Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Kassim Majaliwa Majaliwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ruangwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nianze kwa kusema kwamba sote tunajua wajibu wetu wa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha pia kukutana hapa kwenye kikao hiki muhimu, Kikao cha Saba cha Mkutano wa Kumi na Tisa wa Bunge lako Tukufu kwa ajili ya kuhitimisha mjadala wa hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka huu wa 2020/2021.

Mheshimiwa Spika, aidha, ninakushukuru sana na Mheshimiwa Naibu Spika kwa pamoja na Wenyeviti wote wa Bunge, Katibu wa Bunge na timu yako kwa umahiri mkubwa uliouonyesha katika kusimamia mwenendo mzima wa majadiliano yetu ya hoja hii ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Spika, vilevile natoa shukrani zangu za dhati kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na Kamati ya Kudumu ya Bunge na Bajeti na Masuala ya UKIMWI kwa michango yao mizuri sana kwenye hoja hii ambayo imetolewa hapa kwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, kadhalika nitumie nafasi hii kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri wenzangu mliochangia hoja, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu wote, Wakuu wa Idara, Mashirika, Wakala wa Taasisi zote za Serikali pamoja watumishi wote kwa ushirikiano mkubwa walionipa katika kipindi chote cha mjadala wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, ingawa niliwahi kuwashukuru Mawaziri ambao nafanya nao kazi, lakini nalazimika pia kurudia tena kuwashukuru Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Mheshimiwa Angellah Kairuki, Waziri wa Nchi ambaye anashughulikia Uwekezaji. Pia ninaye Naibu Waziri wa Nchi, Mheshimiwa Mavunde, Mbunge wa Dodoma Mjini pamoja na Mheshimiwa Stella Ikupa, Mbunge na Naibu Waziri anayeshughulikia Walemavu.

Mheshimiwa Spika, bila kuwasahau Makatibu Wakuu ambao wanasimamia na kuratibu shughuli zote za Ofisi ya Waziri Mkuu, Bwana Tixon Nzunda, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu; yuko pia Mama Mwaluko, naye pia ni Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Bwana Massawe ambaye pia tunashirikiana naye vizuri sana akishughulikia eneo la Kazi; bila kuwasahau Watendaji wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu ambao pia tunafanya nao kazi kwa weledi mkubwa.

Mheshimiwa Spika, pia nitumie nafasi hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa pongezi zenu kwa Serikali na kwa michango yenu yenye hoja za kuboresha mipango na kazi zilizokusudiwa kutekelezwa na Serikali, hasa katika mwaka wa fedha ujao wa 2020/2021. Mjadala huu umeendelea kuthibitisha uimara na umakini wa Bunge letu katika kutekeleza wajibu wake wa kikatiba, lakini pia kuishauri Serikali na kusimamia vizuri Serikali yetu ili iweze kufanya kazi yake vizuri.

Mheshimiwa Spika, pia nataka niendelee kutumia nafasi hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote mliochangia na kuipongeza Serikali, pia kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais; na pia sisi wasaidizi wao ambao tunaendelea kushirikiana nanyi Waheshimiwa Wabunge katika kutekeleza shughuli mbalimbali za Serikali. Nami nataka nitumie nafasi hii kuwahakikishia kwamba salamu hizi nitazifikisha kwa Mheshimiwa Rais na Makamu wa Rais ili waendelee kuchapa kazi yao vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ni bajeti ya mwisho ya miaka mitano, binafsi napenda kukushukuru wewe binafsi na timu yako ya Bunge. Niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa michango yenu hasa katika kuchangia mambo yote muhimu ambayo tuliyafikisha mbele yenu na kwa kitendo chenu cha kupitisha bajeti zote zilizopita zile nne. Bajeti zote zimefanya kazi yake na nyie wenyewe mmeona matokeo ya bajeti hizo kwa miradi mikubwa na mingi yenye thamani ya kutosha, ambayo pia inaendelea kutumika na wananchi. Ni matumaini yangu kwamba kwa spirit hiyo hiyo, basi mtaniunga mkono pia kwenye bajeti hii kwa kuipitisha kwa kishindo. Ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja hii ya Waziri Mkuu imechangiwa na Waheshimiwa Wabunge 80. Kati yao Waheshimiwa Wabunge 62 walichangia kwa kuzungumza moja kwa moja hapa Bungeni na Waheshimiwa 18 walichangia kwa njia ya maandishi. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote mliochangia hoja ya Waziri Mkuu. Hata hivyo, kutokana na ufinyu wa muda ninaomba uridhie nisiwataje majina, kwani tayari majina yao yameingia kwenye Hansard.

Mheshimiwa Spika, Serikali imejibu hoja nyingi zilizowasilishwa na Waheshimiwa Wabunge kupitia Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri hapa mbele yetu jioni hii. Aidha, kutokana na ufinyu wa muda pia, hoja nyingine zitajibiwa kwa maandishi na kutolewa ufafanuzi kwa kina na Waheshimiwa Mawaziri wakati wa kuhitimisha bajeti za kisekta.

Mheshimiwa Spika, kupitia Waheshimiwa Mawaziri, wamejibu karibu maeneo mengi ambayo tumeyakusudia kuyajibu leo hii. Nami ninayo maeneo machache sana ambayo nitayakamilisha ili kuweza kutosheleza mahitaji ya ushauri, maeneo ambayo yanahitaji ufafanuzi kwenye mambo muhimu ambayo inabidi yatolewe leo ili yasaidie pia kuongoza katika upitishaji wa bajeti yetu ambayo tunayo leo.

Mheshimiwa Spika, moja ya jambo kubwa ambalo limezungumzwa wakati wa michango yetu ilikuwa ni suala la maafa. Suala la maafa yaliyojadiliwa hasa ni kutokana na uwepo wa mvua nyingi sana msimu huu ambazo zimenyesha na kusababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu mbalimbali zikiwemo barabara, nyumba za wananchi, miundombinu ya taasisi zinazotoa huduma za jamii na pia imesababisha vifo. Haya niliyaeleza nilipokuwa nawasilisha hoja yangu siku ya mwanzo na kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwamba Serikali inaendelea kuchukua za kurejesha hali hiyo, ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini za uharibifu wa miundombinu mbalimbali na pia kuainisha mahitaji ya maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, tumekubaliana kwamba tutafanya hivyo baada ya msimu wa mvua kukamilika au kwisha ili sasa tathmini ziweze kufanywa na kujua kiwango halisi cha mahitaji kwenye maeneo hayo yaliyoharibika ili tuweze kufanya urejeshi wa miundombinu hiyo.

