Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibaha Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HAMOUD A. JUMAA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kuchukua fursa hii ya kipekee kabisa kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha na mimi kuwepo mahali hapa na kuchangia hotuba hii ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu 2020/2021 iliyopo mbele yetu. Hotuba hii inakwenda kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM kama ilivyoainishwa. Napenda kuipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na watalaam mbalimbali kwa kuandaa hotuba nzuri itakayokwenda kuleta mapinduzi makubwa katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo.
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii pia kwa kuanza kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri anayoifanya kumsaidia Mheshimiwa Rais wetu, sisi sote ni mashahidi, tumeona Mheshimiwa Waziri Mkuu akiwa katika maeneo mbalimbali kuhakikisha shughuli mbalimbali za kimaendeleo zinakwenda vizuri bila kusuasua, tumeshuhudia usimamiaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020 ukifanywa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, ni hatua nzuri na ya kujivunia sana tukiwa sisi wanaCCM, kwani tuliahidi kuwaletea maendeleo wananchi wetu bila kubagua.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano tumeshuhudia mafanikio makubwa katika kuimarisha miundombinu, huduma za kiuchumi na kijamii, utawala bora, mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi pamoja na kuhamasisha uwekezaji nchini kwetu, kuvutia wawekezaji mbalimbali kuja kuwekeza na kuzalisha ajira.
Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa awamu ya tano kwa uongozi wake mzuri na kuhakikisha utekelezaji wa Ilani ya CCM 2015/2020 unakwenda vizuri. Aidha napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na Serikali kwa ujumla kwa kuendelea kupambana na janga la virusi vya corona (COVID-19), ikumbukwe janga hili ni la kimataifa kama WHO walivyokwishatangaza hapo awali. Janga hili linaendelea kusumbua na kuathiri watu wetu, idadi ya wagonjwa imekua ikiongezeka na hivi karibuni imethibitishwa kuwa mgonjwa mmoja aliyekuwa na virusi hivi na kulazwa katika treatment centre iliyopo karibu na Hospitali ya Mloganzila amefariki dunia. Ni kipindi kigumu sana tunachopitia kulingana na mazingira yetu, lakini ni wajibu wetu kuendelea kushirikiana na kutoa elimu kwa watu wetu juu ya kujikinga na kuchukua tahadhali mbalimbali juu ya ugonjwa huu.
Mheshimiwa Spika, hakika katika kipindi hiki cha janga hili la virusi vya corona (COVID-19) ni vema Serikali ikaangalia ni njia gani ya kukabiliana na janga hili hasa namna ya kuepusha maambukizi mapya kwa wananchi, mazingira yetu yanatofautiana sana na nchi za wenzetu hivyo hatupaswi kuyafanya yale ambayo wenzetu wameyafanya kulingana na mazingira yao, naishauri Serikali kuona umuhimu wa kutenga fedha za kutosha ili kukabiliana na janga hili, hii itasaidia kuweza kukabiliana na aina yoyote itakayojitokeza katika kipindi hiki hatarishi, kwani Tanzania ni moja ya nchi ambazo zina muingiliano mkubwa wa watu, mikusanyiko masokoni bado inaendelea, katika vyombo vyetu vya usafiri bado kuna mrundikano wa watu na baadhi ya maeneo mengine watu wameendelea kukusanyika, maradhi haya hatuwezi yapuuzia, kuwalinda watu wetu ni wajibu wetu. Hata hivyo naipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali ilizochukua baada ya janga hili kutokea, kusitisha mbio za mwenge wa uhuru, kusitisha michezo yote nchini, kusitisha shughuli zote za elimu kuanzia elimu ya awali hadi vyuo vikuu, kusitisha semina, makongamano na mikutano yote ya hadhara, ni maamuzi ya msingi kulingana na aina ya ugonjwa unavyoambukiza.
