Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Anne Kilango Malecela

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Same Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kushukuru kunipa nafasi hii. Pia nimshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye amenipa uhai nikaweza kuwepo Bungeni leo. Naomba niwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Same Mashariki kwa unyenyekevu mkubwa kwa jinsi ambavyo walifanya uchaguzi mzuri sana na kuhakikisha wananirejeshea Jimbo langu la Same Mashariki. Nilishinda kwa kishindo tena kwa haki kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hapo naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais kwa mara ya kwanza amesimama imara akahakikisha nchi yetu inafanya uchaguzi kwa pesa zake za ndani. Nafikiri wote tunaoelewa uchaguzi tumekaa kwenye uchaguzi muda mrefu, siku zote tumekuwa tunabebwa na mataifa makubwa, lakini Mheshimiwa Rais kipindi hiki alisimama imara sana akaiheshimisha nchi yetu tukafanya uchaguzi kwa pesa zetu wenyewe. Waheshimiwa Wabunge naomba hili tulichukue kwa uzito sana na tuone kwamba, Rais ametukomboa kwa kitu kikubwa sana. Vile vile nimpongeze pia Rais alifanya kampeni za kutosha. Alizunguka nchi na aliomba kura na akashinda kwa kishindo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hapo nirudi sasa kwenye hoja iliyoko mbele yetu. Rais ametoa hotuba siku ya kwanza hapa Bungeni, ilikuwa ni hotuba nzito sana. Namuunga mkono katika area tatu ambazo nimeona nizichague; kwanza katika viwanda, pili katika barabara na tatu nitakuja kwenye afya.

Mheshimiwa Spika, nchi yoyote inakua vizuri zaidi inapokuwa na viwanda vya nguvu. Mimi naomba nirudi kwenye Jimbo la Same Mashariki, Jimbo la Same Mashariki sisi tunalima tangawizi kwa muda mrefu. Kwa muda mrefu sana tunalima tangawizi na tumejenga kiwanda cha tangawizi, mnaokumbuka tangu nimeanza kuingia bungeni hapa nazungumzia tangawizi nikasimama na wale wananchi imara tukajenga kiwanda cha tangawizi.

Mheshimiwa Spika, nikiri kile kiwanda kilikuwa ni dhaifu, lakini namshukuru sana Mheshimiwa Mhagama amekuja ziara kwenye jimbo langu akaja mlimani Mamba Miamba kukiona kiwanda kile. Amekuja nikajua ni Serikali imekuja kuona kile kiwanda. Kiwanda kile yeye mwenyewe amesimama imara pamoja na taasisi yake ya PSSSF, ambao wameingia ubia na sisi wananchi tunaolima tangawizi sasa pale Mamba Miamba, sasa pale Mamba Miamba tunakuwa na kiwanda kikubwa cha tangawizi katika Tanzania kwa sababu PSSSF wameamua kuingiza fedha nyingi sana kuwaunga wananchi wangu wa Jimbo la Same Mashariki.

Mheshimiwa Spika, wao wamechukua asilimia 60 sisi tumechukua asilimia 40, lakini ndugu zangu Wabunge hicho ni kitu kikubwa sana. Ina maana kiwanda kile ambacho kitakuwa kikubwa wananchi wangu wataondoka katika umaskini. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais, namshukuru mama Jenista Mhagama mno mno, alikuja jimboni kwangu, nilipata furaha sana ambavyo aliwafanya wananchi wangu wakafurahi. Naipongeza sana Serikali kujali viwanda kwa wananchi. Nimeanza tu kusema kidogo, nitakavyokuwa niko hapa ndani nitaongea sana kuhusu hiki kiwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono suala la ujenzi wa barabara kwenye nchi yetu. Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge tuangalieni tulitoka wapi tuko wapi sasa hivi. Tulikuwa kwenye barabara kwenye miji mikuu, ukiangalia Dar es Salaam, ukienda Arusha, ukija Moshi, ukija Dodoma, barabara zilikuwa za kawaida mno, lakini mimi nikienda Dar es Salaam na dereva wangu kwa sababu, mimi niseme ukweli mimi naishi Dodoma, kama sipo Dodoma niko Same Mashariki, Dar es Salaam mimi ni mgeni; tukienda na dereva wangu Dar es Salaam sasa hivi inabidi tupate dereva wa kuingia na sisi mjini. Dar es Salaam Rais amesimama imara mno, ameisimamia nchi yetu imara sana. Sasa hivi Tanzania katika Afrika Mashariki, sio kwamba tujisifu tuseme ukweli, tunaongoza upande wa barabara.