Mheshimiwa Spika, vilevile Serikali imeweka kwenye mipango yake ya utekelezaji wa suala la urejeshaji wa hali ya miundombinu kwa vipindi vya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu kwa kuzingatia mahitaji husika. Aidha, Kamati za Maafa katika ngazi za Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji zitaendelea kusimamia suala zima la kuzuia, kujiandaa kukabilina na maafa na kurejesha hali pale ambapo wana uwezo napo.

Mheshimiwa Spika, pale ambapo uwezo umewazidi kiasi, basi, taratibu za kawaida kufika Ofisi ya Waziri Mkuu inayoratibu maafa itaambiwa na yenyewe itachukua hatua stahiki ili kushirikiana na Mikoa, Wilaya, Kata, pamoja na Vijiji kwenye maeneo husika. Baada ya tathmini katika kila eneo Wizara za Kisekta zitaendelea kushughulikia athari zilizojitokeza kwa rasilimali zilizopo kwa kuzingatia mipango na bajeti ambayo tumejipangia.

Mheshimiwa Spika, niendelee kutumia nafasi hii kuelekeza Viongozi na Watendaji wote kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kuanzia ngazi ya Mkoa, Wilaya, mpaka Vijijini kusimamia ipasavyo upangaji na utekelezaji wa mipango na matumizi ya ardhi katika ngazi ya Mikoa, Wilaya na Vijiji. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba wananchi wanatambua maeneo salama kwa ajili ya makazi na shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji, biashara pia na shughuli za uwekezaji ambazo zipo kwenye maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, niendelee kusisitiza kuwa Wakala wa Barabara Nchini, TANROADS na TARURA kuendelea kufanya kaguzi za mara kwa mara za madaraja na barabara zetu ili kuchukua hatua kwa wakati na hivyo kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kwenye maeneo yetu. Aidha, wananchi wote wachukue tahadhari kwa kuhama sehemu za mabondeni na kuzingatia taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinapotolewa na mamlaka hiyo hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia taarifa zinazotolewa na mamlaka za hali ya hewa, itatusaidia pia kuchukua tahadhari kabla ya maafa haya kutokea. Kwa sasa tunaendelea kushirikiana na wananchi wa Mkoa wa Pwani, eneo la Wilaya ya Rufiji na Kibiti kupitia Mheshimiwa Mbunge ambaye pia tunaye hapa, Mbunge wa Rufiji, kuona namna ya kuweza kusaidia yale maeneo yaliyopata athari hasa kwenye mafuriko yanayoisha sasa. Tunatambua kuwa mafuriko yamesambaa nchini kote, lakini tutaangalia wapi ambako yamezidi kiasi na athari kubwa zimejitokeza kama vile Rufiji ambako pia kumejitokeza tatizo hilo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naendelea kusisitiza kwamba Serikali itaendelea kushirikiana na wananchi kuhakikisha kwamba maeneo haya tunaendelea kuyasimamia vizuri. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuomba Mungu, mvua tunazitaka, lakini pale ambapo kuna madhara yanajitokeza, basi tuendelee kushirikiana kwa pamoja.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ambalo napenda nilizungumzie ni lile ambalo Mheshimiwa Waziri Jenista Mhagama amelizungumza. Yeye amezungumzia Tume ya Uchaguzi, mimi nataka nizungumzie uchaguzi wenyewe utakaofanyika mwaka huu mwezi Oktoba.

Mheshimiwa Spika, sote tunafahamu kwamba mwezi Oktoba mwaka huu nchi yetu itafanya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani. Hivyo, tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu Mwezi Oktoba, Serikali inatoa wito kwa Viongozi wa Vyama vya Siasa na wadau wengine wa uchaguzi kuzingatia katiba, sheria, kanuni na miongozo iliyopo katika kuendesha shughuli za uchaguzi katika Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa.

Mheshimiwa Spika, lengo hapa ni kuhakikisha tu kwamba nchi yetu inaendelea kulinda na kuenzi tunu yetu ya amani, umoja, upendo na mshikamano wa Kitaifa, kama tulivyoachiwa na waasisi wetu wa Taifa hili. Nami nataka niendelee kuunga mkono kauli ya Mheshimiwa Rais kwamba uchaguzi ujao utakuwa wa huru na wa haki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano kama ilivyokuwa na watangulizi wake itaendelea kulinda amani hiyo, mshikamano wetu na demokrasia yetu tuliyonayo katika nchi yetu. Kwa hiyo, niwasihi viongozi na wanachama wa vyama vyote vya siasa na wananchi kwa ujumla kuendelea kulinda sasa amani ile na kuendeleza mshikamano katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu ili kla mmoja apate haki yake ya kuchagua na kuchaguliwa.

Mheshimiwa Spika, maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu wa 2020 yanaendelea vizuri. Hivi sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi inajiandaa na awamu ya pili ya maboresho ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura yanayotarajiwa kuanza wakati wowote ule mwezi huu. Baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kufanya majadiliano na wadau, maazimio mengi yamekubalika na yamefikiwa. Sasa ni jukumu la Tume kutekeleza makubaliano yale. Lengo la majadiliano yale ilikuwa ni kuwezesha Tume kujipanga, kupata vifaa vyote vinavyohitajika kwa ajili ya tahadhari dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu ya Covid 19.

Mheshimiwa Spika, Tume ya Taifa ya Uchaguzi itatangaza ratiba ya uchaguzi kwa kuzingatia matakwa ya katiba na sheria. Kwa sasa bado ratiba haijatangazwa. Nalisema hili kwa sababu tumeona kwenye mitandao watu wakitamka Ratiba ya Tume ya Uchaguzi. Hiyo iliyotoka kwenye mitandao siyo sahihi. Wananchi wenye sifa za kugombea nafasi mbalimbali waendelee kujitokeza, nanyi Waheshimiwa Wabunge mliomo ndani ya Bunge hili, nami naungana nanyi na pia nawaombea sana na ninaendelea kuwaombea muweze kurudi tena baada ya uchaguzi ujao wa mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo ambalo pia ningependa nilizungumzie ambalo limezungumzwa sana na viongozi wetu au Waheshimiwa Wabunge hapa ndani ni homa kali ya mapafu (Corona).

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge, nami naungana nanyi kueleza kwamba hali ya ugonjwa huu Duniani ni mbaya na kwamba wote mnakubaliana nami kuwa ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona umekuwa na athari kubwa kijamii lakini pia na kiuchumi Duniani kote. Aidha, katika kipindi hiki tumeshuhudia changamoto mbalimbali kutokana na hatua zinazochukuliwa na baadhi ya nchi katika kukabiliana na ugonjwa huu.

Mheshimiwa Spika, baada ya maambukizi ya virusi vya Corona kuingia nchini kwetu na hata kabla ya kuingia nchini, Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli alilitangazia Taifa kuwa ugonjwa huu ni hatari na Watanzania tujiandae na tahadhari kadhaa zilianza kuchukuliwa ndani ya Serikali ili kukabiliana na ugonjwa huu pindi utakapokuja kwa wakati huo. Lakini baada pia ya ugonjwa huu kujitokeza nchini, Serikali pamoja na mambo mengine, tulianza kujipanga vizuri kuanza kukabiliana na ugonjwa huu.

