Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilindi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema, ambaye ameniwezesha kusimama leo kuweza kuchangia bajeti iliyoko mbele yangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, maendeleo siyo upepo. Upepo huwa hauonekani, lakini yakifanyika mambo ambayo yana maslahi mapana na wananchi wa Tanzania na watu wanaona, hatuna budi kupongeza. Naomba tuipongeze Serikali katika hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo vibaya kupongeza kwa mambo ambayo yanaonekana. Nitoe mfano mdogo tu, hapa katika Mkoa wa Dodoma ambao sisi Waheshimiwa Wabunge tupo. Leo hii Dodoma imebadilika sana; ukipita mitaani, barabarani huko unaona mabadiliko. Ila katika maeneo yetu tunakotoka tunaona namna ambavyo vituo vya afya, barabara, majengo ya shule yanavyokwenda. Sasa siyo vibaya hata kidogo Mheshimiwa Mbunge anaposimama na kuanza kusifia. Nadhani ni wajibu wetu Wabunge kuweza kusema yale mazuri ambayo yamefanywa na Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia Hotuba ya Mheshimiwa Waziri, imesheheneza mambo mengi sana. Imegusa kila eneo na hususan mambo ambayo yanagusa wananchi. Tukianzia kwenye Vituo vya Afya, Hospitali za Wilaya, yote yameonyeshwa hapa. Mimi nina ushauri ambao naomba Mheshimiwa Waziri auchukue.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni Mjumbe wa Kamati ya PAC na nilipata bahati ya kutembelea baadhi ya Hospitali za Wilaya ambayo Serikali ilitoa shilingi 1,500,000,000/=. Moja ya changamoto ambayo niliishuhudia na ni jirani tu hapa kwenye Hospitali ya Mtera; tuliona hospitali ile imejengwa kwa force account, jambo ambalo ni zuri kabisa, gharama ilikuwa ni ndogo, lakini kuna baandi ya mambo ambayo hayakuzingatiwa na pengine kama yangezingatiwa leo hii Hospitali hizo za Wilaya zingekuwa zimemaliza kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mmoja ni kwamba katika majengo yale hatukuzingatia nyumba za Madaktari, nyumba za kuweka maiti (Mortuary). Naomba sasa, maeneo yale ambayo yana Hospitali za Wilaya angalieni maeneo haya, hatuwezi kuwa na Hospitali ya Wilaya bila kuwa na Hospitali ya Mganga. Hili ni jambo la kuzingatia sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia na nyumba za wahudumu ni jambo ambalo tulitakiwa tulizingatie. Kama Serikali Kuu hatuwezi kutoa fedha, basi tuangalie namna ambavyo Halmashauri zetu zinaweza zikatoa fedha ili Hospitali ya Wilaya ikikamilika, basi na nyumba za wahudumu ziweze kupatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo napenda kulizungumzia ni suala la TARURA. Mwaka huu maeneo mengi Tanzania yamepata mvua za kutosha. Nichukulie mfano katika Wilaya yangu ya Kilindi mvua zilianza mwezi wa Kumi hadi leo hii, mvua zinaendelea kunyesha. Mvua ni baraka kwa Watanzania na mvua ni baraka kwa wakulima, lakini pia zimeharibu sana miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Waziri mwenye dhamana kupitia TARURA, hebu angalieni maeneo ambayo mvua zimekuwa nyingi sana. Timu zipite kwenda kuangalia kwa sababu wakulima hawa watapata mazao ya kutosha, lakini mazao haya yatapita wapi kama barabara zitakuwa hazipitiki? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano mmoja. Ni kwamba nina barabara kubwa ambazo takribani miezi mitano sasa hivi hazipitiki. Kuna barabara ya Kwinji - Muungano hadi Kilindi Asilia. Ni eneo ambalo lina uzalishaji mkubwa sana, lakini ni eneo ambalo hata pikipiki haipitiki. Mheshimiwa Waziri aliniahidi akaniambia kwamba timu yako itapita Wilaya ya Kilindi kufanya tathmini kuona maeneo ambayo yameharibika. Hadi leo nazungumza hapa ni kwamba watu wake hawajafika. Namwomba Mheshimiwa Waziri kwa heshima kubwa sana, najua Mheshimiwa Waziri ni msikivu, najua Serikali inasikia, maeneo hayo ambayo nimeyataja yaweze kupitiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo eneo lingine ambalo pia ni muhimu sana, ni barabara ambayo inaunganisha Wilaya ya Kilindi na Simanjiro kwenye Kata Saunyi. Pia ni miezi sita haipitiki. Barabara hii ni muhimu sana kwa sababu ina pori tengefu la Handeni, ni pori ambalo lina wanyama sana na eneo la utalii. Namwomba Mheshimiwa Waziri tuangalie namna ambavyo barabara hizi ni za kutengenezwa ili ziweze kupitika.