Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nkenge
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nishukuru kwa nafasi ya kuchangia katika Bunge lako tukufu na mimi kwa nafasi ya pekee naomba nitoe shukrani nyingi sana kwa Mwenyezi Mungu, nitoe shukrani nyingi sana kwa chama changu Chama cha Mapinduzi kikiongozwa na Mheshimiwa John Joseph Pombe Magufuli. Lakini pia niishukuru familia yangu mke wangu watoto wangu lakini kwa nafasi ya pekee pia wapiga kura wa Jimbo la Nkenge ambao walitupatia kura pacha 91% pamoja na Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika, nimesoma hotuba za Mheshimiwa Rais ambazo kwa kweli zinatia faraja, zinatia matumaini zinatoa muelekeo na kuonyesha kwamba Rais yuko kwenye mstari wa kupeleka nchi yetu katika uchumi ambao ni wa juu zaidi kuliko ambavyo tumefikia sasa hivi kwa kazi nzuri iliyofanyika katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Mheshimiwa Spika, tunaona faraja kubwa inatoka wapi katika nchi yetu, kwanza ni kusimamia tunu za Taifa; amani, mshikamano, uhuru wa nchi yetu, Muungano na Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ndiyo inatoa fursa kwa watu walioko nje ya Tanzania kuweza kuona ni fursa nzuri ya kuweza kuwekeza katika nchi ya Tanzania na hii ni ushahidi mwingi kweli tumeona mikataba mikubwa ya madini ikirejewa tumeona mikataba ikiendelea kusainiwa mipya lakini tunaona mapinduzi makubwa ya kiuchumi na hii siyo peke yake ni kwa sababu ya Mheshimiwa Rais akiwa na wasaidizi wake mahiri kuanzia Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mawaziri aliowateua.
Mheshimiwa Spika, tunaona kutokana na taarifa ya IMF ya mwaka 2019 uchumi wa nchi yetu unaendelea kupaa na Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi kumi bora katika Bara la Afrika. Naamini kwa hotuba hii aliyowasilisha katika kipindi hiki basi tutaenda kuwa nchi ya kwanza kati ya hizo kumi katika Bara la Afrika na kuzidi nchi nyingine za Ulaya.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo na nia ya dhati ya kuona Rais anataka kutuvusha katika miaka mitano mingine ijayo niombe kuchangia kidogo katika maeneo mengine. Niseme kwamba hotuba ile imeshamaliza kila kitu, hapa tupo tunaboresha na kuweka kachumbari ili mambo yaende, lakini muelekeo wa nchi umesheheni katika hotuba ya Mheshimiwa Rais na hivyo hatuna budi sisi kama washauri, kama wasimamizi, kama watendaji kuhakikisha sasa tunayaishi haya ambayo Mheshimiwa Rais ametuambia kwenye hotuba yake ili aweze kutufikisha pale ambapo anaona inafaa kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, nishauri kidogo kwenye eneo la viwanda, tunaona nchi yetu ambavyo imeendelea kupambana kuhakikisha kwamba inakuwa na viwanda vya kutosha ili tuendelee kupata mchango mkubwa kutoka kwenye viwanda na tunaona viwanda vingi takribani 8,477 ambavyo vimeweza kuanzishwa katika awamu ya kwanza ya Mheshimiwa Rais. Lakini tunaona mchango wa Pato la Taifa kutoka kwenye viwanda ni zaidi ya 8.5%.
Mheshimiwa Spika, tunaona ajira zaidi ya 480,000 kutoka kwenye viwanda. Niseme kwa kaka yangu Mheshimiwa Waziri wa Viwanda tunapokuwa tunaona kiwanda chochote kinaguswa lazima tuamke tuweze kuona ni jinsi gani ya kukilinda na Wizara zetu niombe ziongee lugha moja ambayo inaweza kuinua Wizara nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nikupe mfano wa kiwanda kimoja kiko katika Jimbo langu la Nkenge, Wilaya ya Misenyi. Kiwanda hicho ni cha Oram kilikuwa ninachakata na ku-grade kahawa ukiangalia capital investment iliyowekwa kwenye kiwanda hicho, sasa hivi kimebaki ni magofu kwasababu ya mabadiliko kidogo ya kisera. Najua nchi yetu inao utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba mambo yanaenda sawa, lakini mambo mengine lazima tuwe flexible kidogo kuona ni kitu gani ambacho tunaweza kufanya ili mambo yote yaweze kwenda. Kuna mabadiliko kidogo ya sheria katika kilimo kwamba kahawa zote zinunuliwe na AMCOS. Kwa hiyo, maana yake viwanda ambavyo vilikuwa vinaendeshwa vyote vika paralyse.
Mheshimiwa Spika, wananchi sasa hivi wanalia, kahawa wanazipeleka kule, zinabaki muda mrefu bila malipo kiwanda hicho kilikuwa kinatoa bei nzuri na wananchi wanalipwa kwa wakati, inachangia Pato la Taifa kinaajiri zaidi ya watu 2000 katika Wilaya ya Misenyi. Sasa hivi vijana wote wamerudi mtaani wapo wanamlilia Mbunge wao sijui nitawapeleka wapi. Kaka yangu Mwambe, kaka yangu Bashe najua nyie mko smart, naomba mkae pamoja mu- harmonize muweze kuhakikisha kwamba kiwanda hicho cha Oram kirudi kufanya kazi ili uchumi wa nchi, lakini na uchumi wa Misenyi uweze kukomboka.
Mheshimiwa Spika, nishukuru kwa muda ulionipa naomba kuunga hoja hotuba ya Mheshimiwa Rais, ahsanteni. (Makofi)