Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Humphrey Herson Polepole

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. HUMPHREY H. POLEPOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia na kwa sababu ni mara yangu ya kwanza namshukuru sana Mungu wa Mbinguni kwa kunipa nafasi hii. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kunipa heshima ya kuwa sehemu ya Bunge hili tukufu, nami nawaahidi Watanzania lakini pia Bunge hili kuendelea kuchapa kazi ili tuweze kufikia malengo ya Watanzania kama ambavyo wanatarajia.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia hotuba aliyoitoa Mheshimiwa Rais katika Bunge hili la Kumi na Mbili lakini nikirejea hotuba aliyoitoa katika Bunge la Kumi na Moja na nitajielekeza katika mambo matatu. La kwanza ni kuhusu viwanda vidogovidogo, vya kati na vikubwa. Mheshimiwa Rais ameeleza katika hotuba yake umuhimu wa viwanda na mchango wake mkubwa katika kutengeneza ajira zaidi hapa Tanzania na tukitazamia ajira milioni nane ambazo Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi inalenga kuzitengeneza katika miaka hii mitano.

Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu kwa Serikali; tukiunganisha viwanda vidogo vidogo na vya kati na Sekta ya Kilimo kuna faida kubwa sana na tutaweza kuona tija ya viwanda hivyo. Natoa mfano mmoja; mahitaji yetu ya mafuta ya kula hapa Tanzania sasa hivi ni wastani wa tani laki tano na uzalishaji wetu wa ndani wa mafuta ya kula ni wastani wa tani laki mbili na nusu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali ikifanyia kazi yenyewe na kwa kushirikiana na Sekta Binafsi pale inapowezekana na pale isipowezekana Serikali yenyewe ichukue dhamana hii kushirikiana na wananchi kutengeneza viwanda vidogo vidogo na vya kati katika maeneo wanapolima alizeti na mawese, ili wakulima ambao wamekosa fursa ya kuuza mazao haya ya alizeti na mawese kwa muda mrefu wawe na soko la uhakika kwa sababu kuna viwanda vya kuchakata alizeti na mawese na kutengeneza mafuta na hatimaye mafuta haya yatapata soko kwa sababu mpaka sasa hivi tuna nakisi ya mafuta ya kula wastani wa tani laki tatu. Maana yake wakulima watapata fedha yao, viwanda hivi vilivyowekeza na Serikali vitarejesha fedha yake na kujiendesha kwa faida, lakini pia walaji watapata mafuta.

Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu; ingependeza sana baada ya kuwa tumefikia kiwango kikubwa cha kuzalisha mafuta nchini, kama zilivyo nchi zingine ambazo zina sera za kulinda masoko ya ndani, (protectionist policies), tuseme marufuku sasa kuagiza mafuta kutoka nje kwa sababu tunazalisha hapa hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ni kuhusu uvuvi; Mheshimiwa Rais ameeleza vizuri sana kuhusu uvuvi wa bahari kuu na katika maziwa yetu makuu ikiwemo ununuzi wa meli, vifaa vya kufanyia uvuvi wa kisasa na kadhalika. Rai yangu kwa Serikali; tulitazame sana Ziwa Victoria na tufanye uvuvi wa kisasa wa vizimba (aquaculture fish farming). Serikali kupitia halmashauri zetu zishauriwe wawekeze kwenye uvuvi wa vizimba (aquaculture fish farming), ni uvuvi wenye faida kubwa na tija kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi mahitaji yetu ya sato hapa nchini bado ni pungufu. Tukiwekeza katika Ziwa Victoria kwa vizimba na tukafuga samaki sato wengi zaidi si tu tutaongeza mapato ya wale ambao wamewekeza wakiwepo watu wa halmashauri, tutaongeza lishe kwa watu wetu wa Tanzania lakini pia tutauza nje sato hao kwa sababu hata katika eneo la maziwa makuu, bado uwekezaji katika ufugaji wa samaki kupitia vizimba haujafanyika vizuri sana. Kwa hiyo tutaongeza pia fedha za kigeni kwa maana hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ni ufugaji. Hapa niseme tu kwa ufupi kwamba kazi nzuri imefanyika. Sisi tunaongoza kwa kuwa na ng’ombe wengi Afrika na hili limeelezwa vizuri sana katika hotuba ya Mheshimiwa Rais. Rai yangu mimi, kitu kimoja hatujafanya vizuri; ufugaji wa sasa ni wa kuhamahama, unafanya tija ya ng’ombe ishuke. Kama tukiwekeza kwenye mashamba ya kulima majani, chakula cha ng’ombe (hay) ambapo sasa hivi kwa utafiti niliyoufanya kuna mashamba mawili tu, nafikiri moja liko kule Mbeya. Kama tukilima hay tukawapatia wakulima, ng’ombe wao hawatahitaji kutembea kila mahali na kuleta migogoro kati ya wakulima na wafugaji. Hata hivyo, hay ikilimwa vizuri hapa Tanzania tukaweka mashamba mengi zaidi ya hay, hay ni fursa kubwa na uwekezaji huu utaweza kutuwezesha sisi kuuza hay kwenda nje ya nchi kwa sababu ni zao ambalo linahitajika sana, si tu hapa Tanzania lakini nchi za nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo matatu nigusie moja ambalo limesemwa na wengi, lakini nami niongezee tu kwa uzito. Mwaka 2000 kiongozi wa UAE, Al-Maktoum alifanya uamuzi wa kununua ndege 59 za Shirika la Emirates. Mwaka kati ya 2000…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. HUMPHREY H. POLEPOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mchango wangu nitauwasilisha kwa maandishi. (Makofi)