Mheshimiwa Spika, kwanza tuliunda Kamati za Kitaifa, moja ya Kamati ya Kitaifa inayoratibu mapambano yote ya virusi vya UKIMWI ikisaidiwa na Kamati ya Makatibu Wakuu na Kamati ya wataalam. Kamati hizi ni za Kitaifa kwamba zinasimamiwa pia na Serikali mbili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, jukumu mojawapo la Kamati hizo ni kuwezesha nchi kupunguza madhara makubwa ya Kijamii lakini na kiuchumi ambayo yanaweza kusababishwa na ugonjwa huu wa homa kali ya mapafu.

Mheshimiwa Spika, upande wa kijamii tunaendelea kutoa elimu na upande wa kiuchumi kama ambavyo Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameeleza ameunda timu ya wataalam, wachumi, wanaendelea kufanya mapitio ya athari zinazoweza kujitokeza katika kipindi hiki kufuatia tatizo hili. Tunajua biashara nyingi zimezorota na zinaendelea kuzorota lakini pia shughuli za kiuchumi nyingi nyingine zimeanza kusimama na kwa hiyo lazima tathmini ifanyike hatimaye Serikali itatoa muelekeo.

Mheshimiwa Spika, vile vile kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, elimu kuhusu namna ya kujilinda dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona inaendelea kutolewa kote nchini katika sehemu mbalimbali pamoja na kuwahusisha kwa karibu zaidi viongozi wa dini, wadau mbalimbali wa sekta na wataalam wenyewe wa Sekta. Niendelee kusisitiza Wizara, Mikoa, Wilaya ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kuendelea kutoa elimu kwa jamii yetu kupitia watendaji wa Serikali walioko kwenye maeneo hayo na wananchi wote wapate kujua nini namna gani wanaweza kujilinda na maambukizi ya ugonjwa huu.

Mheshimiwa Spika, hadi kufikia leo tarehe 6 Aprili, tunao wagonjwa 24, mpaka asubuhi ilikuwa wagonjwa 22 lakini baada ya vipimo vya waliochukuliwa vipimo jana na kufikishwa kwenye maabara zetu mchana huu tumepata taarifa kwamba wagonjwa wawili wameongezeka, mmoja Tanzania Bara na mmoja Zanzibar na kufanya wagonjwa wote kuwa 24. Na hao ndiyo wamethibitika kuwa na ugonjwa huo. Kati ya wagonjwa hao, watatu wamepona na kuruhusiwa kutoka katika hospitali na mmoja amefariki dunia wakati wagonjwa 18 wanaendelea vyema na matibabu.

Mheshimiwa Spika, maelezo ya kitaalam yanaonesha kuwa virusi vya Corona vinaweza kusambaa endapo mtu anagusa majimaji kama mafua, mate na makohozi ya mtu alie na virusi hivyo na kisa kujigusa kwenye mdomo, macho au pua. Kwa kuzingatia hilo, Serikali imeendelea kuwafuatilia watu wote ambao kwa nyakati tofauti wamekuwa karibu sana na wagonjwa hao. Hadi sasa watu 685 walikuwa wanafuatiliwa ambapo watu 289 wamemaliza siku 14 za kufuatiliwa na vipimo vyao vimethibitisha kuwa hawana maambukizi ya virusi vya Corona. Watu wengine 396 waliobaki wanaendelea kufuatiliwa ili kujiridhisha kuwa iwapo wana maambukizi ya virusi hivyo basi waweze kujitenga kwa kukaa kwenye maeneo maalum yaliyopangwa.

Mheshimiwa Spika, hatua zinazochukuliwa katika kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Corona ni pamoja na kudhibiti mipaka yetu, kufanya ukaguzi au screening kwa wageni wote wanaoingia nchini kutoka nje pamoja na kuwaweka katika uangalizi wa siku 14 kwenye maeneo maalum. Aidha, ndege za nje zinazoingia nchini zimeshajifuta zenyewe kwa sababu kwenye nchi wanakotoka wamefunga mipaka na kwamba hakuna kuingia wala kutoka kwa ndege.

Mheshimiwa Spika, pia, ndege zetu nazo tumezizuia kufanya safari za nje, kwa hiyo ndege zetu sasa zinafanya safari za ndani pekee. Tumezuia wafanyakazi kwenda nje ya nchi, tumeimarisha mipaka, sambamba na kuhakikisha wasafiri wote wanaoingia nchini wanalazimika kuwekwa chini ya uangalizi wa lazima kwa siku 14 kwa lengo la kudhibiti mienendo ya wasafiri nchini chini ya ulinzi kwa masaa 24.

Mheshimiwa Spika, nimetoka kuzungumza leo mchana huu na Wakuu wa Mikoa wote tena, nilizungumza nao wiki iliyopita lakini pia leo nimefanya tathmini ya kazi hiyo inavyoendelea na nimepata taarifa ya kila Mkuu wa Mkoa namna ambavyo wamechukua jambo hili kwa umakini mkubwa na kila mkoa umeshatenga maeneo haya na hasa kwenye wilaya zilizoko pembezoni kwenye mipaka yetu ambako abiria wengi sasa wanatamani kuingia kupitia barabara. Maeneo yote yameimarishwa, lakini pia tumetenga na maeneo ya kuhifadhi, kuwatenga hawa wote wanaoingia nchini kwa siku 14 na ujumbe huu utakapofika naamini wao hawatakuja tena nchini.

Mheshimiwa Spika, nchi zote jirani zimefunga mipaka yake, hawaingii wala hawatoki kwa hiyo, automatically hatuwezi kupata mtu yeyote anayeweza kuja. Hata hivyo, wale wote wanaokuja wanaendelea kuwekewa kwa siku 14 na kufuatiliwa afya zao na tumeimarisha ulinzi wa maeneo hayo ili kuzuia hao walioko kwenye ulinzi huo kutoka au watu wengine kuingia kwa maana ya kuja kufanya mawasiliano na walioko pale ndani.

Mheshimiwa Spika, vilevile kutokana na umuhimu wa kuwatenga watu wanaofuatiliwa, Serikali imeagiza mikoa yote nchini kutenga maeneo maalum ambayo leo wametoa taarifa na uangalizi kuimarisha na waimarishaji wote na wafuatiliaji wa afya zao wote wapatiwe vifaa maalum ili kuendelea kufanya kazi hiyo bila kuwa na athari zozote zile za maambukizi kwao.