Naiomba Serikali iendelee kutoa elimu kila wakati katika vyombo vyote vya habari, kuweka matangazo mbalimbali mitaani ili wananchi wapate kujua namna ya kujikinga na janga hili.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kujitahidi kutengeneza fursa mbalimbali za ajira kwa kuendelea kuweka mifumo mizuri ya uwekezaji hasa katika viwanda, ni jambo jema na la kupongezwa, lakini bado tuna changamoto kubwa sana ya ajira kwa vijana wetu, kwa taarifa ya Shirika la Kazi Duniani ya mwelekeo wa ajira kwa vijana ulimwenguni (Grobal Employment Trend for Youth) inaonesha kuwa tatizo la ajira kwa vijana Tanzania wenye elimu kuanzia sekondari na kuendelea ni kubwa kuliko wale wenye elimu ya kiwango cha chini. Aidha, Watanzania wenye elimu za chini wamepata ajira lakini ajira zao ni duni ama kipato cha chini na za mazingira hatarishi kama sehemu mojawapo ya kuwatumikisha kwa kuwa uelewa wao juu ya masuala ya sheria na taratibu za kazi ni mdogo.
Mheshimiwa Spika, lazima tukubali kuwa kilichotufikisha hapa ni aina ya elimu tunayoipata kutoka mashuleni. Hatua ya kwanza ya kulitatua tatizo hili ni kugusa mitaala yetu kwanza, bado ipo kikoloni ndio maana kila kijana anawaza kuajiriwa zaidi kuliko kujiajiri na hili sio kosa lao, yaani hakuna kitu tunachokiogopa kama mitaala yetu ya elimu kuibadilisha ili iendane na mazingira yetu ya sasa ili itusaidie kukabiliana na hili tatizo la ajira kwa vijana.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, tunajifunza mambo mengi shuleni ambayo hayana uhusiano wa moja kwa moja na mazingira yetu. Niliwahi kusema kuwa kwa nini mfano tusikubali kuingiza masomo ya ufundi kwenye shule zetu zote za sekondari kutegemeana na mazingira shule ilipo? Cha kushangaza hata zile shule zinazotoa fani za ufundi kwa sasa zipo taabani, hata tukienda kwenye shule hizo tukaulize wangapi wanasomea masomo hayo ya ufundi tutakuta hakuna. Tabaka hili la ukosefu wa ajira kwa vijana ni kubwa sana na kila mwaka idadi inazidi kuongezeka, hii ni nguvu kazi kubwa ambayo ni wajibu wa Serikali kuiwekea mipango mizuri ya ajira ili iweze kuzalisha, vijana kukosa ajira kuna athari zake kubwa.
Naiomba Serikali ije na mpango mzuri zaidi wa kuwasaidia vijana wetu katika kujiajiri na kuajiriwa, Serikali iweze kuajiri vijana wenye uwezo na kuwatengenezea fursa vijana wengine katika ajira binafsi hasa katika kilimo, nchi yetu ina ardhi kubwa sana hivyo tukiwekeza hasa kwenye kilimo kwa vijana wetu tutapata faida kubwa, kwanza ajira yenyewe kwa vijana, kuingiza kipato na Serikali kupata kodi ya mazao, uzalishaji wa chakula utaongezeka na kupelekea Taifa kuwa na chakula cha kutosha. Lakini tukiendelea kusema vijana wajiajiri na hatujawahi kujiuliza wanajiajirije? Hiyo mikopo wanaipataje? Sote tunajua masharti magumu ya benki zetu hapa nchini, benki hawatoi fedha bila kuwa na asset ya kuweka kama bond, hawa vijana wana asset gani? Ni kijana yupi mwenye hati ya nyumba au kiwanja au chochote anachoweza kukiweka kama bond ili apate mkopo?
Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto zote nilizotangulia kuzisema na kushauri, lakini naipongeza tena Serikali kwa kuweza kutambua umuhimu wa kundi hili la vijana, kama fursa muhimu na kwa maendeleo ya Taifa, naipongeza Serikali kwa kuendelea na uboreshaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
Katika mwaka 2019/2020 Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Vijana umetoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 3.2 ambapo vikundi 586 vyenye jumla ya vijana 4,222 kutoka katika Halmashauri 155 walipata mikopo hiyo. Hata hivyo naishauri Serikali kuwaendeleza wabunifu mbalimbali katika vifaa mbalimbali walivyobuni ili viweze kulisaidia Taifa letu, na sisi tuwe na vifaa vilivyobuniwa hapa kwetu, hili pia litasaidia kuongeza chachu kwa vijana wetu kuwa wabunifu zaidi.