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni kwamba nilibahatika mwezi wa Tatu mwaka 2020, Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya ziara kwenye Jimbo langu la Kilindi. Katika maeneo ambayo alipita ilikuwa ni kwenye Kata ya Kwediboma ambayo Mheshimiwa Waziri alitupatia shilingi milioni 300. Ni kweli kabisa kwamba fedha zile zimefanya kazi nzuri lakini kituo kile hakijakamilika. Bahati mbaya zaidi, Wilaya ya Kilindi ina Vijiji 102, Vitongoji 611, Tarafa nne tuna Kituo cha Afya kimoja tu ambacho kinafanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, hebu tuongezewe shilingi milioni 200 ili Kituo cha Afya cha kwenye boma kiweze kufanya kazi. Kama hiyo haitoshi, tuna Tarafa na Kata ya Tungule ambayo ina umbali takribani kilometa 200 wananchi hawa ili waweze kufika Kituo cha Afya cha Songwe ambayo ni Makao Makuu ya Wilaya, ni umbali wa kilometa 240.
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani kuna umuhimu wa hali ya juu sana kwamba Kata ya Tungule ambayo iko karibu kabisa na Wilaya ya Gairo tuweze kupatikwa Kituo cha Afya. Kwa mawazo yangu ukiniuliza, nitakwambia Vituo vya Afya ni bora zaidi kwa sababu vikijengwa katika ubora unaotakiwa kama ambavyo tunaona vilivyojengwa sasa hivi, tuna uhakika kabisa wa kuwasogezea wananchi huduma hii badala ya kujenga Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, japokuwa sipingi kwamba Hospitali ya Wilaya ina umuhimu, lakini kwangu mimi ukiniuliza Mbunge wa Wilaya ya Kilindi, nahitaji zaidi Vituo vya Afya kwa sababu ndivyo ambavyo vinaweza vikahudumia wananchi wangu na kuweza kufika kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni ushauri juu ya watumishi katika Halmashauri zetu. Imejengeka kwamba watumishi wanatakiwa waweze kuhama baada ya kufikisha miaka mitano au sita, lakini kuna baadhi ya watumishi katika baadhi ya Halmashauri zetu wanakaa miaka hadi 20. Jambo hili halina afya hata kidogo. Halina afya kwa sababu wakati mwingine halimfanyi mtumishi aweze kufanya kazi wala kujifunza mambo mapya. Namwomba Mheshimiwa Waziri; angalia, pitia Halmashauri zako zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa mfano katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, tuna watumishi wamekaa miaka 18 mpaka 20 wilaya hiyo hiyo. Watumishi hawa hawajifunzi jambo lolote lile, hawapati changamoto mpya hususan katika sekta ya elimu. Wakati mwingine unaona kwamba elimu katika baadhi ya maeneo yetu, ufaulu wa wanafunzi hauendi sawa, kwa sababu mwalimu amekaa shule moja miaka 15 mpaka 20 hajajifunza jambo, anaona mazingira ni yale yale. Nashauri sana, namwomba sana hebu aliangalie katika mtazamo ambao unaweza kutusaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine namwomba Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI aangalie namna ambavyo force account inatumika. Force account ni nzuri lakini nadhani elimu haijaenda sawa sawa hususan kwa Wakurugenzi. Na sisi kama Wabunge tunao wajibu wa kueleza nini dhana ya force account, kwa sababu force account inatakiwa isaidie kupunguza gharama, lakini wananchi wanakuwa hawaielewi force account.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hili pengine utengenezwe waraka maalum uende kwa Wakurugenzi waweze kuelezwa nini dhana ya force account kwa sababu wananchi hawaelewi.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele ya pili imeshagonga.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana, shukrani. (Makofi)