Mheshimiwa Spika, hatua hii ni muhimu katika kudhibiti kuenea zaidi kwa maambuzi ya virusi vya Corona na kati ya wagonjwa hawa, walio wengi ni wale waliotoka nje yaani watu wa Mataifa ya nje lakini na Watanzania ambao walisafiri kwenda nje ya nchi na kuja hapa ndani na maeneo haya yaliyotengwa yatatumika na kila mmoja bila kujali wadhifa wake na nalitamka hili kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameeleza hali iliyoko kule visiwani.

Mheshimiwa Spika, ni kweli tulikuwa na Waziri ambaye alitakiwa kwenda kwa matibabu, alikataa baadaye akaenda Mnazi mmoja kwa matibabu na baadaye akatakiwa kwenda kujitenga bado alikataa, lakini Serikali ilichukua hatua na ikamtoa na kumpeleka sehemu ya kutengwa, kwa sasa yuko eneo la kutengwa. Na narudia kutamka hili ya kwamba maeneo haya ya kutengwa yamewekwa kwa madaraja kadri ya uwezo wa anayetengwa. Tumetafuta mabweni ambayo watu wanalala bure, kwa hiyo, asiyekuwa na uwezo wa kulipa atalala huko. Tumetafuta maeneo ambayo yanaweza kulipiwa lakini ya hadhi tofauti tofauti kwa hiyo yeyote anayehitaji kwenda lakini yote yameteuliwa na yanasimamiwa na sio maeneo mengi, ni machache ili kurahisisha usimamizi na kwa hiyo kila mtu atakwenda eneo hilo kulingana na uwezo wake. Tumetafuta watu ambao watatoa huduma ya chakula ilia pate chakula kwa gharama ambayo anaweza kuimudu na maeneo haya yana ulinzi kama ambavyo nimeeleza.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kila mmoja anayetakiwa kujitenga ameenda maeneo ambayo yameandaliwa rasmi kwa gharama ambazo yeye anaweza kuzimudu. Tunafanya hili ili kuondoa manung’uniko yaliyokuwa yamejitokeza awali kwamba watu walikuwa wanapelekwa maeneo ya gharama kubwa wakiwa hawana uwezo. Kwa hiyo, tumeimarisha hilo na sasa malalamiko haya yamepungua.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaimarisha maabara mbalimbali nchini ili ziweze kutoa huduma za upimaji ikiwemo maabara zilizopo kwenye mikoa na mikoa hiyo ni kama vile Arusha tunayo maabara inaweza kupima sasa vipimo vyote vya Kanda ya Kaskazini, Dodoma, hapa katikati ya nchi, Kigoma, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Pwani pamoja na Tanga. Maeneo haya yote yana maabara na kwa hiyo itarahisisha kupeleka vipimo kwa umbali mfumo na kupata majibu kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na vipimo vyote ni lazima ithibitishwe na Mganga Mkuu wa Serikali na atakayetoa taarifa ni Waziri wa Afya pekee. Kwa hiyo, natambua mchango wako Mheshimiwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani juu ya watu kutoa Taarifa kiholela, Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa, kila mmoja anatamka anavyotaka. Tumetoa maelekezo kwamba Taarifa zote za ugonjwa huu zitatolewa na Waziri wa Afya. Kama ni lazima atatoa Waziri Mkuu, kama ni lazima sana, basi atatoa Makamu wa Rais au Rais mwenyewe. Utaratibu huu utasaidia kuleta taarifa za uhakika zilizothibitishwa na watoaji hao ndiyo ambao watahusika. Kwa hiyo, tutalisimamia hili ili tuondoe utamkaji holela wa kila mmoja kadri anavyojisikia.

Mheshimiwa Spika, vipimo hivi pia vinapimwa na hospitali zote za Rufaa, Kanda, za Mikoa nazo zinaratibiwa kutoa huduma za upimaji sambamba na maeneo ya mipakani. Shughuli hizi za upimaji zinafanyika kwa usimamizi wa maabara kuu ya Taifa ya Afya ya Jamii kwa lengo la kuthibitisha ubora na vipimo hivyo kuratibiwa na utoaji wa matokeo pia nao umeratibiwa.

Mheshimiwa Spika, nchi yetu pia imeendelea kushirikiana kwa karibu na Shirika la Afya Duniani, Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika katika kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu na kwa hiyo tunabadilishana mawazo lakini pia tunapeana mbinu mbalimbali za kukabiliana na ugonjwa huu.

Mheshimiwa Spika, yako malalamiko ya baadhi ya Watanzania wakitaka tuchukue hatua ambazo zinachukuliwa na nchi nyingine. Lakini nataka niseme kwamba watu lazima tutambue kwamba nchi hizi zina mazingira tofauti. Tanzania ina mazingira tofauti na nchi nyingine ambazo watu wengi wanazilinganisha na umuhimu ni kwamba Taifa lazima tujipange tuhakikishe kwamba tundhibiti maambukizi kusambaa nchini na hatua tuliyoifikia sasa tunafurahi kwa sababu tunaona tunaanza kupata ushirikiano na wananchi, pindi ikionekana kuna mtu ametoka nje ameingia nchini bila kupitia kwenye vituo vya uhifadhi tunapewa taaarifa na sisi tunachukua hatua za kuwafuata popote walipo na pale ambako kuna mtu ana hisiwa kuwa na tatizo la Corona ili kuitaka Serikali iweze kuthibitisha basi wananchi wanatupigia kwa namba ile 199 na Serikali inachukua hatua ya kuwafuatilia na kuwafanyia vipimo na ikithibitika tunawatenga mahali rasmi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka nieleze tu kwamba nchi yetu iko makini na Serikali inafanya kazi hiyo kwa umakini na tutaendelea kuwahusisha pia wadau mbalimbali ambao watasaidia pia kuungana nasi katika kukabiliana na pambano juu ya jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na maandalizi kadri ya hali ilivyo kulingana na mazingira tuliyonayo kama ambavyo tumeyaeleza lakini Serikali inaendelea pia kufanya tathmini za kila wakati kuhusu changamoto zinazoweza kusababishwa na ugonjwa huu wa Corona na namna ambavyo tunaweza kuzitatua. Tunajua kuna changamoto za kiafya ambako wananchi wetu wengi wanapata madhara haya. Lakini pia kuna changamoto za kiuchumi ambayo nimeeleza mwanzo na Waziri wa Fedha ameeleza yote haya ni yale ambayo tunaendelea kuyafanyia tathmini. Na tathmini hizi zinafanywa na zile Kamati tatu ambazo tumeziteua. Moja, Kamati ya Kitaifa ambayo inasimamiwa na Waziri Mkuu, ya pili Kamati ya Makatibu Wakuu ambayo inasimamiwa na Makatibu Wakuu Viongozi wa Bara na Visiwani pamoja na Kamati ya Wataalam ambao pia kuna madaktari kutoka pande zote mbili ili kuweza kubadilishana. Kwa hiyo, kadri tathmini inavyofannywa, tukipata matokeo tunachukua hatua. Hatuwezi kwenda na hatua zote tunaweza tukaleta mkanganyiko ndani ya nchi. Muhimu zaidi ni kujiridhisha kwamba maambukizi haya hayaendelei.