Mheshimiwa Spika, tunaongoza upande wa barabara, lakini naomba nizungumze kama mama. Mama sisi tunapokuwa na watoto unawaangalia Watoto wako sana, unamwangalia mtoto wako wa kwanza, unaangalia wa pili, unaangalia wa tatu, sisi tuliozaa zaidi unaangalia wa nne. Kila mtu anapozaliwa, anapoumbwa na Mwenyezi Mungu akija duniani ana kitu amepewa, ana kitu Mungu amempa cha kwake kwamba, huyu nampa kitu fulani. Tumshukuru Mungu amempa Rais wetu silika ya kujenga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Rais Magufuli pamoja na usomi wake, amesoma mathematics na kadhalika lakini nadni ya damu yake ni mjenzi, anajenga barabara. Mimi tangu nimekuwa bungeni hapa nimekuwa nae, hiki ni kipindi changu cha tano, yeye ni Waziri wa ujenzi, Waziri wa Ujenzi, sasa ni Rais anaijenga nchi mpaka mimi na Mheshimiwa Mama Sitta tumekaa tukafikiria hivi akiondoka tutafanya nini, lakini Mungu atatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi imejengwa barabara. Mimi najivuna sasa hivi nikiona hata Dodoma yangu inavyofanana. Dodoma inajengwa na Rais Magufuli mno na nampongeza kwa sababu, mume wangu siku moja alisema aah, hivi kumbe kweli hata nikifa kesho Dodoma imekuwa Makao Makuu, alimshukuru Mungu, lakini Malecela anasifu sana, anamsifu Rais mno, naomba umfikishie message, jinsi anavyojenga barabara za Dodoma.

Mheshimiwa Spika, sasa narudi nikwambie hivi TARURA. Sisi Wabunge wengi wa majimbo tunaitegemea TARURA na mimi niko Kamati ya Miundombinu, kuna mgawo wa fedha za kujenga barabara upo 70 kwa 30. TANROADS anapewa 70; TARURA anapewa 30, mimi naona TARURA aongezewe pesa. Waheshimiwa Wabunge wa majimbo simameni imara sana TARURA aongezewe pesa ili wananchi wetu nao wapate barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeshukuru Serikalini. Serikali imeona majiji makubwa, sasa tunaomba Serikali mrudi mtuangalie na sisi ambao tuko vijijini. Vijijini barabara zina hali mbaya sana. Sisi ambao majimbo yetu yako kwenye milima tuna shida kubwa ya barabara, tuna tabu sana ya barabara. Nasema ukweli lazima Wabunge bajeti inayokuja tusimame imara TARURA apewe pesa. Ule mgawo tunaoambiwa ni mgawo wa kisayansi wa 70 kwa 30 TARURA anapata pesa kidogo, Serikali itafute chanzo kingine cha kumpa TARURA pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, narudi kwenye afya sasa; namuunga Mheshimiwa Rais sana mkono kwa jinsi alivyosimama imara kujenga vituo vya afya. Amesimama imara kujenga vituo vya afya. Sasa ahakikishe vituo vya afya vinatoa huduma kikamilifu, Madaktari watoshe na vyombo.

Mheshimiwa Spika, sasa hapo lazima nirudi kwenye Jimbo langu, mimi nina tarafa tatu. Tarafa ya Ndungu ina kituo cha afya kimoja, nimetoka kuongea na Waziri wa Afya pale. Tarafa zangu mbili za milimani zote hazina vituo vya afya. Rais alipokuja Same nilimlilia nikamwambia wananchi wanakufa. Tarafa ya Gonja kuna kituo cha afya lakini ni cha KKKT ni biashara, wananchi hawana uwezo wa kulipia zile gharama pale. Tarafa ya Mamba Vunta kuna kituo cha afya cha Katoliki ni biashara. Nimekwenda kumlilia Mheshimiwa Waziri sasa hivi pale, nimempigia magoti aje aone jimbo langu.

Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie kwa kuunga mkono hoja hii ya hotuba za Mheshimiwa Rais, naipongeza sana Serikali inafanya kazi nzuri lakini naomba mtuangalie na sisi tunaotoka vijijini. Ahsante sana. (Makofi)