Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Segerea
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutumia nafasi hii kwanza kukushuru wewe mwenyewe kwa kunipa nafasi hii, lakini nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais na Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi kubwa ambayo wameifanya katika nchi yetu ya Tanzania katika hiki kipindi cha miaka minne ambacho tunaendelea sasa kumaliza na kuwa kipindi cha miaka mitano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda tu kupongeza kwamba tulikuwa tuna mambo mengi ambayo tuliomba au tuliyaweka kwenye Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi 2015- 2020 na mambo hayo tukiangalia mpaka sasa asilimia 90 au asilimia 88 yote yameshatekelezwa. Kwa uchache tu ninapenda kutaja barabara ambazo zimejengwa, barabara ambazo ni kubwa kwa Mkoa wa Dar es Salaam; tuna flyover ambayo iko pale TAZARA imejengwa kipindi cha Awamu ya Tano, lakini pia tuna barabara ya Ubungo ambayo ni interchange imejengwa kipindi cha Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tuna barabara sita ambazo zinatoka Dar es Salaam mpaka Pwani ambazo zimejengwa kipindi cha Awamu ya Tano. Lakini pia tuna barabara nyingine ambayo inajengwa Nakanazi pamoja na Kasulu ambazo zinajengwa kwa bilioni 260; zimejengwa Awamu ya Tano. Tuna Daraja la Busisi ambalo linajengwa kwa miezi 48, Mheshimiwa Rais ameshalizindua kwa hiyo tuna vitu vingi ambavyo tunaweza kujivunia katika Serikali ya Awamu ya Tano au Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ambayo imeweza kuvitekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutumia nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, Mhehimiwa Jafo, pamoja na Manaibu wake wote kwa kazi kubwa ambayo wameifanya katika Nchi ya Tanzania, hususani kwenye Jimbo langu la Segerea ambapo kwa sasa tuna barabara nyingi za lami ambazo zimejengwa katika kata mbili zilikuwa chini ya Mradi wa DMDP lakini najua ziko chini ya TAMISEMI, barabara za kilometa 16 na masoko sita lakini pia na bustani mbalimbali ambazo wameweza kubadilisha mazingira ya hizi kata mbili. Kwa hiyo, natumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa kuleta maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nampongeza kwa kusimamia na kuangalia suala zima la elimu bure ambapo mpaka sasa hivi tumekuwa na ongezeko kubwa la watoto shuleni, ni kwa sababu wamekuja kwa sababu ya elimu bure. Kwa hiyo, nipende kutumia nafasi hii kuendelea kumpongeza Mheshimiwa Waziri Jafo kwa mambo makubwa ambayo anayafanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ninataka kuliongelea ni kuhusiana na barabara zetu za ndani. Pamoja na pongezi hizo lakini bado tunamuomba Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Jafo, aweze kufanya kazi kubwa kwa kuangalia barabara za Mkoa wa Dar es Salaam lakini pia na mikoa mingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano kama barabara za Mkoa wa Dar es Salaam katika Jimbo la Segerea, Jimbo la Ukonga na Jimbo la Ilala, barabara sasa hivi zina hali mbaya sana, na zina hali mbaya sana kwa sababu ya mvua. Mvua imekuwa kubwa na mvua imeharibu miundombinu na imeharibu miundombinu ni kwa sababu kuna mifereji na barabara nyingi ambazo hazijaweza kutengenezwa kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninataka nimuombe Mheshimiwa Jafo; TARURA haiwezi kubadilisha mazingira yaliyopo sasa hivi kwa bajeti ambayo tumekuwa tukipanga. Kwa kweli barabara ni mbovu sana na ninajua TARURA wanataka kufanya kazi lakini bajeti yao ni ndogo.