Mheshimiwa Spika, lakini pia tunaendelea kukabiliana na changamoto mbalimbali na Serikali kushirikiana na wadau wengine imeendelea kutafuta fedha kwa ajili ya mapambano dhidi ya ugonjwa huu ili kuweza kumudu kupambana dhidi ya maambukizi. Vilevile Serikali imeendelea kupokea michango ya mtu mmoja mmoja kutoka Taasisi mbalimbali kwa lengo la kuunga mkono mapambano dhidi ya ugonjwa huu. Wiki mbili zilizopita nilipokea misaada kutoka kwa wadau mbalimbali yenye thamani ya bilioni 1.8 na tarehe 8 wadau kadhaa wamejitokeza kwa hiyo, tutapokea tena misaada hapa Dodoma kwa kila ambaye ameamua kuchangia watakuja watachangia pale Ofisi ya Waziri Mkuu na tutawatangaza rasmi kwa mchango wao na michango hii yote inayochangwa na wadau hawa itatumika kama ambavyo imekusudiwa. Tunaendelea kuratibu kwa kupata vifaa mbalimbali ili kuwezesha watendaji wetu au wataalam wetu kufanya kazi hiyo bila kuwa na madhara wakati wote wanapohudumia ndugu zetu ambao wamepata madhara hayo.

Mheshimiwa Spika, niendelee kusisitiza kuwa viongozi wa mikoa na wilaya waendelee kusimamia kwa karibu, Kamati za Maafa ziendelee kushirikiana kwa pamoja na madaktari wetu kuhakikisha kwamba wanasaidia kupambana dhidi ya maambukizi haya na kama ambavyo nimewaeleza, nimezungumza na Wakuu wa Mikoa, tumewasisitiza na kuwapata muelekeo wa namna ya kufanya kazi zao kwenye maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, aidha, kwa kuwa suala hili ni mtambuka nitoe wito kwa waajiri, wafanyakazi, wafanyabiashara, wavuvi, wakulima, wasafirishaji na wananchi wote kwa ujumla kuchukua tahadhari zaidi kwani sote tunao wajibu wa kujilinda na kuwalinda wengine ambao wako kwenye mazingira hatarishi. Kadhalika maeneo ya huduma kama vile masoko, hospitali, vituo vya mabasi na vyombo vya usafiri kuepuka misongamano isiyokuwa ya lazima na kuchukua tahadhari ikiwemo kutumia vifaa vya kinga. Haya ni mambo ambayo pia tumeyatolea msisitizo na pia tumewaagiza Wakuu wa Mikoa kusimamia, kila mmoja kwenye mkoa wake kupitia wilaya zake na wananchi nao waelimishwe ili waweze kujua njia zote sahihi za kujikinga na maambukizi.

Mheshimiwa Spika, ugonjwa huu hadi sasa umeonesha kutokuwa na dawa na unaleta madhara makubwa Duniani. Hata hivyo, tukiangalia hali ilivyo nchini mwetu hatuna bdi pia kila mmoja kuchukua tahadhari ya kutosha na tunaendelea kuwatahadharisha wananchi wote kwamba ni muhimu kufuata maelekezo ya wataalam wetu, madaktari wetu na maelekezo ambayo tunayatoa wakati wote.

Mheshimiwa Spika, nataka nitumie nafasi hii kushukuru sana vyombo vya habari kwa namna ambavyo wanafanya kazi yao katika kuelimisha wananchi wetu. Pia niwashukuru wasanii ambao pia wameaanza kutunga hata nyimbo za kufikisha ujumbe wa kuchukua tahadhari huku wakitoa elimu kwa wananchi namna ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona. Lakini pia tuendelee kuzingatia miiko ambayo tumeitoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, fursa ambayo tumeitoa kwenye maeneo machache ni kuwezesha kupata huduma lakini fursa hiyo isitumike vibaya kama vile kuendesha shughuli za kidini, tunataka tu siku za Ijumaa, Jumamosi kwa Sabato na Jumapili kwa wale wanaokwenda kwenye ibada za Jumapili na sio makongamano ya Kidini, hiyo tumezuia. Tunasema watu wakasali na watumie nafasi hiyo kuliombea Taifa. Lakini pia wanapokuwa huko, wazingatie ile miiko yote ya kukaa umbali na tumesema kama nyumba ni ndogo basi wengine wapate nafasi ya kukaa nje kwa nafasi ile ile ili mradi ule muda unaotumika kwa sala au swala utumike huo na watu waondoke waende maeneo yao. Tutaendelea kutathmini hali hiyo kadri siku zinavyokwenda tukiona maeneo hayo yana madhara makubwa, tutakuja kutamka vinginevyo kwa kushirikiana na viongozi wa maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, suala la usafiri tulidhani tukiacha watu wasafiri kutoka eneo moja mpaka lingine linaweza kusaidia na tumeelekeza mabasi yote yasijaze abiria, watu wakae kwenye viti, wasafiri wafike, inaweza kutusaidia zaidi na wakiwa kwenye mabasi kila mmoja azingatie. Tumeanza kuona baadhi ya wasafirishaji wanajali na wengine waendelee kujali na kwa kufanya hivyo itatusaidia zaidi kujikinga na maambukizi kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki ambacho tunaendelea kufanya tathmini ya hali ilivyo, Serikali inasisitiza wananchi kuweka umuhimu wa kufuatilia haya ambayo pia tunahitaji yafanyiwe kazi na watu wote kila mmoja aweze kuzingatia sheria na miongozo ambayo tumeitoa na tahadhari za kitaalam ambazo pia zimetolewa na watu wetu.

Mheshimiwa Spika, wakati tunapokea hoja, kwenye eneo hili nataka niendelee kuwahakikishia kwamba Serikali itaendelea kupokea ushauri wenu na ushauri huo tutauangalia kwa kupitia Kamati zetu za Tathmini ambazo tatu zimeundwa ili tuweze kuchukua hatua kadri tunavyokwenda. Lakini tunashukuru sana kwa michango yenu na ndiyo hasa mijadala yetu hapa kwenye awamu hii ilichukua nafasi kubwa. Kila aliyechangia anazungumza suala la Corona na anazungumzia pia suala la mradi.

