiwango cha lami na hii ni ahadi aliyoitoa yeye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahadi ya tatu aliyoitoa, tulikuwa na tatizo kubwa la Hospitali yetu ya Mkoa ambayo ilikuwa ni Hospitali yetu ya Rufaa iliyojengwa zaidi ya miaka 40 na ilikuwa imeshindikana kuisha. Mpaka hii leo ninavyoongea kwa mwaka jana peke yake kwenye hii bajeti ya mwisho aliweza kutupatia fedha zisizopungua shilingi bilioni 15. Leo kwa furaha niliyonayo ni kwamba katika mwaka huu kabla haujafika mwisho ile hospitali itaanza kutibu, ni Hospitali ya Rufaa ilikuwa imekaa kwa muda mrefu sana. Hayo ni baadhi ya mambo aliyokuwa ameyaahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho lilikuwa ni suala la uwanja wa ndege. Yeye aliahidi kukajitokeza kuwa na mchanganyiko pale lakini bahati nzuri limeisha, tender imetangazwa, Jumatatu tarehe 6 ile tender inafunguliwa.

Mheshimiwa Spika, nimwombe tu Mheshimiwa Waziri Mkuu ampelekee salamu kwamba ahadi zote zile alizokuwa amewaahidi watu wa Musoma, hatumdai hata moja. Tunachosubiri ni kumpa tu kura za kishindo ili aweze kuendelea katika angle nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba kwa Musoma pale yapo tu matatizo madogomadogo sana. Moja ni hili tatizo la huu ugonjwa wa Corona sasa limefanya uchumi wa Musoma ume-shrink maana watu wengi sasa wanashindwa kuhangaika kwa sababu hasa ya hilo tatizo la ugonjwa wa Corona.

Mheshimiwa Spika, tatizo la pili ni miundombinu. Baada ya mvua kunyesha zile barabara zetu sasa siyo nzuri sana, nadhani hapo tu ndipo tuna changamoto kidogo ya kufanya.

Mheshimiwa Spika, la tatu, ni suala la uchumi kwa ujumla hasa suala la ajira kwa vijana. Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye hili suala la ajira kwa vijana, kusema ukweli si Musoma peke yake, ni kwa nchi nzima. Sasa kwa sababu tupo hapa katika kushauri, nashauri mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, la kwanza, kuna hili suala la bodaboda. Leo hii ukitembea katika vituo vingi vya Polisi, zipo pikipiki nyingi pale zimefungiwa na zilinunuliwa kwa fedha za kigeni. Ukiangalia kituo kimoja unakuta kina pikipiki 200 – 1,000 zinanyeshewa na mvua, zinaoza.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu, ni kwa nini isiundwe Tume au Kamati wakaweza kupitia, wakaangalia zile pikipiki ambazo wenye nazo wanaweza kupigwa faini kidogo wakarudishiwa, watarudishiwa ili waendelee na maisha lakini hata zile ambazo zimeshindikana kuliko kuozea pale ni bora Serikali ingezitaifisha kwa maana ingezichukua halafu ikaziuza hiyo fedha ikarudi Serikalini kuliko ambavyo inapotea. Kwa hiyo, hilo ni la kwanza ambalo wala halitugharimu chochote katika kulitekeleza kuliko kuacha ile rasilimali kubwa inaendelea kupotelea pale.

Mheshimiwa Spika, la pili ambalo linahusiana na ajira ambalo ni kwa nchi nzima. Ushauri wangu, yapo maeneo matatu ambayo vijana wetu pale wanaweza wakaajiriwa na wakapata ajira kubwa; moja ni eneo la kilimo lakini la pili ni eneo la mifugo. Ukienda kwenye kilimo, mifugo pamoja na uvuvi vijana wengi sana wanaweza wakapata ajira.

Mheshimiwa Spika, nichukue tu mfano kwa mkoa mmoja tu wa Mara na kama litaonekana linafaa tunaweza tukaifanya kwa nchi nzima. Napozungumzia haya maeneo matatu, leo tumesoma pale kwenye hotuba ya Waziri Mkuu, kila mwaka zaidi ya watoto milioni mbili wanaenda darasa la kwanza, tafsiri yake ni kwamba hao ndiyo watakaomaliza darasa la saba, baadhi yao ndiyo wataenda mpaka chuo kikuu lakini wote hao mwisho wa yote ni kwamba wanategemea ajira.

Mheshimiwa Spika, sasa ajira zilizopo kwa sababu hazitoshi, huku kwenye kilimo, mifugo pamoja na uvuvi tunaweza kuwa-accommodate wengi kwa utaratibu ufuatao. Mimi nichukulie tu kwa mfano wa Mkoa wa Mara. Pale Mara tunayo maeneo, mfano tunalo eneo la Bugwema ambalo ni zuri sana kwa kilimo cha umwagiliaji, pale tu zipo zaidi ya ekari elfu kumi. Ukienda kule Bunda kuna eneo linaitwa Nyatwari zipo zaidi ya heka elfu tatu. Pia hata unapozungumzia habari ya mifugo, ukigusa kule Rorya kwa maana ya Uteji lipo shamba kubwa zaidi ya heka elfu ishirini kwa ajili ya mifugo. Ukienda kule Butiama kuna eneo linaitwa Buhemba Holding Ground kuna zaidi ya ekari elfu kumi mpaka elfu ishirini kwa ajili ya mifugo. Sasa nini kifanyike?

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu ni kwamba tulishaanza utaratibu mzuri wa JKT, tuchukue kila mwaka mfano kwa pale Mara vijana wasiopungua elfu tano tukawapeleka JKT wafundishwe kwanza ukakamavu lakini na ile discipline ya maisha wakitoka hapo tunawapeleka kama miaka isiyopungua miwili ambapo kazi kubwa chini ya uangalizi wa JKT watajifunza kilimo, habari ya mifugo, unenepeshaji wa mifugo na hata uvuvi wa kisasa. Matokeo yake ni kwamba wale vijana wakikaa pale miaka miwili chini ya JKT wakipata hayo mafunzo, siku wakiondoka hapo naamini Serikali itakuwa na mtaji wa kuwapa kwa sababu wao wenyewe wameutengeneza na wamejifunza na kutokea hapo naamini kwamba sasa kijana ataondoka na si chini ya milioni kumi na ataenda kuanza maisha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa utaratibu huo, ukipeleka watoto elfu tano ambapo ukawapa hiyo mitaji ambayo wameitengeneza wao wenyewe matokeo yake ni kwamba si chini ya watoto elfu tatu wataendelea na maisha yao vizuri. Wapo wachache ambao maisha yatawashinda lakini kwa sababu wamelelewa kwenye yale mafunzo ya JKT maana yake wanajua muda, watajifunza ujasiriamali na mambo mengi sana.

Mheshimiwa Spika, hayo maeneo ninayoyazungumzia hayapo Mkoa wa Mara peke yake. Yapo kila mkoa maana bahati nzuri mimi katika mihangaiko yangu nimeweza kutembea katika mikoa mingi, kila mikoa inayo maeneo mengi ambayo yanaweza kuwasaidia.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)