Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Rombo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, wakati tunaelekea katika ukomo wa Bunge hili, napenda kuchukua fursa hii kukupongeza na kuwapongeza Wabunge wenzangu wote kwa kazi tuliyofanya hapa kwa muda wa miaka hii mitano.
Mheshimiwa Spika, tumepata changamoto kadhaa lakini sote tumshukuru Mungu na changamoto hizo zitumike katika kuboresha Bunge la Kumi na Mbili.
Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Waziri Mkuu kuna mambo mengi yaliyozungumzwa. Hata hivyo ningependa kuchangia yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza ni kuhusu elimu kuna ongezeko kubwa la watoto wanaoingia katika shule za msingi na sekondari hasa baada ya Serikali kuondoa ada. Hata hivyo ongezeko hilo haliendani na hali halisi iliyopo katika shule zetu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu uhaba wa walimu, ili kuhakikisha dhamira ya Serikali kukuza elimu inafanikiwa, Serikali inao wajibu wa kuongeza ajira za walimu pamoja na uboreshaji stahiki zao yaani makazi yao, mishahara, posho na stahiki nyingine.
Mheshimiwa Spika, pili ni vyumba vya madarasa, kila mwanzo wa mwaka wa masomo katika kidato cha kwanza na cha sita kunakuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa. Hali hii inaleta usumbufu mkubwa kwa wanafunzi kwa kuwa wengine huchelewa kuanza masomo. Kwa kuwa idadi ya wanafunzi wanaomaliza darasa la saba na wale wanaomaliza kidato cha nne wanajulikana, wataalam wetu wanao wajibu wa kulishughulikia tatizo hili mapema ili kuondoa usumbufu.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo bado tuna upungufu mkubwa wa vyumba vya maabara na vifaa vya maabara, ni vema Serikali kuangalia katika bajeti hii uwezekano wa kukamilisha vyumba vya maabara ambavyo vilianzishwa.
Mheshimiwa Spika, shule nyingi za zamani za msingi zinaelekea kubomoka. Jimboni kwangu kuna shule nyingi zinabomoka na hazikaliki au zinapaswa kufungwa. Kama Serikali ilivyofanya jitihada ya kuboresha shule za sekondari za zamani ione uwezekano wa kuboresha shule za misingi pia.
Mheshimiwa Spika, tatu ni shule za ufundi; ni muhimu tuharakishe ujenzi wa shule za ufundi katika kila Wilaya hasa kipindi hiki ambacho tunahimiza uchumi wa viwanda na kuimarisha private sector ili vijana wetu baada ya kumaliza elimu yao katika ngazi mbalimbali waweze kujiajiri.
Mheshimiwa Spika, mageuzi yaliyofanyika kuanzishwa kwa TARURA yameleta mafanikio makubwa sana katika Halmashauri zetu. Hata hivyo, TARURA inakumbwa na tatizo kubwa la kibajeti.
Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali iangalie uwezekano wa fedha za Mfuko wa Barabara kugawanywa kwa kiwango sawa kati ya TANROADS na TARURA.
Mheshimiwa Spika, tatizo la maji ni kubwa sana nchi nzima. Katika jimbo langu limekuwa kubwa zaidi kwa sabubu ya mabadiliko ya tabianchi yaliyosababisha chemichemi nyingi kukauka, ongezeko la binadamu na wanyama na kadhalika. Pamoja na hayo yote chanzo cha maji kimekuwa kile kile tangu enzi za ukoloni.
Mheshimiwa Spika, napenda kuishukuru Serikali kwa dhamira yake ya kuanzisha chanzo kipya cha Ziwa Chala. Naiomba Serikali iharakishe utekelezaji wa mradi huu ili kupunguza tatizo hili.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo tunapoteza maji mengi sana kutokana na maji ya mvua. Wilaya ya Rombo tuna mito mingi sana ya msimu na inayopitisha maji mengi sana wakati wa mvua na ina makorongo ambayo yanaweza kuzuiwa ili kuhifadhi maji hayo sambamba na kutoa elimu kwa wananchi juu ya kuhifadhi maji.
Mheshimiwa Spika, baada ya kuporomoka kwa vyama vya ushirika Waziri Mkuu amefanya jitihada kubwa za kuufufua na kupambana na ufisadi ndani ya ushirika. Chama cha Ushirika cha KNCU ambacho nacho kiliingiliwa na ufisadi kilikuwa msaada mkubwa kwa wakulima wa kahawa katika Wilaya ya Rombo na Mkoa wa Kilimanjaro kwa jumla. Hivi sasa wakulima wengi wameamua kuachana na kilimo cha kahawa na kupanda mbogamboga na migomba. Licha ya ushirika, pembejeo ni ghali sana, bei ni ndogo na hivyo kuwakatisha tamaa wakulima. Ni vema Serikali iingilie kati ili zao hilo lisije likatoweka maana lilikuwa chanzo kikubwa cha fedha za kigeni na uchumi wa wananchi.
Mheshimiwa Spika, umezuka ukatili wa kuwadhalilisha watoto katika jamii. Watoto wanaingiliwa kinyume na maumbile, wanaingiliana wenyewe kwa wenyewe na mimba za utotoni mashuleni. Wengi hawaongelei jambo hili kwa kuchelea aibu lakini kama Taifa tusipokuwa makini Taifa letu linaweza kuja kugeuka kuwa la mashoga. Serikali iondoe uoga, ichunguze na kushughulikia tatizo hili.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa nishati, kazi inayofanyika kupeleka umeme vijijini na REA ni nzuri na ya kupongeza. Naiomba Serikali kuendelea kumaliza maeneo yaliyobaki na hasa katika jimbo langu yapo maeneo yaliyobaki na yenye malalamiko yafanyiwe kazi ili malengo yaliyokusudiwa yaweze kufikiwa.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa afya, katika awamu hii hospitali na vituo vingi vya afya vimejengwa nchi nzima. Katika Jimbo la Rombo ipo Hospitali ya Wilaya inajengwa na kituo cha afya. Hata hivyo Rombo tuna uhaba mkubwa wa watumishi wa idara ya afya. Ninaishauri sana Serikali kwamba sambamba na ujenzi wa hospitali na vituo hivi vya afya Serikali iajiri watumishi wa afya nchini kote.
Mheshimiwa Spika, mwisho mengi yamefanyika katika awamu hii. Katika miundombinu, sekta zote yaani barabara ingawa mvua zinazoendelea kunyesha imeleta athari kubwa lakini kazi inaendelea, usafiri wa anga na reli kazi zinaendelea, hali kadhalika meli na vivuko katika maziwa yetu yameboresha usafiri na sekta ya uvuvi. Kwa hali hiyo kama Watanzania tunao wajibu wa kupongeza jitihada hizi.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naomba kuwasilisha.