Kwa hiyo, tumelichukua hili kama jambo muhimu na ni jambo la Kitaifa, lenye madhara ya Kitaifa na tumeona namna ambavyo tumeshirikiana wote bila kujali utofauti wetu kiitikadi, kidini, kisiasa lakini tumeendelea vizuri na sisi tumepokea mawazo yenu tutahakikisha tunayafanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, baada ya hoja hii kuwahakikishia Watanzania kwamba Serikali imeendelea kuwa makini nayo na kuchukua tahadhari zote na tunaratibu vizuri. Hoja nyingine ilikuwa ni hoja iliyojadiliwa na baadhi ya Wabunge kuhusu Ofisi ya Msajili wa Vyama Siasa kwamba ihakikishe inasimamia mwenendo wa vyama vya siasa kwa kuendelea kuchunguza na kufuatilia mienendo ya vyama hivyo ili vizingatie sheria, kanuni, taratibu na weledi kwa ustawi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo hili Serikali imepokea ushauri wa Kamati lakini pia Waheshimiwa Wabunge. Serikali inaahidi kuufanyia kazi kwa kuiwezesha Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kusimamia utekelezaji wa sheria ili kuhakikisha kwamba vyama vyote vya siasa vinatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Katiba, sheria na kanuni zilizokubalika kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, pia mwaka huu 2019/2020, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilichunguza na kuvitaka baadhi ya vyama vya siasa vilivyotuhumiwa kuvunja sheria kufuata utaratibu. Maelekezo ya msingi yalitolewa na Msajili, kwa hiyo, ni matumaini yangu kwamba maelekezo yale yatazingatiwa. Katika kuhakikisha kwamba vyama vya siasa vinakidhi na kutekeleza matakwa ya sheria zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ofisi inaendelea kufanya uhakiki wa vyama vya siasa kuhusu utekelezaji wa masharti hayo na matakwa mengine ya kisheria ili vyama hivyo viweze kufuata sheria hiyo ikiwemo na Sheria ya Gharama za Uchaguzi hasa kipindi hiki tukielekea kwenye chaguzi.

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ambayo ilijitokeza ni ile inayosema Serikali iangalie upya taratibu za utoaji wa vibali vya kazi na ukaazi kwa wataalam kutoka nje ikiwemo kuzingatia wataalam ambao hawana elimu rasmi lakini wana ujuzi katika sekta kama vile ukataji wa vito sambamba na kupunguza gharama za vibali vya kazi ili kuvutia wawekezaji. Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mavunde ameitolea ufafanuzi hoja hii lakini naomba niseme machache juu ya hili kwamba utoaji wa vibali vya kazi kwa raia wa kigeni unazingatia matakwa ya Sera ya Taifa ya Ajira ya mwaka 2008. Sera hiyo inabainisha kuwa ajira za wataalam wa kigeni hulenga zaidi katika kuziba pengo la ujuzi adimu na teknolojia. Kwa msingi huo, Serikali imeendelea kuzingatia vigezo muhimu vyenye kuhusisha elimu, ujuzi na uzoefu wa kazi husika katika utoaji wa vibali vya kazi kwa wageni ambao wanaingia hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, kuhusu gharama za vibali vya kazi, Serikali inaendelea na kukusanya maoni kwa lengo la kuifanyia mapitio sheria husika ambapo masuala ya ada pia yanaweza kuangaliwa. Hata hivyo, changamoto kubwa kwa wawekezaji si kiwango cha ada bali ni muda mrefu ambao umekuwa ukitumika kuomba kibali hicho hadi kutolewa. Tumefanya maboresho ili pia vinapoombwa vibali hivi viweze kutolewa kwa muda mfupi zaidi.

Mheshimiwa Spika, Serikali inakamilisha mfumo wa TEHAMA kwa ajili ya utoaji vibali vya kazi ili kurahisisha utoaji wa vibali hivyo kwa kipindi kifupi sana. Hivi sasa kazi ya kuweka miundombinu stahiki inaendelea na utaratibu wa kuzindua mfumo huo utafanywa siku za karibuni ili mfumo huo uanze kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ilikuwa ni Serikali iboreshe miradi ya umwagiliaji pamoja na miundombinu yake ili kuongeza uzalishaji wa chakula hapa nchini. Ni kweli kwamba nchi yetu tunategemea sana mvua badala ya kuimarisha umwagiliaji katika kilimo na kwa maana hiyo mwaka ambako hakutakuwa na mvua nchi yetu inaweza kuingia kwenye baa la njaa. Serikali inatambua tulikuwa na Taasisi ya Umwagiliaji ambapo awali ilikuwa chini ya Wizara ya Maji. Hatua ya kwanza tumeiondoa kutoka Wizara ya Maji tumeipeleka Wizara ya Kilimo, Wizara ambayo inahusika na suala la kilimo ili iweze kuiratibu kwa ukaribu. Bado Tume ipo na inaendelea kufanya kazi yake, tumefanya mabadiliko kadhaa ndani ya Wizara ya Kilimo ikiwemo na kuondoa Wakurugenzi saba ambao awali walikuwa wanaratibu kutokana na matatizo mbalimbali yaliyojitokeza kwenye Tume hiyo na sasa tumeunda timu.

Mheshimiwa Spika, lakini pia tumefanya maboresho ya ufunguzi wa ofisi zake ambapo awali ilikuwa ipo Makao Makuu peke yake na kwenye Kanda. Sasa tumefungua ofisi za mikoa 26 ambazo zitakuwa na Maafisa wa Umwagiliaji lakini tumepeleka Maafisa Umwagiliaji 34 kwenye ngazi za Wilaya na kwenye Wilaya ambazo zina miradi ya umwagiliaji na wanaendelea kufanya kazi yao ili waratibu kwa ukaribu miradi hiyo chini ya usimamizi wa Halmashauri za Wilaya wakishirikiana na Afisa Kilimo.

Mheshimiwa Spika, lengo ni kuhakikisha kila mradi wa umwagiliaji uliopo katika Halmashauri, unapata msimamizi mtaalam ambaye ni kutoka Tume ya Umwagiliaji. Tayari wataalam wa umwagiliaji wamenza kupelekwa maeneo yote na kazi zimeanza. Hatua hizo zinalenga kuiwezesha Tume hiyo kusimamia ipasavyo shughuli za umwagiliaji nchini ili kuongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 475,056 za sasa hadi hekta 1,000,000. Malengo yetu ifikapo mwaka 2025 tuwe tumefikia hatua hiyo.

Mheshimiwa Spika, nikiwa nahitimisha hoja yangu, hayo ndiyo machache ambayo yamejitokeza, yapo mengine machache kama vile eneo la ushirika ambalo lilichangiwa na Mheshimiwa Mbunge kutoka Mkoa wa Kagera alipokuwa anaonesha kutoridhishwa na ushirika uliopo Mkoani Kagera. Nikiri kwamba ushirika huu toka awali haukuwa na mwelekeo mzuri. Ushirika baadaye iligeuka na kuwa ni maeneo ya watu wanaopata nafasi ya kuongoza kuwa ni maeneo ya kula.

