Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibiti
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru kwa kunipa nafasi hii nami kuwa mchangiaji katika hotuba hii ya Mheshimiwa Rais. Naomba tu kidogo nifanye marekebisho hapo jina langu naitwa Twaha Mpembenwe, Seif Mpembenwe alikuwa mzee wangu na tayari ameshatangulia mbele ya haki.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nichukue nafasi hii kukishukuru Chama changu cha Mapinduzi, wapiga kura wa Jimbo la Kibiti kwa heshima kubwa sana waliyonipa mimi na familia yanguna leo hii niko hapa mjengoni nawashukuru sana. Sambamba na hilo, naomba vilevile nichukue fursa hii kuwashukuru watu muhimu sana katika maisha yangu hasa rafiki yangu mpenzi ambaye ni mke wangu mama Sabrina; wanangu Sabrina, Leyla, Naima na Najma. Nawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipoweza kutoa shukrani za dhati kwa aliyekuwa Mkuu wangu wa Wilaya lakini sasa hivi ndiye Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mheshimiwa Joseph Joseph Mkirikiti pamoja na Katibu Tawala wangu wa Mkoa, mama yangu Rehema Madenge wakati nafanyakazi chini yao walikuwa viongozi wazuri na waliweza kuniongoza vizuri na mpaka leo nimekuwa Mbunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi watu wa Pwani ni wakarimu sana, halafu tuna desturi ya kuweza kushukuru. Sasa kabla sijaanza kuichangia hotuba ya Mheshimiwa Rais ningependa kuanza kumshukuru Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa mambo makubwa na mazuri aliyoweza kutufanyia watu wa Jimbo la Kibiti.
Mheshimiwa Spika, katika sekta nzima ya afya katika kipindi cha mwaka 2015 - 2020 Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, aliweza kutupatia fedha takriban shilingi 4,021,493,500,fedha hizo ziliweza kutumika katika kuweza kujenga hospitali ya wilaya, vituo viwili vya afya, zahanati tisa na vilevile tumeweza kukarabati kituo chetu cha afya kikongwe cha pale Kibiti. Tunashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika sekta ya elimu,Mheshimiwa Rais aliweza kutupa fedha takriban shilingi 4,243,607,588.99, fedha hizi zimeweza kutumika katika kuweza kujenga vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, nyumba za Walimu na kuweza kukarabati vilevile shule yetu kongwe ya Kibiti Sekondari ambayo ninauhakika kabisa baadhi ya Wabunge hapa wamepita na kuweza kusoma katika shule ile.
Mheshimiwa Spika,kama hivyo haitoshi Mheshimiwa Rais ametufanyia lingine kubwa ameweza vilevile kutupa fedha takriban shilingi bilioni 14.3 katika Kata ya Salale katika Wilaya ya Kibiti pale katika Kijiji cha Nyamisati limejengwa Gati zuri ambalo kwa namna moja ama nyingine limeweza kuturahisishia sisi watu wa Kibiti pamoja na ndugu zetu wa Mafia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika hili vilevile naomba ku- declare specialinterest, katika gati lile limeweza kuturahisishia sana sisi watu wa Kibiti kwasababu kule Mafia kuna akinamama kule wa kiarabu arabu na sisi watu wa Kibiti tunakwenda kule kwenda kuoa sasa kuweza kuchanganya mbegu zile. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais katika hilo.
Mheshimiwa Spika, vilevile Mheshimiwa Rais ameweza kutupa fedha takriban shilingi 4,021,850,786.38 fedha hizi zimeweza kutumika katika kuweza majengo ya utawala majengo yale ni mazuri jengo kubwa la Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi Mtendaji, bado kuna fedha kama shilingi milioni 700 tumeweza kuziomba kwa Serikali Kuu ili tuweze kumalizia katika miundombinu masuala mazima ya umeme na maji ili wananchi wale sasa waweze ku-enjoy kuweza kumchagua Mheshimiwa Raisna kuweza kuwa na Mpembenwe kama Mbunge wao.
Mheshimiwa Spika, shukrani hizi bado zinaendelea katika Jimbo letu la Kibiti limegawanyika katika sehemu kubwa mbili kuna sehemu ya geta na sehemu ya juu huku. Katika sehemu ya geta kule Mheshimiwa Rais aliweza kutupa fedha takriban shilingi bilioni 2.5, fedha zile katika kujenga daraja, kuna mambo mambo yaliweza kutokea lakini namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI ndugu yangu Mheshimiwa Selemani Jafo aliweza kutia mguu, sasa hivi ninavyoongea wakandarasi wako site, mkandarasi aliyekuwa amejenga gati la Nyamisati ndiyo yuko kule shughuli zinaendelea na vijana wetu pale vilevile wameweza kufunguliwa fursa za ajira, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais katika hilo.
Mheshimiwa Spika, kubwa kuliko yote tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuweza kuturudishia amani ambayo ilikuwa imepotea katika Jimbo la Kibiti. Jimbo la Kibiti amani ilikuwa ni bidhaa adimu sana. Nataka nieleweshe tu kwamba kuku walikuwa na uhuru mkubwa sana kuliko mwanadamu wa kawaida katika kipindi cha mwaka 2018/2019, lakini Mheshimiwa Rais aliweza kusimama katika nafasi yake kama Amiri Jeshi Mkuu na kuweza kuturudishia amani hiyo. Tunamshukuru sana katika hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa shukrani hizo katika Bunge hili la Kumi na Mbili tumefarijika sana kwasababu tuna kiongozi vilevile wa Chama Cha Mapinduzi naye siyo mwingine ni komredi Humphrey Polepole. Nataka niombe vile vile nichukue nafasi hii dakika moja kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi katika Jimbo la Kibiti katika kipindi cha uchaguzi mpaka hivi sasa. Hivi ninavyoongea baada ya kuweza kuwasiliana na wadau mbalimbali nimeweza kufanikiwa kupata fedha shilingi milioni 175 kwa kushirikiana na Mkurugenzi Mtendaji kwa ajili ya kununua ambulance. Fedha hizi zipo sasa hivi katika akaunti ya Mkurugenzi Mtendaji, tukimaliza session hii tu nitamwona Waziri wa Fedha ili tuweze kuweka mustakabali mzima wa masuala ya exemption tuweze kuleta ambulance ile na wananchi wa Kibiti sana waweze kufurahia kuwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli lakini vilevile kuwa na Mbunge mbunifu ambaye ni Mpembenwe.
