Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Njombe Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
3
Ministries
nil
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi nipate kuchangia kwenye hoja iliyo mbele yetu. Kwanza nitoe shukrani kwa chama changu na Mwenyekiti wa Chama kunipa nafasi ya kuwa mgombea na mwisho wa siku kuwa Mbunge katika Bunge hili, lakini la pili vilevile nawashukuru sana wananchi wa Njombe Mjini kwa kuniamini na kunipa nafasi ya Ubunge nasema sitawaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hotuba ambayo Mheshimiwa Rais ameitoa ni hotuba ambayo imetoa matumaini makubwa sana. Ni matumaini yaliyojengwa katika msingi wa mafanikio yaliyopatikana katika miaka mitano iliyopita, yameongelewa hapa kwa wingi hatuna sababu ya kuyataja yote, lakini mimi niongelee moja ambalo limenigusa na litaendelea kunigusa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais tumeshuhudia akifanya mabadiliko makubwa sana katika sekta ya madini. Mimi nasema yalikuwa ni maamuzi sahihi katika wakati sahihi. Tumeshuhudia sasa sekta hii ya madini kuwa ni sekta ambayo inaongoza kwa kuongezea nchi fedha za kigeni, lakini ni sekta inayokua kwa haraka sana. Naomba sasa Serikali iendelee kujikita na kuangalia madini mengine na hasa kwa vile utafiti katika sekta ya madini ni jambo la muhimu sana. Tunaelewa hatuwezi kutegemea wawekezaji kutoka nje kufanya utafiti, kwa hiyo, wazo langu au ushauri wangu kwamba Serikali ijikite kuiongezea STAMICO hela za kutosha ifanye utafiti. Na sisi tunawakaribisha kule Njombe kuna madini ya kila aina waweze kuja kufanya utafiti.
Mheshimiwa Spika, la pili ambalo nilitaka niongelee ni suala zima la viwanda na uwekezaji. Ukisoma hotuba ya Mheshimiwa Rais imejikita sana kuongelea sekta binafsi na viwanda. Ni jambo muhimu na ni jambo ambalo litatufanya sisi tuweze kufikia lengo la zile ajira milioni nane. Kule Njombe tumejikita katika uwekezaji na ukulima, lakini kwetu sisi suala la viwanda ni suala la muhimu sana na Mheshimiwa Rais anaongelea kutengeneza mazingira mazuri ya kuwavutia wawekezaji katika viwanda.
Mheshimiwa Spika, lakini niseme moja kwamba wakati tunawavutia wawekezaji katika viwanda tuangalie wawekezaji waliopo katika maeneo yetu. Kule Njombe tuna zao moja la kimkakati la chai, ni zao ambalo linatakiwa lipewe umuhimu mkubwa sana. Kwa sasa zao hili linalegalega na kuna uwezekano kama hatua za haraka hazitachukuliwa litafikia mahali pabaya.
Mheshimiwa Spika, nitoe wito, naelewa katika hotuba ya Mheshimiwa Rais ameongelea kuweka mazingira wezeshi ambayo yatasaidia uwekezaji uweze kufufuka katika maeneo mbalimbali. Nipende kusema kwamba bado pamoja na kwamba kuna blue print na tunaelewa inakuja, tumeshuhudia kwamba bado kuna tozo za kila aina ambazo zimekuwa ni kero kwa wawekezaji na kero hizo kwa vile ni suala la viwanda na kwa vile tunaongelea chai, tunaongelea mkulima wa kawaida ambaye mwisho wa siku ndiye kipato chake kitashuka.
Mheshimiwa Spika, ukilinganisha ukulima viwanda vya chai ambavyo viko katika maeneo sio tu ya Njombe, lakini na maeneo mengine ya jirani tozo zake ukilinganisha na viwanda vingine vya Kenya vya chai na viwanda vingine vya nchi kama Malawi unakuta wenzetu tozo ni chache sana. Kuna study imefanyika inaonesha tozo za viwanda vya chai peke yake zinafika karibu 19 wakati wenzetu hawana tozo, kwa hiyo, ningeomba Serikali ilitupie macho jambo hilo kwa ukaribu sana.
Mheshimiwa Spika, lakini niongelee vilevile kero nyingine ambazo zinajitokeza katika kushughulikia masuala ya wafanyabiashara, hasa wa mazao ya miti katika Jimbo la Njombe na Jimbo la Njombe ni Jimbo la Njombe Mjini, lakini lina vijiji vingi sana.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, naomba niunge hoja mkono, lakini nipende kusisitiza iko haja ya kutatua kero za wakulima wa miti na mashamba ya mbao kule Njombe kama vile Rais alivyoahidi wakati wa kampeni. Ahsante sana. (Makofi)