Mheshimiwa Spika, tulichofanya ni kufanya mapitio ya ushirika huo na kufanya maboresho lakini pia kufanya uhakiki wa kina katika kila ushirika kuona ushirika ulikuwa na nini na maboresho yake na hatimaye kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa ushirika. Kwa sasa, baada ya uhakiki wa maeneo yote ya Vyama Vikuu vya Ushirika na kubaini kwamba kulikuwa na ubadhirifu mkubwa ikiwemo na WETCO -Mkoani Tabora, NCU - Mkoani Mwanza, KNCU - Mkoani Kilimanjaro lakini pia KBCU ya kule Kagera.

Mheshimiwa Spika, pia hapa karibuni tumeenda kwenye mkonge; maeneo hayo tumefanya uhakiki na kugundua kwamba zipo mali nyingi za ushirika zimetoweka au zimechukuliwa na watu bila utaratibu na kukatisha tamaa wakulima kujiunga kwenye ushirika huo. Baada ya hatua hii, tumeanza kusimamia ushirika huu kurudi kwenye nafasi yake. Kwa hiyo, tumeendelea kuboresha ushirika huo ikiwemo na kusimamia Tume ya Ushirika ambayo inaratibu ushirika.

Mheshimiwa Spika, upo ushirika kwenye maeneo mengi; upo ushirika kwenye mazao ya kilimo ambapo pia kuna Vyama Vikuu vya Ushirika vya Mazao ya Kilimo lakini kuna ushirika wa fedha ambao unasimamiwa na taasisi za fedha, wote upo chini ya Tume ya Ushirika. Kwa sasa tupo kwenye mjadala na wadau wa kuiondoa Tume ya Ushirika kutoka Wizara ya Kilimo ikae ama Ofisi ya Waziri Mkuu au Ofisi ya Rais ili iweze kufanya kazi ya kusimamia ushirika wote ulipo katika Wizara zote ikiwemo Wizara ya Kilimo, Wizara ya Fedha na maeneo mengine na kupata mafanikio makubwa zaidi badala ya kuuweka kwenye Ushirika tukiwa tunajua kuna wana ushirika waliojiwekea fedha za akiba na kukopa kwenye sekta ya fedha. Hayo ni malengo ya kuboresha ushirika kwenye maeneo haya.

Mheshimiwa Spika, sasa ushirika wa mazao ambao tulioupata hapa ni kwamba kazi yao wao ni kusimamia biashara ya mazao lakini pia ushirika huu unatakiwa usimamie kuanzia maandalizi ya kilimo mpaka masoko yake. Kasoro zote zilizojitokeza zinaendelea kurekebishwa ili ushirika huu uwe na tija kwa wakulima na tumeanza kuona manufaa kwenye maeneo mengi ambayo ushirika huu unaanza kusimamiwa, masoko ya mazao mengi yaanza kufikiwa vizuri pamoja na kasoro hizo lakini tunaendelea kuimarisha. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge ambao pia ni Wajumbe wa Ushirika kwenye maeneo yenu au mnao wana ushirika wenye malalamiko kwenye maeneo yenu, endeleeni kuwa na matumaini kwamba mwisho wa zoezi la kuimarisha ushirika huu, tutakuwa na ushirika ambao utakuwa unaringiwa na wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna sekta ya ajira ambayo ilizungumzwa vizuri kwenye hoja yangu nilipokuwa nawasilisha. Naomba tu nifanye marejeo ni kwamba Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli alipokuwa anaingia madarakani moja ya kilio cha Watanzania ilikuwa ni kukosekana kwa ajira. Alipokuja na kauli mbiu ya kuboresha uchumi kupitia viwanda; moja kati ya mkakati ni kufungua milango ya ajira kwenye viwanda vinavyojengwa. Leo hii tunashuhudia viwanda vingi vinavyojengwa nchini vinatoa nafasi za ajira za Watanzania bila kujali elimu. Wapo wanaoajiriwa wasiokuwa na elimu kabisa, elimu ya kati mpaka elimu ya juu na ndiyo malengo yaliyokuwepo ya uanzishwaji wa viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia ajira tumeifungua kwa kuanzisha miradi mingi ya kimkakati. Miradi yote ya kimkakati imetengeneza ajira kwa kuajiri vijana wanaosaidia kufanya kazi lakini wataalam, bado kuna wajasiriamali, wafanyabiashara na wenye makampuni wamepata ajira kupitia miradi hii mikubwa. Hata ile ya ujenzi wa vituo vya afya, hospitali, miradi ya maji nayo pia imetengeneza fursa za ajira kwa wale ambao wapo kwenye maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, suala la ajira ni pana na ni endelevu kama nilivyosema wakati nawasilisha hoja. Hata hivyo, tunachofanya pia, tumeweka programu ya kuwapa ujuzi Watanzania wasiokuwa na ujuzi ili waweze kuajirika kwenye sekta mbalimbali lakini pia waweze kujiajiri kwa kutumia ufundi walionao.

Mheshimiwa Spika, pia tumetoa fursa za Ofisi za Serikali kushiriki kikamilifu katika kuboresha ajira hizi kwa kutengeneza mifumo itakayowapatia mtaji vijana au makundi mbalimbali ili nao pia waweze kujiajiri kwa kuanzisha biashara mbalimbali au miradi mbalimbali ambayo itaweza kuwapatia vipato. Katika kuhakikisha tunahamasisha eneo la ajira, tumetoa fursa kwa kuzungumza na taasisi za fedha kutoa mikopo mbalimbali kwa wajasiriamali ili wawe na mitaji ya kuanzisha biashara zao ikiwa ni sehemu mojawapo la ajira.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, jambo la ajira ni sehemu ya ajenda yetu, ni eneo endelevu na tunaendelea kuweka mikakati kadiri siku zinavyokwenda kuhakikisha kwamba tunawatoa vijana wengi kwenye maeneo ya kukaa na kucheza pool bila sababu kwa kukosa ajira na kila mmoja ashiriki kwenye maeneo haya. Leo hii tumeanza kushuhudia vijana wengi nchini wameachana na kucheza pool, kila mmoja anafanya kazi yake na kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu” imesaidia kuwafanya vijana hawa kushiriki kikamilifu kwenye shughuli mbalimbali za ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiwa nahitimisha naomba nieleze suala la ziara za Viongozi wa Kitaifa ambazo zimefanyika nchini kote kwamba Serikali yetu tuliweka utaratibu wa kuhakikisha kwamba tunawafikia wananchi. Tulikuwa tunaweka msisitizo wa kila mtumishi wa Serikali lazima ajenge tabia ya kuwapokea, kuwasikiliza na kuwahudumia wananchi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali ya Awamu ya Tano iliweka juhudi za kipekee za kuimarisha utendaji na uwajibikaji katika sekta ya umma kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi katika kuwahudumia wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha kuanzia Julai 2019 hado Februari, 2020, ziara mbalimbali zimefanyika zikihusisha viongozi wa Kitaifa, Mawaziri katika maeneo mbalimbali Tanzania Bara lakini pia hata Visiwani. Lengo la ziara hizo zilikuwa ni kukagua miradi ya maendeleo na shughuli mbalimbali za kiuchumi na jamii; kuzungumza na watumishi wa umma; kusikiliza malalamiko na kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi pamoja na kutoa maelekezo mbalimbali kwa viongozi na watendaji husika ili waendelee kuwahudumia Watanzania kwenye maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, ziara hizi zimeleta tija sana kama ifuatavyo. Moja, tumeongeza pia hata nidhamu na uwajibikaji kwa watumishi wa umma katika ngazi mbalimbali. Watumishi wameongeza ari ya kuwatumikia wananchi, kusikiliza malalamiko, kero na kutoa ufafanuzi lakini kubwa zaidi kuwahudumia wananchi bila ya urasimu. Hili litaendelea kusimamiwa wakati wote ili kujenga nidhamu ya utendaji ndani ya nchi, hasa ndani ya Serikali ya kuwahudumia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mbili, tumeongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya huduma za jamii ikiwemo miradi ya elimu, afya, maji pamoja na miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege na umeme. Waheshimiwa Wabunge wote ni mashahidi kwamba Serikali yetu imeyafanya haya na tunaendelea kufanya haya ili kuleta ustawi wa jamii yetu.

