Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Haji Amour Haji

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makunduchi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. HAJI AMOUR HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza napenda kushukuru kupata nafasi hii ya kuja kushiriki katika Bunge letu hili Tukufu ikiwa ni mara yangu ya kwanza.

Napenda kukishukuru Chama changu Cha Mapinduzi kwa kuweza kunichagua kwa kura nyingi sana katika Jimbo langu la Pangawe, Zanzibar. Pia napenda kuishukuru familia yangu kwa kunipa ushirikiano mzuri hadi kufikia hii leo na kushinda katika Uchaguzi Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kisha napenda kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, hasa katika hotuba yake hii aliyoitoa mwezi wa Novemba, tarehe 13 ambayo mimi naiita ni hotuba shirikishi, ni hotuba ambayo imetupa mtazamo ambao ni mkubwa sana katika nchi yetu kwa kipindi cha miaka mitano.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunasema kwamba hii ni hotuba ambayo inazungumzia masuala ya maono, yaani masuala ya programu ya miaka mitano kwa kipindi ambacho kimeanzia kipindi hiki, hasa ntazungumzia katika ushirikishi uliokuwa humo kwa upande wa nchi zetu mbili; Tanzania Zanzibar pamoja na Tanzania Bara, kazungumza mengi sana kiasi ambacho ametupa moyo sisi Wazanzibari ambao tumeshiriki katika Bunge letu hili Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba hii pia, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizungumza vizuri sana katika kumpa ushirikiano Rais wetu wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ambaye pia nampongeza kwa jitihada zake kubwa ambazo anazifanya na kwa weledi ambao ameupata kutoka katika Bunge hili na kwa fikra ambazo amezipata kwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nadhani kwamba huko kila mmoja anasikia kuwa kazi ambayo anaifanya Rais wetu wa Zanzibar, Dkt, Hussein Ali Mwinyi, ni nzuri sana na nampongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba hii imezungumzia suala la kimuungano hasa katika masuala ya kiuchumi, ushirikiano wa uvuvi hasa katika Sekta ya Bahari Kuu ambayo ni sekta ya Muungano. Namshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada zake na ushirikiano wake mzuri na kwa kuona ule umuhimu wetu wa kuunganisha nchi zetu wa kusema kwamba atanunua meli nane ambazo nne zitakuwa kwa upande wa Zanzibar na nne zitakuwa kwa upande wa Tanzania Bara.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tumeona jitihada na tunaona umuhimu wa meli zile katika hotuba ile na kipengele kile kimezungumzia suala la ajira 30,000. Tunatumai katika ajira hizo Wazanzibari labda tutapata ajira 15,000 na upande wa Bara zitakuwa ajira 15,000, itakuwa si haba.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina mengi hasa kuzungumzia suala la ajira. Nitazungumzia suala mtambuka la upande wa Muungano; tuna tatizo kubwa la ajira hasa ajira ambazo wakati mwingine tunazizungumzia kwamba ni ajira rasmi na kuna ajira ambazo siyo rasmi. Nadhani kwamba Waziri wa Ajira upande wa Tanzania yupo hapa; kuna suala ambalo limekuwa ni tatizo hasa linalohusiana na suala la ajira hizi za nje, employment agencies, ambazo hizi kwa upande mmoja kama tutaweza kuziwekea mkazo hasa ni ajira ambazo wakati mwingine linaweza likaleta soko kubwa, hasa kwa vijana wetu waliomaliza na hawana kazi. Kwa sababu wakati mwingine tunazungumzia suala la ajira kwamba labda watu waende kwenye kilimo, waende wapi. Ukiangalia hasa kuna fursa kubwa kwa kwa upande wa Tanzania kwa fursa zinazotokea nje ya nchi ambazo wakati mwingine zinakuwa ni ajira ambazo nazo ni rasmi lakini zinahitaji kuangaliwa ule umuhimu wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kuna ajira ambazo zipo katika Nchi za Kiarabu kule, wakati mwingine tunakuwa na ufahamu ambao ni hasi kuziona kwamba zile ajira wakati mwingine kama ni human trafficking, lakini zipo ambazo zinakuja katika hali ya urasmi na zinakuja kwa mpangilio maalum, hasa kwa mikataba maalum na kwa muda maalum.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kinachosikitisha ni kwamba wakati mwingine zile ajira zinakuja. Zipo ajira karibu, kwa mfano kwa upande wa Zanzibar kipindi hiki niliona zimekuja ajira kwa Tanzania karibu 1,200. Kwa kampuni moja ambayo ni Transguard ambayo iko Dubai pale, lakini utakuta kwamba Watanzania fursa ile tunashindwa kuitumia na kushindwa kwetu maana yake ni kwamba inawezekana milango imeā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. HAJI AMOUR HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba dakika moja tu nifafanue kidogo tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo linalokuja ni kwamba milango kwa upande wa Tanzania Bara ile milango imefungwa kwa kuwaruhusu wale vijana kwenda kufanya kazi kule nje, ile fursa ya kupewa vile vibali, lakini kwa upande wa Zanzibar ile fursa inatumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa namwomba Waziri mhusika kwamba hiyo fursa aitoe na tupange mipangilio mizuri itakayoweza kuwapatia ajira vijana wetu wa Tanzania kwa ujumla na zinapotokea zile fursa maana yake ziwe kwa wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine zile fursa kwa upande wa Zanzibar tunazitumia vizuri, lakini upande wa Tanzania Bara inakuwa kidogo kama kuna milango ambayo imefungwa kwa zile fursa kwa upande wa vijana wetu kwa upande wa huku. Sasa nahisi kwamba tufanye mipango mizuri kupitia Balozi zetu kuunganisha suala hili ili kwamba nayo iwe ni fursa kwa vijana wetu kupata ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, kutokana na muda, naunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano. Ahsante sana. (Makofi)