Mheshimiwa Spika, tuna changamoto pia inayowakabili wenzetu wenye matatizo ya ulemavu, hawa wanapaswa kuendelezwa kulingana na matatizo waliyokuwa nayo, ni wajibu wa Serikali kuhakikisha watu wenye ulemavu wanaendelezwa katika fani mbalimbali ili waweze kujiajiri na si kuwaona baadhi wakiwatumia huko mitaani kuomba omba misaada, hii haileti taswira nzuri kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, kama tunavyojua uwekezaji ni njia pekee inayoleta maendeleo na kuzalisha ajira, tukiwa na wawekezaji wengi hasa katika sekta ya viwanda wataleta tija kubwa na faida kwa wananchi, ni wajibu wa Serikali kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili kuwavutia wawekezaji wengi zaidi. Hata hivyo naipongeza Serikali kwa kuendelea kuratibu na kusimamia shughuli za kuhamasisha na kufanikisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuvutia mitaji, teknolojia na ujuzi ambao ni chachu ya maendeleo katika sekta mbalimbali.
Aidha, tumeambiwa Serikali yetu imeendelea kufanya tafiti za kisekta (investment sectoral profiles) ili kubaini hali halisi ya ukuaji, mnyororo wa thamani, fursa zilizopo na changamoto za kisekta kwa lengo la kutoa mapendekezo ya maboresho katika sekta husika, hii itasaidia sana katika kurekebisha baadhi ya maeneo yenye changamoto. Katika hatua za awali tumeona tafiti hizo zimefanyika katika maeneo ya mbolea na kemikali, mifugo na mazao yake, pamba, uchakataji wa mazao ya kilimo kama vile korosho, michikichi na parachichi, nafaka na mbegu za mafuta. Halikadhalika matokeo ya tafiti hizo yameendelea kutumika katika kunadi fursa mbalimbali za uwekezaji ndani na nje ya nchi na kuishauri Serikali kuhusu mikakati na maboresho yanayohitajika katika kuvutia uwekezaji kwenye sekta husika, mwenendo huu ni mzuri na wenye kuleta tija.
Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali kwa kuandaa mapendekezo ya Bajeti ya mwaka 2020/2021 kwa kuzingatia sera na miongozo ikiwa ni pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2020/2021. Mpango huu ni wa mwisho katika mfululizo wa mipango ya kila mwaka wa kutekeleza Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/2017 – 2020/2021) wenye dhima ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya uchumi na maendeleo ya watu wetu. Ni hatua nzuri na ya kuungwa mkono.
Aidha, naipongeza Serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati na kwa gharama nafuu, Serikali imetuambia Mahakama imeendelea kuimarisha huduma kwa kuweka mifumo na taratibu mbalimbali za kuwafikia wananchi katika maeneo yote nchini ili kupunguza mrundikano wa mashauri na kuhakikisha mashauri hayo yanamalizika kwa wakati. Mojawapo ya utaratibu unaotumika ambao ni mzuri na umeleta tija ni kuwatumia Mahakimu wenye mamlaka ya ziada (extended jurisdiction) kusikiliza mashauri ya Mahakama Kuu, ni utaratibu mzuri wenye kufanya sasa Mahakama zetu kutokuwa na mrundikano wa mashauri.
Mheshimiwa Spika, kutokana na jitihada kubwa zinazoendelea kufanywa na Serikali za kujenga uchumi wa viwanda, napenda kuipongeza Serikali kwa kuwezesha jumla ya viwanda vipya zaidi ya 4,000 vimejengwa katika mikoa mbalimbali. Viwanda vilivyojengwa vinazalisha bidhaa za ujenzi, pamoja na viwanda vya kusindika mazao ya kilimo ikiwemo nafaka, matunda, mafuta ya kupikia na bidhaa za ngozi. Ujenzi huu wa viwanda vipya nchini, umechangia kupatikana kwa ajira mpya 482,601 nchi nzima, ni vyema sasa tukaongeza juhudi zaidi ili viwanda viongezeke, wananchi wetu wapate ajira kwa wingi.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.