Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa rehema alotuwezesha Wabunge sisi wote mpaka leo hii kuwepo hapa kujadili haya ambayo tunayazungumza.
Nitoe pongezi kwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Rais wetu Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya yeye na timu yake yote Mawaziri, Makatibu Wakuu na watendaji wote kwa ujumla. Lakini kipekee nimpongeze Mheshimiwa Jafo kama yeye hongera sana Mheshimiwa Jafo umefanyakazi nzuri kwenye Wizara yako wewe na wasaidizi wako lakini kazi hii hujaifanya tu vizuri kwenye nchi, lakini pia umeifanya vizuri katika Jimbo lako Mwenyezi Mungu atakusaidia utarudi tena In Shaa Allah.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe pia pongezi zangu kwa Makamu wa Rais mama Samia Suluhu, kwa Waziri Mkuu, kwa Rais wa Zanzibar, Makamu wa pili wa Rais Zanzibar kwa jinsi wanavyoweza kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi na kuweza kutufanya Wabunge wa Chama cha Mapinduzi tusimame tukijidai kwamba kazi imetekelezeka. Kipekee pia niwashukuru na niwapongeze Wabunge wote ambao Awamu zote Nne walikuwa wanasema ndiyo ili kazi ifanyike na ninaomba mwaka huu tusisite tena tupige ndiyo ili kazi iliyobaki ikamilike. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuchangia kuhusiana na suala zima la uwezeshaji kiuchumi wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri hadi sasa hivi bilioni 93.3 zimekopeshwa bila riba kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Vikundi 915 vya watu wenye ulamavu vikundi 4266 vya vijana na vikundi 8207 vimepata mikopo hiyo hapo ninachoomba wale waliokopeshwa warudishe lakini hapo hapo halmashauri ziendelee kutoa mikopo hii kwa wananchi kwa sababu hii ni ahadi iliyotolewa na Chama cha Mapinduzi ni lazima itekelezwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia ujenzi wa majengo ya utawala majengo ya utawala yamejengwa 86 kati ya hayo 29 yamekamilika na 57 yako katika hatua za mwisho za kukamilika ili Wakurugenzi, Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa wakae katika maeneo mazuri. Niipongeze sana Serikali yangu kwa kujali watumishi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wameeleze katika sekta ya elimu madarasa 19,808 yamekamilika, napenda niongezee kwamba madarasa 1313 yanaendelea yako katika ujenzi yatakamilika wakati wowote. Lakini kuna maabara 227 zimejengwa nipende tu kuongezea kwamba katika maabara hizo vifaa vya maabara vimeshatolewa katika sekondari 1258 ni jambo zuri sana ambalo Serikali imelifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la matundu ya vyoo ambalo 7922 yamekamilika na mengine 571 yako katika ujenzi na yako katika hatua za mwisho ambazo wanategemea kukamilisha muda si mrefu. Shule kongwe zimetajwa 73 zimekarabatiwa vizuri lakini nilizungumzia masuala ya mabweni mabweni yamekarabatiwa kiasi kwamba yanaonekana ni mapya ile ni kazi nzuri sana ambayo imeonyesha jinsi gani TAMISEMI imeweza kuokoa kwa sababu bila kukarabati yale majengo yangeharibika kabisa na tungepata hasara mpya ya kujenga majengo mapya. (Makofi)
Suala la hospitali zimeelezewa hapo hospitali 98 kuna vituo vya afya kadhaa kuna zahanati kadhaa mchango wangu hapa nilitaka niongeze kwamba Chama Cha Mapinduzi kupitia utekelezaji wa Ilani imeweza kuwezesha upatikanaji wa dawa na vifaa vya tiba kwa 92% hayo ni maendeleo makubwa sana. Lakini kwa kuwa kuna watu ambao roho zao hazina sifa za kusifia hatuwezi kuwalaumu lakini mwenye macho anaona mwenye masikio anasikia na wengine ndiyo huko huko wanaenda kujifungua wanaona zile hospitali wengine ndiyo huko huko watoto wao wanasoma lakini wanashindwa kusifia sisi tumuombe Mwenyezi Mungu tu amuwezeshe Rais wetu na Mawaziri wake wafanye kazi vizuri Mwenyezi Mungu uko pamoja nao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la corona suala la corona limekuja ghafla na kwa kazi kwenye suala hili nimpongeze Waziri wa Afya na timu yake pamoja na Waziri Mkuu lakini pia kipekee niwapongeze watumishi wote wa sekta ya afya popote nchini. Kwa sababu kila mtu anaogopa kufa lakini wale wenzetu inabidi watoke waende kule kuhudumia watu ninawapongeza sana sana sana na ninaomba tufate maelekezo ya wauguzi, madaktari na viongozi wetu. Kwa mfano hapa Ofisi ya Bunge tumejitahidi sana kujilinda kwa namna yoyote lakini je hivi tunavyojilinda tukitoka nje ya Bunge na sisi tunaendelea kujilinda? Kule Chako ni chako tunaacha kwenda? Huku na huku tunaacha kwenda? Naomba hilo tuliangalie kwasababu vinginevyo tutakuwa tunatunzwa vizuri hapa Bungeni halafu tukitoka nje tunabeba ya kule nje tunaleta humu Bungeni inakuwa sawa sawa na bure. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine pia huko kwa wananchi wetu tusaidiane pia kuendelea kutoa elimu isije ikaonekana sisi huku tunatunzwa halafu wananchi wetu wanapata tatu. Kwa hiyo, Wabunge tukitoka hapa tukirudi na sisi tuwajibike. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine tusaidiane na Serikali kwa sababu hili suala lilikuwa haliko kwenye bajeti Mbunge ambaye anaweza kujitolea kwa ajili ya kusaidia visafisha mikono na vitu vingine aendelee kutoa ili muda ukipita basi tujue na Wabunge nao tuliwajibika isije ikawa hapa 90% tunawasema tu Mawaziri, sijui nani hawajafanya nini, je sisi kama Wabunge tumefanya nini? Hilo nalo tujipime na sisi wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka wa uchaguzi dakika za mwisho tusitafutiane fitna na maneno yapo maneno ya kuudhi ambayo yanatugusa sisi wengine hatupendi kuyasema tuombeane dua. Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa ina wajumbe kutoka Zanzibar sita na wanazunguka nchi nzima kufanya kazi sasa mtu anaposema huku siyo Zanzibar hatuendi hivyo tufanye kazi na tuheshimiane.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja ahsante kwa kunisikiliza. (Makofi)