Mheshimiwa Spika, kama hivyo haitoshi wakati tukiwa vilevile katika suala zima la kampeni, nilipita huko vichochoroni, nimeweza kuhangaika kwa wadau wangu mbalimbali kwa kushirikiana na Mkurugenzi Mtendaji ninavyoongea tumeweza kupata fedha shilingi milioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa dispensary fedha hizo zipo kwa Mkurugenzi Mtendaji wakati wowote kuanzia sasa hivi dispensary ile itajengwa kwa kupitia force account. Hilivilevile linafanyika.
Mheshimiwa Spika, kama hivyo haitoshi vile vile naomba nilitaarifu Bunge lako Tukufu pamoja na kiongozi wetu komredi Humphrey Polepole, madawati 100 tayari yalishasambazwa katika Jimbo la Kibiti na hivi ninavyoongea kuna madawati mengine 500 wiki tatu zijazo yatasambazwa katika shule za msingi vilevile pamoja na shule za Sekondari.
Mheshimiwa Spika, pia naomba tu niseme tutaanza ujenzi wa kituo cha Polisi haraka iwezekanavyo kwa kutumia nguvu zetu za ndani.
Mheshimiwa Spika, naomba sasa nichangie hotuba ya Mheshimiwa Rais mimi sitaki kwenda mbali nasema machache tu.
SPIKA: Mheshimiwa Twaha sasa hotuba ya Rais sasa. (Kicheko)
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, ahsante sanakatika kuichangia hotuba ya Mheshimiwa Rais mimi nagusa sehemu tatu muhimu. Kwanza katika suala zima la kilimo, najua Wizara ya Kilimo inafanyakazi nzuri sana. Napenda vilevile kumshukuru ndugu yangu Mheshimiwa Bashe kwa hotuba nzuri sana ambayo aliitoa siku alipofanya mkutano kule Tabora you realkneeled down,nilijaribu kumpigia simu lakini hakuweza kupatikana. Nampongeza sana kwa hotuba nzuri na mikakati mizuri ambayo Wizara ya Kilimo sasa hivi wanaendelea.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo kuna shida kubwa sana katika suala zima la bei ya korosho. Bei ya korosho na ufuta kwa wananchi wa Mkoa wa Pwani hususan katika Jimbo la Kibiti imekuwa ni mtihani mkubwa. Sisi tuna watoto wetu wa asili Wamwera, Wamakonde na Wayao kule, wao wanauza kilo moja ya korosho gredi A shilingi 2,700 wakati mwingine, lakini inashangaza sana kuona kwamba baba zao sisi watu wa Kibiti, kilo hizo za korosho gredi A inauzwa shilingi 800. Kwa hiyo naomba niishauri Serikali sasa tuweze kuangalia mustakabali mzima katika kuweza kuangalia minada hiyo wakati inafanyika, ifanyike kwa pamoja kwasababu minada ikiwa inaanza kule kusini halafu baadaye inakuja huku katika Mkoa wa Pwani, inakuwa shida sana, ndiyo wale wanunuzi wanaanza kufanya illegal price fixing, wakati mwingine wanakuja kununua korosho kwa bei ya chini. Mpaka hivi ninavyoongea sasa hivi bado kuna korosho chungu nzima za wananchi wanahangaika nazo kule.
Mheshimiwa Spika, vilevile naomba nichangie katika sekta nzima ya mambo ya elimu. Tuna wajukuu zetu hawa sasa hivi wana miaka sita elimu bila malipo imeweza kuonyesha kwamba watoto wengi sana wameweza kusajiliwa kuingia Shule ya Msingi, ikifika mwakani tayari watoto hawa watakuwa wamesha-mature miaka saba imetimia. Kwa tafsiri hiyo tusipokuwa makini elimu bila malipo inaweza ikageuka ikawa timing bomb.
Naomba sasa kuishauri Serikali, tuweze kwa namna moja ama nyingine kuwaongezea nguvu watu wa Halmashauri turudishe baadhi ya makusanyo, vyanzo vya mapato viende kwao, hivi sasa wawe na mpango mkakati wa kuweza kutengeneza vyumba vya madarasa. Tukifanya hivyo tafsiri yake pana ni kwamba tutakuwa na uwezo mkubwa sana wa kuweza kufanikisha watoto hawa kuingia Sekondari na bila ya crisis ya namna yoyote.
Mheshimiwa Spika, lingine ambalo naomba nilichangie ni katika sekta nzima ya masuala ya uvuvi, nashukuru kwa kengele lakini bado dakika zinaendelea. Katika sekta hii ya uvuvi ..
SPIKA:Ahsante sana.
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, wananchi wa Delta.
SPIKA: Ooh,muda hauko upande wako Mheshimiwa Twaha.
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE:Mheshimiwa Spika, nashukuru nanaunga mkono hoja. (Makofi)