Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nami nakushukuru kwa kunipa nafasi, lakini kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama ndani ya Bunge lako Tukufu katika Bunge hili la Kumbi na Mbili, naomba niruhusu nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia wote uzima na afya njema na vile vile kwa kuniwezesha mimi mtoto wake kuweza kurejea katika Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee, nataka niwashukuru sana wanawake wenzangu wa Mkoa wa Songwe kwa imani yao kubwa walionionyesha, vilevile kwa kura za heshima walizonipatia na hatimaye nimeweza kurudi tena katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, sasa naomba nianze kujadili Hotuba ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiitazama Hotuba ya Mheshimiwa Rais, nami nimepata muda wa kuipitia na kuisoma; ni hotuba nzito na imebeba matumaini ya Watanzania. Ni hotuba ambayo ina taswira mbili; taswira ya kwanza, ni hotuba ambayo inaeleza namna gani Serikali ya Awamu ya Tano imeshatekeleza masuala mbalimbali na kutatua changamoto mbalimbali za Watanzania. Pia ni hotuba ambayo imeeleza kwa kina sana namna gani ambavyo Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli amejipanga katika kipindi hiki cha pili kuhakikisha kwamba zile changamoto ambazo zilibaki kwenye awamu ya kwanza, zinaweza kumalizika katika awamu yake hii ya pili. Hotuba hii ni nzito na imebeba matumaini ya Watanzania. Ni hotuba inayotoa dira na taswira ya Tanzania tunayoitaka na namna gani ambavyo tutafikia Tanzania hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile hotuba ile ni maelekezo rasmi kwa viongozi wote wa Serikali pamoja na taasisi zake, namna gani ambavyo wanapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia ile hotuba ambayo Mheshimiwa Rais ameitoa. Yapo masuala mengi sana ambapo ukifuatilia ndani ya ile hotuba yameweza kuelekezwa kwa kina zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nijadili suala moja la afya kwa sababu tunatambua katika nchi yoyote, msingi wowote wa maendeleo ni afya ya watu wake. Hakuna namna ambavyo Tanzania inaweza ikapata maendeleo kama watu wake hawana afya ambayo ni stable. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika hotuba hii Mheshimiwa Rais ameeleza namna gani ambavyo miaka mitano ameshuhulikia changamoto za afya kwa Watanzania. Kwa kuwa mimi ni mwanamke, natambua namna gani ambavyo sisi wanawake tulikuwa tunapata changamoto wakati wa kujifungua lakini ndani ya miaka mitano changamoto hizo zimeweza kufanyiwa kazi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ameelekeza namna gani ambavyo kwa hii miaka mitano, kwa kupitia Sera ya Afya ambayo inasema kwamba kutakuwa na Kituo cha Afya katika kila Kata, kutakuwa na Zahanati kwenye kila Kijiji, Hospitali za Wilaya kila Wilaya, Hospitali za Mkoa kila mkoa; na hilo tumeliona limetekelezeka kwa kishindo kweli kweli. Nimesimama hapa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo amefanya katika miaka mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma hotuba vizuri, ameeleza namna gani ambavyo ameweza kujenga Zahanati 1,198, siyo kazi ndogo. Pia amejenga Vituo vya Afya vipatavyo 900, siyo kazi ndogo. Vilevile amejenga Hospitali za Wilaya 90, amejenga Hospitali za Mikoa 10 na Hospitali za Kanda tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tafsiri yake ni nini? Nachotaka kuongea hususani kwenye afya ya msingi, kwa sababu tunatambua asilimia kubwa ya Watanzania huwa wanaanzia kwanza kule chini kwenye afya za msingi, kwa maana ya vituo vyetu vya afya, ukiangalia Vituo vya Afya ambavyo vimejengwa, hoja siyo kwamba vimejengwa vituo 478, hapana.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ni kwamba vituo hivi ambavyo vimejengwa, ukiangalia maeneo mbalimbali ya nchi yetu, vimekuwa na hadhi sawa na Hospitali ya Wilaya. Ukiangalia facilities zote zinazopatikana kwenye hivi Vituo vya Afya, havitofautiani sana na Hospitali zetu za Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naona kwamba ni wakati muafaka sasa kuviita hivi Vituo vya Afya siyo sawa, tutakuwa hatumtendei haki Mheshimiwa Rais. Hivi vinapaswa viitwe Vituo vya Rufaa vya Kata. Kwa sababu ndivyo ambavyo vinachukua wananchi kutoka kule chini kwenye Zahanati wanakuja kutibiwa kwenye hivi Vituo vya Kata. Nataka nitoe ushauri kwa Serikali, kwa sababu tumeona kwamba vituo hivi vimejengwa vizuri, nasi pale kwetu kwenye Jimbo la Tunduma, tunacho Kituo cha Afya kimoja ambacho kimejengwa vizuri kiasi kwamba ukifika pale unashindwa kuelewa kwamba hiki ni Kituo cha Afya au ni Hospitali ya Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vitu vichache ambavyo nadhani kama vikifanyika kwenye hivi Vituo vyetu vya Afya vitasaidia sana kuvipa hadhi sawa na Hospitali ya Wilaya. Nataka nitoe ushauri kwa Wizara ya Afya na pia ushauri kwa Serikali kwamba ni wakati muafaka sasa waangalie, kama kuna uwezekano kwenye hivi Vituo vyetu vya Afya, yaongezewe majengo mawili, kwa maana ya jengo la jumla la wanawake na jengo la jumla la wanaume. Kwa sababu ni Vituo vya Afya viko pale lakini vinahudumia mama pamoja na mtoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini Serikali ikitenga fedha tukapata hayo majengo mawili pale, moja kwa moja tutakuwa tumevipa hadhi ya kuwa Hospitali ya Wilaya. Nasema hivyo kwa sababu, kwa kufanya hivyo, itasaidia sana kuweza kupunguza msongamano kwenye hospitali zetu zile za Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo pia nataka nilizungumzie ni suala la maji. Kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Rais, ameeleza vizuri sana namna gani ambavyo Serikali imeweka pesa za kutosha zaidi ya shilingi trilioni 2.2 ndani ya miaka mitano, zimepelekwa kwenda kutatua changamoto ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais amesema kwamba imejengwa miradi zaidi ya 1,422 katika nchi nzima ya Tanzania. Hata hivyo, ni ukweli ulio wazi kwamba jitihada za Serikali ziko wazi na tumeona namna gani ambavyo Wizara ya Maji imekuwa ikifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kwamba inatatua changamoto za maji, lakini bado changamoto ya maji ni kubwa katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Rais amesema na hotuba ya Mheshimiwa Rais ni maelekezo; nataka nishauri kwamba pamoja na mambo yote ambayo tutaongea ndani ya hili Bunge, lakini bado changamoto itabaki pale pale kwa sababu Mfuko wa Maji chanzo chake bado hakitoshi. Ukiangalia miradi ya maji ni mingi lakini yote inategemea Mfuko mmoja wa Maji ambao fedha zake ni ndogo. Hili suala ndani ya Bunge lako Tukufu tumekuwa tukilizungumza hata kipindi kilichopita kwamba pamoja na jitihada ambazo zitakazofanyika lakini kuna umuhimu na haja kuhakikisha kwamba Serikali inaongeza fedha kwenye Mfuko wa Maji ili kuweza kutatua tatizo la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi hii. (Makofi)