Katika Jimbo la Segerea tuna mafuriko makubwa, mafuriko yamechukua sehemu kubwa. Kama unavyojua Mheshimiwa Jafo kwenye jimbo letu ndiyo umepita Mto Msimbazi, kwa hiyo, katika ule mto umepita sasa hivi unaingia, sio kwamba wananchi wameufuata Mto Msimbazi, sasa hivi maji ndiyo yanawafuata watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kata ya Vingunguti kuna makaburi ambayo sasa hivi yanaondoka na maji. Unakuta makaburi mengi sana, makaburi kama 200 ya Kata ya Vingunguti yameondoka na maji na hayo makaburi zamani yalipokuwa yamepangiwa hayakupangiwa kwenye mto lakini kutokana na uchakavu wa miundombinu, kutokana na uchakavu wa mifereji hayo maji yameacha njia yake na yameshaenda sasa kwenye nyumba za watu na hatimaye kusababisha hayo makaburi kuondoka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tuna mradi mkakati ambao mmeujenga Kata ya Vingunguti, machinjio ya kisasa. Mheshimiwa Jafo machinjio ya kisasa tunakupongeza sana, ni machinjio mazuri ambayo yatawasaidia wafanyabiashara wadogowadogo hata kufanya shughuli zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri barabara ya kukufikisha kwenye hayo machinjio ni barabara mbovu sana, imeharibika kutokana na miundombinu ya mvua na kutokukarabatiwa kwa muda mrefu. Kwa hiyo ninakuomba sana katika bajeti yako hii ya 2020/2021, naomba utuangalie katika hizo barabara ambazo tumezitaja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ninachotaka kuongelea ni kuhusiana na Ugonjwa wa Corona. Nitumie nafasi hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy, pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wanaifanya. Nimpongeze Mkuu wangu wa Mkoa, Paul Makonda, pamoja na Mkuu wangu wa Wilaya, Dkt. Sophia Mjema, ambao wamekuwa wakifanya kazi kubwa kwa ajili ya uhamasishaji wa watu jinsi gani ya kujikinga na huu ugonjwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nipongeze Wizara kwa kazi kubwa ambayo imefanya kwa ajili ya kutoa utaratibu kwanza wa utoaji taarifa kwamba ni Waziri na Mheshimiwa Waziri Mkuu ndio watakaohusika kutoa taarifa nani ana Corona na wagonjwa wangapi wapo. Hiyo inatusaidia sisi kutokupata taarifa ambazo sio makini au sio sahihi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kutoa ushauri kutokana na huo Ugonjwa wa Corona. Kuna wananchi wetu wengi ambao walikuwa wanafanya biashara mfano kama hizi biashara za mamantilie au biashara za kupika, biashara nyingi tu ambazo zimeathiriwa na Ugonjwa wa Corona. Sasa wananchi wengi wamechukua mikopo benki kwa sasa hivi kwa kuwa biashara hakuna na hawa wananchi wako nyumbani.
Ninaomba kupitia Wizara ya Fedha kuongea na Benki Kuu ili waangalie hizi benki ndogondogo kama wanaweza kuwasaidia hawa wananchi ambao walikuwa wanalipa labda kwa mwaka mmoja, waweze kuongezewa mwaka mmoja mbele. Kwa sababu sasa hivi kama watawaacha waendelee hivi ina maana wananchi wengi wanaweza wakauziwa vitu vyao. Kwa hiyo, ninaomba sana Wizara ya Fedha ifanye kitu kama hicho ili kuweza kuona kwamba hawa wananchi wetu tunawakinga na janga hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watendaji wetu, kwa sababu kila kata kuna bwana afya, sasa hawa mabwana afya kwa wakati huu tunamuona tu Mheshimiwa Makonda anatoa taarifa au anahamasisha pamoja na yeye kuhamasisha lakini bado tuna watendaji wa afya ambao tayari wana utaalam wa afya ambao wanaweza kwenda mitaani waweze kuwaelekeza watu jinsi ya kujikinga na Ugonjwa wa Corona. Kwa hiyo, ninaomba hawa watendaji wa afya kwa kipindi hiki waweze kutembea na kuweza kuwaambia watu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kingineā¦
(Hapa kengele Ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Muda umekwisha Mheshimiwa Bonnah, ahsante sana.
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)