Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Dr. Thea Medard Ntara

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii ya kuingia kwenye Bunge hili kwa mara ya kwanza. Pia nichukue nafasi hii kuwashukuru wanawake wa Mkoa wa Ruvuma na wanawake wa Taifa hili wale wajumbe wa Baraza Kuu ambao walinifanya mimi nikapita na nimeweza kuingia Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja katika kuchangiaspeech ya Rais. Najikita zaidi kwenye mikopo ya elimu ya juu. Bajeti ya mikopo bado ni ndogo sanana wanafunzi wengi sana wanakosa mkopo. Sasa ili tuweze kusaidia kuondoa manung’uniko kwenye suala la mikopo ningeshauri Serikali itoe fedha kwa wanafunzi wote angalau wote wapate flat rate kama ni asilimia 80 mpaka 85 itasaidia, lakini kama wengine wanapata asilimia 100 halafu wengine hawapati kabisa basi hili suala la mikopo litaendelea kuwa na manung’uniko mengi sana. Kwa hiyo cha kufanyika sasa hivi ni kuhakikisha kwamba watoto wote wenye vigezo vya kuingia Chuo Kikuu wapewe mikopo kwa rate ambayo itafanana wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine sasa hivi tuna wanafunzi wengi sana katika vyuo vikuu. Unaingia darasa lile kufundisha lina wanafunzi 1,000, Walimu ni wachache, wafanyakazi ni wachache. Miaka miwili iliyopita kila wakati wanasema Walimu wataongezeka, Wahadhiri wataongezeka, watendaji ndani ya vyuo vikuu wataongezeka lakini bado hawaongezeki. Hilo linasababisha hata ufundishaji ndani ya vyuo vyetu unakuwa sio ufundishaji wa kufundisha kama tunavyotegemea. Kwa hiyo napendekeza kwamba lazima idadi ya Wahadhiri iongezeke, vyuo vikuu waruhusiwe au wapewe dhamana ya kuajiri Wahadhiri wa kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine katika kuboresha maarifa na ujuzi. Sasa hivi tunalalamika kwamba wanafunzi wetu wakitoka vyuo vikuu hawana life skills, vocational skills lakini hii yote kwa sababu bado ile competence approach hata Wahadhiri bado hawaijui. Ningeishauri Serikali kwamba wajitahidi sana kuongeza bajeti kwa TAIili TAIwaweze kutoa seminar au waweze kutoa hayo masomo kwa Wahadhiri pia na wao waweze kufundisha vizuri inavyotakiwa kama vile ambavyo wanatoa semina au ujuzi wa Tutors. Kwa hiyo pia hata Wahadhiri wanatakiwa wapewe hizo semina ili wafundishe katika ubora unaotakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali. Kulikuwa na jambo limetokea katika vyuo vikuu kuhusu rushwa ya ngono. Mimi niwapongeze sana TAKUKURU kwa lile jambo walilolifanya, lakini niwaombe kama walifanya utafiti na kugundua kwamba kuna baadhi ya wahadhiri sio waaminifu wanatumia nafasi zao kupokea rushwa za ngono kutoka kwa wanafunzi wetu, basi tuwaombe hao wakuu wa vyuo pamoja na Wizara inayohusika wawachukulie hatua mara moja. Suala la ngono ni ngumu sana kupata ushahidi, lakini wengi wakikutaja wewe, watu 20 wanakutaja watu 50 wanakutaja, kwanini wasimtaje mtu mwingine? Viongozi wachukue hatua mara moja.Niwapongeze sana wale wakuu wa vyuo ambao wamechukua hatua ya kuwasimamisha kazi baadhi ya Wahadhiri wanaowatumia watoto wetu kuwageuza kuwa vyombo vya kustarehe.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, niwaombe TAKUKURU, baada ya kufanya tafiti zao, ile feedback waipeleke kwenye vyuo.Isibaki kwao. Ukishafanya tafiti lazima wewe ile ripoti uwape vyuo vikuu waone, wasome, kwamba ninyi mnafanya mambo hayana haya machafu. Sio ngono tu, watoto wetu wa kiume pia wanaombwa pesa. Kwa hiyo Serikali iingilie hilo na wasaidiane na TAKUKURU kuona kwamba sasa tunapata elimu bora na sio elimu ambayo imepitia huko kwenye rushwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nikushukuru sana.(Makofi)