Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kunipa fursa ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa tarehe 13 Novemba, 2020.
Kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kurudi tena katika jengo hili. Pia nakishukuru Chama change Cha Mapinduzi, Jumiya ya UWT, wapiga kura wangu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja na wote kwa namna moja au nyingine walioshiriki kunifikisha katika jengo hili, ahsanteni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, natoa pongezi pia kwa Mheshimiwa Rais wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mama Samia na Waziri Mkuu Mheshimiwa Majaliwa. Pongezi hizi hazitatimia kama sitaweza kutoa pongezi kwa Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais na Makamu wa Pili wa Rais ninawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hotuba zote mbili nilizisikia na nilizisoma kwenye vitabu. Nitachangia kwa machache nikianza kwanza kwa kuungana na wenzangu kuunga mkono asilimia mia moja hotuba hii. Pia niseme kwamba wengi wanatuambia tunapenda sana kupongeza, niseme tu tunapongeza kwa sababu vya kupongeza vipo, kama hakuna vya kupongeza hatutapongeza, tunaendelea kupongeza kwa sababu vya kupongeza vipo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika ukurasa wa tatu na wa nne ameelezea juu ya Tume ya Uchaguzi ilivyofanya vizuri. Mimi naunga mkono na niwapongee sana, kitendo alichokifanya ni sawasawa na mtende kuota jangwani, kati ya shilingi bilioni 331 wameweza kutumia shilingi bilioni 262 na kubakiza shilingi bilioni 69 hayo ni maajabu. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Kiruswa umevunja utaratibu, umepita kati yangu na mzungumzaji, kwa hiyo, rudi ulikotoka. Kwa Wabunge wageni Mbunge yeyote anayeongea unaacha line yake na Spika huruhusiwi kuikatiza. Endelea Angelina Malembeka.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Spika, naomba nitunziwe muda wangu. Ninaendelea kusema kwamba naipongeza Tume ya Uchaguzi kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa kutumia shilingi bilioni 262 kati ya shilingi bilioni 331 na kubakiza shilingi bilioni 69, nimesema hayo ni maajabu ya mtende kuota jangwani. Hii imeonesha uadilifu mkubwa kwa watumishi wa umma na imeonesha jinsi gani nidhamu sasa ilivyotapakaa, ninaomba hali hii iendelee katika siku zijazo tusisifie sasa halafu baadae mambo yakawa yamebadilika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika ukurasa wa saba Mheshimiwa Rais alielezea jinsi gani ambavyo atatoa ushirikiano wa kutosha kwa Rais wa Zanzibar. Suala hilo sisi tumelifurahia sana kwa sababu wakati hata anaomba kura Zanzibar alisema niletee Dkt. Mwinyi nitawasaidia, nitawanyanyua uchumi wa Zanzibar na sasa hivi tuko katika Zanzibar upya, uchumi mpya tunategemea haya aliyoyasema atayatekeleza na tunamuombea kila la kheri ayatekeleze ili Zanzibar ibadilike kama ilivyopangwa.
Mheshimiwa Spika, katika ukurasa wake wa 11 alielezea mifuko mbalimbali na programu ambazo zimeanzishwa ili kusaidia wananchi ikiwepo Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, Mfuko wa Taifa wa Kuendesha Wajasiriamali, Mfuko wa Kutoa Mikopo, lakini katika mifuko hiyo hakuna mfuko wa wavuvi wadogo wadogo.
Nilikuwa ninaomba basi uanzishwe mfuko kwa ajili ya wavuvi wadogo wadogo waweze kukopa wao kwa riba nafuu au mkopo usio na riba ili waweze kununua vifaa vya kisasa vya uvuvi ambavyo vitasaidia pia kuondoa uvuvi haramu katika bahari zetu na tukiangalia sasa hivi tunaingia katika uvuvi wa bahari kuu na uchumi wa blue ambapo tunategemea kwamba meli kubwa za kisasa zinanunuliwa ziweze kufanyakazi. (Makofi)
Lakini kama tutanunua meli kubwa za kisasa, lakini bado wavuvi wadogo wadogo wanaendelea kutumia mabomu kuvua bado tutakuwa hatujafanya kazi. Kwa hiyo niombe kwamba mfuko maalum uandaliwe kwaajili ya wavuvi wadogo wadogo waweze kukopeshwa.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo uwekezaji katika sekta ya uvuvi basi wale wawekezaji wazawa nao wapunguziwe kodi ili waweze kuleta samaki wengi na wakileta samaki wengi samaki bei itashuka na kila mwananchi ataweza kula samaki na hivyo kuboresha afya zetu. Tukiwawekea kodi kubwa na meli za uvuvi zitakuwepo halafu samaki tutashindwa kununua, kwa hiyo nilikuwa naomba hilo pia liangaliwe.
Mheshimiwa Spika, lingine ambalo nimeona nilizungumzie ni kuhusiana na suala la Corona ambalo katika ukurasa wa 32 na 33 limezungumziwa. Tumeona umuhimu wa kutumia dawa tiba au mitishamba au dawa mbadala, hili suala kwa kweli nimshukuru Mheshimiwa Rais ametupa ujasiri ametupa nguvu tunasimama hatuhangaiki, sasa hivi hata mtu tukimuona anakohoa tunajua jinsi gani ya kufanya, lakini mwanzo ilikuwa hata ukiona jirani yako anakohoa unatafuta kiti cha kuhama umkimbie. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini sasa hivi tumepata ujasiri, tumeendelea kutumia hizo dawa lakini pia nimpongeze kaka yangu Mheshimiwa Jafo kwamba mzee wa nyungu tumepata nguvu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Angelina, tunakushukuru sana.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Ninaomba zile taasisi zinazoshughulika na utafiti pamoja na kutoa vibali kwaajili ya dawa hizo zifanye haraka ili dawa zisambae wananchi wapate huduma naunga mkono hoja ahsante. (Makofi)