Mheshimiwa Spika, tatu, tumeongeza kwa kasi ukusanyaji wa mapato ya Serikali Kuu na mapato ya ndani katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kutokana na uhimizaji wa matumizi ya mashine za kielektroniki pamoja na mwitikio wa wafanyabiashara, wafanyakazi na wananchi kulipa kodi na ushuru kwa hiyari bila shuruti. Naona sasa Watanzania wengi wanapenda kulipa kodi kwa sababu kodi ile inaratibiwa vizuri na inarudi kwao kwa kuwajengea miradi. Kwa hiyo, ari imeongezeka na tunaamini ari itazidi kuongezeka ya kila mmoja kujua kwamba wajibu wake ni kulipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna ongezeko la uzalishaji na tija ya mazao mbalimbali ya kilimo cha biashara na chakula katika maeneo mengi. Pia sekta ya mifugo na uvuvi imepata mabadiliko makubwa. Vilevile na tunaendelea kuwezesha nchi kujitosheleza kwa chakula na kuongeza mapato ya kuchochea maendeleo ya viwanda. Pia tunaendelea kuimarika kwa hali ya usalama, amani na utulivu nchini pamoja na kuongezeka kwa kasi ya mshikamano ndani ya Taifa ili pia tuweze kufanya kazi hiyo kwa pamoja.

Mheshimiwa Spika, najua tuna kazi kubwa ya kupitia bajeti yetu na mimi naomba nihitimishe kwa kusema kuwa sote tumekuwa tukifuatilia kwa karibu mjadala huu kuhusu hotuba ya Waziri Mkuu. Aidha, wakati wa kuwasilisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, nilitumia nafasi hiyo kueleza kirefu mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi cha takribani miaka hii minne na tunaingia sasa wa tano. Hivyo, napenda niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wenzangu na wananchi kote nchini kwa ujumla kuwa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 – 2020 imetekelezeka vema chini ya Jemedari wetu, Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Naomba tu niendelee kwa kusema kuwa tutaendelea kuwahudumia Watanzania na Watanzania waendelee kuiamini Serikali yetu, Rais wetu na wasaidizi wa Mheshimiwa Rais kuwa tupo kwa ajili yao na tutaendelea kuwatumikia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwezi huu wa Aprili una matukio makubwa kidogo. Moja tarehe 7 Aprili, 2020 yaani kesho tutaadhimisha miaka 48 ya Kumbukumbu ya Kifo cha Hayati Mzee wetu Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa kwanza wa Zanzibar. Pia tarehe 12 Aprili, 2020 tutaadhimisha miaka 36 ya Kumbukumbu ya Kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Hayati Edward Moringe Sokoine.

Mheshimiwa Spika, ndugu zangu Watanzania tuendelee kuwakumbuka viongozi hawa. Kesho itakuwa ni siku ya dua maalum kwa ajili ya kumuombea baba yetu Hayati Sheikh Abeid Amani Karume. Kwa hiyo, kila mmoja kwa dhehebu lake atumie nafasi hiyo kumuombea Mzee wetu Rais wa kwanza wa Zanzibar. Pia itakapofika tarehe 12 Aprili, 2020, nako pia familia inaandaa dua. Kwa hiyo, kila mmoja kwa dhehebu na imani yake aendelee kumuombea aliyekuwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Edward Moringe Sokoine na tuendelee kumuomba Mungu aendelee kuweka roho zao mahali pema peponi, Amina. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niwakumbushe Waheshimiwa Mawaziri, viongozi wateule wa Serikali na watendaji wote kutekeleza wajibu wetu ipasavyo. Tufanye kazi kwa bidii zaidi, tuache mazoea, tuchape kazi kwa lengo la kuwa hudumia wananchi wetu hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, Wakristo wote duniani wataendelea na kipindi cha toba ambacho ni muhimu katika imani kuelekea sikukuu ya Pasaka. Niwasihi kuwa maisha mnayoishi katika kipindi hiki yalingane na maisha yetu ya kila siku. Kadhalika kuelekea kumalizika kwa kipindi hiki, niwatakie Watanzania wote kheri ya Pasaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwezi huu pia tuna Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani nao unatarajiwa kuanza wakati wowote ule kuanzia katikati ya mwezi huu. Napenda kutumia fursa hii pia kuwatakia Waislamu wote nchini mfungo mwema na wenye mafanikio ili kila atakayefanya ibada hiyo, aifanye kikamilifu na kama inavyoagizwa katika mafundisho ya Quraan Tukufu basi naamini kila mmoja takuwa anafuata imani hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, naomba sasa Bunge lako Tukufu liridhie na kupitisha Makadirio ya mapato na matumizi kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge letu kama ilivyowasilishwa katika hoja yangu siku ya tarehe 1 Aprili, 2020.

Mheshimiwa Spika, ni matarajio yangu kwa utamaduni uleule na tabia ileile ya ushirikiano wa dhati na kwamba kama ambavyo mmekuwa mkipitisha bajeti zote nne zilizopita, naamini pia pamoja na bajeti hii ya tano inayolenga kuhudumia Watanzania wote, ni imani yangu kwamba Waheshimiwa Wabunge wenzangu mtaniunga mkono kwa kuipitisha kwa kishindo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja, ahsante sana. (Makofi)

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, naafiki.